IV UENDELEZAJI WA LUGHA YA KISWAHILI
22. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Bunge,
Waheshimiwa Wabunge walipokea na kujadili pamoja na mambo mengine Maazimio
mbalimbali. Niruhusu nirejee Azimio lililonigusa sana kuhusu Uanzishaji wa
Kamisheni ya Lugha ya Kiswahili. Awali, Baraza la Kiswahili Tanzania
(BAKITA), Chama cha Kiswahili Tanzania (CHAKITA) na Wawakilishi kutoka Uganda
walianzisha wazo la kuwa na Mpango wa Kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki. Hata hivyo, Baraza hilo
halikuanzishwa, badala yake ikapendekezwa kuanzisha Kamisheni ya Lugha ya
Kiswahili. Azimio la Kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo ya Lugha ya Kiswahili
tumelipitisha katika Bunge hili. Nitumie fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa
Wabunge kwa michango yao mizuri sana mliyoitoa.
23. Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala kuhusu
kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo, michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge imeonesha
umuhimu wa kutumia fursa zilizopo kwa Tanzania kuwa Dira, Mfano na Kitovu cha
Lugha ya Kiswahili. Aidha, Waheshimiwa Wabunge walionesha umuhimu wa kutumia
Kiswahili kama nguzo imara ya Mshikamano, Amani na Utulivu miongoni mwa
Watanzania. Lakini pia majadiliano yamebaini Changamoto zilizopo.
Moja ya Changamoto hizo ni hoja ya Waheshimiwa Wabunge wengi
kwamba, Nchi jirani ya Kenya inatumia fursa zilizopo za Lugha ya Kiswahili
vizuri zaidi kuliko sisi. Kutokana na uzito wa hoja hiyo, ndiyo maana ninapenda
nami niseme machache.
24. Mheshimiwa Spika, Tanzania ni Mdau Mkuu wa
Matumizi ya Kiswahili katika Afrika. Ziko taarifa kwamba Watanzania ndiyo
walioanzisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Ghana, Chuo Kikuu cha Port
Harcourt, Nigeria na Chuo Kikuu wa Sebha, Libya. Inawezekana upo ukweli pia
kwamba leo hii wengi walioko katika Vyuo hivyo ni kutoka Kenya. Japo imekuwa vigumu
kupata takwimu za Ajira ya Walimu wanaofundisha katika Nchi hizo kutokana na
kwamba ajira iko katika Soko Huria. Hakuna Chombo maalum kinachoratibu Ajira za
Walimu hao kwenye Vyuo Vikuu. Nina hakika hii ni moja ya sababu zilizofanya
Wachangiaji wengi kutumia “Uzoefu” zaidi katika kujenga hoja hiyo kwamba
Walimu wengi wanatoka Kenya. Wakati sasa umefika wa kuwa na Utaratibu Maalum wa
upatikanaji wa Walimu wa Kiswahili wenye sifa za kufundisha Nje ya Nchi.
25. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wameainisha
mapungufu mbalimbali ambayo yanachangia katika tofauti iliyopo kati yetu na
jirani zetu wa Kenya. Pamoja na mapungufu hayo, bado Tanzania imekuwa Kitovu
cha Lugha ya Kiswahili Duniani. Walimu wa Kiswahili Nchini Ujerumani, Hamburg,
Berlin, Colon, Leipzig na Chuo cha INALCO Ufaransa, walifundishwa na Walimu
kutoka Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) Zanzibar na Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam. Mwalimu wa Siku Nyingi wa Kiswahili katika Chuo Kikuu
cha London (School of Oriental African Studies – SOAS) anatoka Tanzania,
Prof. Farouk Topan ambaye ndiye alikuwa Mkuu wa Kwanza wa Idara ya Kiswahili,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Walimu wa Kiswahili hadi sasa kule Korea, katika
Chuo Kikuu cha Hankuk wanatoka Tanzania. Walimu wa Osaka, Japan walitoka
Tanzania, katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Zanzibar.
26. Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, yapo mahitaji
makubwa ya Lugha ya Kiswahili kwa sasa. Katika Afrika ya Mashariki peke yake,
Uganda wanahitaji Walimu zaidi ya 10 kwa ajili ya Vyuo vyao Vikuu. Vilevile,
wanataka Walimu katika Shule za Sekondari. Rwanda na Burundi wanahitaji Walimu
na Jamhuri ya Watu wa Kongo (DRC) wanahitaji Walimu kwa ajili ya Vyuo vyao vya
Lubumbashi na Kalemie. DRC wanahitaji pia Vitabu vya Kiswahili Sanifu.
