MAPINDUZI YA KILIMO AU KILIMO CHA KIMAPINDUZI?
Na Mwl. Sabatho Nyamsenda
Mada hii iliwasilishwa katika Siku ya Maadhimisho ya Chakula Duniani
iliyoandaliwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA) na
kufanyika katika ukumbi wa ICE, Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Oktoba 16, 2014, chini
ya kauli-mbiu “Kilimo cha Familia:
Kulisha Ulimwengu na Kutunza Mazingira. Je, Ndoto Itatimia?”
Utangulizi
Nawashukuru sana
MVIWATA kwa kunialika kuja kuwasilisha mada katika maadhimisho haya. Japo nilipewa
mwaliko katika muda mfupi, nilikubali kuja kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza
ni kwamba nilitaka kujifunza. Kila mara nikutanapo na wavuja-jasho – iwe ni
katika daladala, vijiwe, au makongamano – huwa najifunza mambo mengi kuhusiana
na madhila yasababishwayo na mfumo katili wa uliberali mambo-leo pamoja na
mbinu za kupambana nao. Hivyo, kazi yangu itakuwa ni kuchokoza mada, na maarifa
yatatoka kwenu ninyi wakulima wadogo!
Sababu ya pili ya
mimi kuja hapa ni kuwa juma hili ni juma la pekee. Ni juma ambalo wanyonge wa
Afrika wanaadhimisha vifo vya majabali wawili wa mapambano ya wanyonge. Hao ni
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Thomas Sankara aliyekuwa kiongozi wa
Burkina Faso. Mwalimu alifariki Oktoba 14, 1999. Sankara aliuawa kikatili
Oktoba 15, 1987. Mashujaa hawa ni watu waliokula yamini kuubomoa ubepari na
ubeberu, pamoja na taasisi zinazoutumikia. Hivyo leo hii ni siku pia ya
kutafakari fikra zao na mbinu zao za mapambano ili tuzitumie kuendeleza
mapambano dhidi ya mfumo huu katili.
Wahenga walinena
kuwa “wema hawadumu”! Wakati wanyonge wakiomboleza vifo vya akina Sankara na
Nyerere, juma hili pia ni maadhimisho ya miaka 70 ya dubwasha liitwalo Benki ya
Dunia.
Dubwasha hili lililozaliwa
1944 lilikuwa na kazi ya kufufua chumi za nchi za Ulaya baada ya kuharibiwa
vibaya wakati wa vita vya pili vya dunia, ambavyo vilianzishwa na
mabeberu wenyewe. Sijui ni nani aliyelipa hadhi ya kuwa benki ya dunia!? Wakati
wa uhai wake, Nyerere alipambana kuliua dubwasha hili kwa kudai mfumo mpya wa
uchumi wa dunia (New International
Economic Order). Harakati za Nyerere zilibomolewa na aliyekuwa Rais wa
Marekani wakati huo, Ronald Reagan, ambaye aliukataa mfumo mpya.
Sankara aliwataka
viongozi wa Afrika kuungana ili kugomea kulipa madeni, ambayo Benki ya Dunia na
IMF walikuwa wakiilazimisha Afrika kuyalipa. Madeni hayo ni ya kilaghai, na
fedha hizo zimeibwa toka nchi maskini. Akihutubia katika mkutano wa Umoja wa
Afrika mwaka 1987, Sankara alisema: “[Tunapaswa kugoma kwa pamoja] ili kuzuia
tusiuawe mmoja mmoja. Lakini Burkina Faso ikigoma kulipa peke yake, sitakuwepo
hapa katika mkutano ujao”. Na ndivyo ilivyotokea. Aliuawa kikatili mwaka huo
huo, kwa kusalitiwa na msaidizi wake, Blaise Compaore, ambaye alikuwa akitumiwa
na mabeberu[1].
Lakini mapambano ya
akina Nyerere na Sankara hayajafa. Juma hili, wapo wanaharakati waliokusanyika katika
miji mbalimbali duniani kuiombea Benki hii “dua ya kifo”. Wanasema kuwa Benki
hii haikustahili kuishi miaka 70; na ni wakati sasa Benki ya Dunia ife kifo cha
kawaida. Kama haitaki kufa basi angalau istaafu kwa lazima!
Je, Benki ya Dunia
imefanya makosa gani hata kustahili adhabu ya kifo? Naam, imetenda dhambi
zisizosameheka. Ni benki hii, pamoja na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF),
iliyozilazimisha nchi maskini duniani kufuata sera za kiuaji na kiporaji za
uliberali mambo-leo. Madhara ya sera hizo za ubidhaishaji, ubinafsishaji,
uwekezaji na ufedhaishaji yamesababisha vifo vya wanyonge, uporaji wa ajira,
uporaji wa rasilimali na uharibifu mkubwa wa mazingira.
