MAUAJI YA HALAIKI YA WATOTO WA TANZANIA KUPITIA KATIKA LUGHA YA KUFUNDISHIA SEKONDARI NA VYUONI
F.E.M.K Senkoro
Makala kwa Ajili ya Warsha ya Usambazaji wa Matokeo ya Tafiti Kuhusu Kuhusu Lugha ya Kufundishia Sekondari na Vyuoni Tanzania Desemba 5, 2006 F.E.M.K. Senkoro Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Kwanza kabisa, nieleze matukio mawili ambayo nimekutana nayo hapahapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Asubuhi moja nilikutana na mwanafunzi wangu mmoja akiwa anatoka jasho chapwachapwa mwili mzima. Kwa vile yalikuwa majira ya baridi hapa Dar es Salaam, nilimwuliza kama anaumwa. Alinijibu kuwa hakuwa anaumwa, bali alikuwa na uhudhurishaji wa swali la semina siku hiyo. Kidogo alinishangaza kwani katika semina zangu na hata katika mitihani yangu alikuwa akifanya vizuri sana. Sikuelewa kwa nini alikuwa anaogopa semina ile hadi aliposema, “Afadhali semina yenyewe ingelikuwa ya Kiswahili. Hii ni kwa Kiingereza, na sijalala usiku kucha, na hata chamshakinywa kimenishinda asubuhi hii. Unajua Profesa, si kwamba mawazo sina, ila siwezi kuyatoa vizuri kwa Kiingereza, na siwezi hata kuonyesha hisia zangu kikamilifu kwa lugha hiyo. Basi tu. ” Nilidhani anatania, lakini nilipomwangalia usoni nilijua kuwa hakuwa anatania hata kidogo. Niliamua kuwauliza wanafunzi mbalimbali kuhusu hali hiyo, na karibu wote wakanijibu kuwa hali ile huwapata kila wanapokabiliwa na zoezi la kuhudhurisha kwa Kiingereza katika semina. Na hawa hawakuwa wa mwaka wa kwanza tu, bali hadi wa mwaka wa nne wote walilalamikia hali hiyo.
Tukio la pili lilinitokea hivi karibuni sana nilipokaribishwa na mwalimu mwenzangu kwenda kutoa muhadhara kuhusu ngano ambazo zinavuka mipaka ya kijiografia na kiutamaduni. Muhadhara huu ulikuwa kwa Kiswahili. Na mwishoni niliwaeleza wanafunzi kuwa nilikuwa na kifikirishi kuhusu mada ile na kwamba ningempatia mwakilishi wa darasa kitini hicho. Nilipowaeleza tu kuwa kifikirishi chenyewe kilikuwa kwa lugha ya Kiingereza, wanafunzi wote waliguna na kuonyesha kukata tamaa. Walionyesha dhahiri kuwa kifikirishi cha Kiingereza kisingewafikirisha kwani wasingeambulia kitu.
Tutarejelea matukio haya mawili hapo baadaye. Kwa sasa ningependa kulihusisha suala la lugha ya kufundishia na Katiba Mama ya nchi yetu. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza kuwa kila mtu ana haki na uhuru wa kutoa maoni yake, na pia uhuru wa kujieleza, kutafuta, kupokea na kusambaza mawazo na habari kupitia chombo chochote kile bila kujali mipaka ya kitaifa; pia ana haki ya uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa. Inasisitiza pia kuwa kila mtu ana haki ya kutoa fikra zake kwa uhuru kabisa. Nimekuwa nikiwaza sana kuhusu haki na uhuru huo, sambamba na suala zima la lugha ya kufundishia katika sekondari na vyuo nchini Tanzania, na nimekuwa nikijiuliza kama serikali haiendi kinyume na Katiba ya Jamhuri kwa kuwalazimisha waalimu na wanafunzi kutumia lugha ya kufundishia ambayo licha ya kuwa ni ngeni kwao, tafiti nyingi zinaonyesha pia kuwa hawaimudu kabisa, kwa hiyo hawana uhuru wala haki ya kujieleza kwa lugha wanayoiweza, lugha inayobeba utamaduni na dhana nyingi wazielewazo.
