Ulikuwa wakati wa mapumziko ya chakula. Kwa kuwa nilifika ukumbini wakati mkutano ukiwa umekwishaanza ilinibidi kuwasalimia washiriki mmoja mmoja na kuulizana habari za kazi, mapambano na familia. Kwa mzunguko niliokuwa nimeuanza, Padri Privatus Karugendo angekuwa wa mwisho. Na nilipanga hivyo makusudi ili tutembee pamoja kuelekea katika mgahawa wa Seashells ili kujipatia chakula cha mchana. Lakini nahisi aliona utaratibu wangu unamchelewesha. Alinifuata nilipokuwa nimesimama ili kunisalimia.
Tulisalimiana kwa bashasha za baba na mwana, huku akiniuliza kwa nini sikwenda nyumbani kwake kwa ajili ya chakula cha asili cha Kihaya kama tulivyokuwa tumekubaliana mara ya mwisho tulipokutana. Nilijitetea. Alinielewa. Papo hapo mazungumzo yetu yalihamia kwenye siasa. Hii ilikuwa miezi ya mwanzo ya nusu ya pili ya mwaka 2020, joto la Uchaguzi Mkuu likiwa limepanda. Tulikaa meza ya peke yetu huku mwenzetu mmoja akijiunga nasi.
Kwa kawaida nikutanapo na Padri Karugendo huwa nakuwa mpole. Kazi yangu ni kusikiliza kwa umakini wa mwanafunzi mwenye kiu ya maarifa isiyokatika huku nimemtumbulia macho nikishangaa maajabu ya mtu mmoja kuwa na unyenyekevu, busara na maarifa ya kiasi kisichomithilika. Hapa na pale nitachombeza mazungumzo kwa maswali ili afunguke zaidi, lakini hukaa tuli nikisikiliza.
Siasa za Bongo na Bongo za Wanasiasa
Kama ilivyo ada, siku hiyo pia Padri Karugendo alinitembeza katika vichochoro vya siasa za Bongo na bongo za wanasiasa. Tukaingia pamoja katika vyumba vya mikutano na majukwaa ya kisiasa ili kuhoji maamuzi ya wakubwa. Kisha tukazama vichwani mwa wanasiasa ili kuona namna wanavyofikiri wafanyapo maamuzi. Katika hili, mazungumzo yetu yakagusia katika simu aliyopigiwa siku chache zilizopita na mkubwa mmoja ambae alikuwa amepita ubunge bila kupingwa, huku Padri Karugendo akikosoa mwenendo huo katika mitandao ya kijamii.
“Kwa nini anaogopa kushindana na wenzake?” aliuliza kwa masikitiko, japo uso wake ulibeba tabasamu lake la kila siku. “Katika siasa za ushindani, ni aibu na fedheha kubwa kwa mwanasiasa kupita bila kupingwa” akasisitiza. Alinieleza hofu yake juu ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 na mengi aliyotabiri yalitokea. Wengi wataendelea kukumbuka msimamo wake katika utetezi wa siasa za vyama vingi huku akijenga urafiki na wanasiasa aliowaamini bila kujali vyama vyao.
Hata hivyo, mtazamo wa Padri Karugendo kuhusu demokrasia ulikuwa mpana zaidi. Kwake yeye, demokrasia ni tunda la mapambano lenye sehemu mbili: sehemu ya nje, ambayo ni uhuru na haki ya NCHI kujiamulia mambo yake yenyewe, na sehemu ya ndani ambayo ni uhuru wa kujieleza na haki ya WANANCHI kuamua kuhusu nani awaongoze na sera za aina gani zitekelezwe ndani ya nchi yao. Kama ambavyo alipinga WATAWALA kutumia mabavu ya dola dhidi ya WANANCHI, ndivyo pia alivyopinga MABEBERU kutumia mabavu ya kijeshi na kiuchumi kukandamiza na kuzipora nchi za dunia ya tatu, hasa Afrika. Kwa maana nyingine ni makosa kuuuza uhuru wa Afrika kwa kisingizio cha kuleta demokrasia ya Afrika.