Hivyo, nami pia nimekuja
hapa kuishtaki Benki ya Dunia kwenu ninyi wakulima wadogo. Hivi sasa Benki ya
Dunia imepiga hatua ya juu kabisa ya uporaji, kwa kulazimisha nchi maskini
zikumbatie sera za “mapinduzi ya kijani” ambazo katika mada hii nitaziita
“mapinduzi ya kilimo”! Hapa Tanzania, kuna mkatati uitwao Kilimo Kwanza, ambao
ni utekelezaji mahsusi wa sera za mapinduzi ya kilimo.
Sera hizi zimelenga
kumuangamiza kabisa mkulima mdogo, na kumfanya atoweke katika uso wa dunia. Ni
sera za kiuaji. Ni sera za kijambazi. Ndio maana, wanaharakati walioungana
kuipinga Benki ya Dunia wanatuambia kuwa tupinge kwa nguvu zote “sera za
maendeleo za kiuendawazimu na kiuaji ambazo huweka mbele ukuaji wa nguvu za
kampuni za kibepari; na ambazo hupuuza ukweli kwamba dunia inalishwa na watu wa
kawaida walimao mashamba madogo madogo, na sio kampuni za kibepari; na ambazo
zinaukataa ukweli wa kisayansi uthibitishao jinsi mashamba yetu, mito yetu na
hata miili yetu inavyolishwa sumu itokanayo na kilimo cha kemikali na mashine,
ambacho hufaidisha asilimia moja tu ya watu wa dunia hii”[2]
(tafsiri yangu).
Katika makala hii,
nitaonyesha namna ya kupambana na sera za kijambazi na kiuaji za Benki ya
Dunia. Nayo ni kuachana na “mapinduzi ya kilimo” ili kukumbatia “kilimo cha kimapinduzi”.
Je, nini tofauti kuu ya dhana hizo mbili? Tutazifahamu kadiri tusomavyo makala
hii.
Kilimo Kwanza: Mvinyo wa zamani katika chupa
ya mpya
“Kilimo Kwanza” ni
mkakati ulioasisiwa 2009, ukiwa na lengo la kuongeza uzalishaji katika kilimo
ili kukidhi mahitaji ya ndani, lakini hasahasa ukilienga soko la kimataifa.
Mzalishaji mkuu katika mkatati huo ni mkulima mkubwa, ambaye mbinu zake za
uzalishaji zinapaswa kuigwa na wakulima wadogo na wa kati. Mkakati wenyewe
ulikuwa ni makubaliano kati ya serikali ya Tanzania pamoja na wafanyabiashara
wakubwa nchini, makubaliano yaliyopelekea wafanyabiashara hao kupewa maelfu ya
ekari za ardhi kwa ajili ya kilimo.
Wakulima wadogo
hawakushirikishwa, japokuwa mara baada ya kikao cha Rais na mabepari uchwara wa
Bongo tukasikia sauti. Sauti hii haikutokea nyikani, bali hotelini,
palipofanyikia kikao: “Enyi wakulima wadogo msiostaarabika. Ninyi
mnajifukarisha wenyewe. Sasa achaneni na jembe la mkono. Nunueni power tillers”.
Kwa kuwa “Kilimo
Kwanza” ni mfano mzuri wa mikakati iliyopangwa kuleta mapinduzi ya kilimo au
mapinduzi ya kijani, ni vema tukianza kwa kuitazama historia ya mapinduzi ya
kilimo.
Mapinduzi ya Kilimo
Dhana ya “mapinduzi
ya kilimo” au agricultural revolution,
ni dhana ya kibepari. Imejengwa katika msingi wa chuki na mtazamo hasi dhidi ya
mkulima mdogo. Mkulima mdogo huonekana kama chanzo cha ufukara wa nchi kwa kuwa
uzalishaji wake haujikiti katika kulimbikiza faida. Ni uzalishaji duni wa
kutumia jembe la mkono, na mbinu za kale za uzalishaji. Hivyo, mashabiki wa
mapinduzi ya kilimo hutaka mkulima mdogo a-sasa-ishwe, yaani afanywe kuwa wa kisasa
(“the peasant should be modernized”). Na kwa kuwa inasemekana kuwa mkulima
mdogo huugomea usasaishaji, basi mashabiki wa mapinduzi ya kilimo husema kuwa
njia pekee ni kumyang’anya ardhi ili akawe manamba katika shamba la mkulima wa
kibepari.
Kwa hiyo basi, kwa
ufupi, katika mapinduzi ya kilimo, “injini” ya uzalishaji ni mkulima-papa. Uzalishaji
wa mkulima-papa hutegemea pande kubwa la ardhi (large-scale agriculture), na hutumia dhana na mbinu za “kisasa”.
