Nani hasa “alimpa” Magufuli Urais?

Dastan Kweka

@KwekaKweka

Hivi karibuni, Rais John Pombe Magufuli alitoa kauli, akiwa katika ziara “ya kikazi” huko Mbeya, na kusema kuwa hakustahili kuwa Rais, bali “wananchi” ndio walioamua kumpa hiyo nafasi.

Nanukuu:

“Mlinichagua kuwa kiongozi wenu, mimi sikustahili kuwa Rais, ninyi wananchi wa Mbarali na wananchi wengine mliamua kuwa Magufuli tunampa Urais na ninafahamu mlikua na sababu za msingi za kufanya hivyo… .”

Kauli hii iliibua mijadala kiasi, hasa kwa sababu ya utata wa tafsiri ya dhana ya “kutostahili” ambayo Rais aliitumia. Utata kwa sababu kutostahili kunaweza kumaanisha:

 (i) kukosa sifa au vigezo vya kushika nafasi husika;

 (ii) unyenyekevu, hasa kwa kuashiria hadhi ya juu ya nafasi husika (Urais);

(iii) ukuu wa wananchi, kwa maana ya wao kuwa chanzo cha mamlaka ya serikali. 

Je, Mheshimiwa Rais alikua akirejea maana ipi kati ya hizi?

Katika kauli yake, Rais alitamka kuwa wananchi ndiyo walioamua kumpa Urais. Maana yake ni kuwa, wao ndio waliomchagua, miongoni mwa wengi walioitaka nafasi hiyo. Hata hivyo, katika mfumo wetu wa uchaguzi, vyama huchagua na kusimamisha wagombea, kisha kuwanadi kwa wananchi, wakiwashawishi na kutarajia chaguo lao litaungwa mkono. 

Isitoshe, kutokana na “kutamalaki” kwa chama tawala nchini – Chama cha Mapinduzi (CCM) – mtia nia ambae huteuliwa na CCM kugombea, hasa katika kiti cha Urais, huwa kama Rais ambaye anasubiri kuapishwa tu. Maana yake ni kuwa, linapokuja suala la nani anakuwa Rais, CCM ina kura ya turufu (katika muktadha wa kutamalaki kwake), kama “alivyo nayo mwananchi.” 

Swali la msingi hapa ni: 

Je, kwa nini Rais hakusema ni chama ndicho kilichompa Urais?

Mchakato wa kumpata mgombea wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi, katika uchaguzi wa mwaka 2015 uligubikwa na mengi, na kujeruhi wengi. Miongoni mwa walionekana kujeruhiwa, hasa kwa kuzingatia ukali wa maoni yake, ni Mzee Hassan Nassoro Moyo, ambae alivuliwa uwanachama kabla hata ya uchaguzi Mkuu. Yeye, baada ya kutokea ambayo hakuyatarajia, hakukaa kimya.

Alinena: 

“Viongozi wetu walikua na watu mfukoni, wakaona wamchukue yeyote barabarani. Unawezaje kumteua mtu ambaye hajawahi kuwa hata balozi wa nyumba 10? Je, anaijua misingi ya chama? Anakijua Chama? Anatosheleza?”

Kauli ya Mzee Moyo iliashiria uwepo wa viongozi katika chama tawala ambao walikua na nia ya kumteua mgombea waliyemtaka. Pia alituhumu kuwa walifanya hivyo, kwa kukiuka kanuni. Lakini, je, inawezekana kikundi cha viongozi ndani ya CCM kikawa na ushawishi kwa kiwango cha kuweza kumteua mgombea wa Urais kinayemtaka, mbali na kwamba Mkutano Mkuu wa chama ni mkusanyiko wa wajumbe kutoka nchi nzima, na wenye masilahi na machaguo ambayo hayashabihiani mara zote? 

