Leo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imemtangaza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuwa mshindi katika Uchaguzi wa Rais 2010 kwa 61.17%. Katika uchaguzi huu wapiga kura wapatao 5,276,827 walimpigia kura ikiwa ni takribani 10% ya Watanzania wote. Kiwango hiki cha ushindi kimeshuka kwa takribani 20% ukilinganisha na uchaguzi wa 2005. Uchambuzi wa awali unaonesha kuwa matokeo haya yanadhihirisha kuwa Rais Kikwete ana changamoto kubwa ya kurudisha ari na imani kubwa iliyofanya wapiga kura wamchague kwa kishindo katika uchaguzi uliopita wakitegemea ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania’. Hatua ya awali ya kurudisha hiyo hali, ama uhalali huo wa kuongoza, mioyoni mwa wapiga kura hao ambao hawakumpigia kura safari hii, ni kuunda Baraza la Mawaziri dogo tena lisilo na nyuso tata ambazo wananchi walizikataa kwenye uchaguzi tete huu ama kutokana na utendaji mbovu au tuhuma nzito za ufisadi. Hatua nyingine ni kuhakikisha kuwa Serikali inabana na kupunguza matumizi yake hasa katika kipindi hiki kigumu kinasobabishwa na mtikisiko mkubwa wa uchumi ulimwenguni. Wananchi tumetoa tamko letu katika uchaguzi huu – ni tamko kuu ambalo Rais hawezi kulipuuza katika kusimamia utendaji/uwajibikaji wa Serikali hasa kama anaitakia kweli mema nchi yetu.

Mungu Ibariki Afrika
Wabariki Viongozi Wake
Hekima Umoja na Amani
Hizi ni Ngao Zetu
Afrika na Watu Wake

Ibariki Afrika
Ibariki Afrika
Tubariki Watoto wa Afrika

Mungu Ibariki Tanzania
Dumisha Uhuru na Umoja
Wake kwa Waume na Watoto
Mungu Ibariki Tanzania na Watu Wake

Ibariki Tanzania
Ibariki Tanzania
Tubariki Watoto wa Tanzania