Hizi hujumuisha mashine za kulimia na kuvunia, mbolea za kemikali zizalishwazo
viwandani pamoja, dawa za kemikali za kuulia wadudu, na mbegu zilizobadilishwa
vinasaba.
Lengo la uzalishaji
wa mkulima-papa ni kulimbikiza mtaji, na hivyo kipaumbele chake huwa ni mazao
ya kibiashara. Ikitokea mkulima-papa akazalisha chakula, lengo lake huwa ni
kuuza sokoni ili pate faida zaidi, bila kujali kuwa chakula hicho huenda
kumlisha nani. Soko linalolengwa hasa ni soko la kimataifa – soko la nje – hata
kama ndani ya nchi husika kunaweza kuwa na watu wanaokumbwa na njaa.
Sera ya mapinduzi ya
kilimo siyo ngeni kama mashabiki wake wanavyotaka kutuaminisha. Japokuwa
mashabiki wa mapinduzi ya kilimo hutumia mifano ya Mexico (1940 – 1970) na
India (1960 – 1990) kama nchi waasisi wa mapinduzi ya kilimo, ukweli ni kwamba
dhana hii ni mvinyo wa zamani katika chupa mpya. Historia ya mapinduzi ya
kilimo ndiyo historia ya mfumo wa ubepari.
Mapinduzi ya Kilimo Uingereza
Mapinduzi ya kilimo
huhusishwa na mapinduzi ya viwanda, yaliyotokea Uingereza kati ya karne ya 18
na 19. Mapinduzi hayo ya kilimo ya nchini Uingereza yalitokea kwa
kuwanyang’anya wakulima ardhi yao katika kile kilichojulikana kama “enclosure
movement”. Uporaji huo ulianza karne ya 15 kwa kuendeshwa na makabaila wenyewe
na kuongezeka zaidi kati ya karne ya 18 na 19 pale ulipohalalishwa kwa
kutungiwa sheria. Ardhi iliyoporwa iligawiwa kwa wakulima wa kibepari ili
wazalishe zaidi.
Wapo wasomi wasifiao
uporaji huo kwamba ndio uliochochea mapinduzi ya kilimo, na hatimaye maendeleo
ya viwanda nchini Uingereza. Wanadai kuwa iwapo ardhi ingeachwa mikononi mwa
wakulima wadogo, basi kusingekuwa na mapinduzi ya viwanda nchini Uingereza.
Je, ni kweli kuwa
kulikuwa na mapinduzi ya kilimo nchini Uingereza? Jibu ni hapana. Uchambuzi
uliofanywa na Profesa Utsa Patnaik[3]
unaonyesha kuwa chakula kilichozalishwa nchini Uingereza baada ya uporaji wa
ardhi hakikutosheleza kabisa kuwalisha watu wa nchi hiyo. Ni katika kipindi
hicho pia ndipo Uingereza ilipoandamwa na maradhi yatokanayo na ukosefu wa
lishe bora. Uingereza ilitegemea chakula kutoka katika makoloni yake ya Amerika
na Asia, na baadaye Afrika!
Je, uporaji huo
haukuwa na madhara nchini Uingereza? Yalikuwepo. Tena makubwa. Lakini kwa
bahati, wazalishaji wadogo walioporwa nyenzo zao za uzalishaji-mali walipelekwa
mijini kufanya kazi viwandani, huku malipo yao yakiwa ya kijungu-jiko tu.
Lakini viwanda havikutoa ajira za kutosha, hivyo watu wote wasio na ajira
pamoja na wafungwa (wao wakiwaita surplus
population, yaani watu waliozidi) wakahamishwa na kupelekwa katika Bara la
Amerika kwenda kuanzisha nchi mpya. Moja ya nchi zilizoanzishwa ni Marekani. Huko
waliletewa “mashine” za kulimia na kuchimba madini. Hazikuwa mashine za
kutengenezwa viwandani, bali ni Waafrika waliogeuzwa watumwa!
Mfano huu wa
Uingereza unatupatia mafunzo ya aina mbili juu ya mfumo wa ubepari. Mosi, ubepari
hujengwa kwa kuwapora wanyonge njia za uzalishaji. Ndicho kilichowakumba
wakulima wadogo wa Uingereza: walipoteza ardhi yao, ambayo walikuwa
wakiitegemea kuishi. Kwa hiyo, uporaji ni moja ya mbinu ambazo hutumiwa na
mabepari kulimbikiza mtaji.
Ubepari hutengeneza
matabaka. Tabaka la kwanza ni la wenye mtaji, ambalo ni tabaka la mabepari.
