MAPITIO
YA RASIMU YA KATIBA

Wakati vikao vya Bunge la Katiba vinakaribia kuanza kule
Dodoma, ni muhimu kwa Watanzania wenye kujali mustakabali wa nchi hii kuendelea kutoa mawazo juu ya Rasimu ya Pili ya Katiba na mchakato mzima wa kutunga
Katiba mpya ili kupanua na kukomaza mjadala ndani na nje ya Bunge hilo.

Rajua (Maono) na Mtazamo wa Rasimu ya Pili ya Katiba

Katiba ya Kidemokrasia au Kitaifa hupaswa kuwakilisha maono
ya Umma au Taifa kwa jumla kuhusu masuala muhimu ya Uhuru na Utambulisho wao, mfumo
wa utawala wanaoutaka, uhusiano kati ya watawala na watawaliwa, majukumu ya
watawala na mipaka ya mamlaka yao, haki na majukumu ya raia, na aina ya mfumo
wa kijamii-kiuchumi wanaoutaka. 


Mgogoro mkubwa ulimo ndani ya Rasimu hii unahusu mgongano
kati ya rajua ya “kumwezesha mnyonge” (aliyoishadidia Mwenyekiti wa Tume ya
Kuandika Katiba) na mwelekeo wa Katiba wa kujenga uchumi huria wa kibepari na
demokrasia ya wachache dhidi ya (au kwa niaba ya?) wengi. Mgogoro huu
umeibuliwa na ukweli kuwa hakukuwa na Mwafaka wa Kitaifa kuhusu aina ya jamii
tunayotaka kuijenga kabla ya kujitosa katika kuandaa Katiba ya kutekeleza azma
hiyo.Maana, baada ya yote,
Katiba ni chombo tu cha kutekeleza azma ya jamii nzima au ya makundi fulani
yenye nguvu ndani ya jamii. Hivyo swali kuu la kujiuliza ni, je, Katiba yetu
inanuwia kutekeleza azma ya kina nani
katika jamii yetu?

Kwa upande wa mfumo wa
uchumi, ambao hatimaye ndio msingi wa Katiba yoyote ile, tungeweza kukubaliana
kuwa tujenge mfumo mmojawapo kati ya hii ifuatayo:

      
Ubepari huria

      
Ujamaa wa kisoshalisti

      
Ubepari wa kitaifa/kizalendo

      
Uchumi-mchanganyiko (usoshalisti + ubepari
pamoja kwa viwango mbalimbali).

Kwa
kadiri nilivyoielewa Rasimu ya 2 ya Katiba, naona inatuelekeza zaidi kwenye
Ubepari huria, lakini wenye uliberali ndani yake, ingawa baadhi ya vifungu
vyake vinagongana na azma hiyo.  Hili
linashiria jambo moja: kwamba, ingawa hapakuwa na mwafaka wa kitaifa, lakini
palikuwa na mwafaka wa kitabaka wa
tabaka tawala nchini kuhusu aina ya jamii na utawala wanayoitaka. Katika muktadha
huo, ni muhimu kujiuliza ni ubepari wa aina gani unaojengwa – ule wa
kitaifa-kizalendo, au ule wa kikuwadi-kibarakala (compradorial). Mapitio haya yanafanywa kwa kuzingatia muktadha huo.
Nje ya muktadha huo hapahitajiki mapendekezo bali Katiba mpya kabisa yenye
mchakato na mwekeo tofauti.

MAPITIO
YA KATIBA YENYEWE

Utangulizi wa Rasimu ya Pili ya Katiba unaeleza rajua na
baadhi ya azma muhimu za Taifa zinazozingatiwa katika Katiba hii:

      
…Kwa kuwa sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayoheshimu na
kuzingatia misingi ya utu, uhuru, haki, usawa, udugu, amani, umoja na
mshikamano katika nyanja zote za maisha yetu;

     …na kwa kuwa , tunaamini
kuwa misingi hiyo inaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye…

      
kujenga Taifa huru na linalojitegema…

         
kujenga umoja na mshikamano
utakaowezesha kutimiza malengo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kimazingira na
kulinda urithi kwa ujumla;

Tunaweza kuchukulia kuwa azma hizi ni vielelezo vya rajua
ya Katiba (si ya Taifa) kuhusu aina ya nchi inayotakiwa kujengwa. “Kuheshimu
misingi ya utu na haki…” na “Kujenga Taifa huru linalojitegemea” ni mambo yanayohusu
takriban nyanja zote muhimu za maisha – hasa uchumi, utamaduni, elimu, sayansi,
siasa na ulinzi na usalama. Je, ni mfumo gani wa uchumi na utawala utatuwezesha
kuyatimiza?

