Tarehe 15/12/2021 Rais Samia Suluhu Hassan alifungua mkutano wa wadau wa siasa ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na Baraza la Vyama vya Siasa. Tukio hili liligubikwa na mambo makuu mawili: mosi, kususia mkutano kulikofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na pili: kitendo cha Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo) kuhudhuria mkutano na kutumia fursa hiyo kumsihi Rais Samia ‘asaidie’ kuiondoa nchi katika mkwamo wa kisiasa kwa kutafuta namna ya kisheria ya kumwachia huru Mwenyekiti wa CHADEMA, ndugu Freeman Mbowe.

Mbowe yupo rumande akikabiliwa na mashitaka ya ugaidi na uhujumu uchumi. Chama cha National Convention for Construction and Reforms (NCCR-Mageuzi) pia kilisusia mkutano huu. Lakini kutokuwepo kwa CHADEMA na kuwepo kwa ACT ndiko kulikozingatiwa zaidi.

Mjadala mzito umeibuka, na shutuma kali zimetolewa na pande zote mbili kupitia ama viongozi waandamizi au wafuasi wao.

Kwa CHADEMA, Zitto anatuhumiwa kusaliti dhamira yao ya mapambano ya kidemokrasia kwa kukubali kuhudhuria mkutano na zaidi kuwasemea juu ya Mbowe. Zitto amejitetea, akisema hatua yake hiyo ilikuwa na baraka za uongozi wa CHADEMA. Pia alilalamikia chuki dhidi yake inayotokana na uhasama wa kisiasa baina yake na baadhi ya wanachama na wafuasi wa CHADEMA.

Tuwaelewe CHADEMA
CHADEMA ni chama kikuu cha upinzani Tanzania Bara. Katika miongo miwili iliyopita, chama hiki kimejiimarisha hata kuizika ile dhana kwamba vyama vya upinzani havina wafuasi vijijini. Kwa ukubwa wa CHADEMA, hakuna mwafaka wa kisiasa unaweza kupatikana nchini bila ushiriki wake.

Chama hiki ni kama tembo aliyeingia chumbani kwako, katu huwezi kusema eti humuoni!

CHADEMA wanajua nguvu hii waliyonayo na wakati mwingine unaweza kuona kwamba wanaamini hawahitaji kuungwa mkono na chama kingine cha upinzani kufikia malengo yao, walau kwa Bara. Chama hiki kina madai kadhaa kwa Rais Samia na serikali yake: kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya, tume huru ya uchaguzi, kuachiliwa huru wafungwa wote waliofungwa kwa sababu za kisiasa, kufutwa kwa kesi dhidi ya mwenyekiti wao, na kuruhusiwa kufanya siasa bila bughudha ya vyombo vya usalama.

Msimamo mkali wa CHADEMA kwenye kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa nchini unachangiwa na ukweli kwamba hawaoni kwamba hali yao inaweza kuwa mbaya zaidi ya ilivyo sasa. Kama ilivyodokezwa hapo juu, mwenyekiti wao anakabiliwa na kesi nzito. Mwezi Machi 2020, Mbowe na viongozi wengine waandamizi wa chama wapatao nane walihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela au faini ya shilingi 350 milioni. Walilipa faini na kuepuka jela. Lakini pia Mbowe alishawahi kukaa mahabusi bila dhamana kwa miezi mitatu kati ya mwaka 2018 na 2019.

Katika uchaguzi wa 2020, CHADEMA walishinda kiti kimoja tu cha ubunge kutokana na kile wanachoita ni ‘uchafuzi’ na si uchaguzi. Katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2019, wagombea wao wengi walienguliwa kiutatanishi hali iliyopelekea kususia uchaguzi wenyewe. Wanachama wake wakiwemo viongozi waandamizi wamehamia chama tawala katika mazingira ambayo CHADEMA wanaamini walinunuliwa.

Makamu Mwenyekiti wao, Tundu Lissu, anaishi uhamishoni nchini Ubelgiji baada ya kuponea chupu chupu kwenye jaribio la kumuua ambalo lilisababisha amiminiwe risasi 16 mwilini mwake. Aliyekuwa Mbunge wao, mwanasiasa machachari Godbless Lema pia anaishi uhamishoni Canada.