Haishangazi basi, pale mabeberu walipoivamia Libya mwishoni mwa mwaka 2011 kwa kisingizio cha kuleta demokrasia, Padri Karugendo alipaza sauti dhidi ya udhalimu huo. “Kifo cha Gaddafi kitufumbue macho,” aliandika katika makala yake ya mwaka 2011, yenye kichwa, “Kifo cha Muammar Gaddafi Ni Kifo cha Uhuru wa Afrika.” Hakumung’unya maneno katika kuitaja nia halisi ya mabeberu kuivamia Libya:
Wanataka mafuta ya Libya! Wanataka rasilimali za Afrika, wanataka soko la Afrika; wanataka Afrika isiungane na kuwa na nguvu ili waendelee kutugawanya na kututawala. Wanataka kuendeleza ukoloni na utumwa, wanataka kuzirudisha sera za mababu zao zilizoteketeza bara la Afrika.
Je, Waafrika wafanyeje? Padri Karugendo anaendelea kufafanua:
Ni lazima Waafrika kushikamana na kusema hapana! Ni lazima kukataa mbinu hizi za wakoloni kutaka kutuchagulia viongozi. Ni lazima kuwakataa hawa vibaraka wao na kuwa tayari kulilinda bara letu la Afrika ili liwe salama kwa vizazi vijavyo. Ni bora kufa tukilitetea bara letu kuliko kuliacha likachukuliwa na hawa wakoloni wajanja wanaojifanya wanaipenda Afrika kumbe ni mbinu za kuhakikisha bara letu linabaki gizani na kuendelea kunyonywa. Uhuru wetu unakufa ni lazima tusimame kuutetea.
Ujamaa wa Yesu
Turejee katika mazungumzo yangu na Padri Karugendo…. Mara tukahama kutoka vichwani mwa wanasiasa na akanipeleka katika makazi yao ili nione namna wanavyoishi maisha ya anasa ilhali wananchi walio wengi wakiwa katika ufukara wa kutupwa. Hapo tukamgusia rafiki yetu mmoja aliyekuwa na cheo kikubwa kisiasa, ambaye Padri Karugendo aliniambia, “Yule bado ni mjamaa hasa, hajabadilika.” Wakati tukizungumza kuhusu ujamaa, alinidokezea kuwa yeye ujamaa wake umetokana na kufuata mafundisho na matendo ya Yesu Kristo pamoja na Mwalimu Nyerere.
Nilimuomba anifafanulie kuhusu ujamaa wa Yesu. Hapo tukaingia katika Biblia. Biblia haitakiwi kupewa tafsiri si-si-si, aliniambia. Nikakumbuka namna Padri Karugendo alivyotofautiana na msimamo wa Kanisa Katoliki juu ya mambo mbali mbali, pale alipohamasisha matumizi ya kondomu ili kujikinga na Virusi Vya Ukimwi (VVU). Msimamo wake huo ulikuwa moja ya sababu zilizopelekea yeye kuvuliwa daraja la upadri mwaka 2009.
Padri Karugendo alinipitisha sura moja baada ya nyingine ya Biblia ili nimshuhudie Yesu aliyechagua kuzaliwa katika zizi la ng’ombe badala ya jumba la kifalme. Yesu yule ambaye hakujilimbikizia mali huku akikasirishwa na wafanyabiashara kuligeuza kanisa kuwa gulio. Alinifafanulia baadhi ya mafundisho ikiwemo mfano aliotoa Yesu wa urahisi wa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuuona ufalme wa mbingu.
Lakini zaidi ni matendo yake Yesu mwenyewe, ikiwemo ufufuo wa Pasaka. Pasaka, Padri Karugendo aliniambia, sio ufufuo wa mwili wa Yesu bali wa matendo ya Yesu, na tendo kuu, akasisitiza, likiwa ni kumegeana mkate.Kama ambavyo Padri Karugendo alifafanua katika mtandao wa jamii wa twitter Aprili 6, 2021:
Muujiza wa Pasaka si ufufuko bali ni kile kitendo cha kumtambua Yesu, alipoumega mkate. Rejea simulizi ya Emmaus ya Yesu na mitume wawili. Kuumega mkate, kuwalisha, kumjali jirani, kutoa maisha yako kwa wengine. Heri ya Pasaka!”
Akilinganisha mkate na rasilimali pamoja na faida inayozalishwa nchini, Padri Karugendo alisisitiza kuwa kunapaswa kuwa na mgawanyo sawa wa rasilimali na faida. Kufanya hivi ni kwa manufaa ya watu wote badala ya kutajirisha watu wachache. Na, kama alivyofanya Mwalimu Nyerere, mjamaa anapaswa kujitoa maisha yake kwa ajili ya mapambano ya ukombozi ya watu wanaonyonywa na kukandamizwa.