Nimekuwa nikijiuliza maswali mengi kuhusu hali ilivyo katika shule za sekondari na vyuo vingi nchini Tanzania ambako watoto wa Kitanzania wamepigwa marufuku kuongea lugha zao, ikiwemo ile ya taifa, Kiswahili, na hata huadhibiwa kwa kubebeshwa matambara machafu au hata mawe na magogo pindi wanapokutwa wakizungumza lugha hizo. Badala yake wanalazimishwa kuongea Kiingereza, lugha ambayo ni ngeni kwao na imebeba tamaduni ambazo ni ngeni kwao. Watoto hao basi, hawana haki ya kutoa fikra zao kwa uhuru hata kidogo. Maswali yamekuwa mengi zaidi niyawazapo haya sambamba na kauli ya Mwalimu Nyerere kuwa taifa lisilo na utamaduni wake lenyewe ni taifa lisilo na uhai, ni taifa lililofilisika lisilo na utu wala roho yoyote. Lugha ni sehemu muhimu sana ya utamaduni wa jamii; na kwa hakika lugha ni kielelezo na kielezo cha utamaduni huo. Lugha ni sehemu mojawapo ya ufahari wa kitamaduni wa jamii fulani. Ndio maana Mwingereza anajivunia sana lugha yake ya Kiingereza, na vivyo hivyo Mfaransa, Mreno, Mjerumani, Mjapani, Mnorwei, Mdenish na wengi wengineo. Kinyume chake, Mtanzania anapigwa marufuku kuitumia na kujivunia lugha yake; badala yake anapoitumia anaadhibiwa kwa kubebeshwa tambara bovu, jiwe, au gogo. Ni kama kwamba, ndani ya ubongo wake, Mtanzania anatakiwa aionee aibu lugha yake ya taifa, na aikumbatie lugha ya utamaduni wa mtawala wake wa zamani. Anatakiwa aione lugha yake ya taifa kuwa ni sawa na tambara bovu, jiwe, au gogo.
Matokeo ya hili ni kwamba tunamlea mtoto wa Tanzania aukane utu wake, na awe na woga wa kujieleza. Tunamfanya ajinyamazie tu kwani anaogopa kujieleza kwa lugha anayoimudu asije akaadhibiwa, na anaogopa kujieleza kwa lugha ngeni asiyoweza kujinasibisha nayo hata chembe, kwani anajua kuwa haijui na atakayoeleza yataonekana kuwa ni kichekesho. Nimekuwa nikiwaza sana kuhusu utandawazi ambao umechangia katika kumfanya mtoto wa Tanzania azidi kujivunia lugha na utamaduni wa kigeni, lugha na utamaduni wa Mwingereza, kwa kumfanya aamini kabisa, yeye na wazazi wake pamoja na watunga sera, kuwa akifundishwa kwa kutumia lugha hiyo ataimudu na itamsaidia apate kazi na aweze kuwasiliana na watu wa mataifa mengine.
Nimekuwa nikijiuliza inakuwaje Wachina, Wajapani, Wakorea, Waswidi, na wengi wengineo ambao wanatumia lugha zao kufundishia vijana wao, bado wamepata kazi za kimataifa, wamefaulu mitihani yao, wameendeleza nchi zao na wameweza kuwasiliana na watu wa mataifa mengine. Hawa wamemudu kuyafanya yote hayo kutokana na kuthamini na kuzitumia lugha zao kufundishia shuleni na vyuoni. Utandawazi umetumika kama kisingizio cha kuigeuza dunia si kuwa kijiji kidogo bali ni msitu mdogo ambamo wanyama wakubwa sasa wanawapata wanyama wadogo kama mlo wao kiurahisi sana.
Utandawazi umekuwa chanzo cha wakubwa kuwanyamazisha wadogo, na, kama mtu mmoja alivyowahi kusema, badala ya tangazo la “Punguza mwendo, kazi inaendelea mbele”, utandawazi umeweka kibao cha “Nyamaza, mbele yanafanyika maendeleo!” Wale walionyamazishwa kwa kuaibishwa wakijieleza kwa lugha zao, wanatakiwa wabaki wakiwa wameduwaa wakati wenzao duniani kote wakipiga hatua nyingi za maendeleo. Badala ya kuwa washiriki na washirika wa maendeleo, wamefanywa wabaki kuwa watazamaji tu na kuelekezwa la kufanya, tena wakati mwingi wakielekezwa pabaya kuhusu maisha yao bila wao kuling’amua hilo kwani limeelezwa kwa lugha na utamaduni usio wao; hadi wanaposhituka mambo yakiwa yameharibika.
