Mhadhiri Shangwe Ameandika Haya Kuhusu Uzoefu Wake:


Kwa
kuanza kabisa niweke msimamo wangu mbele: Kiswahili kitumike kama lugha ya
kufundishia. Kiingereza kifundishwe.

Naomba
nitoe uzoefu wangu kama mwanafunzi wa Kiingereza kwa takribani miaka 24 sasa.
Sina tofauti sana na Ndugu Chambi hapo [chini], mpaka leo nikiandika jambo kwa
lugha ya Kiingereza, au kuzungumza, natumia nguvu nyingi sana kuliko nikitumia
Kiswahili ambacho kwa lugha ya mtaani huwa ‘natiririka’ kama maji ya mto
Rufiji! Lakini kupitia kazi yangu ya ualimu (tena ngazi ya Chuo Kikuu) ambayo
nimeifanya kwa muda mfupi tu, na kwa kuzingatia uzoefu wangu kama mwanafunzi
katika mfumo huu wa Kiingereza kama lugha ya kufundishia, nimegundua kwamba
hakika wanafunzi huwa hawaelewi. Wanakariri.

Kama
mwalimu (narudia tena mwalimu wa chuo, maana mnasema wale wa sekondari na shule
za msingi walifeli – mimi sikufeli!), mimi mwenyewe hulazimika kutumia
Kiswahili mara kwa mara ninapofundisha. Awali nilidhani nafanya vile ili
kuwasaidia wanafunzi lakini baada ya muda nikagundua kumbe nafanya vile
kujisitiri mwenyewe! Maana yapo mambo mtu unataka kuyasema lakini kauli haitoki
kwa kukosa msamiati mwafaka, na hapo ndipo hukimbilia Kiswahili. Unaweza kusema
mbinu hii ilikuwa ya msaada mkubwa kwa wanafunzi kama ilivyokuwa kwa mwalimu mimi!

Kuna
hali ya kujidanganya katika hili, kama ambavyo nilikuwa nikijidanganya kwamba
kwa kutumia Kiswahili kuelewesha wanafunzi basi nilikuwa nawasaidia wanielewe na
kamwe si udhaifu wangu wa lugha ya Kimombo. Nakumbuka nilipokuwa Sekondari jinsi
tulivyokua tukikariri mambo mbali mbali lakini tulikuwa hatuelewi. Juzi rafiki
yangu kanikumbusha kitu kinachoitwa “round-bottomed flask” na “flat-bottomed
flask”, ni vifaa vitumikavyo katika maabara na tulisoma katika somo la Kemia.
Nakumbuka tulivyokua tukipata tabu kukariri vifaa hivi na wakati mwingine hata
kuchanganya wakati wa kuvichora, yaani badala ya kuchora “round-bottomed flask”
unachora “flat-bottomed flask”. Mwisho tulikariri, tukajua kwa kukariri kila
kimoja kutoka kingine. Lakini hatukuelewa maana ya maneno “round-bottomed” au “flat-bottomed”.

Pamoja
na kujua maana ya “round” na “flat” sikuweza kuoanisha maneno haya yalipotumika
pamoja na neno “bottom” kwenye “round-bottomed” au “flat-bottomed” ili kuleta
maana!!! Laiti ningejua hili la kuchanganya “round-bottomed” na “flat-bottomed”
lingetoka wapi? Miaka mingi baada ya kumaliza shule ndipo nilipogundua kwamba
kumbe nilitumia nguvu kubwa sana kujifunza kitu kirahisi. Nguvu hiyo ingetumika
sehemu nyingine sidhani kama somo lile la Kemia ningepata alama ya D!

Lakini
miaka mitatu iliyopita nilikuja China kwa masomo. Nikatakiwa kusoma lugha ya
Kichina kwa mwaka mmoja. Walimu wanaofundisha Kichina ni Wachina, na wanatumia
Kichina kufundishia, hata kwa wageni. Mwalimu wangu wa kwanza kabisa
hakuzungumza Kiingereza japo neno moja. Sikumbuki. Kabla ya kuanza somo la siku
kuna orodha ya misamiati inayotumika katika somo hilo na tafsiri ya kila
msamiati katika lugha ya Kiingereza. Pamoja na kwamba sikupata shida sana kwani
misamiati mingi niliielewa maana yake lakini mara kadhaa nilijikuta kurejea
kamusi ya Kiingereza ili kuelewa maana ya msamiati ule wa Kichina. Kwamba
unatoka neno la Kichina, unapewa tafsiri yake kwa Kiingereza, unagundua kwamba
hilo la Kiingereza nalo hulijui/hulielewi hivyo inabidi kutafuta maana yake
pia!!

Na
niseme kwa kujifunza Kichina pia nimejifunza Kiingereza kwa kiasi kikubwa
wakati huo huo nikigundua kwamba maneno mengi ya kawaida kabisa sikuyajua kwa
Kiswahili. Majina ya wadudu, matunda, chakula, miti, wanyama, n.k. siyajui kwa
Kiswahili!! Sikujua Kiswahili wala Kiingereza, lugha ambazo zingenirahisishia
sana mimi kujifunza Kichina! Zaidi kwa lugha ya Kiswahili, ingeniwia rahisi
sana kuelewa mambo mengi ambayo maana yake inaendana na mazingira na utamaduni
nitokako. Sidhani kama ugumu huu uliwapata wenzangu waliotoka nchi zinazotumia
lugha zao kufundishia. Sikufanya utafiti lakini sidhani.

Hizo
takwimu za Kenya kuwa na 25% tu ya watu wanaoelewa Kiingereza ni za kushitusha.
Tanzania ni asilimia ngapi? Haiwezi kuzidi 10, hapana? Kumbe suala la lugha ni
suala la demokrasia!! Huwezi kutumia lugha ambayo watu wako zaidi ya 85%
hawaielewi. Hawa “elites” 25% ndiyo taswira ya “demokrasia” yetu. Hawa ndiyo
tunawaona tukitaka kupima maendeleo yetu ya kiuchumi. Hawa ndiyo ishara ya
maendeleo. Hatima ya jamii zetu tumewakabidhi watu hawa wachache. Kuna
udikteta unaozidi huo?

Maswali
haya yanatuhitaji kutafakari si tu masuala ya lugha bali utaifa wetu ambao
umejengwa kutokana na matokeo ya mkutano wa Berlin wa mwaka 1884-85. Lakini
tuanze na hili la Kiswahili. Kitumike kufundishia. Ngazi zote.