MLIZINGATIA MAONI YA NANI, WARIOBA?

· Tume imechakachua maoni ya Wazanzibari.

· Watu elfu 16 kuamua hatma ya taifa la watu milioni 45.

Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

Ilikuwa majira ya saa 11 jioni, tarehe 30 Desemba 2013, muda mfupi baada ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukabidhi Taarifa yake pamoja na rasimu ya pili ya
katiba kwa marais wa Muungano na Zanzibar, simu yangu ya kiganjani
iliponiashiria kuwa nimepokea ujumbe. Nikausoma: “Haujambo? Vipi, siku zako za
mwisho zikoje?”  Rafiki yangu wa Kijerumani
aliyekuja hapa nchini alitaka kujua nimejiandaaje kuondoka nchini siku chache
zijazo kwa ajili ya masomo ya juu. Nami kwa uchokozi nikamjibu, “Unaulizia siku
za mwisho, unanitakia kifo?” 


“Nilijua tu utasema hivyo”, alijibu. Kisha akalipua bomu ambalo lilinifanya
nidondoshe machozi: “Nimerudi kutoka Zanzibar leo. Ni kuzuri, na watu wake ni
wakarimu kama wa huku Dar. Ama kweli nchi yenu imebarikiwa. Mna kila aina ya
utajiri, tangu maliasili hata umoja na ukarimu!”


Eti huyu ndugu angependa kuwaona Wabara wakijivunia rasilimali na vivutio
vya Zanzibar. Bila shaka huko Visiwani pia aliwasimulia mengi kuhusu mlima
Kilimanjaro na uzuri wa Bara na kuwaambia ni vyao. Maneno “nchi yenu” na “umoja”
yalijirudiarudia akilini mwangu. Nilisikia mwili ukinisisimka, moyo ukanidunda,
kijasho chembamba kikanitoka huku machozi yakidondoka. Mjerumani huyu alikuwa
amenisimulia hadithi nyingi za kwao, na namna ukuta wa Berlin ulivyoangushwa
mwaka 1989, na Wajerumani wakaiunganisha nchi yao.


Hivyo nikamjibu kijana huyo, “Labda hukukosea kunitabiria kifo. Hivi
karibuni naelekea kufa kama Mtanzania, na kuzaliwa upya kama Mtanganyika. Ama
kweli, sijui mlitumia uchawi gani kuturoga. Mpaka sasa tunatukuza mabaki ya
ukoloni.” 
Akanipa matumaini, “Usikate tamaa rafiki. Wapenda Muungano endeleeni
kupambana. Tanzania yenye marais watatu, na Afrika yenye marais 54 haina
mustakabali katika dunia ya leo.”


Hebu nieleze, ewe msomaji wangu, ingekuwa wewe ungejisikiaje? Huyu ndugu
sio Mwafrika. Ni Mjerumani. Anaihurumia Afrika kwa kuendeleaza siasa za
utengano. Yeye anajivunia kwamba nchi yake imeungana, na wanapigana kuunganisha
Ulaya. Huku kwetu ndio kwanza tunazalisha vi-nchi, halafu tukitegemea tutakuwa
na nafasi katika dunia ya leo?


Pengine kilichoniumiza zaidi sio maneno ya heri toka kwa mzungu huyo. Ni
maneno niliyoyasikia katika hotuba ya Jaji Joseph Sinde Warioba, wakati wa
makabidhiano ya taarifa ya Tume. Kabla sijaichambua nitaomba tukumbushane kitu
kimoja: Wakati wa uzinduzi wa rasimu ya kwanza, Jaji Warioba alisema kuwa uamuzi
wa Tume wa serikali tatu ulizingatia maoni ya watu walio wengi. Baadaye, na
hasa baada ya kugundua kuwa mabaraza ya Katiba yamejaa wajumbe wa chama tawala,
alibadili msimamo na kusema kuwa katika rasimu ya pili uamuzi wa Tume
hautaangalia tena uwingi wa watu bali uzito wa hoja! Alidiriki kuwaambia
wajumbe wa mabaraza ya Katiba wajadili mambo mapya, kwani ya zamani yote Tume
inayo na hakuna haja ya kuyarudia. Kwa maana nyingine, aliwatisha wajumbe
kurudia suala la Muungano, huku akijua wazi kuwa masuala ya msingi kuhusu
maisha ya wananchi kama elimu, maji, afya, ardhi, serikali za mitaa n.k
hayakuwa masuala ya Muungano, na kuyajadili kwake kungetegemea muundo wa
utakaoundwa.