Tukianza na suala la
kujenga Taifa huru linalojitegemea, vifungu vya Katiba vinavyohusu suala hili
vinasema Utawala utahakikisha kuwa: 

Ibara ya 10 (3) (c):


 (c)
kiuchumi, Serikali inachukua hatua zinazofaa ili –

(i) kuwaletea
wananchi maisha bora kwa kuondoa umaskini;

(ii)
kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo
zitahakikisha kuwa utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa
manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine;


(iii) kuweka
mazingira bora kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa
wakulima, wafugaji na wavuvi….


Maelezo haya
yanatupeleka kwenye mfumo ulio kinyume na ubepari, kama si mfumo mchanganyiko
wa uchumi. Mathalan, katika mfumo wa ubepari, haiwezekani “kuzuia mtu kumnyonya
mtu mwingine” maana mfumo mzima umejengwa kwenye msingi wa unyonyaji wa mwajiri
kwa mwajiriwa.  Je, Katiba hii
inatupeleka kwenye Ujamaa? Ibara zinazofuata zinakanusha dhana hii:

Ibara ya 10 (3)(c)(xi):

“kuhamasisha
uwekezaji wa pamoja baina ya raia na wasio raia katika miundombinu ya uchumi,
uvunaji wa rasilimali na maliasili za Taifa;” Katiba inaona kuwa hii ni njia muhimu
ya kuelekea kwenye uchumi wa kujitegemea. Maoni yangu ni kuwa njia hii inaweza kufanikisha
kujenga tabaka la mawakala wenyeji wa mabepari wa kigeni. Ili kujenga Taifa
huru linalojitegemea kikwelikweli katika uwanja wa uchumi, ningeshauri kifungu
hiki kipanuliwe kwa kuzingatia maudhui yafuatayo:

      
kuhamasisha uwekezaji wa Watanzania katika
mihimili mikuu ya uchumi,  miundombinu ya uchumi, na uvunaji wa rasilimali
na maliasili za Taifa. Uwekezaji huo unaweza kufanywa na raia binafsi, au
kupitia katika vikundi vyao vya uzalishaji, vijiji, vyama vya ushirika au
serikali za mitaa na serikali kuu kupitia mashirika ya Umma kama NDC, TPDC,
TANESCO, n.k., Pale ambapo uwezo na rasilimali za ndani hazitoshi, dola
itahamasisha uwekezaji wa pamoja baina ya raia na wasio raia, na baina ya
serikali ya Tanzania na mashirika yake 
na serikali au makampuni ya kigeni, katika maeneo muhimu ya kiuchumi,
hasa viwanda vikubwa, kilimo, nishati na uvunaji wa rasilimali….

Hapa tunaangalia
maudhui zaidi. Maelezo yanaweza kuwekwa katika lugha ya kisheria baadaye. Maana
ya pendekezo hili ni kwamba tukubali kujenga uchumi mchanganyiko ukiwamo
uwekezaji wa dola, vyama vya ushirika, vikundi vya wazalishaji, na watu
binafsi.  Tukubali ukweli kwamba hakuna
bepari wa kigeni atakayetujengea uchumi unaojitegemea; kazi hii inabidi ifanywe
na sisi wenyewe; kwa kuwa mabepari binafsi wenyeji ni wachache na dhaifu, dola
haina budi kuingilia kati.

Suala la kujenga
“umoja na mshikamano” linaambatana na mambo mengi, kama vile utamaduni na utambulisho
(pamoja na kuwa na lugha moja na mfumo amali – value system – wa kitaifa), na hasa kutambua na kulinda haki za
raia, na kuwa na mfumo wa uwakilishi unaowapa sauti wanyonge.

Katika Rasmu ya sasa,
kuna juhudi ya kutoa haki kwa raia (ibara ya 27 na nyingine kadha), lakini
katika suala la uwakilishi kuna matatizo makubwa. Rasimu imeainisha makundi
kadha ya “wanyonge” wakiwamo wanawake, walemavu, wavuvi na wafugaji (Ibara ya
10 (3)). Makundi mengine makuu ya wanyonge imeyaacha. Makundi hayo ni: vijana,
watu wasio na ajira, na wafanyakazi wa ujira. Kadhalika, haki za wazee (Ibara
ya 48) hazijapewa uzito unaostahiki, hususani kuhusiana na haki ya kulipwa
pensheni inayostahili, na kuwakilishwa Bungeni. Je hawa watawakilishwa pia
Bungeni? Watawakilishwa na nani?