27. Mheshimiwa Spika, mahitaji ya Kiswahili yako
katika Nchi nyingi. Chuo Kikuu cha Kwazulu, Natali, Afrika ya Kusini
kimeanzisha masomo ya BA Kiswahili, hivyo, watahitaji Walimu. Chuo Kikuu
cha Zimbabwe kinahitaji Walimu wa Kiswahili. Namibia wameomba Walimu kuanzisha
Kiswahili katika Chuo chao Kikuu. Jamaica Wanahitaji Walimu wa kuanzisha masomo
ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha West Indies. Baadhi ya Vyuo Vikuu vya
Marekani kikiwemo Chuo Kikuu cha Lugha cha Monterey, California wanahitaji
Walimu wa Kiswahili. Hapa Nchini Vyuo Vikuu zaidi ya 20 kando ya Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam vimeanzisha Masomo ya Kiswahili na vitahitaji Walimu wenye
Shahada za Uzamili na Uzamivu katika Kiswahili. Hivyo, mahitaji ni makubwa
kupita kiasi na hivyo hii ni fursa kubwa kwa Watanzania wenye sifa kujipatia
ajira.
28. Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Desemba 2005,
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
akifungua rasmi Bunge jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema na
nanukuu:
“Lugha ya Kiswahili imeanza kupata umaarufu Afrika na
Duniani. Umoja wa Afrika umekubali Kiswahili kuwa moja ya Lugha zake Kuu.
Aidha, Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu zimekubali kutumia na kuendeleza
Kiswahili. Serikali ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa juhudi hizi zinaendelezwa
na kuhakikisha kuwa Lugha ya Kiswahili inakua Nje ya Mipaka ya Afrika”.
Mwisho wa Kunukuu.
29. Kwa maneno haya ya Mheshimiwa Rais, ni dhahiri kwamba,
Serikali inajali umuhimu wa kuendeleza Lugha ya Kiswahili, kwa vile ina nafasi
nzuri ya kupanuka na kushiriki katika ujenzi wa Jamii ya Watanzania na Jamii
mpya ya Afrika ya Mashariki na hata Duniani kote.
30. Mheshimiwa Spika, tunayo Changamoto ya kukifanya
Kiswahili kiwe Lugha ya Dunia. Lakini pia tunalo jukumu la kuhakikisha kwamba
Lugha ya Kiswahili inafundishwa na kutumika Mashuleni, ikiwa ni pamoja na Shule
za Msingi, na kwamba inafundishwa katika Shule za Sekondari na Vyuo vya Elimu
ya Juu. Aidha, tunahitaji kuhakikisha kwamba Lugha ya Kiswahili inatumika
vizuri na kwa ufasaha katika Shughuli za Serikali, hapa Bungeni, katika
Mahakamani na maeneo mengine kwa faida ya Wananchi wetu na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, pamoja na msisitizo huo, yapo maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia
kazi zaidi. Kwa mfano:
Moja:Bado kuna maeneo mengi yanayohusu Taaluma ya Kiswahili ambayo
hayajafanyiwa utafiti wa lugha. Utafiti ndio uhai wa Taaluma na chimbuko la
maarifa mapya. Ni kazi ya Wanataaluma wa Kiswahili kufanya tafiti za kina
ambazo zitakifanya Kiswahili kitumiwe Kimataifa.
Pili:Vyuo Vikuu vilivyoanzishwa, pamoja na kuweza kufundisha somo la
Kiswahili kwa Wanachuo wa Shahada ya Kwanza, bado havina Wahadhiri wa kutosha
wa kufundisha mafunzo ya Uzamili na Uzamivu. Tunalo jukumu la Kuanzisha
Programu za Shahada za Uzamili na Uzamivu zitakazokidhi mahitaji makubwa ya
uhaba wa Wataalamu wa Kiswahili Ndani na Nje ya Nchi.
Tatu:Hapa Nchini hakuna Chuo Kikuu kinachotoa mafunzo ya Ukalimani. Watu
wanaohitaji stadi hii ya ukalimani wanalazimika kwenda kusomea katika Vyuo
Vikuu vya Nje ya Afrika Mashariki. Mimi najiuliza, hivi hili nalo tunalikubali
wakati Lugha ni yetu? Ninaamini tunao uwezo wa kutumia Vyuo Vikuu na Vyuo
vingine tulivyonavyo kufanya kazi hii ya kufundisha Wakalimani. Ni vizuri Vyuo
vyetu Nchini vianzishe Idara za Mafunzo ya Ukalimani ili kupunguza tatizo hilo.
Nne:Imebainika pia kwamba, hata kama kukiwepo na Wakalimani, bado hakuna
Kumbi za kisasa zenye vifaa vya kusikilizia Tafsiri za Lugha mbalimbali. Kumbi
nyingi tunazofanyia Mikutano tukiacha Ukumbi wa Kimataifa wa Arusha (AICC)
hazina Vifaa hivyo. Changamoto tulio nayo kama Nchi na hasa Wawekezaji wa Kumbi
za Mikutano ni kuhakikisha Kumbi zinazojengwa na zilizopo zinakuwa na Vifaa vya
kutoa huduma ya Ukalimani. Lengo ni kutumia fursa hiyo katika kukuza Lugha yetu
ya Kiswahili.
