Hivi karibuni nilitumiwa makala iliyokuwa ikieleza juu ya unyakuzi wa ardhi kwa ajili ya kuzalisha mazao yanayotumika kutengeneza nishati uoto (biofuels) kaskazini mwa Ghana. Katika makala hiyo, Bakari Nyari (Vice Chairman of Regional Advisory and Information Networks Systems RAINS), anaelezea juu ya Kampuni ya nishati uoto ya Kinorway na namna kampuni hii ilivyofanikiwa kumrubuni Chifu wa eneo hilo kwa kutumia mbinu ile ile iliyotumiwa na Karl Peters kwa Chifu Mangungo wa Msovero.

Kama ilivyo nchini Tanzania, msukumo wa kuelekea katika nishati mbadala umetokana na masuala ya kiuchumi na mabadiliko ya hali ya hewa katika dunia. Kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na mabadiliko hasi ya hali ya hewa duniani vimechangia kwa kiasi kikubwa wimbi la utafutaji nishati mbadala ili kukabiliana na uchafuzi wa hali ya hewa na pia kuleta uhuru katika matumizi ya nishati. Bila kuwa na mikakati madhubuti na sera za kushughulikia suala hili nchi za Kiafrika zimejikuta zinaingia katika mchezo ambao hazikushiriki katika maandalizi yake.

Katika makala hiyo ndugu Nyari anaeleza kwamba Kampuni hiyo inayojulikana kwa jina la Biofuel Afrika (Nishati uoto Afrika) ambayo ni tawi la Biofuel Norway ilijipatia umilki wa jumla ya hekta 38,000 baada ya kumrubuni Chifu wa eneo hilo aliyesaini makubaliano hayo kwa kidole gumba! Baada ya kuisoma makala hiyo nilijifunza mambo mengi hasa nikifananisha mazingira ya Ghana na Tanzania ama walau eneo hilo na aina ya mbinu zilizotumika kuwafanya wakazi wa eneo hilo na Chifu wao kukubali kutoa ardhi yao kwa ajili ya kuzalisha Jatropha (Mibono).

Jambo la kwanza nililojifunza ni kwamba kuna athari za kimazingira kwa jamii hasa katika maeneo ya vijijini. Mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha mfumo wa mvua usiotabirika umeongeza ugumu wa maisha kwa jamii zetu hasa vijijini. Kutokana na hali hii na kukosa msaada kutoka serikalini jamii katika maeneo ya vijijini zimejikuta katika hali ya kuvutwa na ahadi za uongo kutoka kwa yeyote anayeweza kuahidi miujiza ya kuwatoa katika matatizo yanayowakabili. Kwa mfano, nilipata fursa ya kuongea na wakazi wa Kisarawe katika kijiji cha Mtamba ambapo nilitaka kujua vigezo vinavyotumika katika kugawa ardhi ya kijiji. Kwa mujibu wa wajumbe hao wa serikali ya kijiji, wao hutoa ardhi kwa mtu anayeweza kutatua sehemu ya matatizo yanayowakabili kwa mfano kama wana tatizo la maji, shule, zahanati barabara, n.k mwombaji akijitolea kujenga ama kisima cha maji ama nyumba ya mwalimu anapata ardhi bila kipingamizi chochote. Katika mazingira kama haya ni rahisi sana kwa wanavijiji kurubuniwa kutoa ardhi.

Pili, nimejifunza kuwa mashabiki wa nishati uoto wanatumia kisingizio cha ajira na kipato. Hii imekuwa ni mojawapo ya silaha inayotumiwa na wawekezaji walio wengi, ukiachilia mbali ushawishi wao kwa serikali juu ya ajira watakazozalisha na kipato kitakachopatikana kwa maana ya kodi kwa serikali. Hivyo, inakuwa ni rahisi zaidi kwao kuwashawishi wanavijiji juu ya suala zima la ajira na kipato kwa maana ya soko kwa mazao yao ama bidhaa mbalimbali wanazozalisha. Katika nchi yetu mbinu hii ya kurubuni kwa maana ya kutoa ajira na ongezeko la kipato imetumika katika maeneo mbalimbali. Kwa mfano, katika Wilaya ya Rufiji wanavijiji katika vijiji vinavyopakana na hifadhi ya Seleous na vinginevyo kwenye ukanda huo waliahidiwa ahadi za ajira na kipato pindi watakaporidhia kutoa maeneo yao kwa kampuni ya nishati uoto kwa jina la SEKAB. Mheshimiwa Rais katika ziara yake katika kijiji cha Mloka, mojawapo ya vijiji vilivyopokea ma ombi ya ardhi kutoka katika kampuni hii kwa lengo la kuzalisha mazao ya nishati uoto, alirudia dhana hii ya ajira na kipato na pia kuimarishwa kwa miundombinu pindi wawekezaji watakapoanza uzalishaji!