Zaidi ya hapo, makumi kwa makumi ya wafuasi wake ama wamefungwa jela au wana kesi mahakamani, kesi ambazo wao wanaamini ni za “mchongo.” Ni kwa namna gani Wanachadema wanaweza kuwa katika hali mbaya zaidi ya hii waliyopitia na wanayopitia? Ni wazi CHADEMA wanadhani hawana cha kupoteza.

Tuwaelewe ACT-Wazalendo
Hiki ni chama kikuu cha upinzani Zanzibar. Kama ilivyo kwa CHADEMA Bara, hakuna mwafaka wa kisiasa utapatikana Zanzibar bila ushiriki wa ACT. Ni chama kichanga kiumri lakini chenye ushawishi wa wastani Tanzania Bara.

ACT wameonesha dhamira yao ya kujenga siasa za maridhiano. Wameanzia Zanzibar kwa kukubali kuwa sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na wanataka kujaribu kudurufu siasa za aina hii kwa upande wa Bara. Tofauti na CHADEMA, sidhani kama ACT wanaamini wanaweza kufikia malengo yao bila kushirikiana na chama kingine, walau kwa upande wa Tanzania Bara.

Ni wazi kwamba Zitto na chama chake hawawezi kuliangalia hili la mkwamo wa kisiasa kwa namna inayofanana na ile ya CHADEMA. Zitto amesikika mara kadhaa akisema mapambano haya yanahitaji mbinu mseto, ikiwemo ya mazungumzo. Kwa ACT, fursa yoyote ya kukutana na kiongozi wa nchi ni ya kuchangamkia. Ni mbinu ambayo inaifanya ACT kuwa katika sehemu ya hadhi kisiasa, kitu ambacho ni kizuri kwa ustawi wa chama.

Dhamira ya maridhiano inayosemwa na viongozi wake ni hoja inayoshawishi, lakini kamwe haiwezi kutenganishwa na dhamira ya chama kutaka kujiimarisha. Vilevile, ACT wanaamini Rais Samia ni tofauti na mtangulizi wake. Wako tayari kumpa nafasi.

Tumuelewe Rais Samia…na CCM?
Upo mjadala unaolenga kumfananisha Rais Samia na mtangulizi wake, hayati John Magufuli. Yeye mwenyewe amesisitiza mara kadhaa kwamba hana tofauti na Magufuli. Hata hivyo, upo ushahidi wa kutosha unaoonesha kwamba wawili hawa hawafanani kwa mengi.

Mfano, Rais Samia ametangaza ‘kuifungua’ Tanzania ambayo ilitiwa makufuli na Magufuli. Ameigeuza kichwa chini miguu juu sera ya UVIKO-19 ya mtangulizi wake. Katika hotuba zake kadhaa ameongelea juu ya umuhimu wa uhuru na demokrasia.

Tatizo ni kwamba baadhi ya haya anayosema bado hayajasadiki kivitendo. Ni halali kuuliza, shida ni nini? Mfano, kwa nini hadi leo kuna katazo kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, katazo ambalo liliwekwa na mtangulizi wake?

Rais Samia amesema pia, tena hadharani, kwamba hatakubali kamwe kubebeshwa mzigo wa awamu iliyopita (mtaani wanaita kuangushiwa jumba bovu!) Hii yaweza kuwa ishara ya kiongozi anayetaka kuanza upya. Akijibu ‘ombi’ la Zitto juu ya Mbowe, Rais Samia alisema yuko tayari kusikiliza, kuzungumza, na kusamehe.

Lakini huyu ni Rais Samia, vipi kuhusu chama chake? Je, Rais Samia anachukua tahadhari kupitiliza ili asije ‘akawapa’ wapinzani kilicho kingi mapema mno (giving away too much too soon)? Ni wazi chama chake hakitapenda wapinzani kufurahishwa.

Pamoja na kwamba msimamo wa chama chake kwenye masuala haya haujawa wazi, historia inaonesha kwamba CCM haipo tayari kuona wapinzani wakifurahi au kufurahishwa. Mfano, CCM na serikali zake zilizopita wamekwepa jukumu muhimu sana la kuwa na katiba mpya inayoendana na mahitaji ya mfumo wa vyama vingi. Wamekwepa wajibu huu kwa miongo mitatu!