Pasaka ya Nyerere
Jambo lililomuumiza sana Padri Karugendo ni kutokuwepo nchini kwa Pasaka ya Nyerere:
Tunaambiwa wafuasi wa Yesu waliwatambua kwa kumegeana mkate. Kama matendo ndiyo yanafufuka, ina maana Tanzania nzima hakuna mtu anayetenda matendo ya Mwalimu Nyerere? Hakuna viongozi waadilifu kama Mwalimu? Hakuna Watanzania wazalendo wenye kupenda haki na kuitetea kama alivyofanya Mwalimu? Mbona hatujasikia mtu akitangaza kufufuka kwa Mwalimu?
Siku Padri Karugendo aliposafiri na kundi la vijana kutembelea vijiji vya Sumbawanga alifurahia sana kuona namna vilivyopangiliwa. Wanavijiji wakisema wazi kuwa umaridadi wa vijiji vyao, pamoja na jitihada zao za kufanya maamuzi ya pamoja na kujitegemea kwa kujenga miundombinu ya usafiri na huduma za jamii, ni zao za sera za Ujamaa na Kujitegemea. Aivutiwa sana na vijiji hivyo, jambo lililompelekea kutangaza, “Mwalimu Nyerere Amefufuka! Yuko Sumbawanga!” katika makala yake iliyochapishwa Novemba 11, 2012.
MIUMBI
Wakati simulizi hizi zimekolea hatukujua kuwa zaidi ya saa moja ilikuwa imepita, na wenzetu walikuwa wamesharudi ukumbini. Mmoja wa waratibu alikuja kutushtua kutoka katika lindi hili la tafakuri ili turudi ukumbini kuungana na wenzetu. Huko ukumbini tulikuwa tukijadili kuhusu Mikataba ya Uwekezaji baina ya Nchi Mbili (MIUMBI), au kwa Kiingereza Bilateral Investment Treaties (BITs). Padri Karugendo na mimi tulikuwa sehemu ya Kikosi Kazi cha kushughulikia MIUMBI, yeye akiwakilisha wanahabari na mimi nikiwakilisha wanazuoni.
Kikosi Kazi chetu kilikubaliana kuwa MIUMBI ni kanuni mpya ya ukoloni mamboleo iliyowekwa mahsusi na nchi za Magharibi ili kuzuia nchi za Dunia ya Tatu kujenga uchumi unaojitegemea. Na mbaya zaidi, pale nchi kama yetu inapochukua hatua za kudhatiti uchumi wake, inaweza kushtakiwa na wawekezaji wa kutoka katika nchi ya Ulaya iliyosaini MIUMBI na kupelekea Tanzania kupoteza mabilioni ya fedha ambayo yangeweza kuboresha huduma za umma. Kikosi Kazi chetu kilichukua msimamo wa kuitaka Tanzania kujiondoa katika MIUMBI.
‘Balimanyaila’
Uchambuzi wa aina hiyo, wa siasa uchumi ya mfumo wa kimataifa wa ubepari na madhara yake kwa nchi maskini, haukuwa mpya kwa Padri Karugendo. Katika makala zake nyingi alifuata nyayo za Mwalimu Nyerere kupinga unyonyaji na uporaji unaofanywa na nchi za Magharibi kwa nchi masikini kwa kisingizio cha utandawazi. “Ni kweli kwamba dunia sasa hivi imekuwa kijiji kimoja?” aliuliza katika makala yake yenye kichwa “Siasa Zetu Zilenge Kuujenga Uchumi wa Nchi ya Tanzania” iliyochapiswa katika gazeti la Mwananchi Agosti Mosi 2018. “Kwa vigezo gani?” aliendelea kuuliza, huku akijibu:
Lakini basi hakuna mwenye uwezo wa kupinga jambo hili sasa hivi, utaitwa kichaa. Tukubaliane kwamba dunia ni kijiji kimoja, kijiji ambacho wajanja wanaishi kwa anasa na wapole wanauzwa mnadani kama njiwa!” Hayo yote yanakifanya kijiji-dunia kuwa “pango la wanyang’anyi.
Je, tulifikaje huko? Ni kwa sababu ya kukumbatia mfumo kutengeneza faida kwa watu wachache. Padri Karugendo anatolea mfano wa walanguzi “wanaonunua mazao vijijini, mfano kahawa, mahindi na maharagwe.” Hivi hasa ndivyo wanavyofanya:
Debe lao moja moja unaweza kujaza madebe matatu ya kawaida. Madebe haya yana jina la ‘Balinyamaila,’ ikiwa na maana ya ‘Itawachukua muda kugundua ujanja wetu’. Kuna watu waliotajirika na kuendelea na bado wanaendelea kutajirika kwa kutumia mfumo huu wa ‘Balimanyaila’.
