Nilipopewa wasaa wa kusema maneno machache kuhusu mada ya kusoma na vitabu, nilimfikiria bibi yangu mzaa mama, yaani, mama yake mama yangu. Yeye akiitwa Salama binti Rubeya. Baba yake alifariki angali yeye mdogo. Kwa hivyo bibi yangu alilelewa na babu yake, bwana Mahfudh.

Bibi alinisimulia kwamba nyumba aliyokulia utotoni ilikuwa Kilwa Kivinje. Uwanjani palikuwa na ngamia waliofumbwa macho wakati wa kusindika ufuta ili kupata mafuta ya uto. Kutokana na simulizi zake, katika akili yangu, niliweza kuwaona hao ngamia wakivizunguka vinu na kusindika huo ufuta hadi ukawa mwepesi utasema kitambaa cha hariri.

Bwana Mahfudh alikuwa mfanyabiashara maarufu. Alikuwa mhusika mahsusi kwenye hadithi nyingi za maisha ya utotoni mwa bibi yangu. Kwa kweli nilifaidika kupokea simulizi ambazo bibi alisimuliwa na wazee wake. Wao bila shaka walizipokea kutoka kwa wazee wao.

Kulikuwa na hadithi za bibie aliyekula wali kwa sindano, bwana aliyeokoa watu kwa kupika uji wa moto kwenye chungu ambamo joka lililokuwa likitisha kijiji lilitumbukia na kuungulia mbali, pia hadithi za msichana aliyeokolewa kwa kupewa vitunga na ajuza mmoja. Hivyo vitunga ndivyo vilivyomwezesha kurudi kwao. Bila hivyo msichana huyo angaliuwawa na mmewe ambaye alikuwa zimwi.

Na baadaye nilipokuwa nikikua – wale wa rika langu watakumbuka kwamba kulikuwa na kipindi redioni cha ‘mama na mwana’ ambamo kulikuwa na hadithi kemkem. Kwa hivyo hadithi ziliuzunguka utoto wangu. Ni hizo hadithi zinazoweza kutupa mbinu na uwezo wa kuusimulia ukweli wa maisha yetu kama tunavyouona na kuuelewa.

Ninasema hivyo kwa sababu katika historia yetu, fasihi simulizi na usomaji vimekuweko sambamba. Tunapotazama fasihi yetu, jambo hili ni wazi kabisa. Waandishi wabobezi kama Abdulrazak Gurnah, wameipata athari ya kuhadithiwa simulizi na bibi zao majumbani.

Kwenye tafsiri ya Paradise ambayo nimeifanya na kuiita Peponi, kuna simulizi nyingi kama za kina Abakari bin Mwenye Chande na Waswahili wengine wanaozungumzia safari zao kwenda sehemu tofauti kama Umanyema, Nyasa na Urusi (tazama Velten, 1901: Safari za Wasuahel). Pia kuna simulizi zilizoshabihiana na zile za kwenye Alfu Lela U Lela kama ile ya mwanamke ambaye jini alimweka kwenye pango lililojaa vito vya thamani. Lakini hakuweza kustahamili na baadaye alimsaliti jini na yakampata yaliyompata.

Kitu ninachotaka kusema hapa ni kwamba simulizi kama hizi zimekuwa na nafasi adhimu sana katika jamii yetu. Zimeweza kutupa hisia za starehe, huzuni na uelewa wa uhai na uweko wa binadamu – kifikra na kiitikadi – yote ambayo hufanya kitabu kiwe hai na kinoge. Ninafikiri maandiko yenye ladha hasa huanza kama simulizi.

Nikifikiria maandiko yetu, kwa mfano  Hadithi za Abunuwas na pia vitabu vya waandishi kama Shaaban Robert, Muhammad Said Abdullah aliyeandika Kisima cha Giningi, vyanzo ni simulizi. Basi katika fikra zetu kama tunaotaka kuandika na tunaopenda kusoma—hasa kama lengo letu ni kujikomboa kutokana na fikra za kimagharibi; basi ni muhimu kuanza hapo.

Jambo la pili ambalo limeunganika na hilo la kwanza, pia limenijia kwa kumpitia bibi yangu, Salama binti Rubeya. Katika miaka ile ya zamani, hakuruhusiwa kuenda skuli kwa sababu alikuwa msichana. Lakini alitaka sana kusoma.

 Alipokuwa msichana kule Kilwa, katika uwanja alipokulia kulikuwa na mtoto mdogo wa kiume ambaye alikwenda skuli. Bibi yangu alimwomba amfundishe kusoma. Awali huyo mtoto alikataa, lakini baadaye bibi yangu alipata wazo zuri – akamwambia atakuwa akimlipa visenti kiduchu ili amfundishe. Hapo kikwazo kikapotea na yule mtoto alimfundisha – tena kwa vile bibi yangu alikuwa msichana, ilibidi asindikizwe na wenzake kwa hivyo darasa lilijumuisha ndugu na binadamu wengine wasichana ambao nao wakafaidika.

