Kwa kiasi cha nifahamuvyo, Kiswahili fasaha na sanifu ni kusema maiti huyu – kama ambavyo twasema mtu huyu au mwanaadamu huyu. Kwa sababu, kama alivyoeleza mwenzetu, Eric Mnene, mwanaadamu hata akifa bado hubaki kuwa ni mwanaadamu ingawa roho yake imetengana na mwili wake. Na kulingana na utamaduni wa lugha ya Kiswahili, huko kufa hakumpokonyi mwanaadamu huyo cheo chake cha ubinadamu. Chembelecho Eric, mtu huyo aliyekufa “hageuki kuwa kitu kwa sababu ya mauti.”

Hata hivyo, twawaona au kuwasikia watu wengine wakiandika au wakisema maiti hii, na wingi wake kuwa ni maiti hizi. Au kuandika na kusema maiti itazikwa, na kadhalika. Yangawa hivyo, hicho si Kiswahili fasaha wala si sanifu. Na matumizi hayo yampokonya huyo maiti utu wake, na badala yake kumtia katika kundi la vitu ambavyo katika sarufi ya Kiswahili vimo kwenye ile ngeli ambayo pia huitwa Ngeli ya N: kwa mfano, vitu kama vile nyumba hii/hizi, ndizi hii/hizi, kalamu hii/hizi, treni hii/hizi, na vyenginevyo kama hivyo.

Kumetolewa huja (hoja) tatu na baadhi ya wenzetu kuthibitishia matumizi hayo, ambayo twasema kuwa si Kiswahili fasaha wala si sanifu hicho. Huja ya kwanza iliyotolewa ni kwamba huyo aliyekufa hana tena uhai. (Ali Mugenzi). Kwa hivyo, si sawa kusema maiti huyu. Yaani neno hilo huwa halimo tena katika lile kundi la ngeli itumiliwayo wanaadamu, wanyama na wadudu.

Huja ya pili ilikuwa ni kwamba huyo aliyekufa aweza akaendelea kutumiliwa hiyo ngeli ya wanaadamu lakini iwapo tu kama kutatumiwa neno marehemu badala ya maiti. (Solombi) Yaani, kwa mujibu wa Solombi, ni sawa kusema marehemu huyu, lakini si sawa kusema maiti huyu. Lakini huja hii haisimami, kwa sababu huyu marehemu naye pia hanao tena huo uhai; na neno hili pia lina asili ya lugha ya Kiarabu kama hilo maiti. Kwa ufupi, basi, huja hizi mbili zitakuwa zishajibika kwa tuliyoyaeleza hapa juu: kwamba, kwa utamaduni wa Kiswahili, hilo la kutokuwa na uhai halimpokonyi mwanaadamu huyo ubinadamu wake.

Huja ya tatu iliyotolewa ya kutilia nguvu matumizi ya maiti hii, ni kuwa hili neno maiti liliingia baadaye katika Kiswahili kutoka lugha ya Kiarabu; na kwamba neno mwili “ndilo lililokuwepo kabla Wapwani kuamua kutumia neno la Kiarabu, maiti.” (Jumbe Omar). Itakuwa vyema tukijulishwa ni sehemu zipi za Pwani ya Afrika Mashariki ambako neno mwili ndilo lililokuwa likitumiwa kabla ya neno maiti kuingia katika Kiswahili. Nijualo ni kwamba katika baadhi ya maeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki, maneno yaliyokuwa yakitumiwa kabla ya neno maiti kuingia katika Kiswahili, yalikuwa ni mfu na kimba (kwa mtu aliyekufa); na nyamafu, kibudu au mzoga (kwa mnyama).

Matumizi ya makosa ya maneno kama hilo maiti, zaidi yametokana na kuongezeka kwa idadi ya wazungumzaji wa lugha hii kutoka maeneo mbalimbali ya nchi zetu. Na makosa kama hayo yanaporudiwarudiwa na watu wengi, baadaye huja yakaonekana na watu wengine kwamba ndiyo sahihi. (Kwa mfano, neno jengine litumiwalo na baadhi ya watu siku hizi, na linikeralo sana, ni “umauti” badala ya mauti – ambalo ndilo lililo sahihi na sanifu. Labda wasemao hivyo wameona kuwa kwa vile kinyume cha neno hilo, yaani uhai, laanza kwa u-, basi wakafikiri na hilo nalo pia liongezewe kiambishi u-).