Mabepari hupata mtaji wao kwa kuwapora wazalishaji wadogo. Tabaka la pili ni la
wanyonge. Hawa hawakuzaliwa wakiwa maskini. Umaskini wao ulisababishwa na wao
kuporwa nyenzo zao za uzalishaji, kama ardhi. Hivyo, wakawa hawana njia
nyingine ya kuishi isipokuwa kwa kuuza nguvu-kazi yao kwa mabepari.
Funzo la pili
tulipatalo ni sura ya kimataifa ya uporaji. Wakati ambapo wanyonge wa Uingereza
waliporwa ardhi yao, Waafrika walipoteza nguvu-kazi yao ambayo ingelijenga bara
lao. Vijana wa kiafrika, wake kwa waume, waligeuzwa bidhaa, wakauzwa sokoni, na
kupelekwa Marekani kuzalisha migodini na mashambani. Utumwa uliendelea kwa miaka
400, na baadae kufuatiwa na miaka ipatayo 100 ya ukoloni. Hivyo basi, umaskini
wa Afrika umesababishwa na mfumo katili wa kiporaji wa ubepari.
Wakati wa ukoloni,
wakulima wadogo wa Afrika walinyang’anywa ardhi yao ambayo iligawiwa kwa
wakulima wakubwa wa kizungu. Uporaji huo ulitamalaki katika baadhi ya makoloni
kama Kenya, Zimbabwe na hata Afrika Kusini.
Kwa maana hiyo basi,
tunapaswa kujifunza kuwa suala la uporaji wa ardhi ndio kiini cha ubepari. Kuirejesha
ardhi iliyoporwa ni mapambano ya muda mrefu.Wazimbabwe wamefanikiwa kurejesha
ardhi yao miaka ya hivi karibuni baada ya mapambano ya muda mrefu.
Huko Afrika Kusini,
sehemu kubwa ya ardhi yenye rutuba bado inamilikiwa na kikundi cha watu
wachache wenye asili ya Kikaburu. Afrika Kusini ni nchi inayoongoza kwa pengo
kubwa kati ya walionacho na wasio nacho duniani. Wanyonge wa nchi hiyo sasa
wanapambana kurejesha ardhi mikononi mwa watu weusi. Badala ya kujifunza kutokana na mifano hiyo ili tulinde ardhi yetu, watawala wetu sasa wanagawa
ardhi bure kwa kampuni za kimataifa! Tunataka kuwa kama Zimbabwe na Afrika
Kusini?
Kwa
bahati, huko Uingereza baada ya uporaji wa ardhi, watu wote wasio na ajira (surplus population) wakapelekwa Marekani
na kuanzisha nchi mpya, huku nguvu kazi ya kuzalisha ikiwa ni watumwa. Sisi
watanzania hatuna Marekani ya kuwapeleka watu wetu walioporwa ardhi!
Mapinduzi ya Kijani Mexico na India
Nchini Mexico,
mapinduzi ya kilimo yaliasisiwa na mashirika ya Marekani ya Rockefeller Foundation na Ford Foundation, mwaka 1941. Mapinduzi
hayo yalifika India mwaka 1961, chini ya ufadhili wa mashirika hayo. Hakuna
ubishi ya kuwa, baada ya utengenezaji wa mbegu zinazostahimili ukame na
utumiaji wa mbolea za kemikali pamoja na kemikali za kuulia wadudu, kulikuwa na
uzalishaji mkubwa wa chakula uliosaidia kuondoa tatizo la njaa.
Hata hivyo,
wakosoaji wa sera hizo wanabainisha kwamba njaa haikuondolewa na ongezeko la
uzalishaji bali serikali kuingilia katika uchumi ili kuhakikisha upatikanaji wa
chakula kwa wanyonge. Na pale serikali ilipojitoa, hata kama uzalishaji ulikuwa
mwingi, kulikuwa na njaa kubwa. Eric Holt-Gimez na Raj Patel wanatolea mfano wa
nchi ya India: “Mwaka 2001, pamoja na kwamba maghala yalikuwa yamesheheni
chakula cha ziada kiasi kwamba mamlaka za India zikapendekeza kukimwaga
baharini, vifo vitokanavyo na njaa viliripotiwa katika majimbo 12 ya nchini
India. Idadi ya vifo vya aina hiyo haikuwahi kusikika tangu miaka ya 1960”[4].
Sera za mapinduzi ya
kijani pia zinakosolewa kwa kuegemea katika wazalishaji-papa na hivyo kuwatenga
wakulima wadogo. Na wakulima papa walipotanuka, waliishia kupora ardhi ya
wakulima wadogo. Uchambuzi uliofanywa Eric Holt-Gimez na Raj Patel, unaonyesha
kuwa katika jimbo la Punjab, nchini India, ambalo ndilo kitovu cha mapinduzi ya
kilimo, “miliki za ardhi kwa wakulima wadogo zilipungua kwa takribani 40%, huku
zile za wakulima-papa zikiongezeka kwa zaidi ya 50%” kati ya 1970 na 1990[5].