Sitashangaa kuona kuwa mojawapo ya vyanzo vya watu kuweka sahihi katika mikataba ambayo inaonyesha dhahiri kuwa hawaielewi, ni suala la lugha ambapo historia inajirudia sawa na pale Karl Peters alipowafanya mababu zetu waridhie kutwaliwa kwa ardhi yao kwa kusaini mikataba wasiyoielewa. Mimi nina uhakika kabisa kuwa chanzo cha kubaki nyuma kimaendeleo ni ule ukimya utokanao na sera ya lugha ya elimu inayowanyamazisha watoto wa Tanzania, kwa kuwalazimisha wasijieleze wanavyopenda kwa kutumia lugha yao ya taifa, na badala yake kuwalazimisha, bila mafanikio, wajieleze kwa lugha ngeni kwao.
Iko hadithi moja ambayo mimi hupenda kuirejelea kila mara ninapoongelea suala la lugha ya kufundishia. Ni hadithi itokayo katika kitabu cha Charles Dickens cha Hard Times chenye wanafunzi fulani wawili kwenye shule ya mjini, ambao wanaombwa watoe maelezo kuhusu farasi. Mmoja, msichana aitwaye Jupe, ameishi na farasi maisha yake yote huko kijijini, na mwingine, mvulana aitwaye Blitzer, amesoma tu kuhusu farasi katika Encyclopedia. Jupe anashindwa kueleza farasi ni nini kwani katakiwa afanye hivyo kwa lugha ya kisomi, na Blitzer ambaye hajawahi hata kumwona wala kumgusa farasi anafaulu kueleza farasi yukoje kwa kutumia maana za ki-encyclopaedia. Watoto wetu tumewageuza kuwa Jupe, ambaye pamoja na kuelewa fika kuhusu farasi, kanyimwa haki ya kueleza farasi ni mnyama wa aina gani kwa kulazimishwa ashikile maana za kikamusi za mnyama huyo. Ameishi na kuwagusa na kuwajua fika wanyama hao, lakini elimu inamlazimisha asieleze kuhusu awajuavyo bali awaeleze kama kamusi zinavyowaeleza.
Vivyo hivyo, kwa Tanzania, tafiti nyingi, mathalani zile zinazotokana na mradi wa utafiti kuhusu lugha ya kufundishia Tanzania na Afika ya Kusini (LOITASA) zimedhihirisha kuwa wanafunzi wengi mno wangeweza kufaulu mitihani yao vizuri zaidi iwapo wangefundishwa kwa Kiswahili, kuulizwa maswali kwa Kiswahili na kutakiwa wajibu kwa Kiswahili. Na zimeonysha dhahiri kuwa kama wangefundishwa hivyo, hata lugha za kigeni kama Kiingereza wangezimudu vizuri zaidi. Lakini, badala yake, wameulizwa maswali hayo kwa Kiingereza – lugha ambayo hawaijui, na hawawezi kujinasibisha na utamaduni wake. Wamegeuzwa kuwa akina Jupe kwa kunyimwa uhuru na haki ya kujieleza.
Haya yote yanatuongoza katika mjadala wa maana ya lugha, maana ambayo sitaikita katika malumbano ya kitaaluma, bali nitaielekeza katika hali halisi ya lugha ya kufundishia nchini Tanzania. Tusemapo kuwa lugha ni chombo cha mawasiliano baina ya mtu na mtu, tuna maana kuwa mawasiliano yoyote, yawe baina ya mzazi na mtoto, marafiki, mwalimu na mwanafunzi, yanahusu matumizi ya lugha. Lugha na ishara na taswira zinazowakilishwa nayo hufinyanga na kuathiri tabia na mikabala aliyo nayo mtu. Maneno yanayotumika humweka msemaji katika nafasi fulani miongoni mwa watu wengine – na nafasi hiyo huweza kuwa ile ya masafa marefu au mafupi baina ya msemaji huyo na wenziwe, au inaweza kuashiria mamlaka au ubia baina ya wahusika. Nafasi hiyo huwaathiri wahusika kwa namna moja ama nyingine, wakati mwingine kwa kuwadarakisha au hata kuwadogosha, kuwashawishi na kuwahimiza au kuwakatisha tamaa, kuwafanya wajione wako kwao au kuwagenisha. Kwa hakika, matumizi ya lugha wakati huohuo yanaingiliana na mtazamo wa kitamaduni kwani ili kusiwe na uhusiano hasi baina ya watumiaji wa lugha fulani, yale mambo ya ndani ya utamaduni mahsusi unaobebwa na lugha mahsusi hayana budi kueleweka kwa wote wanaowasiliana kwa lugha hiyo, la sivyo, mawasiliano yatakuwa ya upande mmoja tu.