Hebu tuvipitie
vipengele vyenye utata:

Suala la Utamaduni na TEHAMA

Utamaduni
umezungumziwa kwa mtazamo wa kijadi kwa kuuhusisha na mila, desturi, lugha,
mambo ya kale, n.k. Kuna haja ya kupanua wigo na kuongeza mkazo katika suala la
Utamaduni kama roho na utambulisho wa Taifa, ambao inabidi ulindwe na kuenziwa
kwa kila hali, huku ukiendelezwa na kubadilishwa kulingana na mahitaji ya sasa.
Hivyo maelezo kuhusu utamaduni katika Ibara ya 10 yarekebishwe kwa kuongezewa
madhui yafuatayo:

      
Kujenga Taifa linalojivunia utambulisho wake, lenye
utamaduni imara unaokwenda na wakati, lenye kujali historia na mashujaa wake,
kuthamini vitabu na usomaji, na kuhimiza, kuendeleza na kutumia TEHAMA katika
elimu na maisha ya kila siku.

Kulinda Haki za Raia

Ibara ya 10 inaeleza
vizuri kuhusu hatua zitakazochukuliwa na serikali kulinda haki za raia,
zikiwamo za kiuchumi, kisiasa na kitamaduni.Haki ambazo hazijapewa
uzito wa kutosha ni:

  
haki za wafanyakazi wa ujira, ikiwamo haki ya
kulipwa ujira wa haki kwa kazi wanazofanya, na haki ya kugoma ili kudai malipo
ya haki;

  
Ibara
27(1) inatoa haki ya uhuru kwa kila mtu. Pia haki ya kutonyang’anywa uhuru bila
ya kufuata sheria. Hata hivyo, ibara za 39 na 40 zinanatoa mwanya kwa mtu
kuwekwa kizuizini bila kupitia katika mfumo wa kimahakama. Hii ni sheria ya
kale ya kikoloni, na ni hatari; inafaa ielezwe wazi kuwa hakuna mtu au mamlaka
yenye madaraka ya kumweka mtu kizuizini (kwa muda unaozidi saa 48) isipokuwa
mahakama.

Haki ya Uwakilishi

Hapa napo kuna utata.
Katiba inabainisha namna makundi mawili ya Walemavu na Wanawake yatakavyowakilishwa
Bungeni, lakini haibainishi namna makundi mengine ya “wanyonge” yatakavyowakilishwa.

Ibara ya 10(3) ( c) (iii):kuweka mazingira bora kwa ajili ya
kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi…

inaibua maswali mengi. Haifafanui
“mazingira bora” ni yapi na watu hao watawakilishwa wapi au katika chombo kipi,
na watawakilishwa na nani.

Aidha, uwakilishi wa
wanawake na walemavu una utata:

  • Wanawake:Watakuwa asilimia 50 ya wabunge wa Bunge la
    Muungano [Ibara ya 113 (3)]. Likitazamwa kijuujuu hili ni pendekezo zuri
    kwa kuwa linaweka “uwakilisha sawa” baina ya wanawake na wanaume. Hata
    hivyo, pendekezo hili linapochambuliwa linaibua masuala mapya. Kimsingi mantiki
    ya pendekezo hili ni kwamba mgongano au mtafaruku mkuu katika nchi hii ni
    wa kijinsia kati ya wanaume na wanawake, na hii ndiyo njia ya
    kuutatua.  Dhana hii inachukulia
    kwamba wanawake wote, bila kujali hali, tabaka, imani, n.k. wana hali
    sawa, maslahi na mawanio sawa, na wanaume vivyo hivyo. Hivyo mwanamke
    yeyote anayeingia Bungeni anawakilisha wanawake, na mwanamume yeyote
    anayeingia Bungeni anawakilisha wanaume. Mtazamo huu si sahihi na
    unakanushwa na uzoevu wetu wa miaka 50 ya uwakilishi wa wanawake Bungeni.
    Kwanza unaficha tofauti za kitabaka na kijamii miongoni mwa makundi hayo
    mawili ya kijinsi. Hapa mwanamke au mwanamume mnyonge wa kijijini au mtaani
    anaweza asiwakilishwe.  Kuna
    uwezekano wa kundi dogo la wanaume na wanawake wenye uwezo, elimu na hali
    nzuri kushirikiana kushika madaraka kwa maslahi ya kundi lao (kama livyo
    sasa ambapo wakubwa wanakwenda Bungeni na wake/waume zao) dhidi ya
    wanawake na wanaume wanyonge. Hili haliepukiki iwapo wabunge hao wa kike
    na kiume watadhaminiwa na vyama vya siasa (vinavyomilikiwa na kutawaliwa
    na wanaume) na vyenye itikadi na maslahi ya tabaka tawala. Iwapo kifungu
    hiki cha uwakilishi wa kijinsia kitabakia, itabidi yaongezwe maelezo kuwa
    wawakilishi hao wa wanawake si lazima wadhaminiwe na Chama cha siasa;
    wanaweza kudhaminiwa na asasi huru za wanawake (bahati mbaya hili la
    uwakilishi wa asasi huru za kijamii Bungeni – kama ilivyo katika baadhi ya
    nchi za kimaendeleo – halijaingizwa katika Katiba), au kusimama wakiwa
    wagombea binafsi (wanaojidhamini au wanaodhaminiwa na asasi mahsusi za
    utetezi wa wanawake). Bila kufanya hivyo tutaishia kuwa na wabunge
    wanawake wa “mrengo wa kiume” Bungeni. Huu utakuwa ni uwakilishi wa
    kitakwimu, hautakuwa uwakilishi wa kweli.
  • Aidha, pendekezo la uwakilisha sawa wa kijinsia
    halitafanikiwa iwapo Katiba itabakiza kifungu kinachowazuia wanyonge (wakiwamo
    wale wasio na elimu ya kidato cha IV au wasiojua Kiingereza) kugombea
    Ubunge (Ibara ya 125 (1) (a) na (b) inatamka: 