Kutokeapo hitilafu na utatanishi wa matumizi ya maneno, pendekezo langu huwa ni kuyatizama maneno hayo jinsi yalivyotumiwa katika methali, misemo na nyiso. Mara nyingi mwahali kama humo utayakuta maneno yametumiwa kama yalivyokuwa yakitumiwa kabla hayajavurugwa. Kwa mfano, katika hizi methali maarufu zihusianazo na maiti, twaona kuwa neno hilo limetumiwa kulingana na sarufi ihusianayo na mwanaadamu aliye hai:

Adhabu ya kaburi aijuaye ni maiti – (si iijuayo)

Maiti akiwa atoka/ (atolewa), kilio huzidi – (si ikiwa inatoka/inatolewa)

Maiti haulizwi/hapatilizwi sanda – (si haiulizwi/au haipatilizwi)

Makamusi ya Kiswahili Sanifu ya nyakati zetu hizi pia yamelieleza neno maiti, kwa ngeli hiyo hiyo itumiliwayo mwanaadamu aliye hai. Kwa mfano, tizama Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Toleo la Pili), Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Dar es Salaam, Oxford University Press, 2004; Kamusi la Kiswahili Fasaha, Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), Oxford University Press, 2010; Kamusi Kuu ya Kiswahili, Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Longhorn, 2015; Kamusi Elezi ya Kiswahili, The Jomo Kenyatta Foundation, 2016.

Tumeshaelezwa kuwa maiti ni neno lililoingia katika Kiswahili kutokana na lugha ya Kiarabu. Hapa nataka kuongeza kuwa neno hili liliingia katika Kiswahili kutokana na athari ya Uislamu pia. Na katika dini hii, kuna mambo mane ambayo Mwislamu akifa ni lazima afanyiwe; ni haki yake: aoshwe, akafiniwe (avikwe/avalishwe sanda), aswaliwe na azikwe. Nimevipitia vitabu vine vya madhehebu mbalimbali ya Uislamu vinavyoeleza mambo ya kumfanyia maiti.*

Maelezo yaliyomo katika vitabu vyote hivyo yanamwashiria maiti kwa ishara kama zitumiwavyo kwa mtu aliye hai; kwa mfano: kumwosha, kumkafini, kumswalia, kumzika (wala si kuiosha, kuikafini, kuiswalia, kuizika). Nimezipitia pia tafsiri tano za Kiswahili za Qur’ani na kuziangalia Aya zilizomtaja maiti zimefasiriwaje.** Katika tafsiri zote hizo, neno hilo limetumiwa kama litumiliwavyo kwa mwanaadamu aliye hai.

Kwa ufupi, yote hayo tuliyoyaeleza hapa juu yatuthibitishia kuwa vilivyo sahihi, fasaha na sanifu ni kusema maiti huyu wala si maiti hii. Basi, chembelecho ule msemo wa Kiswahili, “Farasi ni hawa, na nyangwa ni hizi!”

*Vitabu vyenyewe ni Mambo Anayofanyiwa Maiti, cha Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy (1968); Vipi Uzike Maiti, cha A. Suleiman; Muongozo Katika Mazishi, cha Bakir Muhammad Rashumi, (kimefasiriwa kwa Kiswahili na Masoud Abbas kutoka Kiarabu); na Mambo Yanayomhusu Maiti, cha Sayyid Muhammad Mahdi (1976).

** Nazo ni Qur’ani Takatifu, Sheikh Abdullah Saleh Al-Farsy, The Islamic Foundation, Nairobi, (1969 na 1993); Qur’ani Tukufu: Aali Imran – An-Nisaa, Sheikh Al-Amin bin Aly Mazrui, Shungwaya Publishers, Nairobi (1981); Tarjama ya Al-Muntakhab Katika Tafsiri ya Qur’ani Tukufu, Ali Muhsin Al-Barwani (2006); Qur’ani Tukufu, Tarjama ya Kiswahili ya Hassan Ali Mwalupa, kutoka Kiarabu, ya Tafsir Al-Kashif ya Sheikh Muhammad Jawad Mughniyah, Al-Itrah Foundation, Dar es Salaam (2012); na Qur’an Tukufu, imefasiriwa na Jumbe Omar Jumbe, Centre for Peace and Spirituality, New Delhi, India (2022).