Historia ya jamii zetu nyingi za Kiafrika inaanzia pale ambapo Mwafrika alikuwa anajitawala, anajitegemea na anajiletea maendeleo yake yeye mwenyewe. Historia hii ilipoingiliwa na ukoloni na ubepari, ukawa mwanzo wa kudidimia kwa maisha ya Mwafrika. Ukoloni na ubepari havikuja vivi hivi tu. Vilitanguliwa na kutawaliwa kimawazo kwa Mwafrika huyo, akaletewa dini, mila, desturi na tamaduni za nje, zikiwemo lugha ngeni, akafanywa aviabudu hivyo na kuvidharau vyote vilivyokuwa vyake. Alifanywa azione dini, mila, desturi na tamaduni zake kuwa ni za kishenzi zisizofaa mbele za mtawala wake. Akaiga kila kitu cha nje, na kudharau kila kitu chake.
Vita vya uhuru vililenga kumkomboa Mwafrika huyo ili aondokane na minyororo ya ukoloni na ubepari. Vilinuia kumtoa Mwafrika katika lindi la kujidharau na kuudharau utu wake. Lakini ubepari hauruhusu mambo kama hayo. Ubepari hujigeuza nyuso zake kama kinyonga, na kama awali ulikuwa joka la vichwa saba, sasa, baada ya uhuru wa bendera na wa wimbo wa taifa ubepari uligeuka kuwa joka linalotabasamu, lenye vichwa sabini, na kila uchao vichwa hivyo huongezeka. Kichwa cha hivi karibuni ni kile cha utandawazi ambao ni dhahiri kuwa ni kielelezo cha kuanguka kwa utaifa wa Mwafrika na kukita kwa mizizi ya kiliberali. Tabasamu la dudu hili liko ndani na nje ya mataifa mengi ya Kiafrika. Wako viongozi ambao tabasamu hilo limewakatisha tamaa kabisa kuhusu utu wa watu wao, na wamebaki kushangaa huku wakishangilia tabasamu hilo, na kulisifu tabasamu hilo kwa kuliruhusu lishamiri kwa njia nyingi, ikiwemo ile ya kurudisha mikabala ya ukoloni, mikabala inayosifu vya kigeni na kudharau vya “wenyeji”. Hapo ndipo tuonapo mawaziri wetu wa elimu wakikikumbatia Kiingereza, na wakidharau tafiti mbalimbali zilizofanyika zinazoonyesha kuwa watoto wetu hawaambulii chochote madarasani wanapofundishwa kwa lugha hiyo ya kigeni.
Hapo ndipo tuonapo zikichipuka shule nyingi ziitwazo za kimataifa, zenye kutumia lugha ya Kiingereza kuwafundishia watoto wetu, tangu chekechea hadi sekondari. Tabasamu hili la ubepari ambalo limejengeka ndani ya dude liitwalo utandawazi ndilo linaloleta programu kama ile ambayo ghafla inamwonyesha Waziri Mkuu wa Uingereza akiwa na huruma ya ajabu kwa Afrika hadi kuunda Kamisheni ya kuushughulikia umasikini ambao, kwa hakika, nchi yake ilishiriki mno kuuleta Afrika na bado inashiriki kuusambaza duniani kote, hata inapolazimu kwa mabavu. Na viongozi wetu wameonyesha kulifurahia tabasamu hilo la Blair walipoteuliwa kuwa wanakamati wa kamisheni hiyo. Pamoja na hayo yote, tabasamu hili linajitokeza pia katika juhudi za wazi kabisa za Baraza la Uingereza au British Council la kukisambaza Kiingereza duniani kwa kumwaga pesa nyingi kwa wizara za elimu kwa kile kiitwacho programu za kuimarisha Kiingereza. Kama tujuavyo, ubepari hugeuza kila kitu kuwa bidhaa sokoni, na lugha ya Kiingereza ni mojawapo ya bidhaa muhimu sana kwa Waingereza kiasi kwamba mapato yatokanayo na kuuzwa kwa bidhaa hii duniani hutangazwa kila mwaka katika bajeti ya Uingereza. Mfumo wetu wa elimu, hasa sera zake za lugha ya kufundishia, unatufanya sisi tuwe wateja wakubwa wa bidhaa hii, huku tukiikanyagakanyaga bidhaa yetu muhimu, lugha yetu ya Taifa, Kiswahili. Hauhitajiki utafiti kudhihirisha kuwa hakuna nchi hata moja duniani iliyopata kuendelea kwa kutumia lugha ya kigeni.