Kiu ya kupata faida haiondoki, bali huzaa kiu nyingine isiyokatika ya ulimbikizaji. “Faida inazaa ziada,” Padri Karugendo anaendelea kuandika. Hatimaye hiki ndicho kinachotokea:
Ziada inaleta kishawishi cha kutaka ZIADA zaidi: ZIADA zaidi ni hatari! Inazaa Unyang’anyi. Alienacho anataka awe na zaidi na anajitahidi kuunda mifumo ya kulinda njia zake za kuleta ziada; yuko tayari kulinda njia zake kwa gharama yoyote ile! Ifikapo hapo, huwezi kukwepa vita!
Kiongozi pekee wa Tanzania ambaye alipambana na mfumo huo wa kijahili wa ‘Balinyamaila’ kwa mujibu wa Padri Karugendo alikuwa Mwalimu Nyerere. Kwanza, kwa sera zake za kijamaa na ujenzi wa uchumi wenye kujali maslahi ya wengi, huku akizingatia kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini. Pili, kwa kupambana dhidi ya majahili wa kimataifa, yakiwemo mashirika ya kimataifa ya fedha kama IMF na Benki ya Dunia. Anasema:
Wale ninaolingana nao na wale wanaonizidi umri, wanakumbuka vizuri mapambano ya Mwalimu Nyerere na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)… Mwalimu Nyerere alikuwa anakataa kushusha thamani ya shilingi kwa kukwepa ujanja wa ‘Balimanyaila’. Mashirika kama IMF na Benki ya Dunia ni mtindo ule ule wa ‘Balimanyaila’. Jambo linalosikitisha na ndicho kichocheo cha kuandika makala haya, hata wataalamu wa uchumi wa Taifa letu hawakumwelewa Mwalimu.
Na hapo Padri Karugendo analimulika kurunzi lake kuwaangazia wasomi. Tena anawaangazia wote, wakiwemo wachumi, ambao wamekumbatia nadharia za kuturejesha utumwani ili kuwatumikia “Balimanyaila.” Anasema:
Wachumi wetu wamezama kwenye vitabu na utafiti. Kazi kubwa wanayoifanya ni kuendelea kuyanufaisha mashirika ya IMF na Benki ya Dunia.
Padri Karugendo anauona huu ni usaliti kwa taifa huku akitabiri dhahama katika mfumo wa uchumi wa kibepari:
Mashirika ya kimataifa hayawezi kutusaidia. Kama yameshindwa kwingineko itakuwa Tanzania? Miaka kumi iliyo mbele yetu ukiangalia vizuri yale yanayotokea katika mfumo wetu wa uchumi tutashuhudia kukwama kiuchumi kama nchi zote zilizokumbatia masharti ya IMF.
Anamalizia makala yake hiyo muhimu kuwataka wasomi wabadilike ili watumie taaluma zao kuiokoa nchi dhidi ya unaofanywa na mabepari wa kimataifa pamoja na mashirika kimataifa ya fedha. “Wakati ni huu,” Padri Karugendo anaonya. “Vinginevyo kizazi kijacho kitaifukua mifupa yetu na kuichoma moto kwa hasira,” anahitimisha.
Japo ametumia nafsi ya kwanza wingi katika onyo lake la mwisho, ukweli ni kwamba Padri Karugendo hakuwa mmoja wa wasomi hao wasaliti. Kalamu yake aliitumia bayana katika mapambano ya ukombozi. Na tena akiandika mambo magumu kwa lugha rahisi yenye kueleweka na walio wengi.
Dira ya Mapambano
Nilianza kuandika makala haya kama tanzia, nikiwa na huzuni ili kuomboleza kifo cha Padri Karugendo, aliyeaga dunia Juni 25, 2021 baada ya kuugua ghafla. Lakini kadiri nilivyovuta kumbukumbu za mikutano yangu na yeye na kuyadurusu maandiko yake, nilijikuta nikitabasamu na kufurahia. Nikagundua kuwa tunapaswa kusherehekea zaidi maisha yake.
