Juzi tarehe 11 Oktoba, Ndugu Salim Himid Msoma aliaga dunia. Yamkini kwa kizazi chetu cha vijana wa leo, jina hili ni geni kwenye ngoma za masikio yao na mboni za macho yao.
Kwa bahati mbaya hata mimi, kutokana na ukweli kuwa tumefahamiana na Salim Msoma nusu muongo na ushei tu uliopita, sina uhalali wa kutosha wa kuandika Tanzia inayoweza kuichora vizuri safari yake ya kimaisha, fikra na misimamo yake.
Ambacho nina uhalali nacho kwa hakika na ndicho ninakifanya kwenye andiko hili ni kumlilia Ndugu yangu Salim Msoma kwa vile kwa kipindi hicho kidogo nilichomfahamu na kwa machache niliyosimuliwa na kuyasoma juu yake, ni dhahiri kuwa alikuwa mjenzi mzuri wa hoja, mjamaa moyoni mwake, mpenda haki na mtu muungwana sana.
Kazi ya kumuelezea vizuri inaweza kufanywa vyema na Makomredi wenzake ambao miaka ya sitini kupitia Chama chao cha kiharakati Cha USARF (University Students Revolutionary Front-USARF) na jarida lao la “Cheche” (lililopigwa marufuku baadaye na Serikali ya Mwalimu Nyerere) walijipambanua hususani kwenye fikra za ujamaa na umajumui wa Afrika (Pan Africanism).
VIDEO: Harakati za Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mwaka 1969
Sahibu zake wa enzi hizo, Rais Yoweri Kaguta Museveni, Prof. Issa Shivji, Prof. Karim Hirji, Mama Zakhia Meghji na wengine ambao bado wapo hai wanaweza kutueleza mengi ya ujana wake. Watusimulie matukio ya kusisimua ya enzi zao ikiwemo hatua ya baadhi yao kwenda kwenye mstari wa mbele wa vita ya ukombozi ya Msumbiji kwenda kupigana bega kwa bega na FRELIMO.

Kutoka kushoto Salim Msoma, John Saul, Karim Hirji, Farida Hirji na Pat Saul (Picha kwa hisani ya Karim Hirji)
Vilevile, wenzake katika safari yake ya utumishi wa umma kutoka Zanzibar na Bara, safari iliyomfikisha hadi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano wanaweza kutueleza sifa zake kwenye utumishi wa umma. Prof. Mark Mwandosya aliyekuwa Waziri wake yeye akiwa Katibu Mkuu, akipata wasaa anaweza kutujuza zaidi.
Pia, wenzake kwenye Bodi za Shirika la Ndege (alikopambana bila mafanikio kuinusuru Air Tanzania Company Limited-ATCL) na Mamlaka ya Bandari ambazo aliziongoza wanaweza kutueleza Salim Msoma alikuwa mtu wa namna gani hasa kiuongozi.
Mbali na kumsoma kwa mara ya kwanza kwenye kitabu cha Cheche: Remiscences of a Radical Magazine kilichohaririwa na Prof. Hirji, nilijuana na kufanya mawasiliano kwa barua pepe na Salim kwa mara ya kwanza mwaka 2016. Mwaka huo, chama chetu Cha ACT Wazalendo kiliandaa Semina ya Wajumbe wa Kamati Kuu kuhusu masuala mbalimbali ya uendeshaji wa chama kitaasisi. Tulimwalika Salim Msoma kutoa mada kuhusu ujenzi wa Oganaizesheni na Utawala wa Chama kwa kuzingatia uzoefu wake kwenye masuala ya kiutendaji na utawala. Ingawa hakuweza kuja, Salim amekuwa miongoni mwa wasomi ambao wamekuwa huru kutoa maoni mbalimbali ya kiuchambuzi kuhusu ACT Wazalendo.
Baadaye, nilionana na Salim nikiwa sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Mshikamano Kati ya Tanzania na Sahara Magharibi (Tanzania Sahrawi Solidarity Committee-TASSC) ambayo lengo lake ni kupinga kitendo cha Morocco, kinyume na sheria za kimataifa, kuendelea kuikalia kimabavu Nchi ya Sahara Magharibi. Salim akiwa Mwenyekiti wa Chama cha Mshikamano na Watu wa Cuba, alitushirikisha kwenye baadhi ya mambo ambayo aliona ni muhimu tuwe na msimamo wa pamoja.
Tofauti na baadhi ya wastaafu, Salim alikuwa mshiriki mzuri wa mijadala kwenye majukwaa mbalimbali ya makongamano na mitandaoni. Alikuwa mwepesi kutoa maoni yake hasa kuhusu Cuba, Sahara Magharibi, Palestina, haki na masuala mbalimbali yahusuyo historia na hatma ya Zanzibar.

