Juma lililopita tulijadili kwa sauti Matokeo Darasa la 7: Je, kuna uhusiano wa Hisabati, Kiswahili na Kiingereza? Majadiliano yalifanyika kwenye chumba cha mtandao wa jamii wa Twitter/X kijulikanacho kama Spaces. Pia tuliandika makala haya: Hisabati ni Lugha ya Kigeni kama Kiingereza. Tulitumia takwimu za jumla zilizotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) na kuwasilishwa vizuri kabisa kwa picha na The Chanzo.
Kampuni ya kuchakata takwimu kwa kutumia teknolojia ya CITVAS yenye tovuti hii https://www.citvas.com na akaunti hii ya twitter @citvas sasa imezichakata takwimu hizo. Tumeshtushwa japo hatujashangazwa sana na jinsi matokeo ya mkoa wa Dar es Salaam yalivyotofautiana na mikoa mingi. Ni kwenye lugha moja tu Dar haikuwazidi wengine kivile.
Lugha hiyo siyo Kiingereza. Ni Kiswahili.
Kwa nini?
Ni kwa sababu Kiswahili ndiyo lugha ambayo Watanzania walio wengi wanaitumia. Nyumbani. Mitaani. Viwanjani. Sokoni. Hospitalini. Kanisani. Msikitini. Ndiyo, kuna makanisa yanatumia Kiingereza na Kiarabu hutumika misikitini. Lakini mawasiliano kwa kawaida ni kwa Kiswahili.
Pamoja na kuwa na lugha nyingi za makabila katika mikoa ya Tanzania, Kiswahili ndiyo lugha ambayo kiujumla Watanzania wanaielewa. Ni kweli wapo watoto wanaoanza shule kwenye vijiji vya ‘mikoani’ wakiwa wamezoea kutumia lugha za ‘kikabila’. Ila matokeo ya darasa la saba yanaonesha wengi wanakuwa wamezoea na kukielewa Kiswahili wakihitimu.
Ndiyo maana leo tumeamua kutumia dhana za kihasibu kulielezea hili. Tanzania haina nakisi ya Kiswahili. Ina bakaa. Yaani tuna Kiswahili ‘kingi’ cha kutosha kutumika kufundishia masomo.
Lakini Tanzania ina nakisi ya Kiingereza. Yaani tuna Kiingereza ‘kichache’ cha kuweza kutumika kufundishia nchi nzima. Ndiyo maana baadhi yetu tumekuwa tukisisitiza kuwa tuwekeze kwenye kujifunza Kiingereza kama lugha ya pili na/au ya Kigeni. Tufanye hivyo badala ya kudhani kwa kukitumia Kiingereza ‘kichache’ kama Lugha ya Kufundishia (LyK) basi muujiza utatokea tu na sote nchi nzima tutakijua. Ni sawa leo tuamue kutumia Kisukuma kama LyK kisa kuna Watanzania kadhaa wanakijua na kutegemea nchi nzima itakujua hima.
Grafu walizozichora CITVAS hizo hapo. Zinaonesha ukweli huu mchungu kuwa kama nchi na Taifa, Tanzania tuna nakisi kubwa mno ya Kiingereza na bakaa kubwa sana la Kiswahili.
Tutumie bakaa. Tuzibe nakisi.
Kubajeti kuko hivyo.
Ni hayo tu.