Jabali huyu wa mapambano hajafa – ataendelea kuishi mioyoni mwetu. Na maandiko yake yatakuwa ni dira ya ujenzi wa Afrika mpya, yenye ustawi kwa wote. Afrika huru iliyojidhatiti dhidi ya udhalimu wa watawala, mabepari na mabeberu.
Makala nzuri sana ambayo imeandikwa kwa weledi wa hali ya juu hususani katika kuoanisha mawazo na maoni ya mwandishi (Sabatho) na mawazo ya hayati (Karugendo).
Msomaji wa makala hii ni rahisi kumfahamu Karugendo hata kama katika uhai wake hakubahatika kumsikiliza au kumsoma kwa kina.
Ni dhahiri kuwa Hayati Karugendo ni zaidi ya alivyoandikwa hapa. Mapambano yake katika namna alivyoitafsiri imani na dini yake inamfanya kuwa mmoja wa Mapadre wachache wenye mitazamo na maamuzi ya kimapinduzi katika dunia ya sasa ambayo watu kwa kupenda matumbo yao wamekuwa waimba korasi ya nyimbo za watawala aidha katika siasa au katika dini.
Niungane na mwandishi wa makala hii kusema kuwa Hayati Karugendo ataendelea kuishi katika maisha ya wana mapinduzi wa fikra na matendo yaliyolenga kuwakomboa wananchi wanyonge ambao mifumo ya kiutandawazi ya kibepari imewatenga katika kupaza sauti zao dhidi ya udhalimu wanaofanyiwa hususani katika kuporwa rasilimali zao kwa kisingizio cha kukuza uchumi wa kwenye makaratasi.
Pumzika kwa amani Kamaradi Karugendo! Mapambano ya wanyonge yatakuenzi vizazi na vizazi.
Nakara hii nimhim sana katika kufumbua macho ya wanyonge yaliyofumbwa kwa kigezo cha kukuza uchumi nivyema ikasambazwa zaidi hata kwa njia ya redio
Hongera sana Sabatho Nyamsenda. Makala haya ni moja kati ya makala bora kabisa katika kuelezea mambo magumu kwa lugha nyepesi. Nilibahatika kusoma makala chache za hayati Fr Karugendo. Niseme tu, alikuwa mwanazuoni makini sana. Udadisi, ahsanteni kwa kushea nasi.
Asante kwa tafakuri hii ya kasisi mwanamapinduzi Karugendo. Apumzike katika nguvu ya mababu wanamapinduzi alioungana nao. Nasi tukiendelea kusherehekea maisha yake, tuendelee kuomba roho yake ya kimapinduzi idumu katika mioyo ya wale wote wenye hasira dhidi ya Balimanyaila. Tuziishi fikra na falsafa zake kwa kuendeleza mapambano dhidi ya pasaka ya KUJIMEGEA na kurejesha paska halisi ya KUMEGEANA mkate.
Asante sana Sabatho. Najivunia sana kukufahamu. Nadhani kama nitajaribu kufuata nyayo zako basi pasi na shaka nitavuka ng’ambo.
Fikra zake za kimapinduzi zililenga manufaa ya wengi kwa bahati nzuri ama mbaya uandishi wake wenye kufikirisha kwa kina uliwafikia wachache kwa muktadha ule ule tarajiwa. Naam fikra zake zitaishi leo na kesho. Apumzike kwa amani Padre Karugendo.
Ama kwa hakika Komredi Sabatho umedadavua vyema maisha ya Mzee wetu Hayati Fr. Karugendo.
Mbio zake amemaliza, wachache tuliomegewa mkate wa maarifa kutoka kwake bado tuna kazi kubwa ya kuhakikisha mapambano hayakomi.
Katika makutano na Wajamaa waliolala mapema bila shaka ni shangwe.
#RIPFrKarugendo
Makala yenye virutubisho jwa afya ya ubongo.
Ahsante sana Mwl wangu. Nimeshiba kwa chakula chako.
Nilikuwa namukubali sana Privatus Karugendo… Rest…. In… Peace
Tatizo la ‘tatizo la Afrika’ ni nini maana ya ‘maana ya ki-Afrika’!
Afrika itajengwa na Waafrika wenyewe wenye dhamira safi dhidi ya Bara let. Kongole Kamaradi.
Ujamaa haukuelewema Tz enzi za Mwl, Leo Demokrasia imekwenda kuzimu kuzimua na mabeberu,
big up brother Sabatho,
Ukumbukwe milele Kamanda uwa uhuru na mkombozi wa fikra za mTz Fr Karugendo…