Athari za
kimazingira za mapinduzi hayo pia zinajulikana: kemikali zitokanazo na dawa za
kuulia wadudu pamoja na mbolea za viwandani sio tu kwamba zimeharibu rutuba ya
ardhi, lakini zimeingia katika vyanzo vya maji na kusababisha madhara makubwa
ya kiafya kwa binadamu, na viumbe hai wengine. Ndio maana kilimo cha kibepari
kitumiacho mashine (industrial
agriculture) huchangia asilimia 30 ya gesi za ukaa. Gesi hizi huchafua
anga, na kuna hatari ya kutoweka kwa uhai duniani siku za usoni kutokana na
mabadiliko ya tabia nchi yatokanayo na gesi hizo[6].
Ningependa
kusisitiza juu ya haja ya kuutazama uchafuzi wa mazingira (environmental pollution) katika historia ya ubepari kwani uchafuzi
wa mazingira, na madhara yake yote, ni matokeo ya mfumo wa kibepari. Nchi ziongozazo
kwa uchafuzi ni zile zenye maendeleo ya viwanda, lakini mzigo wa usafishaji
wanaubeba wanyonge wa nchi maskini.
Kwa hiyo, hapa
tunajifunza sifa nyingine ya uporaji wa kibepari. Hii ni ile ambayo Karl Marx
aliita “double robbery”, yaani uporaji wenye pande mbili. Kwa upande mmoja,
ubepari huwapora wazalishaji wadogo ardhi yao na kuwanyonya wafanyakazi wa
viwandani. Lakini ubepari hauishii hapo. Huipora pia ardhi rutuba yake, na
kugoma kuirudishia virutubisho vyake. Rutuba ya ardhi huchukuliwa katika mimea
na wanyama. Hivyo, pale binadamu atumiavyo vitu hivyo, yale mabaki anapaswa
kuyarudisha katika udongo – iwe ni nguo tuvaazo au taka–mwili za binadamu na
wanyama. Lakini mapebari hawawezi fanya hivyo kwa kuwa uwekezaji wa aina hiyo
hauna manufaa kwao. Hivyo, huamua kutumia mbolea za kemikali ambazo huenda
kuharibu rutuba ya ardhi!
Pengine kubwa kuliko
yote ni kuwa sera hizi zimemfanya mkulima mdogo kuwa tegemezi kwa kampuni kubwa
za kibepari. Mbegu, ambazo hapo awali zilikuwa za aina mbalimbali, na zikiwa
chini ya mkulima, hivi sasa sio mali yake tena. Ni mali ya kampuni za kibepari.
Mbegu za “kisasa” zilizofanyiwa “ukarabati” wa vinasaba hupandwa kwa msimu
mmoja tu – na ni makosa kwa mkulima kumgawia mwenzake. Ukiachilia mbali mbegu,
mkulima pia huwa tegemezi kwa mbolea za viwandani, dawa za kuulia wadudu,
mafuta ya kuendeshea mashine za kulimia na kuvunia, vipuri, n.k.
Kila mara mkulima
aingizapo mkono wake mfukoni kutoa fedha kwa ajili ya kununua pembejeo hizi,
huchangia kuzitajirisha kampuni za kibepari zijihusishazo na biashara
hizi. Na kwa kuwa basi wakulima wadogo
hawana fedha za kununulia vitu hivyo, hujikuta wakikopa katika mabenki kwa
kuweka rehani ardhi yao. Mwisho wa siku, kwa kuwa bei ya soko haitabiriki,
wakulima hawa kujikuta wamepoteza ardhi yao waliyoitumia kama dhamana. Nchini
India, mpaka kufikia mwaka 2008, wakulima wapatao 200,000 waliamua kujiua kwa
sababu ya madeni. Hapa tunapaswa kujifunza kwamba wale wanaopigia debe
urasimishaji wa rasilimali za wanyonge (mfano: kutoa hati za ardhi kwa
wakulima) huwa la lengo la kurahisisha uporaji wa ardhi hiyo.
Kwa ufupi basi,
kiini cha msukumo wa sera za mapinduzi ya kijani ni kampuni hodhi za kimataifa zenye
lengo la kutengeneza faida kupitia bidhaa zao za mbolea au mbegu
zilizobadilishwa vinasaba. Hivyo, haishangazi kwamba kampuni hodhi za mbolea
(Potash, Mosaic na Yara), kampuni hodhi za chakula (Cargil, ADM na Bunge) na
kampuni hodhi za teknolojia ya mbegu (Monsanto, Syngenta na Bayer)
zilitengeneza faida kubwa kati ya mwaka 2006 na 2008, wakati dunia ikiwa katika
anguko la uchumi, ambalo lilisababisha bei ya chakula kupanda kati ya 70% na
90%[7].