Mara ya mwisho wapinzani walipokaribia kufurahishwa na kinachojulikana kama Rasimu ya Jaji Warioba, CCM hawakupendezwa. Kilichoendelea kinafahamika. Rais Samia analifahamu hili pengine kuliko mtu yoyote maana alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la kujadili Rasimu ya Warioba. Yawezekana hii ndiyo sababu ya kutotaka kuwafurahisha wapinzani mapema huku akiwa anajua msimamo wa chama chake.

Hitimisho
Mosi: CHADEMA na ACT-Wazalendo hawaaminiani. Pamoja na Zitto kumuunga mkono mgombea wa urais wa CHADEMA katika uchaguzi wa 2020, Lissu, na kuonesha kwa matamshi na vitendo kwamba yupo bega kwa bega na chama hicho kwenye mapambano ya kidemokrasia bado haaminiki machoni mwa baadhi ya Wanachadema.

Kuna ‘damu chafu’ baina ya Zitto Kabwe na Wanachadema hawa, kitu ambacho kama hakitatafutiwa suluhu ya kudumu kitaathiri sana harakati za vyama vingi nchini.

Kwa sasa, vyama hivi vikuu vya upinzani vinagombea fito wakati ambako wanajenga nyumba moja. Huu ni wakati wa kuratibu shughuli zao na kugawana majukumu. Kazi iliyopo mbele yao inategemea sana mbinu mseto. Tatizo kubwa ni baadhi ya wanachama wa vyama hivi kufanya mambo ya kufurahisha nafsi (egoism). Ipo nguvu inatumika kwa pande zote kuonesha kwamba upande wa pili haufai, na kwamba kukubaliana ni ishara ya udhaifu. Nguvu hii imeonekana sana kwenye mitandao ya kijamii.

Nimemsikia Zitto akisema amejitahidi sana kusahau yaliyopita na kuwataka wenzake wagange yajayo. Ni lazima pande zote mbili zijitahidi kwenye hili kwa sababu upo ulazima wa kufanya hivyo. Bahati nzuri Zitto na Lissu wanazungumza. Huu ni ukomavu wa kisiasa ambao unatakiwa ujengewe uzio na kulindwa.

Wawili hawa ni magwiji wa siasa za Tanzania ya zama hizi. Utayari wao wa kujitoa kwa ajili ya malengo makubwa ya wanamageuzi wa nchi hii utakuwa na maana kubwa. Wapambe wao wasiotaka kuona wawili hawa wakipikika chungu kimoja hawana budi kudhibitiwa kwa hoja.

Pili: Nchi yetu imepitia kipindi kigumu katika miaka ya karibuni. Zipo nyufa kubwa zinazotishia utaifa wetu. Umasikini uliokithiri na tofauti kubwa ya walio nacho na wasio nacho ni moja ya nyufa hizo. Lakini upo mpasuko mkubwa wa kisiasa baina ya chama tawala CCM na vyama vya upinzani (hasa CHADEMA na ACT).

Mpasuko huu umepelekea kuminywa kwa haki za msingi za kiraia kama uhuru wa kujieleza na usawa mbele ya sheria. Mwanazuoni nguli Issa Shivji katika insha yake juu ya utawala wa Magufuli aliandika kwamba katika historia ya nchi yetu, hatujawahi kuwa na hofu ya ukandamizaji kama ilivyokuwa katika kipindi hicho. Hii ndiyo nchi ambayo Rais Samia ameirithi toka kwa mtangulizi wake.

Wakati vyama vya upinzani vinaeleweka pale vinapotaka mageuzi ya kimfumo, Rais Samia na serikali yake hawataeleweka kwa nini watataka kuendeleza hali iliyopo. Zipo sauti za ndani na nje zitapazwa kushinikiza mageuzi. Nimewahi kuandika mahali kwamba tofauti na Magufuli, Rais Samia anaonekana kunyimwa usingizi na sauti za aina hii.

Katika muktadha huu, yeye, serikali yake, na chama chake wana wajibu mkubwa zaidi kudhihirisha nia njema waliyonayo ya kuleta maridhiano, pengine zaidi kuliko vyama vya upinzani ambavyo kimsingi bado vinaugulia “ubatizo wa moto.” Wanaweza kudhani kufanya hivi ni kujishusha kulikopitiliza na kusikokuwa na ulazima. Ni sawa, lakini kama apendavyo kusema mtu mmoja, tutaelewana tu!