Mbali na hoja za kimchakato, Mzee Moyo alihoji kama mgombea wa CCM alikua “anastahili” kwa kukosoa historia yake ya uongozi katika chama, labda kwa lengo la kusisitiza hoja ya ukuu wa chama.

Katika juhudi za kujibu baadhi ya manung’uniko ya wanachama wenzake, kama Mzee Moyo, Rais wa wakati huo – Jakaya Mrisho Kikwete – alizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni za Urais za CCM Mkoani Mwanza, na kusema yafuatayo (kuanzia dakika ya 6:02 mpaka 6:06):

“Mwenyezi Mungu akitaka lake linakuwa.”

Kisha kuanzia dakika ya 7:40, Kikwete anasikika akisema:

 “Kura zilimwangukia Magufuli.” 

Ukisikiliza hiyo hotuba, utaona kuwa Rais (mstaafu) Kikwete, alitumia lugha ya kukubali matokeo. Lugha inayoonesha kutokuwa na ushawishi (wa kutosha?) katika mchakato wa kumpata Rais (Magufuli). Kwamba, aliyemtaka Rais Magufuli ni Mwenyezi Mungu.

Je, hii ni ishara kuwa Magufuli hakuwa miongoni wa “watu” ambao viongozi waliokua nao “mfukoni”, na hivyo Mzee Moyo hakuwa sahihi?

Katika hotuba ya Rais wa awamu ya 5 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli, aliyoitoa mara tu baada ya kuapishwa, alimshukuru sana Rais Mstaafu Kikwete kwa kusema yafuatayo (kuanzia dakika ya 9:48 na kuendelea):

“Kama haitoshi, mzee huyu akiwa mwenyekiti wa CCM akanipa nafasi na dhamana ya kupeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya Urais.”

Je, kura za Urais, na hivyo Urais, “ulimwangukia” Magufuli, kwa kudra za Mwenyezi Mungu, kama alivyosema Rais (mstaafu) Kikwete, au ni Kikwete “alimpa” kama asemavyo Magufuli, na alivyotuhumu Mzee Moyo?

Hata hivyo, katika hotuba hiyo hiyo, Rais anasikika akizungumza yafuatayo kwa unyenyekevu mkubwa (kuanzia dakika ya 10:03):

“…. mimi Magufuli ni nani hata wanione na kuniamini kati ya wengi. Kwa kweli sina cha kuwalipa wazee wangu hawa (Mkapa na Kikwete) zaidi ya kulinda heshima yao, na imani yao kwangu.”

Katika nukuu hii, Rais anaibua dhana ya “kutokustahili”, ingawa kwa namna ambayo siyo ya moja kwa moja, na kuashiria kuwa, wako wengi ambao wangeweza kupewa nafasi ambazo yeye amezishika katika safari yake ya uongozi.

Je, Mheshimiwa Rais anapozungumzia “kupewa” Urais anarejea maana ipi hasa? Ya Mzee Moyo, ambaye hakumuona ana vigezo (vya kutosha)? Au ya Rais mstaafu – Kikwete – ya kwamba kura “zilimwangukia”, na hivyo ni ushindi wa bahati, ambao wananchi waliufanya “stahili” baada ya kuuhalalisha kwenye kura, na hivyo kustahili shukrani?

Na inawezekana ni Mwenyezi Mungu alitaka lake liwe, maana “wakati wake (Magufuli) ulikuwa umefika”, ikiwa tutaazima busara ya Mzee Thabit Kombo, akimshauri Kikwete, na kumsihi awe na subira, miaka mingi kabla ya kufanikiwa kutimiza ndoto yake, miaka kadhaa baadaye.

Sisi ni nani hasa hadi tustahili kufahamu Mheshimiwa Rais alikuwa na maana gani?

Na, pengine, kama asemavyo January Makamba, mgombea mwingine ambaye wakati wake ulikuwa bado haujafika, “Mungu humpa ampendaye. Mungu humnyima ampendaye.”

Hatelezi.