Cuba na Kilimo cha Kimapinduzi
Nchi ya Cuba
hupigiwa mfano kwa kilimo cha kimapinduzi (revolutionary
agriculture), kilichoanza miaka ya 1990. Cuba ilikumbatia kilimo cha
kimapinduzi baada ya kushindwa kwa mapinduzi ya kilimo. Ilitokeaje hasa?
Mwaka 1959, Fidel
Castro na wenzake, waliupindua utawala wa kiimla wa Batista, ambaye alikuwa
kibaraka wa Marekani. Kabla ya mapinduzi ya 1959, Cuba ilikuwa ni shamba na
danguro la Marekani. Ilikuwa shamba kwa
sababu sehemu kubwa ya ardhi ya Cuba ilimilikiwa na mabepari wa Marekani,
wakiitumia kuzalisha miwa. Wa-Cuba wenyewe walikuwa ni vibarua katika ardhi
yao. Kadhalika, mabepari wauzao madawa ya kulevya waliigeuza Cuba danguro, kupitia
vilabu na makasino waliyoyajenga huko. Mabinti wa Cuba walikuwa ni vyombo vya
starehe kwa mabepari wa Marekani. (Hii inatufundisha sifa nyingine ya ubepari:
katika mfumo huu binadamu anapoteza utu wake na anageuzwa kuwa chombo cha
uzalishaji ama chombo cha starehe).
Mapinduzi ya akina
Castro yaliuondoa uonevu huu na kuwarejeshea wa-Cuba utu wao. Miongoni ya hatua
zilizochukuliwa ni kutaifisha njia kuu za uzalishaji-mali na kuziweka mikononi
mwa dola. Hivyo, Castro aliwanyang’anya makabaila wa Kimarekani na ki-Cuba
ardhi waliyokuwa wamehodhi. Ikumbukwe kuwa baba yake Castro naye alikuwa ni
kati ya makabaila wakubwa. Miongoni mwa ardhi iliyotaifishwa ni ile ya baba yake
Castro!
Sehemu fulani
(asilimia 30) ya ardhi iliyotaifishwa iligawiwa kwa wakulima wadogo, lakini
sehemu kubwa (asilimia 70) ya ardhi hiyo
iliwekwa mikononi mwa dola. Dola la kijamaa la Cuba likawa likimiliki mashamba
makubwa ya miwa. Miwa iliyozalishwa iliuzwa kwa dola la Kijamaa la Urusi, na
kwa bahati nzuri, Urusi ilikuwa ikiilipa Cuba mara 5 zaidi ya bei ya soko la
dunia. Mashamba hayo makubwa yalitumia mbinu na zana za “kisasa” za
uzalishaji: mbolea za viwandani, matrekta, dawa za kuulia wadudu, n.k. Kwa kuwa
Cuba haikuwa na teknolojia ya kuzalisha matrekta, wala haichimbi mafuta yake
yenyewe, vitu vyote hivyo viliagizwa kutoka nje. Kwa bahati nzuri, Cuba ilivipata
toka Urusi, tena kwa bei ya chini kuliko ile ya soko.
Kwa hiyo, kwa ufupi,
Cuba likawa ni taifa tegemezi. Likitegemea teknolojia, mafuta, pembejeo, vipuri
vya mashine, n.k. kutoka nje. Pengine utegemezi hatari kuliko wote ni ule wa chakula.
Cuba iliagiza takribani 70% ya chakula chake kutoka nje. Hivyo, Cuba haikuwa
taifa linalojitegemea kwa chakula. Ni bahati njema tu kwamba Urusi ilikuwepo
kuisaidia Cuba! Na pia ni bahati njema tu kwamba Cuba ilifuata sera za kijamaa,
na hivyo, faida iliyopatikana ilikwenda kuwahudumia wanyonge. Cuba ikawa na maendeleo
makubwa ya kisayansi, hasa katika upande wa tiba za afya, na watu wake wakapata
huduma thabiti za maji, makazi, afya, na elimu.
Ubovu wa uchumi
tegemezi ni kwamba pale taifa-tegemewa linapoyumba, taifa-tegemezi nalo pia huyumba.
Ndivyo ilivyotokea Cuba. Baada ya kusambaratika kwa Muungano wa Urusi mwanzoni
mwa miaka ya 1990, Cuba haikuwa na pa kuegemea. Sukari yake ikakosa soko. Na
kwa kweli, hata uzalishaji ulianguka kwa sababu Cuba haikuwa na fedha za
kununua vipuri na mafuta kwa ajili ya mitambo ya uzalishaji. Cuba ikashindwa
hata kuagiza chakula kwa kuwa haikuwa na fedha!
