Nani atawaandikia waandishi?
KAMA nikiamua nichague kati ya kuwa na nchi yenye Vyombo Imara vya Habari na ile yenye Serikali Imara, nitachagua nchi yenye vyombo imara vya habari (Thomas Jefferson,Rais wa zamani wa Marekani)
NIMEYAKUMBUKA maneno haya mazuri ya Rais Thomas Jefferson wa Marekani aliyoyatoa zaidi ya karne tatu zilizopita lakini umuhimu wake ukiwa dhahiri hadi leo.
Na ikumbukwe kwamba wakati Jefferson akiyazungumza hayo niliyoyanukuu mwanzoni, alizungumza wakati kukiwa hakuna redio, televisheni wala mitandao ya kijamii. Leo hii, magazeti yameungana na vyombo hivyo vya kielektroniki kutengeneza himaya kubwa ya vyombo vya habari.
Lakini kuna tofauti nyingine kubwa; kwamba magazeti yaliyokuwa chanzo kikubwa cha habari wakati huo, leo hii yanaelekea kuwa si kitu tena na badala yake mitandao ya kijamii inaelekea kuwa na nguvu zaidi.
Labda niseme mapema kwamba hali hii mbaya iko kwa vyombo vyote vya habari lakini athari ni mbaya zaidi kwa vile vyombo ambavyo vilikuwa vimezoeleka (traditional media) zaidi ya hii mitandao ya kijamii (social media).
Mimi ninafahamu kwamba karibu vyombo vyote vya habari vilivyoko hapa nchini kwa sasa vimepunguza wafanyakazi wake katika lengo la kubana matumizi. Vile ambavyo havijapunguza wafanyakazi, vimeamua kuendelea kuwa na wafanyakazi wake ingawa sababu kubwa ni kwamba havina uwezo wa kulipa stahili zote za wafanyakazi wanaopunguzwa kwa mujibu wa sheria. Wafanyakazi hawa hawalipwi mishahara kwa wakati, wanaolipwa wengi wao wanalipwa ujira mdogo usiokidhi mahitaji na bahati mbaya zaidi ni kwamba watu wengi huku nje hawafahamu kwa sababu hakuna mtu wa kuandika madhila yanayowakuta wanahabari makazini kwao.
Katika kitabu chake maarufu cha Republic, mwanafalsafa mashuhuri wa Kiyunani, Plato, alipata kuhoji kuhusu changamoto ya ulinzi wa walinzi wetu. Naye Malenga wa Kirumi, Juvenal, alihoji “Quis custodiet ipsos custodies” yaani; Ni nani atatulinda dhidi ya walinzi wetu?” Leo hii, swali la namna hiyo hiyo linaweza pia kuulizwa kuhusu mustakabali wa waandishi wa habari wa Tanzania – kwamba “nani ataandika kuhusu waandishi?”
Lakini hilo ni jambo kwa ajili ya siku nyingine. Leo nijikite zaidi kwenye hali halisi ya vyombo vyetu na namna gani ya kutoka hapa.
Na nitangaze maslahi mapema. Mimi ni mwandishi wa magazeti. Hivyo, nitajikita zaidi huko kuliko kwenye vyombo vingine kwa sababu huku ndiko ninakufahamu zaidi.
Ieleweke kwamba athari za kufa kwa biashara ya magazeti haziko Tanzania pekee. Ni jambo ambalo linaumiza vichwa vya wengi katika tasnia hiyo duniani kote. Kama hakutafanyika jitihada za makusudi, magazeti mengi yatapotea katika uso wa dunia.
Tumeona hapa Tanzania namna ambavyo vyombo karibu vyote vya habari vinapitia katika wakati mgumu hivi sasa. Hali ni ngumu kwa vyombo vyote vya habari. Lakini kwa sababu magazeti ndiyo makongwe zaidi na njia yake ni ya kigeni (kusoma), hali inaonekana kuwa mbaya zaidi.
Idadi ya wasomaji imeshuka. Nayo idadi ya waandishi mahiri ambao wangeweza kuwa msaada mkubwa kuinyanyua sekta hiyo imepungua kwa sababu mbalimbali na matangazo kutoka serikalini ni kama yamekauka. Nimelielezea hili kwa ufupi katika mada yangu humu Udadisini iliyohoji: Kwa Nini Waandishi wa Safu Wanapungua?
Katika nchi ambayo, kihistoria, serikali ndiyo ilikuwa mtoaji mkuu wa matangazo, kitendo cha kupunguza matangazo kimeathiri kwa kiasi kikubwa wale waliokuwa wanategemea matangazo hayo kama chanzo kikuu cha mapato. Tanzania ni tofauti na nchi kama Kenya ambako sekta binafsi ina nguvu kibiashara kuliko serikali. Vyombo vya Kenya vinategemea zaidi matangazo kutoka sekta binafsi kuliko serikalini. Kwa Tanzania, kama nilivyoeleza, hali ilikuwa kinyume chake.
