Tarehe 28 Oktoba 2020, mimi ni miongoni mwa Watanzania wengi tuliopiga kura. Na tena nilikuwa miongoni mwa watu wa kwanza, kwanza kufika kituoni. Siku hiyo nakumbuka nilikuwa kituoni saa moja kasorobo asubuhi. Mpaka ilipofika saa moja unusu nilishamaliza kupiga kura yangu kwa raisi, mbunge na diwani.
Nilipokuwa kituoni, niliona kwa macho yangu kuanza kupigwa kwa kura bila mawakala wa vyama vya upinzani. Eneo nililopigia kura lilikuwa na vituo 9, nilipouliza huku nikaambiwa hawajafika, kule nikaambiwa hawana barua n.k. Kama Watanzania wengi, nikapiga kura yangu hivyo hivyo tu.
Kisha nikapiga selfie, nikaposti kwenye mitandao ya kijamii, nikaenda kunywa supu, nikarudi nyumbani. Sikubaki kulinda kura kama tulivyoombwa. Wala sikufanya jitihada yoyote kuhakikisha mawakala wanakuwepo vituoni.
Usiku wa tarehe 28 niliamua kulala mapema badala ya kushindwa kuhimili majuto na hasira nilizokuwa nazo. Ripoti za mawakala kuondolewa vituoni, kura feki kukamatwa, na kadhalika vilinifanya nipate msongo wa mawazo. Kilichoniumiza sio kwa nini vitendo hivyo vinafanyika, ila kwa nini tunaacha vitendo hivyo vifanyike. Why  can’t we do anything about it?
Maana wote tulijua kwa yakini kuwa haki itaporwa. Na bado tukaiacha iporwe. Iliniumiza.
Usingizi ulikata majira ya saa tisa usiku. Kuingia kwenye mitandao nikakutana na habari za matokeo ya jimbo la Hai. Niseme ukweli, moyo wangu ulikufa ganzi, felt numb.
Siku hiyo hiyo ya tarehe 29, nikafanya safari kurudi kituo changu cha kazi, maana nilisafiri kwa ajili ya kupiga kura. Jioni ya siku hiyo, nikaanza kuhisi kale ka-weird feeling ka ‘I told you so’ kwa miaka 3. Niliitwa alarmist, niliambiwa nina hasira, nazidisha chumvi, mambo si mabaya kama ninavyoamini, n.k.
Maumivu ya kupoteza marafiki na kuondoka kwenye jumuiya niliyokuwa nayo pamoja kwa zaidi ya miaka 10 kwa sababu tu ‘am alarmist’ yakayeyuka kama theluji jangwani maana kuna kipindi nilianza kujihisi labda mimi nina tatizo, labda mtazamo wangu sio sahihi. Lakini siku ile dunia iliona kile tulichokuwa tunakihofia kwa miaka 3. Nasikitika kusema, it can get worse, and the worst happened!
Alfajiri ya tarehe 30, nilipokuwa kwenye mkeka nikisali, ndipo nikaanza kusikia maumivu makali ya dhulma iliyotokea. Nikaanza kujiuliza, what does this mean to our democracy? And more so to the future of my 3 kids? Sasa tumerudi kwenye chama kimoja na demokrasia imekanyagwa.
Zaidi nikawaza, kama sauti ya umma kwenye uchaguzi imezimwa, je miaka 5 ijayo tutaruhusiwa hata kukohoa? Kitu kilichonipa faraja ni imani kuwa kwa kuwa Watanzania wameona yaliyotendeka basi sasa tutaichukua haki yetu. Pia niliamini kuwa kuwaondoa viongozi wote manguli wa upinzani ni bad move – kuwaleta mtaani kutachochea vuguvugu na kutafuta haki itakuwa both ‘a collective and personal fight.’
Nakumbuka niliuliza kwenye ukurasa wa twitter, kuwa je tumefika hicho kinachoitwa ‘tipping point’. Wengi walinijibu bado. Niliumia. Nilikaribia kupata kichaa nilipoona watu wanabeza wapinzani, wamekubali matokeo, na wanataka maisha yaendelee.

Most urged Tanzania cant change unless we get to what is known as “tipping point” is this it? Au bado?