Ilipotoka rasimu ya kwanza, tupo tuliohoji uhalali wa Tume kupendekeza
serikali tatu. Je, ilifikiaje uamuzi huo? Ilizingatia maslahi ya nani? Maswali
hayo yalikosa majibu kwani Tume haikuwa imetoa ripoti. Ni ripoti ya Tume ndiyo
ingetuondoa katika giza.


Na sio kweli kwamba tume yoyote hufikia kutoa mapendekezo kwa kuzingatia
idadi ya wananchi waliozungumza. Tume ya Nyalali ilipendekeza vyama vingi licha
ya kuwa takribani ya asilimia 80 ya watoa maoni walipendekeza tuendelee na
mfumo wa Chama kimoja. Hali kadhalika, Tume hiyo ikapendekeza serikali tatu
licha ya kuwa watoa maoni wengi walitaka tuendelee na serikali mbili. Uzoefu
huu unatuambia kwamba kazi ya Tume ni kusikiliza maoni na kisha kuyafanyia
uchambuzi wa kina kwa kuzingatia hali halisi ya nchi na dunia pamoja na
misukumo inayowafanya watu watoe maoni ya aina fulani.


Kwa uzoefu ambao nchi iliupitia kutokana na utawala wa kiimla wa chama
kimoja pamoja na mabadiliko yaliyokuwa yakitokea duniani, haikuwa busara
kuendelea na Chama kimoja hata kama ndiyo yalikuwa matakwa ya wengi. Lakini
watoa maoni wengi ni watu ambao walikuwa wameaminishwa na chama tawala kuwa
upinzani ni vita na uvunjifu wa amani. Tume ya Nyalali iliyazingatia haya
ikapendekeza vyama vingi.


Je, Tume ya Warioba imezingatia hali halisi ya Dunia ya sasa? Imezingatia
historia ya nchi za kiafrika zilizojaribu kuungana na kisha muungano kuvunjika?
Imezingatia ukweli kwamba watoa maoni wengi kuhusu Muungano ni watu waliolishwa
“sumu” na vyama vyao kutaja idadi za serikali (mbili, tatu, mkataba)? Je,
iliona wimbi la kuvunjika kwa Muungano?


Na sio kweli kwamba Tume ya Warioba ilizingatia idadi ya wananchi waliotoa
maoni. Hebu tuzichambue kidogo takwimu zilizotolewa na Warioba kuhusu Muungano.
Kwa Tanzania Bara, waliozungumzia Muungano walikuwa 39,000. Kati yao, ni watu
27,000 tu ndio waliozungumzia Muundo. Na kati ya hao 27,000, watu 3,510 (au
13%) walitaka serikali moja, 6,480 (au 24%) serikali mbili na 16,470 (au 61%)
serikali tatu. Kwa Tanzania Visiwani, waliozungumzia Muungano walikuwa 38,000
na ni nusu yao tu (19,000) waliozungumzia muundo. Kati ya hao 19,000, watu
6,460 (au 34%) walitaka serikali mbili, na 11,400 (au 60%) serikali ya mkataba,
na watu 25 (0.001%) walitaka serikali moja. Katika mikutano ya Tume huko
Visiwani wapo pia waliopendekeza serikali nne : ya Tanganyika, ya Pemba,
ya Unguja na ya Muungano, huku wakisisitiza kuwa Muungano uwe kati ya
Tanganyika na Unguja. Hao, idadi yao, Jaji Warioba kakwepa kuitaja!