Ukiondoa matangazo, ni wazi pia kwamba vingi ya vyombo vya habari vya Tanzania havikuwa vimewekeza ipasavyo katika eneo la mitandao ya kijamii. Hadi leo, ni magazeti machache tu ambayo walau una uhakika wa kukuta toleo la mtandaoni likitoka kwa wakati.
Lakini tatizo si kuandika habari mtandaoni. Tatizo kubwa liko kwenye kufanya biashara na ubunifu unaofaa ili kukidhi kiu iliyopo. Magazeti yamezidiwa nguvu na watu binafsi na mitandao ambayo haina uwezo wa kutoa maudhui ya kutosha lakini inajua namna ya kufanya biashara.
Matokeo yake ni nini? Kuna matokeo ya aina mbili; ya kuonekana na yasiyo ya kuonekana hadharani walau kwa sasa. Lililo wazi ni kwamba mitandao inayoongoza kwa kuangaliwa na Watanzania wengi si ile ambayo inafanya uchambuzi makini wa matukio bali ni ile ambayo ina uwezo wa kutoa habari ‘chapchap’ na wakati mwingine zisizo na umuhimu wowote kwenye ujenzi wa taifa imara.
Angalia mitandao unayopenda kuitazama kufuatilia matukio na uone kama ina uhusiano wowote na kaulimbiu ya Tanzania ya Viwanda au ujenzi wa uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Ni habari tu za chapchap na vipande, ukijumlisha na umbea, ngono, ulevi na burudani za hapa na pale. Hili ni rahisi kuliona.
La pili ambalo ndilo mwenendo (phenomenon) mpya kabisa katika tasnia ya habari hapa nchini ni tabia ya makampuni ya biashara kuanza kutangaza biashara zao kupitia watu binafsi badala ya magazeti au televisheni kama ilivyokuwa zamani. Kinachofanyika ni hiki:
Kampuni X ilikuwa na mkataba wa matangazo kwa mfano na gazeti laRaia Mwema.Wakifanya uchunguzi na kubaini kwamba gazeti hilo sasa linauza nakala 70,000 kwa wiki badala ya 105,000 kama ilivyokuwa huko nyuma (huu ni mfano tu), kampuni hiyo inabadili mkakati.
Litamtafuta, kwa mfano tu, Mange Kimambi, ambaye anafuatiliwa na watu milioni tano kwenye ukurasa wake wa Instagram. Kwamba, kampuni hii inaona kwamba tangazo likitoka kwa Mange litasomwa na watu wengi kuliko likitoka kwenye gazeti linalosomwa na watu laki moja.
Kimsingi, ni nafuu zaidi kutangaza kwa watu binafsi kuliko kwenye magazeti au televisheni. Lakini, hii ni mbaya kwa sababu fedha ile iliyokuwa inaingia kwenye kampuni ya redio, luninga au magazeti ilikuwa inahudumia watu wengi zaidi badala ya mtu mmoja mwenye akaunti ya Instagram.
Hata hivyo, haya ni mawazo yangu mimi lakini inaonekana, kwa kadri muda unavyozidi kwenda, makampuni haya yanaanza kuwekeza zaidi kwa mtu mmoja mmoja badala ya kampuni kama ilivyokuwa zamani. Hivi ndivyo mfumo wa kibepari unavyofanya kazi.
Ndiyo sababu, kwa baadhi ya watu, ina maana kubwa sana kuwa na wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii. Wafuasi wengi humaanisha fedha. Yapo makampuni ambayo kwao maudhui si kitu isipokuwa wanaangalia tu ni kwa kiasi gani watu wanaingia kutazama kurasa hizo za watu binafsi.
Tunatokaje hapa?
Kuna mambo kadhaa ambayo nadhani yakifanyika yanaweza kusaidia kupunguza mserereko huu kuelekea shimoni wa vingi ya vyombo vya habari hapa kwetu.
La kwanza ambalo nadhani ni muhimu kufanyika ni kwa serikali kuamua kwa dhati kufanya tena biashara na vyombo vya habari. Nafahamu kwamba huko nyuma wapo maofisa wa serikali waliotumia vibaya upenyo wa matangazo kujiingizia fedha nyingi isivyo halali. Hata hivyo, kama mtangazaji namba moja, serikali haina budi kuchukua jukumu hili la kutoa matangazo yake kwa vyombo vya habari.
Sina sababu ya kutaja majina. Lakini kuna vyombo vya habari vikifa nchi itapata hasara. Inawezekana hasara hiyo haitaonekana kwenye kizazi hiki. Ila, tusipobadili hali hii, pasipo shaka watoto watakaotokana na kizazi hiki watarithi nchi ya hovyo.
Yule Rais wa zamani wa Marekani hakukosea alipozungumzia umuhimu wa vyombo vya habari imara. Jukumu hili la kufanya biashara na vyombo vya habari haliwezi kukwepwa na serikali mpaka pale itakapojengwa sekta binafsi imara. Kwa hali ilivyo sasa, sekta yenyewe binafsi inachechemea.