Hapo ndipo Cuba
ikapata funzo: ilikuwa imekumbatia mapinduzi ya kilimo. Mbali na utegemezi wa
kiuchumi, mapinduzi hayo yaliwanyang’anya wakulima wadogo maarifa
waliyokuwanayo juu ya uzalishaji, na kuwafanya kuwa tegemezi kwa mitambo. Cuba ikaamua
kujirekebisha kwa kufanya maboresho makubwa katika mfumo wake wa kilimo.
Mashamba makubwa
yaliyokuwa yakimilikiwa na serikali yaligawiwa kwa wakulima wadogo, mmoja
mmoja, na kwa kupitia vyama vyao vya ushirika. Msisitizo ukawekwa katika mazao
ya chakula kwa ajili ya kuilisha nchi. Cuba pia ikaachana na kilimo cha
mashine kitegemeacho mafuta na vipuri toka nje. Ikakumbatia kilimo cha jembe la
mkono na jembe la kukokotwa na ng’ombe. Mbolea za viwandani na dawa za kemikali
zikapigwa marufuku. Badala yake wa-Cuba wakarejea kutumia mbolea za asili
zitokanazo na mabaki ya mimea na wanyama, pamoja na dawa zisizo na kemikali za
viwandani (au mimea ifukuzayo wadudu). Leo hii Cuba ndiyo nchi pekee duniani
inayotajwa kuwa na maendeleo endelevu (sustainable
development), kwa kuwa na mfumo wa uzalishaji unaotunza mazingira.
Kwa ufupi, Cuba ilihama
toka mapinduzi ya kilimo kwenda kilimo cha kimapinduzi! Wakulima wadogo
wakalazimika kuyakumbuka mafundisho na mbinu za kilimo za babu na bibi zao, na
wakazitumia kuliokoa taifa lao![8]
Hapo awali Cuba iliagiza zaidi ya 70% ya chakula toka nje. Leo hii, inaagiza
takribani 10% tu. Hii ni kusema kuwa Cuba inajitosheleza kwa chakula kwa takribani
90%. Wataalam wa ugavi huenda kujifunza kwa wakulima na kisha kutumia uzoefu
huo kwa ajili ya kufanya tafiti na kutengeneza dawa za kuulia wadudu
zisizotumia kemikali.
Tena kilimo cha
kimapinduzi kiliwaamsha hata watu wa mijini. Kilimo cha bustani pamoja na
ufugaji vilitamalaki katika miji ya Cuba. Wa-Cuba wa mijini wakatumia hadi
mapaa ya nyumba zao kwa ajili ya bustani ili kukidhi mahitaji yao ya chakula.
Waliodhani kuwa Ujamaa wa Cuba utaanguka, walikosea: mpaka leo Cuba bado
haijajisalimisha kwa Marekani, na inaendelea kutekeleza sera za kijamaa. Huduma
za elimu, afya ni bure kwa watu wote, na dola hutoa ruzuku ya chakula kwa
wanyonge wa mijini.
Mshikamano wa kitabaka
Katika dhana ya
mapinduzi ya kilimo kama tulivyoona, lengo la uzalishaji wa wakulima ni kwa
ajili ya soko, yaani huzalisha chakula kwa ajili ya kulisha ng’ombe, nguruwe na
kuku ili wakubwa wa Ulaya wapate nyama iliyonona, au kuzalisha mazao ya
kutengenezea mafuta ya magari (biofuels)
ili wakubwa watembee wakiwa wamekaa! Ni nani atawalisha wanyonge wenzao wa
mijini na vijijini? Benki ya Dunia inasema wanyonge wa mijini watajijua wenyewe,
alimradi wakulima wakizalisha vyakula kwa ajili ya kulisha wanyama na magari,
watapata fedha. Hivyo, wakulima hawapaswi kujali kuhusu wanyonge wa mijini[9].
Kinyume chake,
kilimo cha kimapinduzi humlenga binadamu. Msingi wa uzalishaji na umiliki wa
ardhi ni wazalishaji wadogo na lengo la uzalishaji ni kuilisha familia ya
mkulima pamoja na wavuja-jasho wenzake mijini na vijijini (mama ntilie,
machinga, wapiga debe, wakulima wadogo, vibarua mashambani, wafugaji wadogo,
wafanyakazi wa ngazi za chini katika viwanda). Na kwa kweli, maskini wa mijini
ni watoto wa wakulima, ambao wamekimbilia mijini kutokana na ugumu wa maisha au
kuporwa ardhi na wawekezaji-papa. Maisha waishiyo huko mijini ni magumu kama
(au pengine kuliko) yale ya wanyonge wenzao wa vijijini. Wakulima hawapaswi
kuwatupa wanyonge wenzao!
