Shikamoo

Unashangaa nini?

Msiba kwetu nyumbani

Kisiwani mwa amani

Kizazi hadi kizazi

Sisi tumeuzoea…

Mgeni kwetu nyumbani

Kamwe si hayawani

Twamthamini mgeni

Kuliko hata mwenyeji

Sisi tunampokea…

Biashara kwetu ndani

Haikosi mshitiri

Bara hata visiwani

Nyanda juu hadi pwani

Sisi tunaiwezesha…

Walokuja kwa jahazi

Wakisukumwa na kusi

Wa merikebu za mbali

Mizinga zikisheheni

Sisi tuliwaitika…

Wengine wakichuuza

Na baadhi kulowea

Bara wakitangatanga

Kuzitafuta ngawira

Sisi tuliwaonyesha…

Nasi hatukukaidi

Kuwapokea kwa jadi

Walipoibisha hodi

Na misafara kuhodhi

Sisi tuliwapenyeza…

Hatukuuanza leo

Ukuwadi tufanyao

Tulianzia na hongo

Kwa kila jino la tembo

Sisi tulijitwalia…

Mambo yalipogeuka

Tukageuzwa ngawira

Ndiposa wenye dhamana

Bei walipotupiga

Sisi tuliwahofia…

Ni hawa hawa wakuu

Wa jana na leo yetu

Wanaofanya mizungu

Kutugeuza vizuu

Sisi tunawatazama…

Wametuweka jamvini

Kututia msibani

Tulie kwa ufakiri

Na mali zetu lukuki

Sisi tumehamanika…

Leo ushangae nini

Kwani ulikuwa wapi

Nyuki wakipigwa moshi

Na kulala usingizi

Sisi tukisuasua…

Masega yalipovunjwa

Na asali ikarinwa

Na wanapozindukana

Nta wakasake tena

Sisi tulinung’unika…

Lini tutakuwa mbogo

Tuyakatae makombo

Tukashikane mikono

Tusitoe shikamoo?

Sisi tunajiuliza!

©demere kitunga, 2012