Mimi Mwanaharakati Muasherati!
Mwanahamisi ‘Mishy’ Singano
Kiukweli nilikuwa natafuta jina sahihi litakaloelezea harakati zangu kwa kina. Naam, Mwanaharakati Muasherati ni jina sahihi kabisa. Pambe hasaaa! Tena hasa kwa kuwa limetoka kwa nguli wa harakati, mimi ni nani nilikatae?
Imekuwa ni sehemu ya tambiko langu, kila niamkapo asubuhi kusujudu na kumshukuru Muumba kwa kunipa pumzi na afya, kutazama juu na tabasamu lenye hasira kushukuru wanaharakati nguli, waliopambana kwa machozi na damu, kunifanya mimi leo nikawa Mishy mwenye sauti na kiburi cha kusema yale yanayonipendeza, mwenye fursa ya kuishi maisha ninayotaka miye, siyo maisha niyayopangiwa na waja. Bila wao – wanaharakati nguli – hakuna miye. Kwao najidogosha na kujinyenyekeza.
Hasira kwenye tabasamu langu kwao siyo tu kwa kuwa najua wamenipa dhima ya kufanya zaidi ya waliyoyafanya wao. Mara nyingi natanzika na uwezo wangu dhalili wa kufikia hata theluthi ya waliyofanya. Ila zaidi napata hasira kujua mimi si wao, siishi kikazi chao, sizifuatizi mila zao, siwajui bibi zao na hakika sitafanya mambo na harakati kama walivyozifanya wao. Hili hunitia hofu na hasira kwa kuwa, kibinadamu, wote tunataka na kupenda kuwa kama walivyokuwa masomo na manyakanga zetu.
Lakini narudisha tabasamu tena ninapokumbuka maneno ya mmoja wa wanaharakati nguli nilipokuwa namlalamikia kwa kutokutulea vyema kwenye harakati. Alinijibu, “na sisi hatukulelewa, kila kizazi kina utume wake, tafuteni utume wenu.” Bila shaka utume wangu umetimia kwa kutawazwa rasmi kuwa mwanaharakati muasherati.
Utume wa kizazi hiki, ukiniuliza mimi, ni kuanza kuuliza maswali magumu. Tukianzia kwenye swali la msingi, je, uwanawake ni nini hasa? Sasa ukiwauliza wanawake wa zama hizi labda watakujibu,
Uwanawake
Ni wepesi wa akili yako
Ni upana wa busara zako
Ni ukubwa wa hekima zako
Ni kung’ang’ana na ndoto zako
Ni ujasiri wa kufanya kitu kipya kisichofikirika
Ni kusimamia unachokiamini
Ni unene na ujazo wa akaunti zako
Ni ukubwa wa mjengo wako
Ni mng’aro wa kucha zako
Na kadhalika.
Tupo kwenye kizazi ambacho uwanawake siyo tu uhodari wa kupiga deki, kupika vipopooo na samaki wa kupaka, kuengaenga mume na kufua nepi za watoto. Kizazi hiki, tunajiuliza kuna kitu gani kati nasaba au damu kinachofanya eti uwanawake uwe ni kuhusu kupika na kupiga deki? Kwa nini mahaba na tashtiti ziwe za upande mmoja tu – kutoka kwa mwanamke kwenda kwa mwanaume? Kwa kuna tatizo gani mimi nikiwa namtungia kikuba, yeye achemsha chai ya mchaichai na mdalasini, kisha twakutana utangani, nikimsinga kwa msio naye akinipaka liwa?
Pia kwa nini uwanawake wangu unavuliwa pindi nitakapoamua kuacha kupiga deki? Uvuaji huu unamnufaisha nani? Hoja ya msingi hapa siyo kupiga deki au kupika kama sehemu ya kazi zinazotakiwa kufanywa na yeyote awaye yule, bali vitendo hivi sasa vimefanywa kuwa ‘SIFA’ au ‘VIGEZO’ vya uwanawake.
Naam, ‘kazi za ndani na unyenyekevu uliopitiliza’ kuwa ndiyo sifa bora za mwanamke ni mjadala ambao tumeukwepa kwa miaka mingi sana. Mosi, kwa sababu si wengi wangefurahia kuitwa wanaharakati waasherati. Pili, ni mjadala ambao unaleta ukakasi kwa kuwa unatupasa tuchambue makuzi yetu, mila zetu, tamaduni zetu na hata dini na imani zetu. Na sote tunajua kuwa ni rahisi kubadilisha sera za nchi kuliko kubadilisha imani inayotaka mimi niamini kuwa pepo ya mwanamke iko chini ya miguu ya mumewe.
Sasa uesherati wa kiharakati pekee ndiyo unaweza kukupa ujasiri wa kuleta mijadala inayolenga kuhoji imani na mazoea yetu. Ni muda muafaka sasa kwa kizazi hiki cha leo kuchambua na kujadili ‘mahusiano ya kifamilia na kinyumba’ na ‘mgawanyo wa madaraka na majukumu katika vyumba na vitanda vyetu.’ Mjadala mpana wa nani hasa anamlalia nani na kwa nini katika kaya na nyumba zetu.
Dunia tunayoishi sasa inanitaka mimi mwanamke eti kufanya kazi mara tatu zaidi ili nionekane naweza na kujua kazi yangu. Ni dunia inayonitaka kutafuta zaidi ili kukidhi mahitaji yangu mwenyewe na kupata fursa ya kukimbia manyanyaso. Pia inanitaka kutumia fursa niliyonayo kushiriki katika ukombozi wa wenzangu. Na hapo hasa ndipo dhana ya uesherati wa kiharakati inapoleta maana kamili.
Mimi kama muumini wa ‘utashi wa mtu’ naamini pia kuwa utashi wetu nao ni matokeo ya mazoea na mapokeo. Hivyo, bila jitihada za dhati za kutoyazoea tuliyoyapokea, tutaendelea kuwa makuwadi wa mfumo dume kwa kujua au kutokujua, kwa makusudi au kwa bahati mbaya. Kuwa mwanaharakati muasherati ni kukataa katakata kufanya vitu kwa mazoea tu bila tafakuri tunduizi ya mantiki ya mapokeo. Najivunua huu uwanaharakati asherati.