Ni wiki yangu ya tatu sasa nimekaa ndani naiangalia dunia kupitia dirisha langu la ukumbini huku nikitamani kutoka lakini wapi. Si jambo rahisi kukaa tu ndani na kuzunguka sehemu hiyo hiyo mara elfu, unatoka chumbani, ukiingia sebuleni, mara jikoni na msalani. Utatafuta kila jambo la kufanya, kuanzia kusoma vitabu, kujipikisha, hata kusakata rumba ilimradi siku ipite.

Jambo ambalo halikwepeki hasa kwa kazi yangu pia ni kusoma na kuangalia habari siku nzima. Bahati mbaya sana kila unapotazama TV, kusikiliza redio na mitandao ya kijamii hakuna taarifa yoyote kubwa zaidi ya COVID-19 duniani kote. Ni corona kila kona.

Unaweza kusema ni bahati nina uwezo wa kufanya kazi nyumbani maana si kazi zote zinaruhusu kukaa ndani. Japo nashindwa kuwasilisha habari kama ilivyo ada kwa mtangazaji lakini haimaanishi huwezi kuchangia katika kazi yako. Utaratibu tu unabadilika.

Mchango wangu kwa sasa ni kusaidia katika kuandaa taarifa mbalimbali zinazotoka hewani. Teknolojia imesaidia sana, si haba, kwani mawasiliano ya timu yetu nzima ya Dira ya Dunia TV tunaifanya kupitia simu kwa kutumia pia programu tumishi ya Zoom. Hapo ndio fursa ya kufanya mikutano yetu na kujadili taarifa za siku.

Haya mabadiliko baadhi ya watu wanashindwa kuyaelewa na kuyahimili. Pia baadhi ya viongozi hushindwa kubadilika, kila mmoja akiwa na sababu zake. Lakini MABADILIKO ni lazima kama tunataka kuvuka salama katika janga hili la maradhi haya yanayosababishwa na virusi vya corona. Virusi hivi, kama tujuavyo, vilianzia nchini China na kusambaa kwa kasi ya ajabu hadi karibu kila nchi duniani, huku mataifa mengine yakiathirika kuliko mengine.

Kwa hapa nilipo nchini Uingereza, athari ya virusi vya corona imekuwa kubwa sana miongoni mwa nchi za bara la Ulaya. Kwa taarifa za mpaka tarehe 24 Aprili, 2020 watu waliokufa kutokana na virusi hivyo mpaka sasa ni 18,791 na hao wengi wao ni ambao wamepoteza maisha hospitalini. Bado kuna waliokufa nyumbani na nyumba za kuwatunzia wazee ambazo hazijajumlishwa. Hata hivyo serikali inasisitiza kuwa itafanya jitihada kuweza kupima watu 100,000 kwa siku japo chama cha Labour kikitilia shaka suala hilo.

Idadi hiyo inayokaribia elfu 20 imezua mjadala kwa wingi hapa Uingereza vikiwemo vyombo vya habari. Magazeti kadhaa kama ya Times na The Guardian yamerushia lawama moja kwa moja kwa Waziri Mkuu, Boris Johnson kwa kutoipa uzito athari ya kusambaa kwa virusi hivyo tangu mwanzo na kwamba alichelewa kuchukua hatua stahiki. Mwanasafu mmojawapo wa gazeti la The Guardian anasema raia wa Uingereza hawatosahau namna ambavyo Waziri Mkuu huyo ndio kwanza alienda likizo ya wiki mbili huku virusi vikiendelea kusambaa na pia namna alivyojigamba kusalimiana kwa mikono na waathirika wa virusi hivyo Machi 3.

Pia anatuhumiwa kupoteza siku 38 kabla ya kuchukua hatua thabiti na kwamba alichukulia kuwa China iko mbali hivyo virusi hivyo haviwezi kufika Uingereza. Waziri Mkuu huyo pia analalamikiwa kwa kushikilia sera ya Herd Immunity (Kinga ya Kundi) iliyojikita katika imani kuwa kasi ya maambukizi itapungua baada idadi kubwa ya watu kuambukizwa na hivyo wengi wao kujengea kinga dhidi ya kirusi. Sera hiyo tata inaonekana kushindwa vibaya Uingereza na hivyo kusababisha mabadiliko ya kisera ya namna ya kukabiliana na janga hilo la COVID-19.

Baada ya kusuasua kiongozi huyo alichukua hatua yake kubwa ya kwanza tarehe 20 Machi kwa kufunga shule, migahawa, hoteli, sehemu za kuogelea na kadhalika. Lakini hii ilikuwa takriban mwezi mmoja baada ya mgonjwa wa kwanza kutangazwa tarehe 28 Februari nchini Uingereza. Hata hivyo, siku tatu tu baadae uamuzi ukatolewa wa kufungia takribani kila kitu (lockdown).

