Na Jasper “Kido” (@KidoJapa)
Salamu nakutumia,
pole nakuambia,
Kaka Pole, nakuandikia,
Kaka, pole nakuusia
Pole kwa matanga
Kwako na kwangu pia,
Pole kwa majanga
na dhahama za dunia
Pole kwa kufiwa
na simanzi ilokufika,
Pole kwa ukiwa,
Mzazi amekutoka
Pole kwa mamlaka
wadhfa na kadhalika,
Pole kwa kuchoka
kwa utendaji ulotukuka
Si shaka ulitutenda
Mitano tulitendeka,
Kazio uliipenda
wala hukukwazika
Ila leo kuruta…
Amri imekukuta,
Ile “nyuma geuka”
Kizito kimekufika
Si kingine hata
cha sheria zenye ukuda,
Urasimu zizojikita
Hasimu zimekukwida
Pole kwa makasia
na mbizi usiku kucha,
Dhoruba mekufikia
chombo sasa kimekuchocha
Ukuu umekimbia
Ukambo umesalia,
Hadeki wakufikia
Waswahili wakuambia
Pole kwa kuchetuka,
Ilikupasa kwa hakika,
Tambo zako na dhihaka,
kwetu zote zilitufika
Ya nguoni ulituvika
Tukakoma na kukomoka,
Sujuda uliitaka,
Tukakuvika na ya ukoka
Pole kwa pilika
mtaala kuusuka,
Pole kwa patashika,
na gharika za mamlaka
Kongole kwa maarifa
na shule ilotukuka,
Jamii inayo ufa
wa elimu ya matabaka
Tatizo unayefundisha
Moyoni umetutoka,
Mbona leo kutupasha
Habari za madaraka?
Jana haikukufaa?
Au hukuupata wasaa?
Mawili kuyashika
Yangeweza kuponyoka?
Au haikuwa haja
na shule haikuwa tija?
Baba alikukosha
ukakosa cha kufundisha?
Bado nina mashaka,
Pengine alikataza?
Na sasa kapumzika
Nawe unateleza
Pole kwa fedheha
na kadhia zinazokufika,
Pole kwa waso staha
Japo nduguzo wa uhakika
Kikulacho ki nguoni
Wahenga walitujuza,
Kinjano, kijani,
Hadharani chajikweza
Si kingine, cha tawala,
Kidumu kisicho dira
Kigumu kilicho dola,
Chaitafuna hadhira
Pole kwa kuchelea
Shuka kulikumbuka,
Pole kwa kupelea
Na jikoni ukatoka
Pole kwa kurejea
Duniani kwenye shuruba,
Pole kwa kukemea
kwa kuyakosa mahaba
Pole kwa kuchochea
Moshi upate kuwaka,
Pole kwa kuchelea
Samaki keshakauka
Pole nakusisitizia
Kwa ukuu kukukimbia,
Mtu baki mesalia
Nchini Tozonia
Pole kwa hujuma,
Wahuni si watu wema
Mirathi wamekunyima,
Wamekutenda yatima
Hakimiliki
Comments are closed.
Wahuni si watu wema. Vitaliti Maembe alisema, “kuweni makini na watawala, mkinona watawala”.
Nami niseme pole,
Ila nenda polepole,
Dunia ndiyo shule,
Walinena wa kale.