      
125(1) Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika Ibara hii, mtu yeyote
atakuwa na sifa za kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo:

(a) ni raia
wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja wakati wa
kugombea;

(b) anajua
kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kiingereza na ana elimu isiyopungua
kidato cha nne;


(c) ni
mwanachama aliyependekezwa na chama cha siasa au mgombea huru;



      
Kifungu
hicho kinawanyima kijanja asilimia kama 70% ya wananchi wote haki ya kugombea
Ubunge, na kuwapa haki hiyo wasomi wachache wasiozidi 30%. Huu si ukiritimba wa
kisiasa tu, bali ni ukaburu wa kisiasa, na unapingana na Ibara ya 7 (g) ya
Katiba hii hii ambayo inasema mamlaka ya nchi itahakikisha kwamba:

      
“ kunakuwepo fursa na haki zilizo sawa kwa
wananchi wote, wanawake na wanaume, bila ya kujali rangi, kabila, nasaba,
itikadi, dini au hali ya mtu”

Ibara ya35(2)inasema: 


…Kila mtu ana haki na fursa sawa kushika nafasi yoyote  y a  kazi, uongozi au shughuli yoyote  iliyo chini ya mamlaka ya nchi. …

na Ibara ya 25(3-4)inaongeza:

(3) Ni
marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya
Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa
taathira yake….

(5) Kwa
madhumuni ya masharti ya Ibara hii, neno “kubagua” maana yake ni kutimiza
utashi, haki au mahitaji mengineyo kwa watu mbalimbali kwa kuzingatia utaifa
wao, kabila, mahali walipotokea, maoni yao ya kisiasa, rangi, dini, jinsi,
ulemavu au hali yao katika jamii kwa namna ambayo watu wa aina fulani
wanafanywa au kuhesabiwa kuwa dhaifu au duni na kuwekewa vikwazo au masharti ya
vipingamizi ambapo watu wa aina nyingine wanatendewa tofauti au wanapewa fursa
au faida iliyoko nje ya masharti au sifa za lazima.


Napendekeza Ibara
125(1) irekebishwe kama ifuatavyo:

125(1) Bila ya kuathiri masharti yaliyomo
katika Ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa
Mbunge endapo:

(a) ni raia
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja
wakati wa kugombea;

(b) anajua kuongea,
kusoma na kuandika Kiswahili;

(c) ni mwanachama aliyependekezwa na chama
cha siasa au kikundi cha kijamii, au ni mgombea huru;



“Kikundi cha kijamii”
hapa ni vyama vya watu wenye hali na maslahi maalumu, kama vile wafanyakazi,
wakulima, wanawake, wazee, vijana, wasanii, waumini, wavuvi, wafugaji,
wafanyabiashara, n.k. Uwakilishi wa vikundi hivyo unatakiwa uwe huru – usidhibitiwe
na vyama au Rais. Hivyo wawakilishi wa
makundi hayo wasiteuliwe na Rais (angalia Ibara ya113(b)), au vyama vya siasa, bali
wachaguliwe moja kwa moja kwa kupigiwa kura na wanachama wa makundi hayo, na
wasilazimishwe kudhaminiwa na vyama vya siasa. Ni wazi kuwa hili ni pendekezo
jipya lenye mtazamo tofauti na ule wa Katiba, ambayo mtazamo wake unajikita
katika ubunge wa kupitia vyama vya siasa au watu binafsi tu.


Uzoevu wetu wa sasa wa
uteuzi wa Wabunge wa Bunge la Katiba uliofanywa na Rais umeonesha kuwa
wawakilishi wa vikundi wanaoteuliwa kwa utaratibu huo huenda wakamwakilisha
Rais na Chama chake badala ya kuwakilisha vikundi vinavyohusika.

