MTAZAMO WA KUTETEA
Uamuzi wa ACT unafanana na hekima ya ‘Uamuzi wa Busara’ wa TANU wa mwaka 1958
Na Marwa M. Maswi
Kususa mara nyingi hakujawahi kuwa suluhisho la mkwamo au mgogoro wa siasa. Hata katika mazingira fulani fulani ambapo mbinu hii imefanikiwa, kufanikiwa huko hakukutokana na kususa pekee, bali kwa kuchagizwa na mashinikizo mengine pia hususan kutoka nje. Tena mara nyingi imekuwa mbinu ya mpito ambapo muda fulani ukipita inapoteza maana.
Siasa, tofauti na mambo mengine, ni mpambano wa kutafuta mamlaka (power and authority). Ni mpambano katili na wenye lengo siku zote la kumpokonya na kumfilisi mshindani wako jumla (Zero Sum Game). Inapotokea mnalazimika kupoteza kiasi au kugawana mamlaka, ni kwa kukosa tu namna. Na mara nyingi kwa kuepusha tu zahma. Hii inafanya mbinu ya kususa kutofaa sana maana ukisusa unamsaidia yule unayepambana nae kupata mamlaka yote ambayo pengine asingeipata. Yaani, ‘Ukisusa, wenzio twala’.
Historia yetu ni tajiri wa mifano na mafunzo ya hii mbinu ya kususa. Tunajifunza kuwa mara kadhaa, kususa ni moja ya mtego ambao mshindani wa kisiasa anamuelekeza mwenzake aunase ili yeye afanikiwe kuchukua jumla. Ni njia ya kuchokonoa hisia za mpinzani wako ili atumie hasira kufanya maamuzi asuse. Akisusa unaendelea. Inakuwa ile hadithi ya “hasira za mkizi furaha ya mvuvi”.
Ipo mifano miwili kuhusu kususa katika siasa nchini yenye matokeo mawili tofauti. Mfano wa kwanza unaotupa funzo kuhusu hili la kususa, ni mazingira ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wenzake wa TANU walitegwa nao. Mwaka 1958, Mkutano Mkuu wa TANU ulikutana ukiwa na wajumbe 300. Katika moja ya agenda zake, ilikuwa ni kujadili iwapo TANU ishiriki uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria au la. Uchaguzi huo, kinyume na matakwa ya TANU, ulikuwa uwe wa kura 3, yaani kura ya Wazungu, kura ya Waasia na kura ya Waafrika. TANU ikitaka kura iwe moja na ipigwe na wote kuamua hatma ya Tanganyika.
Ikumbukwe kuwa wakati huo, tayari kulishakuwa na jitihada zilizofeli huko Kenya na iliyokuwa Rhodesia Kusini (Zimbabwe) za kutaka kupitisha Katiba za Uhuru ambazo zililenga kulinda maslahi ya wakoloni na walowezi na si wazawa. Jaribio hilo lilikuwa linainyemelea Tanganyika pia. Wengi katika mkutano ule, walitaka TANU isusie uchaguzi huo kwa madai kuwa kushiriki uchaguzi ule ambao kulikuwa na hofu kuwa ungegubikwa na ubatili, TANU ingeweza kushindwa, ushiriki wao ungetumika kuhalalisha uharamia na ingekuwa ni kukisindikiza Chama cha wahafidhina wa Kikoloni wa United Tanganyika Party (UTP).
Uamuzi wa Busara wa viongozi wa TANU wakiongozwa na Mwalimu Nyerere na wenzake ulifanikiwa kuushawishi Mkutano ule ulioketi tarehe 21 Januari 1958 kule Tabora kutokususa. Hoja ya Mwalimu na wenzake ilikuwa kwamba, iwapo watasusa, Serikali ya kikoloni ingeendelea na uchaguzi huo bila TANU. Ikiwa wangeendelea, wagombea wa UTP wangepita bila kupingwa kisha wangeingia Barazani na kuwa na mamlaka ya kutunga Sheria na Katiba waitakayo wao. TANU na wazalendo wasingepata kitu kabisa. Mwalimu aliendelea kujenga hoja kuwa, kwa kushiriki, hata kupata viti vichache na kuingia ndani, TANU ingekua sehemu ya maamuzi na ingepata jukwaa la kusimamia maslahi ya wazalendo wa Tanganyika.
