KITABU NILICHOKISOMA JUNI 2015
Na Godfrey Eliseus Massay
Jina la Kitabu: Uchambuzi wa Sera, Uongozi na Maslahi ya Watanzania.
Mwandishi: Chachage Seithy L. Chachage
Mpigachapa: E&D Vision Publishing
Mahali ilipochapishwa: Dar es Salaam
Mwaka: 2014
Muhtasari wa Kitabu
Kitabu hiki
kinajumuisha jumla ya makala 21 zilizoandikwa na hayati Profesa Chachage Seithy
Chachage kati ya mwaka 2000 hadi kabla ya kifo chake mwezi Julai 2006. Prof.
Shivji ambaye ni rafiki wa karibu wa mwandishi ameandika utangulizi wa kitabu. Kitabu
kimegawanyika katika sehemu tatu ambazo zinadadisi kwa kuuliza swali
kumfikirisha msomaji. Sehemu ya kwanza, Utandawazi au Utandawizi? Ina makala
sita (6). Sehemu ya pili, Soko Huria au Soko Holela? Ina makala sita (6). Na
sehemu ya tatu, Mwelekeo Bora au Bora Mwelekeo? Ina makala tisa (9). Katika
makala zote, Profesa Chachage anachambua madhara ya mfumo wa utandawazi katika
jamii ya Watanzania. Binafsi sitaelezea kila makala imesema nini bali
nitaelezea dhima kuu zailizojadiliwa katika kila sehemu ya kitabu. Lengo ni kukutia
hamasa ya kukisoma kitabu hiki wewe unayesoma makala haya.
Sehemu ya Kwanza
Sehemu
hii inaonyesha kwa kina namna ambavyo mfumo wa utandawazi umekuwa ukitumia
propaganda za kuhadaa na kidanganyifu katika kufukarisha na kuharibu mifumo ya
jamii. Mwandishi anaeleza namna ambavyo mfumo unaikuza lugha ya Kiingereza kama
lugha bora ya kidunia hata kuifanya lugha ya Kiswahili ionekane haina nafasi.
Anaeleza kwa umahiri mkubwa namna ambavyo utamaduni, lugha na maendeleo ya Nchi
yanavyohusiana. Anapinga vikali ukandamizaji wa lugha ya Kiswahili katika maendeleo
ya Nchi. Aidha, mwandishi anaeleza namna ambavyo muziki umetumika kueleza
madhara ya mfumo wa utandawazi nchini. Vijana kama kundi kubwa ambalo
limeathiriwa na mfumo huu wamebuni nyimbo na misamiati kuonyesha namna
wanavyoathiriwa na ugumu ya maisha. Madhara makubwa yaliyowapata wananchi na
Taifa kutokana na uchimbaji wa madini na mapambano ya Umma dhidi ya mbinu za
unyanyasaji na ukandamizaji yanaelezewa kwa kina. Mwandishi anatoa mifano ya
mapambano katika sehemu mbalimbali duniani huku akionyesha namna Watanzania
walivyopambana kuupinga ukandamizaji tangu kipindi cha vita vya Maji Maji.
Mwandishi hakuishia hapo, anaeleza madhila ya wafanyakazi yatokanayo na mfumo wa
Utandawazi kwa uwazi na ufasaha mkubwa. Kama namna ya kutafuta njia ya kutafuta
mwarobaini wa matatizo yao, Nchi za Afrika zilitengeneza mpango wa ushirika
mpya wa maendeleo ya Afrika-NEPAD. Mwandishi anaonyesha kuwa mpango huo si
chochote bali namna nyingine ya
kuwanyonya na kuwakandamiza Waafrika. Ni mpango ambao ulipata kibali na unategemea fedha kutoka kwa
mataifa makubwa ya kibeberu na wenye lengo la kutengeneza mazingira mazuri ya
uwekezaji wa makampuni ya kibeberu barani Afrika.