Je, takwimu hizo zinatueleza nini? Ukijumlisha idadi ya watu ambao
hawakugusia muundo wa Muungano, Bara na Visiwani, ni 31,000. Hawa ni wengi
kuliko watu 16,470 waliotaka serikali tatu. Jumla ya waliotaka serikali moja na
mbili ni 16,475, na idadi hii pia ni kubwa kuliko waliotaka serikali tatu. Tume
inaweza kujitetea kuwa watakao mkataba wakikosa sana wanaweza kuhamia kwenye
serikali tatu. Ukikokotoa jumla ya waliotaka mkataba na serikali tatu ni watu
27,870, na hawa ni 36%  (takribani
theluthi moja tu) ya watu waliozungumzia Muungano. Na jumla hii ni kijitone cha
maji baharini ikilinganishwa na watu wapatao 333,537 waliotoa maoni katika Tume ya Katiba. Pia hakuna utafiti
wowote wa kisayansi unaoonyesha kuwa sampuli ya watu 16,000 inaweza kuwa
inawakilisha maoni ya Watanzania milioni 45. Wanaweza kuwa ni watu wa wilaya au
mkoa mmoja.

Katika lugha rahisi, ni kuwa waliotaka mkataba au serikali tatu walikuwa
asilimia nane tu ya waliotoa maoni. Pia, watoa maoni 287,537 sawa na asilimia 86% 
hawakugusia kabisa kuhusu Muungano au muundo wake. Je, uwingi aliousema
Jaji Warioba kautoa wapi? Na kwa nini adanganye mchana kweupe?


Ni vema tukajifunza kutokana na mchakato wa Katiba mpya, ambao ulitekwa na
Wajasiria-Katiba kutoka vyama vya siasa na asasi zisizo za kiserikali. Na mvutano
 baina yao ndio ukateka mijadala na
kufifisha maoni ya wananchi wa kawaida. Kuna wakati ambapo baadhi ya asasi
zilitaka kwenda mahakamani kuusimamisha mchakato baada ya kuona kuwa umetekwa
nyara na chama tawala. Chama kikuu cha upinzani pia kikatishia kujitoa na hata
kumwandikia mjumbe wake barua ili ajitoe.

Lakini baada ya kunong’onezwa yaliyomo kwenye rasimu, wakafyata. Rasimu
ilipotoka, hata kabla hawajaisoma wakaisifu na kusema imezingatia maoni ya
wananchi! 


Sasa takwimu ndio hizo, je, ni maoni gani ya wananchi
yaliyozingatiwa? Huko Zanzibar, hakuna kitu kinachoitwa serikali tatu: wengi
hawakugusia muundo. Wowote utakaokuwepo kwao sawa. Kwa waliogusia muundo, wengi
wanataka mkataba, kwa maana kwamba Muungano uliopo uvunjike, nchi washirika
zipate mamlaka kamili kisha ziamue kushirikiana kama zikipenda. Kwa nini Tume
imeyapuuza maoni yao?


Sababu zilizotolewa na Warioba kwamba Muungano kwa sura yake ya sasa
hauwezi kudumu pia hazina mashiko. Eti kwamba Zanzibar tayari imeshajitangaza
kuwa ni nchi, na Wabara wanaionea wivu. Na hapa, Warioba anasema, kuna majawabu
mawili: ama Zanzibar ibadili katiba au Tanganyika nayo ijitangazie uhuru
kamili. Kuhusu Zanzibar kubadili katiba, Tume inaona kuwa “ukarabati” huo
hauwezekani, hivyo bora Bara nayo iwe na mamlaka kamili. Kwa maneno ya Warioba,
“Hii ndiyo sababu kubwa ya kupendekeza muundo wa serikali tatu!” Kwa hiyo, hapa
tunaona kabisa kuwa sababu ya kupendekeza serikali tatu sio maoni ya wananchi
bali “busara” za Tume.


Lakini kwa busara hizo hizo, Tume ya Jaji Warioba inaiomba Zanzibar ikubali
kubadili katiba ili uraia uwe ni suala la Muungano. Kwa maana nyingine, Tume ya
Warioba inataka Zanzibar iendelee kuwa nchi/dola (state) lakini isiyo na raia! Na katika busara za Tume ni kuwa hilo
ni jambo linalowezekana.