Lengo la mshikamano
wa kitabaka sio kwa ajili ya kupatiana chakula tu, bali ni kwa ajili ya kujenga
nguvu ya pamoja ya kuukabili ubepari. Historia imetuonyesha kuwa ni vigumu kwa
wanyonge kuukabili ubepari pasipo kuungana. Na kwa jinsi ubepari ulivyo, tuna
chaguo moja: ama kuubomoa, au kuuacha utubomoe!
Kazi ya wanyonge
kuungana isiachwe mikononi mwa mabwanyenye-uchwara kupitia vyama vya siasa au
asasi zisizo za kiserikali (NGOs). Hawa wote, katika nafasi zao, ni watumishi
wa mabepari wa kimataifa. Hata kama hapa na pale huonekana kuwa na ugomvi,
ugomvi huo huwa haulengi katika kuubomoa ubepari. Wote hawa wanapigania nafasi
ya kuwa mawakala wema wa mfumo wa kibepari. Ndio maana, hapa nchini, hakuna
chama cha siasa chenye nia ya dhati ya kuleta mfumo mbadala, na harakati
zao zinalenga kuepusha mapambano ya kitabaka katika jamii.
Mshikamano wa tabaka
la wavuja-jasho unapaswa kuongozwa na itikadi pana. Itikadi hiyo sharti
izipinge itikadi finyu za udini, ukabila, ujana (vijana vs. wazee), ujinsia
(wanawake vs. wanaume), urangi (racism), ukanda na u-nchi (“parochial
nationalism”—mfano, uzanzibari na utanganyika), na uzawa (indigenization). Itikadi
finyu zote hizi ni mazao ya mfumo wa kibepari, na huzalishwa na tabaka la juu
ili kuwazuia wanyonge wasiwe na mshikamano wa kitabaka. Ni itikadi pana za umajumui wa Afrika
(“pan-Africanism”) na Ujamaa (“socialism”) ndizo zinazopaswa kuongoza mapambano
ya wavuja-jasho dhidi ya wavuna-jasho (mabepari na mawakala wao)!
Wavuja-jasho wote wa Afrika
unganeni. Hamna cha kupoteza isipokuwa minyororo yenu. Mapambano yenu
yataikomboa Afrika!
Marejeo
[1] Majuma mawili baada ya
kuwasilishwa kwa mada hii, Compaore alilazimika kujiuzulu na kukimbilia
uhamishoni kufuatia maandamano yasiyo na kikomo ya kupinga muswada uliokusudia
kumfanya aendelee kukaa madarakani. Jina la Sankara ndilo lilitumika
kuhamasisha waandamanaji.
[2] Imenukuliwa
kutoka katika Jon Queally, “#WorldVsBank:
Small Farmers, Global South Demand End to World Bank’s ‘Moral Bankruptcy’”,
2014, katikahttp://www.commondreams.org/news/2014/10/10/worldvsbank-small-farmers-global-south-demand-end-world-banks-moral-bankruptcy
[3] Utsa Patnaik and Sam Moyo, The Agrarian Question in the Neoliberal Era:
Primitive Accumulation and the Peasantry, 2011.
[4] Imenukuliwa toka Eric
Holt-Gimenez and Raj Patel, Food
Rebellions! Crisis and the Hunger for Justice, 2009, uk. 32.
[5] Imenukuliwa toka Eric
Holt-Gimenez and Raj Patel, Food
Rebellions! Crisis and the Hunger for Justice, 2009, uk. 33
[6] Chanzo: African Centre for
Biodiversity, Understanding the Impacts
of Genetically Modified Crops in Africa, uk. 16.
[7] Chanzo: African Centre for
Biodiversity, Understanding the Impacts
of Genetically Modified Crops in Africa, uk. 12 – 13.
[8] Rosset,
P.M. “Cuba: A Successful Case Study of Sustainable Agriculture”. In Hungry
for Profit: The Agribusiness Threat to Farmers, Food, and the Environment, eds. Magdoff, F., J. Bellamy–Foster and F.H. Buttel, 2000.
[9] Binswanger-Mkhize, H.P. and M. Gautam. 2010. “Towards an
Internationally Competitive Tanzanian Agriculture”. A World Bank Draft Report presented at joint Government of Tanzania and World Bank workshop on
Prospects for agricultural Growth in a Changing World, February 24-25, 2010 and
at the 15th Annual Research Conference of the network for Research for Poverty
Alleviation, March 19-20, 2010, as well as to a cabinet seminar chaired by his
Excellency the Prime Minister Pinda, on March 20, 2010.