Ninafikiri pia ni muhimu kwa vyombo vya habari vya Tanzania kuanza kufikiria kama sekta nyingine za uchumi. Kwenye sekta nyingine kama benki, teknolojia, mitaji nk, ni kawaida kwa kampuni kuungana na kuendelea na biashara zake. Nchini kwetu watu wako tayari kufa na tai shingoni.
Kuna magazeti yana waandishi wa habari wazuri lakini hawana mtaji. Kuna mengine yana fedha lakini kwa bahati mbaya hayana waandishi wazuri. Hawa wawili wakiungana, wanaweza kutengeneza kampuni moja yenye mtaji na waandishi wazuri.
Zikiendelea kama zilivyo zote mwisho wake ni mbaya tu. Yenye mtaji itashindwa kibiashara kwa sababu haina maudhui mazuri. Isiyo na mtaji itafilisika kwa sababu haina uwezo wa kuchapa gazeti. Usalama wa wawili hawa ni kuunganisha nguvu.
Bahati mbaya ni kwamba hili halijawahi kutokea Tanzania walau katika kumbukumbu zangu. Hata hivyo, ukipatikana mfano mmoja na ukafanikiwa, itakuwa rahisi kwa wengine kuiga na mwisho utakuwa mzuri.
Nayaona makampuni ambayo yana uwezekano mzuri wa kuunganisha nguvu na kuwa kampuni nzuri zaidi. Lakini hili ni suala ambalo wamiliki wa vyombo hivyo kupitia jumuiya yao, yaani Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania/Media Owners Association of Tanzania (MOAT), wanaweza kushughulika nalo.
Lingine kubwa ni kufikiria uwezekano wa kufanya kazi kwa kushirikiana katika kazi kubwa na nzito za uchunguzi. Huwa napenda sana kutumia mfano wa ile kazi ya Panama Papers . Hii iliweza kushirikisha vyombo mbalimbali vya habari duniani.
Kitabia, vyombo vya habari vya Tanzania vimekuwa vikifanya kazi zake kwa kushindana kama ulivyokuwa utaratibu miaka ya nyuma. Hata hivyo, dunia inabadilika na sasa. Wenzetu wanafanya kazi kwa pamoja.
Uzuri ni kwamba, kwa kuandika michanganuo ya miradi (proposals), ziko taasisi kwa mfano Fuko la Vyombo vya Habari/Tanzania Media Fund (TMF) ya hapa kwetu, ambazo zinaweza kutoa fedha kwa ajili ya kazi zenye maslahi kwa taifa na dunia kwa ujumla. Kazi za namna hii zinaweza kufanya vyombo hivyo visaidiwe kifedha kutimiza majukumu yake na hilo litapunguza mzigo kwa vyombo husika.
Pia, vyombo vyetu vinatakiwa, pasipo shaka yoyote, kuikumbatia dunia hii ya mitandao ya kijamii. Kama Mange anaweza kupata wafuasi milioni tano, ina maana kuna vitu magazeti yetu yakifanya yanaweza kupata wafuasi milioni mbili, tatu au hata tano. Yakiweza hilo, ina maana yataendelea kuvutia makampuni kutangaza kwao badala ya kukimbilia kwa watu ambao kila kukicha wanaonesha wanakula kula, wanakunywa nini, wamelala na nani au kama wananyoa nywele zao za sehemu za siri au la.
Namna ya kufanikisha hili ni kuamua kuwekeza kwenye kupokea na kufanyia kazi ushauri wa wataalamu wa masuala haya ya mitandao ya kijamii. Ziko taasisi ambazo ziko tayari kuleta wataalamu wao katika nchi hizi zinazoendelea kufundisha namna ya kuingia katika dunia hii mpya. Wakati mwingine gharama pekee inakuwa ni muda tu wa kusikiliza mafunzo kwa sababu mengine yote yanakuwa yamelipiwa.
Lingine ni kutambua mchango wa makundi maalumu kama wanawake na vijana katika upashanaji wa habari. Sehemu kubwa ya wasomaji wa mitandao ya kijamii ni vijana na akina mama. Ni lazima maudhui yaliyomo kwenye vyombo vyetu yaangalie makundi hayo kwa jicho la pekee kabisa.
Kama una habari ambayo unajua haivutii vijana na wanawake kuisoma, ujue kabisa kwamba hapo hakuna habari. Hawa wanatengeneza sehemu kubwa ya wafuasi wa watu na taasisi katika mitandao ya kijamii. Ndilo soko lenyewe la habari hilo.
Mimi ni muumini wa dhana kwamba biashara ikiwa nzuri, vichwa vizuri vitavutiwa tu kujiunga na tasnia ya habari na wale waliokimbia wakiwa na mapenzi, wanaweza kuvutwa kurejea tena.
Lakini la kwanza, ni lazima biashara irejee kuwa nzuri.
Na ni kweli “biashara matangazo”.