Uongozi, Utawala Bora na Uwajibikaji

Miongoni mwa mambo
yanayoweza kuvuruga umoja na mshikamano wa kitaifa unaopendekezwa na Katiba ni
udhaifu au ubovu wa uongozi. Suala hili rasimu ya Katiba imelizungumzia sana,
na hata imeweka masharti na miiko ya uongozi (Sura ya 3 ya Katiba). Hata hivyo,
ili kuwa na uongozi bora, haitoshi tu kuweka maadili na miiko ndani ya Katiba,
bali inatakiwa pia kuwa na mifumo ya udhibiti na usimamizi wa viongozi walioko
madarakani.  Miongoni
mwa mifumo hiyo ni:

·      Uwazi
katika utendaji wa serikali na vyombo vyake;

·     
Udhibiti
wa madaraka ya viongozi kwa njia ya Bunge, mahakama n.k.

·      Uhuru
wa vyombo vya habari

·      Bunge huru lisilodhibitiwa na chama
kimoja na lenye wabunge wengi wasiotoka katika vyama vya siasa

·      Uwezekano
wa kiongozi, akiwamo Rais, kushitakiwa na hata kuvuliwa madaraka pindi
anapovunja maadili

·     
Vyombo
imara vya kudhibiti ufisadi.

Katiba hii inatoa
mwanya wa kuwadhibiti viongozi, lakini wakati huo huo inaufinya mwanya huo
kuhusiana na Rais kwa kuruhusu Bunge pekee kumshitaki, na kuzuia watu wengine
kumshtaki kwa makosa ya jinai aliyofanya akiwa madarakani
au kabla au baadaye:

Ibara ya 87:

87(1) Wakati Rais akiwa madarakani,
hatashitakiwa wala mtu yeyote hataendesha mashtaka ya aina yoyote dhidi yake
mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai….

(3) Isipokuwa
kama ataacha kushika madaraka ya Rais kutokana na kuondolewa madarakani na
Bunge, haitakuwa halali kwa mtu kumshtaki au kufungua mahakamani shauri lolote
la jinai au la madai dhidi ya mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya
kuacha madaraka hayo kutokana na jambo alilofanya wakati alipokuwa bado
anashika madaraka ya Rais.


Ibara hii ni
mbaya na iondolewe; itasaidia kulinda ufisadi. Katika kipindi cha miaka 50
tangu tupate uhuru, Watanzania tumeona aina mbalimbali za Marais, wengine
waadilifu, wengine wezi na mafisadi. 
Kama Rais ni mwizi, fisadi, mbakaji, muuaji au mhalifu wa kivita, hakuna
sababu ya kumlinda kikatiba; ashitakiwe na kupata adhabu yake. Kutoa uwezo wa
kumshitaki Rais kwa Bunge tu ni njia tu ya kumlinda, hasa iwapo Bunge limejaa
wabunge wa chama chake.

Ibara ya 40 (3) inasema:

Raia wa Jamhuri ya Muungano hatapelekwa katika nchi ya nje yoyote kujibu
mashtaka au kufanyiwa mahojiano ya aina yoyote kinyume cha ridhaa yake,
isipokuwa kwa mujibu wa sheria za nchi na mikataba ya kimataifa na wajibu wa
nchi katika uhusiano wa kimataifa….

Ingawa kijuujuu
kifungu hiki kinaonekana kuwalinda “raia”, lakini  kwa hakika kinawalinda viongozi. Na bila
shaka kifungu hiki kinamhusu Rais pia.  Sasa
kama mtu huyo hawezi kushtakiwa hapa nchini, na hawezi kushtakiwa nje ya nchi (ICC
Uholanzi?), atashtakiwa wapi?  (Hivi sasa
Marais wa Afrika wanafanya kampeni ya kuzuia wenzao wasipelekwe The Hague katika
mahakama ya ICC kushtakiwa kwa makosa ya mauaji ya halaiki wanayotuhumiwa
kuyatenda).

Pendekezo:Ibara ya  87
irekebishwe kama ifuatavyo:

87(1) Wakati Rais akiwa madarakani,
hatashitakiwa wala mtu yeyote hataendesha mashtaka ya aina yoyote dhidi yake
mahakamani kwa ajili ya kosa lolote la jinai isipokuwa Bunge tu. Hata hivyo,
itakuwa ni halali kwa mtu kumshtaki au kufungua mahakamani shauri la jinai au
la madai dhidi ya mtu aliyekuwa anashika madaraka ya Rais baada ya mtu huyo kuacha
madaraka hayo kutokana na jambo alilofanya kabla, wakati au baada ya kushika Urais.

