Baada ya kutuma mtandaoni uchambuzi mfupi wa nafasi ya Mwalimu Nyerere katika kututafutia ‘Mgombea Safi’ (‘Mr. Clean’) mwaka 1995 nimejulishwa kwamba kuna utata/tatizo/walakini katika uchambuzi huo. Inasemekana siyo kweli kwamba Nyerere alihusika na kuhakikisha kwamba Mkapa anamshinda Kikwete. Kwa kuwa mimi ni muumini wa kuweka historia sawa, ningependa tujadili suala hili kwa kutumia vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha hatupotoshi historia/ukweli hasa mwaka huu – 2015 – wa uchaguzi.

Wakati wa uchaguzi wa 1995 nilikuwa nasoma shule ya sekondari ya Azania. Nyumbani nilikuwa nasaidia kukata vipande vya magazeti kwa ajili ya uchambuzi wa kisiasa. Kipindi hicho nilikuwa navutiwa sana na harakati za kisiasa za Kikwete na nilifuatilia sana msisimko uliotokea wakati yeye na Lowassa walipopanda ndege ndogo ya kukodi na kwenda Dodoma kuchukua fomu za kugombea dakika za lala salama. Bado naitafuta picha hiyo ila kwa sasa nimepata picha hizi mtandaoni: https://udadisi.com/2014/08/tujikumbushe-miaka-iliyopita-boys-ii.html. Hali kadhalika nilikuwa nafuatilia kwa karibu sana hotuba za Nyerere na vile vitabu vyake alivyovitoa kabla ya uchaguzi huo ambavyo, kwa uelewa wangu, kimsingi vilitumika pia, kwa namna moja au nyingine, kuhakikisha kuwa mwaka 1995 Malecela hapati Urais (hasa) baada ya lile sakata la OIC na G55.

Kwenye mjadala wa Wanazuoni mnamo mwaka 2009 kuhusu Why didn’t Nyerere groom good leaders? niliwahi kuandika maneno yafuatayo: “When Nyerere was asked that question, I am told, he responded by saying that he was unlucky, implying that two people in particulary that he groomed died prematurely: [Hussein Ramadhani] Shekilango (from whom we get the name of that road in Dar) and Edward Moringe Sokoine. Another person that he groomed but, due to malicious campaigns, never became our President (The President who never was as Zitto Kabwe calls him) is Dr. Salim Ahmed Salim. Now we are struggling with the legacy of a president Nyerere ‘chose’ for us in 1995 but if we look at what was in his mind as his 1995 book Our Leadership and the Destiny of Tanzania reveals, we will realize that his was a genuine attempt to make sure that the other folks that he groomed to be good leaders – and turned bad according to his standards – do not take over. Now should we blame him for who we become?”

[Grafu ya Ongezeko la Fedha Walizoweka Watanzania Uswizi]

Hayo maneno hapo juu nimeyakumbuka maana wanaoona kuna walakini kwenye ‘madai/hoja’ kuwa Nyerere alikuwa na ‘mkono’ katika kumzuia Kikwete kuwa Rais mwaka 1995, wanasisitiza – na nakubaliana nao kabisa – kuwa mgombea wa Nyerere alikuwa ni Dakta Salim. Lakini tatizo ni kwamba kwenye kile kinyang’anyiro cha 1995 hakuweza kuingia ulingoni kutokana na sababu ambazo nadhani sote tunazielewa. Hivyo, pia ni rahisi kuelewa madai/hoja nzito inayosema kwamba Nyerere alimpigia debe Kikwete aingie kwenye ‘tano/tatu’ bora ya wagombea wa Urais kupitia CCM ili wagombea wote wasiwe wa dini moja hasa ukizingatia kwamba ‘nyufa za udini’ zilishajitokeza katika medani ya siasa/kampeni na ilibidi azikemee mara kwa mara  (Rejea Hotuba ya Mwalimu Nyerere hoteli ya Kilimanjaro June 14, 1995 (Michuzi Blog)).

Lakini tukumbuke kabla ya kinyang’anyiro cha awali tunaambiwa Kikwete alienda kuonana na Nyerere nyumbani kwake Msasani. Inasemekana aliitwa (aende) mwenyewe ila akaenda na Lowassa. Na kuna tafsiri kinzani kuhusu taarifa mbalimbali za wakati huo zinazosema kwamba Nyerere aliona kuna tatizo na Lowassa japo pia tunaambiwa alibariki uamuzi huo wa Kikwete wa kwenda kugombea (Rejea http://www.teamlowassa.com/news/madai-ya-nyerere-kumkataa-lowassa-ukweli-na-ushahidi-huu-hapa/  na linganisha na http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/803005-katibu-wa-nyerere-jina-la-mwalimu-linatumiwa-vibaya-na-kambi-ya-lowassa.html).

Pamoja na hayo, Kikwete na Lowassa wakaenda Dodoma. Baada ya hilo la Kikwete kuendelea kuwa pamoja na Lowassa kweli tunaweza kusema bado Nyerere alikuwa hajachagua ‘amsapoti’ nani kati ya Mkapa na Kikwete kwenye raundi za mwisho za kinyang’anyiro cha kuchaguliwa kugombea Urais kwa tiketi ya chama tawala pale Dodoma? Kweli Nyerere alikuwa anaona ni sawa yeyote katika ya Mkapa na Kikwete akishinda hivyo hakutumia mbinu yeyote ya kuzuia Kikwete asishinde maana (eti) alikuja tu kugundua kuwa yeye na Kamati Kuu ya CCM ‘wamepigwa changa la macho’ mwishoni kabisa kabla tu ya kupiga kura ilipoonekana Kikwete amedhamiria kumteua Lowassa awe Waziri Mkuu iwapo atashinda nafasi hiyo?

Sasa kuna hoja nyingine ya msingi kabisa, kwamba kambi ya Kikwete ilikuwa haijasoma/haijaelewa vizuri katiba/kanuni za CCM kuhusu ‘kutosha kwa kura’ ila (eti) kambi ya Mkapa ndiyo ilikuwa inalijua suala hilo fika, hivyo, basi ikautumia mwanya huo kuhakikisha kwamba pamoja na Kikwete kupata kura nyingi zaidi kuliko Mkapa, kikanuni, kura zipigwe tena na hivyo kwenye raundi ya mwisho ya kinyang’anyiro Mkapa akamshinda Kikwete baada ya wengi wa wale waliopigia kura wale wagombea wengine walioenguliwa mwanzoni/katikati kumpigia Mkapa. Ni hoja ya msingi maana ina(wa)saidia kutuonesha/kututhibitisha kwamba siyo Nyerere aliyemzibia Kikwete bali lilikuwa ni suala tu la kikanuni (na kampeni za kambi) lililopolekea kura zipigwe tena na zile zingine zihamie kwa Mkapa hivyo ‘kumuovateki’ mwenzake.

 Lakini swali la kujiuliza: Ni kina nani hao waliokuwa kwenye hiyo kambi (ya kampeni) ya Mkapa maana kwa uelewa wangu walikuwa ni ‘Wanyerere’ (‘Nyerereists’) wakuu? Kama ni hivyo, wako upande gani leo hii hasa wanapoona Nyerere wao anatumiwa ‘ndivyo sivyo’ katika kampeni za uchaguzi wa wagombea Urais? Wajitokeze sasa basi kutusaidia kuiweka historia sawa hasa ukizingatia mwaka huu wa 2015 una mengi sana yanayofanana na yale yale mwaka 1995.