Nchi zote tuonazo zikiinukia kimaendeleo leo hii, kwa mfano zile za Asia na Uchina, zimeendelea na zinazidi kuendelea kwa kutumia lugha zao. Nchi hizo zinaendelea kujitegemea kimawazo na kiuchumi kwa vile masuala yote muhimu yamo katika mawazo yanayoelezwa kikamilifu kwa lugha zao. Na imeshadhihirika kiutafiti, kuwa wale wanaotumia lugha zao kufundishia shuleni na vyuoni, humudu kujifunza lugha nyingine za kigeni vizuri zaidi. Hali nchini Tanzania ni kinyume na hali katika nchi hizo. Twaelekea kuamini kuwa tunaweza kupiga hatua ya maendeleo kwa kutumia Kiingereza, na hata mara nyingi, katika kuidharau lugha yetu ya taifa, Kiswahili, utasikia mtu akisema sentensi kwa Kiswahili halafu anasema, “Kwa lugha ya Kitaalamu, maana yake ni kwamba….” akimaanaisha kuwa kwa Kiingereza aliyoyasema yana maana fulani. Huu ni uleule utumwa ambao tumeutaja awali, wa kudharau chetu na kukumbatia cha kigeni.
Tumefikia hata hatua ya kuaminishwa na huo utandawazi kuwa kuna utamaduni wa kimataifa bila kujua kuwa popote pale palipo na mwenye nguvu na mnyonge, utamaduni wa mwenye nguvu huutawala ule wa mnyonge. Na hili linaanzia hata katika ngazi ya kitaifa ambako suala la lugha ya kufundishia ni la kitabaka. Kimataifa, tunaona leo hii jinsi ambavyo utamaduni wa Marekani na wa mwenza mkuu wa Marekani, Uingereza, umetawala duniani. Ni katika utawala huu wa kitamaduni ndimo mlimojificha siri za kuabudu Kiingereza na Ukingereza bila kujali athari zake katika utoaji wa elimu nchini Tanzania na kwengineko Afrika. Lugha na utamaduni ni vitu ambavyo vimo ndani ya ubongo na roho ya jamii. Tunapowalazimisha watoto wetu washindwe kujifunza na kujieleza kwa lugha yao iliyobeba dhana mbalimbali za utamaduni wanaouelewa, tunaunda lile taifa alilolikemea Mwalimu Nyerere, taifa mfu lisilo na uhai. Tunawaandaa watoto wetu wawe wazungu weusi, tena wazungu wenyewe ni wazungu koko wasio na nyuma wala mbele kwa kuwadanganyia gololi zinazong’ara huku wakizitupa dhahabu za tamaduni zao na lugha zao.
Tunashuhudia historia ikijirudia! Tunapowafanya vijana wetu watokwe jasho na washikwe na woga kila inapowabidi kujieleza kwa lugha isiyo yao, wakati ambapo wangejengewa misingi ya kujieleza vizuri kwa lugha ya utamaduni wao wasingepata matatizo hayo, hatuendi tu kinyume na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu haki ya kupata elimu na ile ya kutoa maoni na kujieleza kwa lugha anayoimudu mtu, wakiwemo wanafunzi wetu, bali, kwa hakika tunafanya mauaji ya kiakili na kiroho ya watoto wetu, mauaji ya halaiki ambayo yatatufanya tuhukumiwe na historia.
Maana yake "Kifikirishi" ni nini? Na "uhudhurishaji wa swali la semina"?
Asante,
Mwafunzi wa Kiswahili