Rais au kiongozi au raia yeyote wa
Tanzania anayetuhumiwa kutenda makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu au ufisadi
ulikothiri anaweza kupelekwa kujibu mashtaka nje ya nchi kwa mujibu wa sheria
za Kimataifa.

MUHTASARI
WA MAPENDEKEZO/ MAPENDEKEZO MADOGOMADOGO

      
 Ibara ya 19: kuh.mali ya umma, ongeza
kifungu:


      
 …kiongozi wa umma hatajimilikisha au kujiuzia au
kuuziwa mali ya umma kama vile ardhi, nyumba, gari au mitambo wakati wa uongozi
au baada ya kutoka katika nafasi yake ya uongozi;…

Ibara ya 24(5):
rekebisha suala la ubaguzi wa aina yoyote katika hali na fursa, ikiwa ni pamoja
na kipingamizi cha kielimu kwa wagombea wa Ubunge [pia 34(1)]; hivyo ibara
itaoana na(35)(2):  “Kila mtu ana haki na
fursa sawa kushika nafasi yoyote  ya  kazi,
uongozi au shughuli yoyote iliyo chini ya mamlaka ya nchi.

– Ibara ya 36 (1):Haki za
wafanyakazi: Ongeza  haki ya kugoma ili kudai maslahi bora baada ya njia nyinginezo
kushindwa.

Ibara ya 40 (1): Kuna haki ya kuweka watu kizuizini? Ni mamlaka
yapi yamepewa haki hiyo?

Ibara ya 40 (1): Mazingira si suala la mtu binafsi tu; serikali
inawajibikaje?(k.m. miundo mbinu ya maji taka; kutunza misitu, mito na
maziwa, kuwekeza katika nishati mbadala, kuzuia uchafuzi unaotokana na kelele, n.k.)?

Ibara ya 42(1):
Inatoa haki ya elimu bora ya msingi bila malipo. Elimu ya msingi hapa ieleweke
kuwa ni hadi Kidato cha IV.

Ibara ya 43 (1):
Haki za mtoto – si kupewa jina la uraia tu, bali pia kulinda utamaduni na
utambulisho wake.

Ibara ya 44: Haki na wajibu wa vijana si
kushiriki katika maendeleo tu, bali pia katika ulinzi wa Taifa lao.

Ibara ya 47 (1): Haki za wanawake:
ongeza “haki ya kumiliki na kurithi mali”

Ibara ya 59:  Ifafanue vizuri haki za mtu huyo mwenye asili
ya Tanzania

Ibara za 60-69: Hizi zinahusu muundo wa
shirikisho la serikali tatu. Rasimu imejaribu kutekeleza matakwa ya
makundi-tawala yenye maslahi katika muundo wa aina hiyo, lakini katika kufanya
hivyo imelegeza muungano hadi kuufanya ukaribie kupoteza maana. Muundo
unaopendekezwa unaelekea zaidi kwenye ushirikiano
kuliko muungano. Unaweza kuwa na
maana tu iwapo utakuwa ni hatua ya awali ya kwenda kwenye Shirikisho la Afrika
Mashariki. Vinginevyo, huenda ukatupeleka kwenye utengano. Muundo wa serikali
mbili ulikuwa unalinda vizuri utambulisho wa Zanzibar; utambulisho wa Tanzania
Bara haukuhitaji kulindwa kwa kuwa haukutishiwa na Zanzibar au Muungano. Kilichoikwamisha
Zanzibar hata ikashindwa kuendeleza watu wake vizuri zaidi si muungano tu, bali
pia siasa na sera zake za ndani zilizodhibitiwa na kikundi kidogo cha wateuliwe
kilichozifuja rasilimali zilizokuwapo kwa jina la “mapinduzi.”

      
Ibara ya 60 (1): Kinahitajika kifungu kinachozibana serikali za
Zanzibar na Tanganyika zisikiuke Katiba hii katika Katiba zao na utendaji wao.

 Ielezwe kuwa Katiba hii ndiyo Katiba Mama;
Katiba za Tanganyika na Zanzibar sharti zikubaliane na masharti ya Katiba hii;
chochote kilicho nje kitakuwa batili.

      
72(1)(j) na (k):Kutoa msamaha kwa wafungwa na
kuidhinisha adhabu ya kifo yanaweza kuwa majukumu ya Marais wa Tanganyika na
Zanzibar badala ya kuwa ya Rais wa Muungano, ila kama wahusika wamekata rufaa
kwa Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho.

      
Ibara ya 79(d):Umri wa mtu kuruhusiwa kugombea
Urais ushushwe hadi miaka 35.

       Ibara ya 79(e):“Shahada ya chuo cha elimu ya juu”
ni ipi? Haiko wazi. Hoja muhimu ingekuwa ni kwamba awe na elimu ya kutosha ya
darasani au inayolingana nayo.

