Nini chura na tembo yu mtoni?
Katu, ye hasemi,
Atenda tuu,
Tena usiku gizani,
Si mwanga hata,
Ila ye na jua hawapatani,
Pengine hajali,
Au ajua keshachelewa
Na ishamfika ajali,
Hii saa…
Maumivuye makali
Naye afanyeni, hajui,
Au pengine hasemi
Hana sauti
Au imemkwama kooni,
Au labda asema
Ila si ndo hatuko makini,
Au hajui asemeni
Na ishamfika shari,
Hata aseme nini
Ajua dhahiri
Hawezi ibadilisha hali,
Naye awaulizeni,
Nisemeni?
Nizitaje zipi nambari?
Za walotutoka tayari
Au za walo safarini?
Mnataka niwaelezeni?
Niibue tafrani?
Nini nisababishe shari
Nilipoteze tumaini?
Aku mi sisemi
Msinitie lawamani,
Nani huyo hasemi?
Swali gani’lo jamani?
Eti aitwa nani?
Simtaji asilani,
Naye aniweke ndani!
Hataaa… ‘sinitie hatiani.
©2020
Jasper “Kido”