Ushauri wa Mwalimu Nyerere na wenzake ukawa kwamba TANU itafute wagombea miongoni mwa jamii za Wazungu na Waasia wanaowaunga mkono wawasimamishe. Mwalimu aliwaambia, “Ni busara ikiwa mtu amedai kiasi fulani kwa mdeni wake, akimlipa sehemu fulani ya kiasi anachodaiwa inafaa kipokewe kiasi hicho na pale pale iendelee kudaiwa sehemu iliyobaki, kwani hata hicho kidogo ni haki yake. Hivyi hivyo unaweza kuendelea kulipwa mpaka haki yako yote uipate”. TANU iliazimia kushiriki uchaguzi huo uliofanyika katika awamu mbili mwezi Septemba 1958 na Februari 1959. TANU iliibuka na ushindi katika viti vyote 15 ambavyo 3 kati ya hivyo ilipita bila kupingwa. Kufuatia ushindi ule, TANU ikamiliki mamlaka ya Baraza la Kutunga Sheria na kuwa katika nafasi ya kutengeneza Katiba ya kuelekea Tanganyika Uhuru.
Upande wa pili wa somo la kususa tumelipata katika marudio ya uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2015 uliofanyika baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa awali ambayo yaligubikwa na utata. Chama cha CUF wakati huo chini ya uongozi wa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, na Katibu Mkuu na Mgombea Urais wa Zanzibar wa wakati huo, Maalim Seif Sharif Hamad ukaamua kususa kushiriki uchaguzi ule wa marudio. Walishangiliwa na kupongezwa sana na wanachama na mashabiki wao. Uchaguzi ukafanyika ukihusisha wagombea wa CCM na vyama vingine ikiwemo ADC. Wagombea wa CCM wakashinda katika ngazi zote Unguja na Pemba kuanzia Urais, Uwakilishi hadi Udiwani. Wakashinda hata katika yale maeneo ambayo walikuwa hawashindi huko nyuma ikiwemo Pemba na majimbo 3 ya Unguja likiwemo Malindi. Isitoshe, CUF ikaingia katika migogoro na kusambaratika.
Matokeo ya kususa kule yakaipa CCM ‘mamlaka jumla’ ya Zanzibar katika Baraza la Wawakilishi. Fursa hiyo ikatumiwa na Serikali ya CCM kufanya chochote kile walichokitaka ikiwemo kubadilisha vipengele vya Sheria ya Uchaguzi. Ikaongeza kipengele ambacho kimekuwa mwiba katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Kipengele hicho ni kile cha kuruhusu vyombo vya Ulinzi na Usalama kupiga kura siku moja kabla ya kupigwa kura kwa wapiga kura wengine wote. Ilipofika wakati wa uchaguzi, chama cha ACT pamoja na kutopendezwa na utaratibu huo hawakuwa na jinsi zaidi ya kushiriki uchaguzi katika mfumo wasioupenda. Matokeo yake, kura ikapigwa tarehe 27 na 28 Oktoba, 2020 na chama cha ACT kikaambulia majimbo 4 tu ya Uwakilishi na Ubunge na katika Urais wakapata asilimia 19.
Kutokana na mafunzo hayo mawili katika historia yetu, nachelea kuunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu ya ACT wa kuamua kurejea katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Vyombo vya Uwakilishi. Ni uamuzi wa kijasiri, kishujaa na kimkakati. Ni uamuzi unaotokana na kujifunza na kujisahihisha. Ni uamuzi wa kikomavu.
Ikumbukwe kuwa ACT ni chama cha siasa na si Jumuiya ya Kiraia (CSO) wala Taasisi Isiyo ya Kiserikali (NGO). Ni chama kinachosaka dola na mamlaka. Kwao hakuna hekima wala busara yoyote ya kususa na kuwa nje ya ama Serikali au Vyombo vya Uwakilishi ikiwa wanayo fursa hiyo. Hakuna, kwa sababu uhusiano wa Chama cha Siasa na Dola ni kama uhusiano wa Samaki na Maji. Uhai na ustawi wake ni kuwemo ama Serikalini au Bungeni na sio vijiweni na mtaani.
Wala hatuhitaji kuumiza vichwa, wale wanaoamini ACT inapaswa kususa na kuwa nje ya Serikali na vyombo vya uwakilishi watuambie vyama vilivyoko nje ya Serikali vina afya gani? Uamuzi wa Kamati Kuu ya ACT kwa niaba ya wanachama wao ni uamuzi sahihi katika mazingira waliyopo. Kuingia kwao hakubadilishi madai yao. Si lazima kuwa wamekubaliana na matokeo, si lazima kuwa wamepuuzia machungu na maumivu ya waliojitoa muhanga, wala si kwamba ni wabinafsi na waroho wa madaraka. Bali kama alivyosema Mwalimu Nyerere katika Mkutano Mkuu ule wa TANU wa 1958, chukua kwanza kilichopo ambacho pia ni haki yako, kisha endelea kudai kile kingine hapo hapo. Nikiazima pia hekima ya Hayati Meles Zenawi, yeye alisema, “tutajadiliana tukiwa tunapigana na tutapigana tukiwa tunajadiliana”. Madai na mapambano yanapaswa kutumia kila fursa inayopatikana. Tukiachilia mbali busara hizo mbili, zipo hoja za msingi kwa nini uamuzi huu ni wa hekima.