       Ibara ya 88(5):Tume ya kumchunguza Rais isiwe na
wajumbe walioteuliwa naye katika nyadhifa walizo nazo (k.m. Jaji Mkuu wa
Jamhuri anateuliwa na nani?)

       Ibara ya 103:Masharti ya mawaziri kuhudhuria
vikao vya Bunge yamebana mno; wao ndio wawakilishi wa serikali Bungeni, hivyo
ni bora wahesabiwe kuwa Wabunge kwa mujibu wa nyadhifa zao, kama alivyo
Mwanasheria Mkuu, na wahudhurie vikao vya Bunge wakati wote bila haki ya kupiga
kura. Bunge haliwezi kusimamia serikali ambayo haiko Bungeni kupokea maagizo na
mapendekezo ya Bunge hilo.

-Dhana ya
“Waziri Mwandamizi” haina tofauti na ya Waziri Mkuu isipokuwa labda katika
maslahi.

Ibara ya 113 (2):  Wabunge wa kuwakilisha walemavu au kikundi
chochote cha watu wasiteuliwe na Rais, bali wachaguliwe na walemavu wenyewe (au
wanakikundi wanaohusika) kupitia vyama au vikundi vyao, na wasipitie vyama vya
siasa (wanaweza kuhesabiwa kuwa wabunge binafasi kwa mujibu wa Katiba hii).
Kanuni hii hii itumike kwa makundi mengine: vijana, wanawake, makundi ya
kiimani, wafugaji, wafanyakazi, wakulima wadogo wadodo, wafanyabiashara, n.k.

Ibara ya 113 (3-4): majimbo 75 ya
uchaguzi yataainishwa vipi? Kama ni kimikoa, kuna haja ya kuweka utaratibu wa
uundaji wa mikoa ili kuzuia ufisadi wa kisiasa kutumika katika uundaji huo kwa
lengo la kuwezesha chama fulani au watu fulani kuingia au kubakia katika
madaraka.

Ibara ya 113 (3): kuweka nafasi za wabunge
2 – mwanamke na mwanamume kunatoa picha kwamba mgawanyiko au mtafaruku mkubwa
nchini ni kati ya wanawake na wanaume, hivyo wanahitaji uwakilishi sawa. Je
hivyo ndivyo ilivyo? Huu ni uwakilishi wa kitakwimu usioendana na uhalisi. Uzoevu
wetu unaonesha kuwa wanasiasa wanawake na wanaume Bungeni mara nyingi
huwakilisha kundi au tabaka lilelile, mawazo yaleyale na maslahi yaleyale. Kuwa
na wanawake wengi Bungeni hakuna maana kuwa wanawake wanyonge (ambao ndio
wengi) watawakilishwa. Aidha, iwapo katika miaka 50 ya uhuru aghalabu tumekuwa
na wabunge wengi zaidi wa kiume (pengine hadi 70%), kuna ubaya gani kuwa na
wabunge wanawake wengi zaidi ya wanaume iwapo watawakilisha vizuri maslahi na
matakwa ya wapiga kura? Aidha, uteuzi wa wagombea ubunge ndani ya vyama vya
siasa vinavyodhibitiwa na wanaume utahakikishajie kuwa wanateuliwa wagombea
ambao ni wawakilishi wa kweli wa maslahi ya wanawake ni si ya wanaume waliowapitisha?

Ibara ya 117: Ongeza kipengele kuwa
“sheria inayotungwa na Bunge la Muungano na ambayo haikiuki masharti ya Katiba
hii itakuwa na nguvu katika pande zote mbili za Muungano.”

Ibara ya 121(1-2): Haiko wazi; kwa nini Bunge lisitunge sheria kuhusu
mambo hayo yaliyotajwa  iwapo linaona
inahitajika? Kwa nini kibali cha Rais kitangulie wakati hatimaye Rais
atahitajika kutia sahihi?

Ibara ya 125(1):Sifa za kuchaguliwa kuwa Mbunge
zirekebishwe kama ifuatavyo:

-Kipengele
cha elimu ya Kidato cha IV kiondolewe, maana kinawanyima haki ya kuchaguliwa
takriban 70% ya Watanzania.

– Kipengele
cha kujua Kiingereza pia kondolewe kwa sababu kinawabagua Watanzania walio wengi,
wakiwamo wenye digrii (iwapo watapewa mtihani nina hakika wengi wao hawatapita)

-Kipengele (
c) pia kirekebishwe; watu wengine huwa wanafungwa kwa sababu za kisiasa za
kutetea wanyonge; hivyo kufungwa isiwe sababu ya kumnyima mtu haki ya kugombea.
Kipengele hicho kinaweza kutumiwa vibaya na wanasiasa (hasa chama kilichoko
madarakani) kuwanyamazisha wapinzani wao kwa kuwazulia kesi za kufungwa.