Pichani Ado Shaibu akibadilishana mawazo na Ndugu Salim Msoma kwenye moja ya matukio ya Kavazi la Mwalimu Nyerere .
Mjadala uliovuta fikra za wengi ni ule uliomhusisha yeye, Balozi Ali Karume na Wakili Awadh Ali Said kuhusu kile wahafidhina visiwani wanakiita “Kuyaenzi Mapinduzi kwa gharama zozote”.
Balozi Karume alipodai kuwa Mapinduzi ya Zanzibar hayawezi “kupinduliwa” kwa uchaguzi, Salim alimjibu. Ninanukuu sehemu ya majibu yake kwa kirefu hapa chini:
Historia inatufunza kuwa hakuna Mapinduzi yeyote duniani ambayo yataweza kutunzwa na kuenziwa kwa kukandamiza demokrasia. Kama tunadai Mapinduzi yalindwe na kutukuzwa basi hatuna budi kukubali na kuenzi haki ya Wazanzibari wote kujichagulia viongozi wao wa kuyaendeleza na kuyalinda hayo Mapinduzi kwa kufanya chaguzi huru kila awamu ya maendeleo yao kisiasa.
Tabia ya wanasiasa waliopo madarakani kujivisha taji la ufalme wa ulinzi wa Mapinduzi bila ya kuchaguliwa na wananchi kuongoza serikali inayolinda Mapinduzi lazima ikataliwe. Kwani ukweli ni kuwa takriban viongozi wote wanaotawala leo sio tena wale waasisi waliopindua 1964 ambao ni wazee sana au wameshatangulia mbele ya haki.
Nathubutu kusema kuwa hivi sasa hakuna Waziri wa SMZ alieshiriki, kwa mfano uchaguzi wa mwisho kabla Mapinduzi Juni 1963. Hali kadhalika tabia na khulka ya kumsingizia kila anaehitilafiana na viongozi waliopo madarakani ni mpinga Mapinduzi ya 1964 ni hila na njama ya kukashifu na kupaka matope haki ya kila Mzanzibari kuwa na mawazo na fikra mbadala katika mjadala wa kisiasa.
Mwaka 2019 baada ya Maalim Seif na maelfu ya wenzake kujiunga na ACT Wazalendo tukio ambalo lilibadili moja kwa moja ramani ya kisiasa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, nilikutana na kubadilishana mawazo na Salim. Alinieleza kuwa kwa kutazama maslahi mapana ya vuguvugu la Wazanzibari, ACT Wazalendo tumefanya jambo muhimu sana kumpokea Maalim Seif na wenzake kwa heshima kubwa kwa sababu jambo hili limeendeleza harakati ya Wazanzibari ambayo ilitaka kufifishwa kwa kuvurugwa kwa Chama Cha CUF.
Nimeyapitia mazungumzo yetu ya barua pepe baada ya kupata habari za kifo chake na kugundua kuwa alikuwa amenitumia barua pepe 45! Nyingi zinahusu makala na habari mbalimbali ambazo Salim alidhani ni muhimu nizipate na kuzisoma. Nyingine zilihusu mialiko, maswali na hoja mbalimbali ambazo alizileta kwangu kutokana na nafasi yangu kwenye Chama au kile alichoona kufanana kwetu kifikra kwenye baadhi ya maeneo.
Katika kuhitimisha, sina maneno ya kumalizia zaidi ya kuazima maneno ya Dk. Chambi Chachage kuhusu kifo cha Ndugu Salim Msoma kuwa:
Kama msemo wa wahenga unavyosema, Mzee wa Kiafrika akifariki, ni maktaba nzima inakuwa imechomwa ardhini. Hili ni bayana pia kwa Salim Msoma. Pumzika Komredi!
Shukrani kwa maarifa na mijadala ndani na nje ya mitandao. Hakika maktaba imeungua, tumebakiwa na makavazi yako, tutayarejea daima!
Kwa hakika Salim Msoma alikuwa msomi, mzalendo na mwanaharakati mwenye fikra za ujamaa na umajumui wa Afrika. Alikuwa miongoni mwa wakereketwa wachache sana waliobaki ambao walifahamiana kwa karibu na Comrade Abdulrahman Babu na chama cha Umma Party visiwani Zanzibar. Kwa maana hii tumepoteza maktaba. Mimi nimemfahamu tangu tulipokuwa Chuo Kikuu miaka ya sitini na baadae tukashirikiana katika Kamati ya Mshikamanao na Cuba, akiwa mwenyekiti. Pumzika kwa amani Kamaradi Salum- Hamba kahle