Hatua hii ilijumuisha kuzuia watu kusafiri nje ya nchi, kutembeleana ndani ya nchi, kufunga biashara zote, na hata nyumba za ibada. Kwa kifupi, kila kitu kisichokuwa na ulazima au dharura kilipigwa marufuku. Polisi wakapewa amri ya kusimamia hilo.

Na ndipo niliporudi Uingereza kutokea Tanzania nikakuta nchi imezizima. Kimya. Unaona mabasi na magari machache mno barabarani.

Tangu nimerudi nimetoka mara moja tu kwenda dukani kununua vyakula vichache. Na barua ya kwanza niliyoikuta kwangu ni kutoka kwa Waziri Mkuu, Boris Johnson, ambaye kila mkazi wa nchi hii alitumiwa. Barua hiyo mbali ya kukufahamisha hatua madhubuti na za lazima ambazo serikali ya Uingereza inazichukua lakini pia inatambua kuwa mtu anaweza kuwa tafrani hivyo inaashiria kuwa kama kiongozi anaelewa magumu tunayoyapitia katika maisha yetu, biashara zetu na kazi zetu.

Anaendelea kuelezea umuhimu wa kufanya maamuzi magumu ya kuchukua hatua hizo za kukutaka ujifungie ndani mpaka hali itulizane. Kwa kifupi, anasema watu wengi wakiumwa kwa wakati mmoja hospitali zitazidiwa na kupoteza maisha ya wengi. Hivyo, ni jambo la lazima kupunguza maambukizi na kupunguza idadi ya watu wanaohitaji matibabu hospitalini ili kuokoa maisha ya wengi. Akamalizia kwa kusisitizia kuwa ndio maana wanatoa sharti hilo jepesi – lazima ukae nyumbani. Nami nimetii bila shuruti.

Barua hiyo imeeleza wazi kuwa watu watakuwa na wasiwasi hasa katika suala la kiuchumi kwa mtu binafsi na kwa familia, lakini serikali hiyo ikaahidi kusaidia angalau kuhakikisha kila mmoja anapata chakula. Huenda hakikisho na matumaini yaliyotolewa na kiongozi wa nchi hii ndiyo imesaidia watu kutulia ndani na kutii amri ya mkubwa wao si kama nchi nyingine. Kwa mfano, huko Marekani tumeshuhudia kwenye vyombo vya habari baadhi ya watu wakiandamana kutaka watoke nje licha ya hatari kubwa inayowakabili.

Jambo linaloweza kuigwa na nchi nyingine ni utamaduni wa kujitolea hapa Uingereza ambapo kuna mchanganyiko wa jamii mbalimbali kutoka sehemu kadhaa duniani. Ninaamini kabisa barani kwetu Afrika watu wanashirikiana sana na kusaidiana kifamilia na hata katika ngazi ya ujirani. Ila huenda likija suala kama hili mtu haimjii kuwa anaweza kusaidia zaidi kijamii.

Mathalan, nilikuta kipeperushi hapa kwangu ikiomba watu wa kujitolea na mambo ambayo si mazito hivyo. Haya ni pamoja na kusaidia kununua bidhaa mbalimbali kwa ajili ya watu wasiojiweza kwenda madukani wenyewe na kuwapelekea nje tu ya nyumba zao ili kuepuka kuwaambukiza virusi vya corona au wewe kuambukizwa. Au hata kama kuna anayehitaji tu kuzungumza na mtu, kwani kuna watu wapweke sana hasa wakati huu na hawana hata mtu wa kuwaopoa. Hilo ni suala pana zaidi la watu ambao wanayo au wanaweza kupata maradhi ya akili.

Hivyo basi, licha ya jitihada zote hizi kufanyika, huenda suala la kuchelewa kuchukua hatua ndilo likasababisha vifo chungu nzima kutokea. Ila angalau sasa baada ya kujifungia ndani hali inaonyesha kupungua kiasi. Bado tahadhari inasisitizwa na muda wa kukaa ndani nao umeongezwa hadi hapo itakapothibitishwa na ushauri wa wanasayansi kuwa sasa ni salama kuendelea na shughuli kama ilivyokuwa awali.

Wataalamu mbalimbali duniani wanaendelea kutoa mwongozo wa kusaidia kupunguza kusambaa kwa virusi hivyo. Hapa Uingereza huo wa kukaa ndani una masharti ya walau kutusaidia kufanya mambo kadhaa muhimu nje. Kwa mfano, unaweza kwenda hospitali au dukani kununua bidhaa muhimu. Na hapo unapoenda dukani basi unakaa takriban mita 2 kutoka kwa mwenzako na mkusanyiko wa zaidi ya watu wawili nao umepigwa marufuku. Mazoezi nje huruhusiwa lakini isizidi saa moja na yafanyike karibu na maeneo yako tu. Na kwenda kazini ni iwapo inabidi tu, la sivyo kazi zinafanyika nyumbani.

Nikiendelea kutafakari na kutazama nje, nawaza tu. Naikumbuka nchi yangu ya Tanzania. Hakika wahenga hawakukosea waliposema, heri kinga kuliko tiba. Naam, tahadhari kabla ya hatari.