— Mwanahamisi Singano (@MSalimu) October 29, 2020

 

Kwa viongozi wa upinzani hawakutaka maisha yaendelee. Walikuwa very clear kuwa huu ulikuwa uchafuzi, haki imeporwa na walionesha msimamo wao bayana bila woga. Wao kama viongozi wakasema kwa kauli moja wako tayari kuongoza maandamano ya amani, Watanzania wadai haki yao. Kabla ya maandamano, viongozi wakakamatwa, wakalala ndani na maandamano hayakutokea.
Binafsi yangu, suala la maandamano lilinitia woga mno maana moyo wangu ulikuwa na hakika kuwa hakuna atayeandamana na hili litawavunja moyo sana walioitisha maandamano na zaidi, anguko hilo litatumika kama kejeli kwa miaka 5 ijayo. Na kweli, nobody showed up, zaidi ya shujaa wangu mama Ananilea Nkya na wapinzani wachache.

Each Tanzanian must stand firm but PEACEFULY to demand fraudulent election held on 28/10/2020 be nullified.Short of that our country shall never have genuinely elected leaders in the future. My heart is bleeding to see this cruel way of rigging👇an election. pic.twitter.com/goRwpyIHpA

— Ananilea Nkya (PhD) (@AnanileaN) November 2, 2020

Kimsingi, Watanzania wote tumekubali matokeo, maisha yaendelee. Simba na Yanga zinacheza kwa raha zao. Mashabiki tunafurahia burudani huku wenzetu wakiendelea kuugulia na kulia huko Pemba na kwingineko.
Niseme kwa dhati ya moyo wangu, nawaheshimu mnoooo wanaupinzani wote, hasa waliosimama kwenye uchaguzi wa mwaka huu, na waliodumu kwenye siasa za upinzani kwa miaka mitano. Mmefanya kazi kwenye mazingira magumu mno. Mmejitoa sana, na kwenye uchaguzi huu mmefanya kila linalowezekana kibinadamu na kwa mujibu wa sheria. Tuna deni kwenu.
Hivyo hivyo naamini pia Watanzania wamejitoa sana pia kutetea uhuru wetu. Wamefanya kampeni kwa nguvu kubwa. Wamejitokeza kupiga kura kwa wingi. Wamejitolea kuwa mawakala, na wengine hasa visiwani wamepoteza uhai na viungo vyao kwa sababu ya demokrasia yetu.
Tunapopishana ni kwenye what’s next – viongozi walisema uchaguzi hawautambui, Watanzania wadai tume huru ya uchaguzi na uchaguzi mpya kupitia maandamano ya amani nchi nzima. Sisi tukawajibu kwa vitendo, kuwa tumekubali matokeo, uchaguzi tunautambua, kwa hiyo hatuandamani. Viongozi nao ni binadamu, wana mioyo sio mawe, mengine wapunguziwe. Nao wana hisia, wanaumia, wana nyongo, wana damu na mishipa ya fahamu.
Mimi binafsi, najua siku niliyoshindwa kuingia barabarani kupinga matokeo ndio siku niliyojivua uhalali wa kuhoji maamuzi yao, from there on. Ndugu zangu, we can’t have our cake and eat it.

 

Kwangu mimi, nimeamua kuwaelewa. Nitaunga mkono maamuzi yao yote. Wakiamua kuacha siasa, nitawaelewa, they did their part, wakiamua kukomaa, nitawaelewa pia, we need heroes and heroines. Wakitaka kwenda uhamishoni, nitawaelewa na kuwatia moyo, kila mtu ana haki ya kuishi kwa uhuru na amani. Wakibaki kupambana, nitawapa support angalau kwa kidogo nitachojaliwa. Wakiamua kupeleka wabunge itakuwa sawa kwangu, wakisusia pia itakuwa sawa.
Mimi naamini, baada ya yote yaliyotokea kutokea, tunatakiwa kuwatia moyo, kusimama nao kwa shida na raha. Ni muhimu mno kwetu sote kujua, kama tunataka kujipa haki ya kufanya maamuzi kwa ajili yao, tujipe pia wajibu wa kusimamia utekelezaji wa hayo maamuzi. Mimi binafsi, kwa kipindi hiki, na katika muktadha huu, naziamini busara zao.
Nawaelewa.