Kwanza, kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni takwa la Katiba ya Zanzibar ambayo wameshiriki kuiandika mwaka 2010.
Pili, nafasi wanazozuchukua si fadhila kutoka kwa CCM bali zinatokana na kufaulu kwao kupata zaidi ya asilimia 10 za Urais. Ziwe halali au la, hizi asilimia 19 walizopata bado ni zao, ni haki yao na ni kura za wananchi ambazo wanapaswa kuziheshimu na kuzienzi.
Tatu, sharti la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa linazingatia matokeo yaliyotangazwa na Tume haijalishi uchaguzi ulikuwa huru na haki au la. Matarajio ya Katiba ni kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni huru na itaendesha uchaguzi huru na haki. Kwa msingi huo, matokeo ya uchaguzi hayapingiki Mahakamani.
Nne, ACT wamejaribu njia nyingine ikiwemo kususa kwa muda wakiendelea kutafuta maoni ya wananchi. Awali, Maalim Seif mwenyewe aliongoza kwenda kujaribu kuzuia upigwaji kura tarehe 27 Oktoba na akajaribu yeye na wenzake kuongoza maandamano ya kupinga matokeo na madhara yake yakaonekana.
Tano, wananchi wa Zanzibar na waungaji mkono ACT hawakuonesha utayari wa kutumia njia ya machafuko na hawakujitokeza kwa wingi wa kutosha kuleta mabadiliko. Ule pia ni mrejesho. Hekima ilitaka watafute njia nyingine nayo ni kushirikisha wanachama kutoa maoni na kama walivyosema, maoni ya wengi ilikuwa ni warudi wakapambanie ndani.
Nampongeza Maalim Seif, Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe na wenzao kwa uamuzi huo wa kishujaa. Wanaweza wasieleweke leo lakini wataeleweka mbele ya safari. Inawezekana tu wameutangulia wakati. Kuutangulia wakati ndio uongozi maana kuongoza ni kuonesha njia. Abiria wanaweza kuwa na maoni mazuri kuhusu njia lakini aliyekaa katika usukani naye yuko katika nafasi ya kuona yale ambayo abiria hawawezi kuyaona.
Hii haina maana aliye katika usukani anapaswa kupuuzia maoni ya abiria. La hasha, bali anapaswa kuyasikiliza, kuyazingatia lakini hatimaye kwa kuwa yeye ndiye mwenye dhima na dhamana ya kuendesha anategemewa kufanya maamuzi sahihi. Ikiwa dereva atafanya maamuzi tu kwa kuzingatia maoni ya abiria ambao wengine wao hawajui udereva wanajua njia tu na wengine hata njia pia hawaijui vizuri, basi upo uwezekano wa dereva huyo kutowafiksha wanapokwenda na pengine kuyatia maisha yao hatarini.
Sina shaka na hekima ya kutokususa ya uongozi wa ACT. Watashangiliwa na watapuuzwa. Hata waliposusa CUF walishangiliwa na walipuuzwa. Waliposusa, wako wana CUF waliwafurahisha na wako waliowaudhi. Vivyo hivyo safari hii. Wako wanaowapongeza na wako wanaowapopoa mawe ACT.
Maswali ambayo tunapaswa kujiuliza katika kujadili uamuzi wa ACT kuingia Barazani na Serikalini ni haya. Je, kama TANU wangesusa mwaka 1958 hali ingekuwaje? Je, kama CUF wasingesusa mwaka 2015, mabadiliko yale ya Sheria ya Uchaguzi yangefanyikaje wakati nao walikuwa na idadi ya Wajumbe wa kutosha kuyazuia? Je, kususa kuliwapa faida gani? Je, busara ni kwa ACT kuchukua funzo la TANU au funzo la CUF?

MTAZAMO WA KUPINGA
Maoni Yangu
Na Tundu A. Lissu
Kwa maoni yangu, ACT wame-surrender kwa Magufuli na maCCM. Hakuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inayoamuliwa na Wazanzibari wenyewe; bali ile inayoruhusiwa na Watanganyika, yaani Magufuli na maCCM ya Tanganyika.
Sisi Watanganyika ndio waamuzi wa kitu gani kifanyike Zanzibar, sio Hussein Mwinyi na Maalim Seif. Sisi Watanganyika ndio tunaotaka muafaka ambao utamtuliza Maalim Seif na kuituliza dunia ili isituwekee vikwazo vya kiuchumi kwa sababu ya dhulma zetu dhidi ya Wazanzibari.