31. Mheshimiwa Spika, mimi napata shida sana kuona
Warsha yenye Wageni wasiozidi Kumi (10) na Waswahili 200 inaendeshwa
kwa lugha ya Kiingereza, tena bila kujali kama Waswahili hao wanaelewa
Kiingereza au la. Wanachojali ni kuwafurahisha Wageni wachache. Kwa maoni yangu
hii ni kasumba isiyo na maelezo. Changamoto iliyo mbele yetu ni kuondoa
kasumba hii kwa kupenda kutumia lugha yetu ya Kiswahili wakati wote. Tuondoe
wasiwasi katika matumizi ya Lugha ya Kiswahili. Tumeshuhudia Kiswahili
kikikuzwa na kutandazwa katika Mifumo ya Kompyuta ya Linux na Microsoft.
Tumesikia pia kwamba, kama njia mojawapo ya kuboresha matumizi ya Kiswahili
sanifu, tayari Wataalamu wa lugha kwa kushirikiana na Wataalamu wa Kompyuta
wameweza kutengeneza Programu Maalum ya Kisahihishi cha Lugha ya Kiswahili
katika Kompyuta ambayo inatumiwa kusahihisha maneno ya Kiswahili. Haya ni
maendeleo makubwa yaliyofikiwa ya kukiingiza Kiswahili katika Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano Duniani.
32. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba Lugha ya
Kiswahili imekua sana. Wote ni mashahidi kwamba Mashirika makubwa ya Utangazaji
Duniani yanatangaza Kiswahili. Tunajua sana Shirika la Utangazaji la Uingereza
(BBC), Sauti ya America, Radio ya Ujerumani Deutsche -Well na Radio France
International. Wako pia Al Jazeera, Radio Vatican, Radio Japan na Radio ya
Umoja wa Mataifa. Aidha ziko Nchi zenye Vituo vya Radio vinavyotangaza kwa
lugha ya Kiswahili, kwa mfano, China, India, Syria, Misri, Sudan n.k. Hii pia
ni ishara kwamba Kiswahili kinakua kwa kasi sana.
33. Mheshimiwa Spika, tunaweza kuongea mengi ya
nadharia kuhusu lugha yetu nzuri ya Kiswahili kwa muda mrefu. Tunatakiwa sasa
tuanze kutekeleza hayo mengi kwa vitendo. Naomba kuhimiza Taasisi mbalimbali
Nchini, ziweke juhudi zote katika kukuza Lugha ya Kiswahili ili iweze kutumika
katika Nyanja zote za mawasiliano ikiwemo Sayansi na Teknolojia. Vilevile,
natoa Rai kwa Watanzania wote wakiwemo Waheshimiwa Wabunge kujitahidi kila
tunapozungumza Kiswahili kuepuka kuchanganya na maneno ya Lugha ya Kiingereza
kwenye mazungumzo yetu.
34. Baadhi yetu tunamkumbuka Mwandishi na Mshairi wa Riwaya
Bwana Shaban Robert (1909 – 1962) ambaye aliandika kuhusu Lugha ya Kiswahili na
kukifananisha na ladha ya Titi la Mama. Katika moja ya Mashairi yake, aliandika
na nanukuu:
“Titi la Mama litamu, hata likiwa la Mbwa, Kiswahili
naazimu, sifayo iliyofumbwa, Kwa wasiokufahamu, niimbe ilivyo kubwa, Toka kama
mlizamu, funika palipozibwa, Titi la Mama litamu, jingine halishi hamu. Lugha
yangu ya utoto, hata sasa nimekua, Tangu ulimi mzito, sasa kusema najua, Ni
sawa na manukato, moyoni mwangu na pua,Pori bahari na mto, napita nikitumia,
Titi la Mama litamu, jingine halishi hamu”.
Mwisho wa Kunukuu.
35. Anachosema Bwana Shaaban Robert ni kuonesha thamani ya
Kiswahili jinsi kilivyo na utamu wa aina yake katika matumizi. Historia ya
Shaaban Robert, tunaambiwa alithubutu kulikataa kabila lake la Kiyao na kujiita
Mswahili kuonesha jinsi alivyokipenda Kiswahili. Nasi tujivunie Kiswahili, tukipende,
tukitumie, tukienzi na tukithamini. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumechangia
katika kuendeleza Lugha ya Kiswahili.
36. Mheshimiwa
Spika, Watanzania sasa si wakati wa kulalamikiana na kulaumiana juu ya
Matumizi ya Lugha ya Kiswahili, bali sasa tushirikiane kujenga Lugha yetu ya
Kiswahili. Njia iko wazi, nadhani sasa kazi kwetu!
Hotuba:
http://www.pmo.go.tz/docs/Hotuba_ya_Kufunga_Mkutano_wa_Tisa_wa_Bunge.pdf
Picha:
http://4.bp.blogspot.com/-DlAWGTGip1I/UHmhO5OVyrI/AAAAAAAASYg/r0s6gIl48wM/s1600/Mizengo+Pinda.JPG