Tume inadhani kuwa uraia ukibaki katika nchi washirika kutaibuka utaifa
(utanganyika na uzanzibari), na hili ni hatari kwa Muungano. Lakini Tume haioni
shida kama kila nchi ikiwa na bendera yake, wimbo wake wa taifa na serikali
yake. Wala Tume haikuona hatari kwa nchi washirika kuwa na mamlaka ya kushiriki
katika mahusiano ya kimataifa kiasi kwamba siku moja Tanganyika na Zanzibar
zitajikuta zimejiunga katika mashirika ya kimataifa, kila moja kivyake, na
wakifika huko waanze kupigana vikumbo. Lakini kwa busara za Tume, hayo yote ni
bora yakawepo, na hayatatishia kuvunjika kwa Muungano.


Tume inatuambia kuwa serikali tatu ndio ‘kiboko’ cha Tanganyika
iliyoendelea kuimeza Zanzibar kwa kisingizio cha Muungano. Serikali tatu
zitaleta usawa. Ni kweli zitaleta usawa, lakini usawa wa kisiasa. Je, usawa wa
kiuchumi utakuwepo kwa wabia wasio na uwezo sawa wa kiuchumi? Bado Tanganyika,
kama mbia tajiri, ndiyo itabeba gharama kubwa ya kuuendesha Muungano. Amlipaye
mpiga zumari ndiyo huchagua wimbo! Ukaka mkubwa wa Tanganyika ndio utadhihiri.
Hata huo usawa wa kisiasa hautakuwapo kwani katika Bunge la Shirikisho, wabunge
wengi watatoka Tanganyika (wabunge 50 toka Tanganyika dhidi ya 20 wa Zanzibar).
Kwa ufupi, shirikisho litaendelea kutawaliwa na Watanganyika iwe ni katika
gharama za uendeshaji, nafasi za kisiasa na hata utumishi wa umma. Watanganyika
ni wengi kwa idadi, hivyo wao ndio watakaoamua nani awe Rais wa Shirikisho, na
uwezekano kwamba Rais wa Shirikisho atatoka Zanzibar utaendelea kuwa ndoto ya
mchana. Uzalendo finyu ndio utatawala Shirikisho.

Kwa ufupi, muundo wa serikali tatu una matatizo na kero nyingi kuliko ule
wa serikali mbili. Ubabe wa Tanganyika utadhihirika katika mfumo huu kuliko
ulivyokuwa katika serikali mbili, ambako Tanganyika alikuwa kaburini. Na kero
zenyewe ni zile zinazohusu mamlaka ya wanasiasa kwani ndizo zinazotawala
mijadala ya sasa. Wanasiasa wataendelea kupigana vikumbo hata kwa mambo ya
kipuuzi; mathalani, katika itifaki  nani
awe wa kwanza kutajwa kati ya rais wa Tanganyika na yule wa Zanzibar, au nani
mkubwa kati ya Rais wa Tanganyika na makamu wa rais wa Shirikisho. Katika
makabidhiano ya ripoti ya Tume ya Warioba tulimsikia Rais Kikwete akilalamika
wakati wa kutaja itifaki kwamba vyeo vingi kweli. Huko baadaye katika itifaki
wataongezeka rais wa Tanganyika, makamu wake, waziri mkuu, spika wa Tanganyika,
jaji mkuu wa Tanganyika, n.k. Barabarani wataenda kwa ving’ora, hivyo tutegemee
foleni zaidi. Vyeo vyote hivyo vinaendana na mishahara na ‘miposho’ mikubwa mno
ambao ni mzigo kwa wananchi. Na wabara ndio watakaoubeba hasa!


Uchambuzi huu wote unatuambia kuwa tuwe makini wakati wa kujadili rasimu ya
pili ya Katiba. Kabla ya kuijadili lazima kwanza tupate taarifa kamili ya Tume
ili kujua vigezo na busara zilizowaongoza kutupatia mzigo huo wa “Danganyika”.
Nasisitiza mamlaka zinazohusika zitoe taarifa hiyo ya Tume kwa wananchi ili
tuijadili na kuikosoa kwani dondoo tu tulizopata kwa Warioba zinaonyesha kuwa
kuna mengi ya kuhoji! Bado naamini tunaweza kuikoa nchi yetu isitumbukie katika
shimo la utengano. Hii ni kama wengi wetu tutapiga kelele kuuokoa Muungano wetu
na kuwasihi wenzetu waliokuwa wamedandia “Basi la Warioba” kushuka ili
tutafakari kwa kina zaidi!


Mwandishi wa
makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya Sayansi ya
Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com