Tumemtupia Maalim Seif mfupa mtupu (Makamu wa Kwanza wa Rais hana mamlaka yoyote ya maana kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar!) ili atulie na awatulize Wazanzibari wanaomuunga mkono na jumuiya ya kimataifa iliyochukizwa na dhulma zetu Zanzibar na Tanganyika.
Maalim Seif atalipwa mshahara na marupurupu mengine na kupigiwa saluti na mapolisi waliokuwa wanaua watu wake juzi. Zaidi ya hapo hatakuwa na chochote.
Serikali hii ya sasa ni tofauti na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Amani Karume na Maalim Seif. Ya mwanzo ilileta mabadiliko makubwa ya Katiba ya Zanzibar; kwa sababu Karume alikuwa anaunga mkono jitihada za Wazanzibari za kujivua kwenye ‘koti linalobana’ la Muungano.
Hussein Mwinyi ni kibaraka wetu moja kwa moja; tumemweka madarakani kwa bunduki na vifaru vya Bara na kura za Watanganyika waliopelekwa kupiga kura Zanzibar wakati Wazanzibari halali wanakataliwa kupiga kura.
Kibaraka wetu huyu hajampa Maalim Seif na ACT yake chochote zaidi ya vyeo visivyokuwa na mamlaka yoyote. Sasa Maalim Seif atatumika kujaribu kuhalalisha uharamia wa Oktoba 28. Atatumika kama toilet paper ya kusafishia uchafu wa maCCM na madhambi yao dhidi ya Wazanzibari.
Mimi naamini hatafanikiwa. Masikitiko yangu ni kwamba amekubali kutumika namna hii katika uzee wake. Baada ya miaka karibu arobaini ya kusimamia maslahi ya Wazanzibari, sasa amekubali kutumikia maslahi ya Tanganyika!!!
Kama katiba ya zanzibar iko wazi na inasema juu ya serikali ya umoja wa kitaifa.. Kulikuwa na haja gani ya kutoa tamko la kutoutambua uchaguzi na kutaka kuitisha maandamano hadi vulugu zikatokea na watu wakafa mbona hamkujitokeza kutuliza wananchi na kuwaelewesha waache gasia x mlijua kuunda serikali ya umoja ni haki kikatiba.. Vifo vile vya nini kusababisha?
Zito huna hoja🙉
Ni maamuzi mazuri na ya kishujaa. Hongereni sana. Japo wapo watakao beza ila faida yake sio leo bali ni ya kesho.
Naomba Tundu Lissu atume location pin ya hapo alipo anapotolea hayo maoni yake.
Yeye alikimbilia Ubalozini, akaishi humo, akasindikizwa kwa gari na Afisa wa Ubalozi hadi Uwanja wa Ndege, kwenye kaunta ya check in hadi kwenye ndege. Halafu huyu ndio anaye beza wenzake walioamua kurudi mezani kuridhiana kwa lengo la kuondoa maisha ya mashaka kwao na wananchi wao?
Maalim kapitia madhila mengi kuliko yeye na hajawahi kukimbilia Ubalozini wala kukimbia nchi. Lissu atulie tu huko ale shushu.
Duh, hizi siasa nimezivulia kofia. Yaani mwanasiasa akiamua kukuelezea kua Leo no Ijumaa na wakati unaona kabisa ni jumapili, basi usalama wako ni uondoke kabla hajakuelezea zaidi. Ukianza kumsikiliza tu, atakupa hoja hadi utaamini kua yeye ndo yupo sahihi🙌🙌
Maamuzi ya TANU yalijuwa sahihi hadi leo, ACT ilichukua uamuzi sahihi, CHADEMA ipeleke wabunge wa viti maalum ambao ni wapambanaji vita iendelee.
TUNDU ni mbinafsi, mpenda vita na visasi, ni mpotoshaji pia japo yote hayo huyaficha katika koti la upinga maovu, lengo lake ni kupata madaraka kwa njia yoyote ile.
Aliharibu sana alipojaribu kumpotosha Rais kwa kivuli cha uanasheria wake nguli kwenye sakata la mchanga wa madini na kampuni ya ACACIA huku akijua kuwa ilikuwa ni mgongano wa masilahi yeye kuongelea swala hilo kwa kuwa alikuwa mwanasheria wa kampuni hiyo.
Alionesha waziwazi kukoswa uzalendo kwa nchi yake kwa kuitishia serikali kuwa lazima itashitakiwa na kadhalika. Ameonesha kuwa sisi hatuwezi kitu bila mzungu, yuko tayari kumpa mzungu, si msimamo sahihi kwa mtu nationalist.