– Ibara ya 128(1):
sababu za mtu kukoma kuwa Mbunge zirekebishwe ili zisitumiwe vibaya: k.m. (d)
“kizuizi gerezani” huweza kufanywa makusudi ili kumuondoa mtu Bungeni; (g)
kuondoka katika chama cha siasa isiwe sababu ya kuacha Ubunge, bali mbunge huyo
aendelee na ubunge akiwa Mbunge binafsi asiye na chama, maana alichaguliwa na
wananchi wa jimbo lake, si wanachama wa Chama chake tu. Hii itaimarisha uhuru
wa mawazo na kujieleza ndani ya vyama na Bungeni.

       Ibara ya 135(1):Umri wa kuwa Spika uteremshwe hadi
miaka 35.

       Ibara ya 136:Fafanua majina ya wagombea wa
Uspika yatapatikanaje?

       Ibara ya 158:Jaji Mkuu achaguliwe na Jopo la
Majaji kutoka pande mbili za Muungano; asiteuliwe.

       Ibara ya 169:Sioni sababu ya msingi kwa nini
majaji wa Mahakama ya Rufaa wawe “raia wa kuzaliwa” wakati kazi waifanyayo ni
ya kitaaluma/kiweledi zaidi.

       Ibara ya 193(1)(d):Tume Huru ya Uchaguzi isiwe na
madaraka ya kugawa majimbo ya uchaguzi; majimbo yaainishwe kikatiba. Mathalan,
kila mkoa ungeweza kuwa jimbo moja,
na mikoa  isibadilishwe ovyoovyo bali
itajwe kikatiba.

       Ibara ya 195(1):Mkurugenzi wa Uchaguzi asiteuliwe
na Rais, bali aainishwe na kuteuliwa na Tume Huru ya Uchaguzi au chombo
kinginecho.

      
Ibara ya 200 (1):Mwenyekiti wa Tume ya Maadili
asiteuliwe na Rais.Vinginevyo itaingiliwa kinyume cha
Ibara ya 206(1).

       Ibara ya 209:Tume ya Haki za Binadamu isiteuliwe
na Rais bali iainishwe Kikatiba.

       Ibara ya 225(1):Matumizi maalumu na ya dharura
yafafanuliwe – maelezo yanaacha mwanya wa kutumiwa vibaya.

       Ibara ya 237(1):Rais hawezi kuwa Mwenyekiti wa
Baraza ambalo yeye si mjumbe; aorodheshwe miongoni mwa wajumbe.

       Ibara ya 250(1):Viongozi wa nchi washirika wakiwa
na mamlaka juu ya viongozi wa Polisi na Usalama walio chini ya Muungano
utendaji utakuwaje? Naona kuna utata. Labda inahitajika Polisi ya
Tanganyika/Zanzibar nje ya ile ya Shirikisho.

Ibara ya 231(c):
Ugharimiaji wa serikali na shughuli za Muungano unahitaji ufafanuzi zaidi.
Mathalan, kila Mshirika atachangia kiasi gani (fomula gani itatumika? K.m. asilimia
fulani ya GDP?). Hatimaye itakuwa lazima
kuwa na kodi maalumu na tozo za Shirikisho (Federal Tax). Hivyo kila mwananchi
atalazimika kulipa kodi mbili (kama ilivyo Marekani).

Lugha na Uwasilishaji

Tume imejitahidi
kuandika Kiswahili kizuri na sanifu. Kuna makosa madogomadogo ya matumizi,
tahjia na sarufi ambayo yanaweza kurekebishwa baada ya wabunge kukubaliana
kuhusu maudhui.Mifano:

·      Disemba
=> Desemba

·      kuwepo,
kuwemo, n.k. => kuwapo, kuwamo…

·     
kuelekeza
kwa lengo => kuelekeza kwenye lengo

·      Mahali pengi rasimu inatumia istilahi “rushwa” na
“ubadhirifu” badala ya “ufisadi” ambayo ni istilahi jumuishi.Kuna
sababu yoyote?

·      taasisi
=> asasi

·      “sekretariati”
=> lingeweza kuwa “Seketaria” ili kupunguza ukakasi.

·      mwanamme
=> mwanamume.

Pendekezo
hapa ni kwamba baada ya Bunge kukubaliana kuhusu maudhui, wanasheria na
wataalamu wa lugha wakae pamoja na kuuhariri mswada wa Katiba bila kupotosha au
kubadilisha maudhui yaliyokubaliwa.

M.M.
Mulokozi (Profesa Mstaafu), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Februari 2014