Mimi nilipokuwa nikikua, bibi yangu alikuwa anaanza kuzeeka na hakuweza kuona vizuri. Hata hivyo, ninamkumbuka akivaa miwani yake iliyofanya macho yake yaonekane makubwa – na baada ya kuivaa alidodosa na kufurahia kusoma hadithi kama Mashimo ya Mfalme Sulemani ambamo Gagula alitia fora kwa roho ya kikorosho, Kisiwa chenye Hazina, Alfu Lela U Lela – zote ambazo zilikuwa kwenye maktaba ndogo iliyokuwa nyumbani kwetu; kwa kweli alipenda sana kusoma – na nina hakika wanawe wote wameweza kuendelea kimasomo na kuchukua nyadhifa tofauti nchini na nje, kutokana naye.

Na mimi nilipokuwa mdogo, bibi akiniita chumbani kwake takriban kila siku ili nimsomee kitabu au mashairi na hadithi zilizopigwa chapa gazetini. Baada ya kusoma alinipa shilingi moja au wakati mwingine shilingi tano. Kwa hivyo nilifurahia sana kumsomea maana nilijisogeza kwa kupata pesa. Tena nikimwuliza hasa – bibi leo hutaki nikusomee?

Kama hakuwa na hamu ya kusomewa kitabu, alinifanya nishushe masanduku yake na kutoa kanga moja baada ya nyingine. Tena huku nikimwonyesha rinda na miji yao na kumsomea maneno yaliyoandikwa. Na mara nyingi kulikuwa na simulizi kemkem na vicheko kuhusu maneno na kanga zenyewe.

Hapa ninataka tu kusema kwamba, kusoma, na kupenda kusoma, kuthamini vitabu –  kunaanza nyumbani – hasa utotoni. Tamasha la Vitabu limetuletea vitabu kemkem. Kazi ni kwetu sisi kuvichukua na kuvisoma – na hasa, kuhakikisha watoto wetu wanasoma.

Umuhimu wa kusoma hauna haja ya kuzungumziwa kwani sote tunafahamu kwamba kusoma hutuwezesha kuielewa dunia kwa kutufumbulia mengi ya dunia. Kusoma hutupa uwezo wa kuibadili dunia pia. Na leo nimepata moyo baada ya kuona kuwa kuna mikakati ya kufungua maktaba hapa mjini Unguja, jambo jema.

Kwa hivyo ladha ya kitabu inaanzia kwenye simulizi zilizotuzunguka ambazo ni chanzo kwa sisi kuufurahia ulimwengu tofauti na mpya tunaoukuta kimaandiko kwenye vitabu. Maneno yanayopanua upeo wetu, mawazo na uelewa wetu kwa kutupa hisia za kina ambazo zinatuwezesha kujielewa na kuielewa dunia yetu. 

Nitaishia kwa kusema jambo fupi kuhusu tafsiri ya Paradise. Kwanza mapenzi yangu ya kusoma yalizidi kukua jinsi miaka ilivyoenda. Mimi nimekuwa shabiki wa Abdulrazak Gurnah kwa miaka mingi sana. Niliamua kuitafsiri kwa faida yangu mimi mwenyewe kwani Paradise ni kitabu ambacho nimekuwa nikikifundisha kwa miaka mingi sasa kwenye somo la uelewa wa maeneo ya Bahari ya Hindi.

Ni kitabu kinachotupa historia ya Waafrika walio upande wa magharibi ya Bahari ya Hindi. Yaani Afrika Mashariki ambayo ni ya kweli na ni tofauti na ile iliyozagaa kote. Kwa mawazo yangu, Abdulrazak Gurnah ni katika waandishi wachache ambao wameweza kuwakilisha ukweli wa wengi hapa nchini.

Nilipoanza kutafsiri, lengo hasa lilikuwa kunipa shifaa kutokana na ugonjwa mbaya niliogua. Niliumwa sana na kulazwa kwa wiki kadhaa kutokana na maradhi ya UVIKO (COVID). Baada ya hapo nilipewa muda wa mapumziko kutoka kazini na ndiyo nikaanza kutafsiri Paradise mwezi Machi mwaka 2021.

Wazo la kutafsiri alilitoa mama yangu, bi Salha Hamdani. Kwa kweli, ni lazima niseme kwamba sikudhani kamwe kwamba ingeweza kutokea siku tafsiri ikasomwa na watu wengine. Lakini baada ya Abdulrazak kushinda Nobel, sasa kazi imepigwa chapa na Mkuki na Nyota na imepokelewa vizuri na serikali ya Tanzania, hasa Wizara ya Elimu.

Ninawashukuru nyote kwa kuipokea tafsiri hii kwa mikono miwili. Nina hakika kwamba bibi yangu angalikuwa hai, ningalimsomea tafsiri yote – bila shaka angalifurahia sana simulizi zake, hasa jinsi inavyowaelezea watu kama Ami Aziz na Mohamed Abdala na Yusuf mwenyewe. Labda angalinipa walau shilingi mia baada ya kurasa chache