Sehemu ya Pili
Makala
zote za sehemu hii zinaeleza uholela wa soko katika zama za utandawazi. Katika
mahojiano, mwandishi anaeleza sababu zilizomsukuma kuandika na upekee wa Riwaya
yake ya Makuadi wa Soko Huria. Anasisitiza kuwa ni riwaya ya kweli na yenye
kueleza mfumo wa utandawazi katika muktadha wa historia. Mabadiliko
yaliyosababisha madhaifu ya bodi za Tumbaku na Korosho ambazo kwa pamoja
zilisababisha kuanguka kwa soko na ubetuaji wa wakulima yanaelezwa kwa kina. Chachage
anasimulia namna ambavyo takwimu za utalii zinatumika kupotosha ukweli juu ya
mchango wa sekta katika pato la taifa. Suala la takwimu linaelezewa katika
upana wake kwa kujumuisha changamoto za uwezo wa mamlaka husika, upatikanaji wa
taarifa sahihi, na tafsiri ya takwimu. Aidha mwandishi anaeleza mgogoro wa
magunia uliosababishwa na wafanyabishara na serikali na hivyo kuathiri biashara
ya korosho nchini. Mwandishi anajadili pia tatizo la uandishi na uchapishaji wa
vitabu katika zama za utandawazi. Hoja
yake ni kuwa Watanzania hawana tabia ya kusoma vitabu na wengi hupendelea
vitabu visivyo vya msingi kama vile vinavyoelezea mapenzi, upelelezi, mapishi,
urembo, na namna ya kupata utajiri haraka. Haya ni matokeo ya utandawazi.
Sehemu ya Tatu
Hii ni
sehemu yenye makala nyingi zaidi kuliko sehemu zingine. Jumla ya makala tisa
zimejadili kuonyesha ‘bora mweleko’. Nilivutiwa zaidi na mada mbili, moja juu ya
vyama vingi na utamaduni wake na ya pili juu ya biashara ya shahada. Katika
hiyo mada ya kwanza mwandishi anaeleza kuwa mfumo wa vyama vingi una utamaduni
wake ambao umekuwa ukitumika hasa katika nchi zilizoasisi vyama vingi. Kubwa
kuliko vyote ni utamaduni wa kukubali matokeo ya uchaguzi. Hapa Tanzania katika
chaguzi zote, hasa za Zanzibar, kumekuwa na tatizo kubwa la kuuheshimu
utamaduni huu. Hata hivyo, mwandishi anadokeza upekee wa siasa za Zanzibar
ambazo hata Mwalimu Nyerere aliwahi kusema serikali ya mseto ni njia pekee ya
kumaliza mgogoro wa kisiasa kati ya CCM na CUF. Katika mwaka huu wa uchaguzi ni
vyema kujikumbusha kuhusu utamaduni wa vyama vingi na kuuheshimu. Mada juu ya
biashara ya shahada imejikita zaidi katika vyuo vya Uingereza ambavyo vina
matawi nje ya nchi hiyo na namna vinavyotengeza pesa nyingi kutokana na
biashara ya shahada. Hii ni biashara ambayo huangalia fedha zaidi kuliko sifa
za mwombaji. Chachage anadokeza kuwa nchi za Afrika ndizo zinazoathirika kwani
wanafunzi kutoka Afrika ndiyo wanaongoza kununua shahada hizo. Hii inanikumbusha
miaka michache iliyopita, kuna mwandishi alitoa kitabu chenye majina ya
wanasiasa ambao shahada zako zilikuwa na matatizo. Hakuna mwanasiasa hata moja
aliyeenda mahakamani na mwandishi wa kitabu kile alipania kuweka mabango
makubwa yenye picha viongozi hao katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es
Salaam. Hakusikika tena kwenye vyombo vya habari!
Somo
Kitabu hiki
kimenisaidia kuuelewa utandawazi na ubeberu kwa undani zaidi. Kimenionyesha
madhila ambayo wakulima, wafanyakazi na serikali wanayapata na wataendelea
kuyapata kutokana na mfumo huu hapa nchini. Kinanifikirisha katika kutafuta namna
ya kukabiliana na mfumo huu. Kimenipa ari ya kutafuta na kusoma vitabu vyote
alivyoviandika Profesa Chachage. Ili kuelewa zaidi Utandawazi, nashauri usome pia vitabu vilivyoandikwa na David Harvey, Thandika Mkandawire, Issa
Shivji, Karim Hirji, Adebayo Olukoshi na Karl Polanyi.