Tanzania ina historia ndefu ya uwepo wa wanazuoni na wanaharakati wenye ama waliokuwa na itikadi/mrengo wa kushoto hasa wa Kimaksisti almaarufu Makomredi. Katika miongo ya 1960 na 1970 walikuwa wengi na walifanya mengi. Waliandika. Walichapisha. Walijadili. Waliandamana. Walipambana.
Hawa walishiriki kwa namna moja au nyingine katika uibukaji na ukuzaji wa kizazi chao na vizazi vilivyofuata. Waliofuatia nao walichangia mwendelezo huo kupitia wanafunzi wao vyuoni au wafanyakazi wenzao kwenye taasisi za kiuwanaharakati. Kizazi kikazaa vikawa vizazi. Vizazi vitatu vya Makomredi.
Pia tunaona vilinge walivyoanzisha makomredi wa vizazi vyote vitatu na ushehe kama vile HAKIARDHI, JULAWATA, KIGODA, na KAVAZI vikiibua, vikialika na vikichochea mwendelezo wa ukomredi. Pia majarida/magazeti yao kama CHECHE, CHEMCHEMI, RAI/RAIA MWEMA, CHANZO, SAUTI YA UJAMAA, na UDADISI yakitoa nafasi na yakisheheni uchambuzi na mada za kuvijenga vizazi vya zamani, vya sasa, na vya baadaye.
Lakini kuanzia miongo ya 1980 hadi 1990 mtikisiko utokanao na Uliberali Mamboleo uliathiri pia harakati za mrengo wa kushoto na hata kupunguza hamasa ya baadhi ya makomredi. Kufika miongo ya 2000 na 2010 hali ya kukuza ukomredi ikawa imepungua sana kasi yake ya zamani. Hivyo katika zama hizi za muongo wa 2020 kumekuwa na uibuaji na ukuzaji hafifu wa makomredi ukilinganisha na zama za awali.
Kwa hiyo wakati umefika sasa wa kutafutana na kutafakari kuhusu hali na hatima ya ukomredi. Wa kujadili tupo na/au tumepotelea wapi? Na tufanye nini sasa ili kuhuisha utamaduni wa kikomredi wa kuibua na kukuza makomredi?