Niliuliza mwanzoni:

Sera hii ni ya nani?

Serikali kuwa tatu

Hapa Tanzania kwetu?

Ye yote mwenye akili

Asiyekuwa jahili,

Sera hii anajua

Itavunja Tanzania.

Wanajua wanavunja,

Na kusema kwa ujanja

Tanganyika kujitenga

Si kuvunja, ni kujenga.

Ati “ndani ya Muungano”,

Tudhanie ni maneno

Ya uwezo wa hirizi

Kukinga maangamizi.

Misingi mkishavunja,

Msidhani kwa ujanja

Nyumba mtashikilia,

Ikose kuwafukia.

Kwanza fikiri gharama

Zitobebwa na kauma:

Hizi serikali mbili

Sasa twaona thakili,

Sembuse zikiwa tatu?

Wataweza watu wetu?

Nakiri Wazanzibari

Katiba waliathiri,

Nilidhani kazi yetu

Ni kuwabana wenzetu,

Viongozi wa Zanziba,

Waiheshimu Katiba.

Lakini ni Serikali

Ambayo haikujali,

Na kitendo kama hicho

Ikakifumbia jicho,

Na kuanza kufokea

Wale waloikemea.

Wala kuvunja Katiba

Kuvunja Nchi si tiba.

Hivi wakifanikiwa

Na nchi wakaigawa,

Kumbe hawataandika

Katiba ya Tanganyika?

Wataacha utawala

Uwe shaghalabaghala?

Na kama ikiandikwa,

Katu haitakiukwa?

Endapo itatukia

Nayo ikavunjwa pia,

Tanganyika itengane,

Wapate nchi nyingine?

Wanaovunja sharia

Na Katiba Tanzania

Dawa ni kuwashitaki

Waadhibiwe kwa haki:

Nchi yetu kuigawa

Ni uhaini, si dawa.

Tanzania yetu ina

Watu aina aina:

Inao hao Wapemba

Watachomewa majumba,

Sera hii ikipita

Bila ya kupigwa vita.

Lakini ina Wahaya,

Na Wasumbwa na Wakwaya,

Ina Waha na Wamwera,

Na Wakwavi, na Wakara.

Ina Anna ina Juma,

Ina Asha ina Toma,

Kadhaka ina Pateli,

Na wengine mbali mbali.

Uhasama ukipamba

Mkafukuza Wapemba,

Anojua ni Manani

Mbele kuna mwisho gani.

Hivi mnavyofikiri,

Wenzetu Wazanzibari

Walitokea mwezini

Kuja hapo visiwani?

Visiwani humo humo

Wamakonde, Wazaramo,

Wanyamwezi na Wamwera;

Na mbari nyingi za Bara.

Walotoka Arabuni

Waliondoka zamani,

Walobaki ni wenzetu,

Raia wa Nchi yetu.

Mzaramo wa Unguja

Akizuiliwa kuja

Kuishi Darisalama,

Nambieni Msukuma

Mgogo au Mngoni

Aruhusiwe kwa nini.

Na Mchagga watamwacha?

Na Muha na kina Chacha?

Mwajuma wa Zanzibari

Mkimwona ni hatari,

Hivi Juma wa Pangani

Ana uhalali gani?

Na Shabani wa Kigoma?

Na Fatuma wa Musoma?

Na vita vya uhasama

Vitapamba nchi nzima:

Hawa fukuza hawa

Kwa udini na uzawa,

Yalo Yugoslavia

Yatufike Tanzania.

Chuki hizi msidhani

Hazina udini ndani,

Maana behewa hili

Lina watu wa kila hali.

Wamo na maaskofu,

Na mashehe watukufu:

Na wasomi wa sharia,

na wachumi wetu pia,

Kila mtu ana lwake,

Anazo sababu zake.

Hizi pilika pilika

Za kutenga Tanganyika

Ni kutafuta nafasi

Za kupata Uraisi

Tanganyika mnadhani

Ina mvutano gani

Wenye nguvu kuzidia

Umoja wa Tanzania?

Wa Pwani na wa Unguja

Mkiona si wamoja,

Mtawaona wa Mtwara

Ni wamoja na wa Mara?

Wa Pemba mkiwatenga

Na ndugu zao wa Tanga,

Mtaacha wa Tabora

Wadumu na wa Kagera?

Wafipa wa Sumbawanga,

Na Wasegeju wa Tanga,

Wawatenge Waunguja,

Wao wabaki wamoja?

Hivi Waha wa Kigoma

Na Wakurya wa Musoma

Na Wazaramo wa Pwani

Watabaki majirani?

Msidhani Tanzania

Si sawa na Somalia,

Ati mtaitabanga,

Msihiliki kwa janga.

Kikao mchanganyiko

Cha Dodoma huko huko,

Kimesema wazi wazi

Kuwambia Viongozi:

“Serikali kuwa mbili

Si sera ya Serikali,

Bali ni sera ya Chama

Kile kilichowatuma.

Basi kairudisheni

Kwa wenyewe vikaoni,

Wapate kuijadili,

Kibidi waibadili.”

Mimi kwa upande wangu

Nawanasihi wenzangu,

Sera wakiibadili,

Tafadhali, tafadhali:

Chama na kilete hoja

Serikali iwe moja

Nasi twaiga Warusi

Hata katika maasi,

Tuivunje vunje Dola,

Turudie makabila?

Mbegu mbaya imepandwa,

Lakini hatujashindwa,

Tunaweza kuing’oa,

Na nchi kuikoa.

Akipendezwa Jalia,

Itadumu Tanzania,

Amina! tena Amina!

Amina tena na tena!

Julius K. Nyerere, 16.11.1993 (TPH)