Pamoja na ahadi hizo katika baadhi ya vijiji, serikali za vijiji kupitia kwa Mkutano mkuu wa kijiji wamekataa kuridhia maombi hayo mpaka vijiji vyao vipimwe na waweze kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi. Swali la kujiuliza ni je wataweza kupingana na nguvu hizi na vishawishi hivi mpaka lini ili hali Serikali kuu imeridhia juu ya suala hili?

Tofauti kati ya uzoefu wa Tanzaniana wa Ghana kama ulivyotolewa katika makala niliyoitaja hapo awali ni kwamba Serikali kuu yao imeridhia lakini haijajihusisha moja kwa moja katika kufuatilia utekelezwaji wa makubaliano hayo na makampuni. Kama tunavyoshuhudia, kwa upande wa Tanzaniasuala hili limepewa kipaumbele na serikali. Katika mustakabali huu haki za wazalishaji wadogo kama wakulima na wafugaji zitapewa ulinzi unaohitajika? Kulingana na matamshi ya viongozi wetu inaonekana hiyo ndio picha wanayotaka sisi kama wananchi tuiamini, lakini hali ya mambo sivyo ilivyo!

Wakati ambao serikali inajinasibu kwamba ipo katika kuandaa sera kwa ajili ya nishati uoto tayari makampuni ya kigeni na ya ndani yapo katika hatua mbalimbali za kujipatia ardhi kutoka katika vijiji na mashamba yaliyokuwa chini ya serikali na yaliyopona kubinafsishwa! wakati tunafahamu kabisa kwamba sera ndio dira, mwongozo utakaoelekeza nini kifanyike, kwa namna gani na kwa malengo yepi hata haujaandaliwa tayari ardhi ya vijiji kumi na moja katika wilaya ya Kisarawe itahaulishwa na vijiji husika itabidi kupisha mwekezaji, kwa jina la SUN BIOFUELS, ambayo ni kampuni ya nishati uoto ya Kiingereza. Vilevile tayari makampuni mbalimbali yapo katika mikoa tofauti hapa Tanzania na mengine yalishaanza uzalishaji. Bila shaka ushauri wa GTZ hapa ndio uliozingatiwa, yaani mchakato wa kujifunza kwa kutenda (learning-by-doing process) ukurasa wa 122 (Liquid Biofuel for Transportation in Tanzania GTZ Report 2005).

Athari za hali hii zimeanza kujitokeza ambapo baadhi ya wawekezaji katika mashamba makubwa ya mpunga nao wamevutiwa na nishati uoto na hivyo wanakusudia kuacha mazao ya asili katika maeneo waliyochukua. Hii imejitokeza katika shamba la Kampunga katika wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya. Ikumbukwe kwamba shamba hili lilibinafsishwa katika mazingira ya upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi walioomba Serikali iwaruhusu waendelee kuzalisha mpunga. Serikali haikuwa na muda wa kusikiliza kilio hicho pamoja na sauti za wadau mbalimbali. Leo hii kuna mawazo ya kwamba makosa yalifanyika katika ubinafsishaji wa shamba hilo. Wadau walio wengi wakiwemo wasimamizi wa bonde la mto Rufiji wanaishauri serikali ipitie mkataba wake na mwekezaji huyo na ikiwezekana warudishiwe wazalishaji wadogo waliokuwa katika shamba hilo wakati likiwa chini ya usimamizi wa NAFCO.

Katika mazingira ya sasa duniani ambako tunasikia juu ya ongezeko la bei ya chakula, je katika fikra za watunga sera wetu kuna hata mmoja anayefikiria kwamba kama tukizalisha chakula cha kutosha tunaweza kupata soko la uhakika na tukapiga hatua mbele? Mbona kwa Marekani mojawapo ya silaha kubwa huwa ni chakula? Ama katika kuiga utamaduni wa kitandawizi hili la uzalishaji wa chakula halina mashiko? Wazalishaji wadogo ni moja tu kati ya makundi ambayo yapo katika wakati mgumu kwa sasa juu ya uwekezaji katika nishati uoto. Mwelekeo wa makampuni yaliyo mengi ni kujinyakulia ardhi za vijiji na sio vinginevyo. Hivyo ni vyema tukaelimishana kuwa suala la kutoa matumaini yasiyo na msingi ili kuwafanya wananchi waishi kwa matumaini ya kupata faida kubwa kutokana na nishati uoto halipo. Ushahidi unaonyesha kwamba wawekezaji wengi macho yao yapo katika kujitwalia ardhi za vijiji kwa ajili ya faida zao binafsi.

Mwandishi: Bernard Baha