Joakim Paschal Ishengoma
Tangu kugundulika kwa mgonjwa wa kwanza na maambukizi ya virusi vya corona katika mji wa Wuhan jimboni Hubei nchini China mwishoni mwa mwaka 2019, kesi za maambukizi mapya katika nchi nyingine yanazidi kuripotiwa sehemu tofauti tofauti ulimwenguni. Italia, Iran, Hispania, Ujerumani na Korea ya Kusini ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi nje ya China ambako ugonjwa huu ujulikanao kitaalamu kama COVID-19 uliripotiwa kwa mara ya kwanza. Hivi karibuni Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeujumuisha kuwa miongoni mwa magonjwa hatari ya mlipuko. Katika bara la Afrika, Misri ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza kuthibitisha mgonjwa wa COVID-19 huku Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi za hivi karibuni kuthibitisha mgonjwa mwenye virusi vya corona. Kwa mujibu wa takwimu zinazotolewa mara kwa mara na Chuo Kikuu cha John Hopkins, hadi kufikia tarehe 18/03/2020 nchi 155 zimethibitisha maambukizi na watu 198,178 wameambukizwa ugonjwa huu huku ukiwa umechukua maisha ya zaidi ya watu 7954.
Kwa wale ambao wamekuwa wakifuatilia kwa makini matukio juu ya COVID-19, watakuwa wamekutana na dhana ijulikanayo kwa Kiingereza kama #FlattenTheCurve au #FlatteningTheCurve. Kwa mujibu wa Dokta Anthony Fauci, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Mzio na Magonjwa ya Kuambukizwa nchini Marekani, inaweza kutumika dhidi ya kasi ya kuenea kwa COVID-19. Akielezea kuhusu dhana hii, anasema “ukiitazama kasi ya mlipuko, utagundua kuwa inapanda zaidi na kisha inashuka. Tunachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kuwa mlipuko unapokuwa chini basi unabaki chini palepale ambao utafanya kuwapo kwa watu wachache walioathirika hali ambayo itapunguza idadi ya vifo vile vile.”
Natambua kuna jitihada mbalimbali zinazoendelea za kuitafutia tafsiri rahisi ya Kiswahili dhana hii. Lakini katika makala haya ningependa kuitafsiri kama #PunguzaMlipuko. Kwa muktadha huu, kuzuia na/au kupunguza mlipuko ni mkakati unaohusu mapambano dhidi ya ongezeko la idadi ya waathirika wa virusi vya corona katika eneo au nchi husika. Fauci anairejelea dhana hii kama mkakati unaolenga kuongeza muda kwa gonjwa hili hatari hali ambayo itasaidia watoa huduma za afya katika jamii kutoelemewa na idadi kubwa ya waathirika wanaohitaji kuhudumiwa katika vituo na sehemu nyingine za kutolea huduma za afya.
Ukiutazama huo mchoro ubadilikao hapo chini kutoka kwa Matthew McQeen wa The Conversation utaona kuwa huo mstari wenye videshi au vidoti hapo katikati unawakilisha uwezo wa mfumo au sekta ya afya ambao unaweza kubaki hivyo hivyo au kuongezeka kadri muda unavyokwenda. Hicho kinachopanda chenye umbo kama la mlima, mlima, kichuguu, au tuta kinawakilisha idadi ya maambukizi. Kadri mlima, mwinuko, kichuguu au tuta hilo linavyopanda ndivyo maambukizi yanavyopanda na kadri linavyoshuka ndivyo yanavyoshuka. Kinachotakiwa ni kuhakikisha tunazuia na/au kushusha na kupunguza kupanda huko ili kuwa chini ya huo mstari unaowakilisha uwezo wa sekta yetu ya afya kutoa huduma. Kwa maana nyingine, ni kuhakikisha hali inakuwa ndani ya uwezo wetu wa sasa huku tukiendelea kuujenga uwezo huo katika hospitali, zahanati na vituo vyetu mbalimbali vya afya, vipimo, na tiba.
Hivyo, dhana hii dhidi ya mwendelezo na kasi ya kuenea kwa corona inaweka bayana njia, mikakati na mbinu sio tu za kuzuia bali kujikinga na maambukizi mapya ya COVID-19. Miongoni mwa mikakati inayotajwa ni pamoja na:
Kuhakikisha mifumo ya Huduma za Afya katika jamii inakuwa salama muda wote na haielemewi na idadi kubwa ya wagonjwa. Ripoti ya jarida la MarketWatch kupitia kwa Jacob Passy inasema kuwa kupitia ufanisi katika uboreshaji wa huduma za umma utasaidia kupunguza idadi ya maambukizi mapya tofauti na pale ambapo uboreshwaji wa huduma hizo hautachukuliwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya awali iliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia Wazee na Watoto nchini Tanzania kupitia waziri wake Mh. Ummy Mwalimu; mifumo yote ya huduma za jamii inapaswa kuwa na sabuni, maji na dawa za kuoshea mikono kabla au baada ya kupata huduma sehemu za umma. Maeneo hayo ni kama sehemu zenye mashine za bank kwenye ATM, vyoo vya umma, ukaguzi katika malango ya kuingia na kutoka kwa watu kutoka sehemu tofauti tofauti. Kuepuka safari na mikusanyiko isiyo ya lazima. Kuepuka kusalimiana na kukumbatiana, kukaa mbali na watu wanaohisiwa kuwa na dalili za maambukizi au historia ya kusafiri katika nchi zenye mlipuko wa ugonjwa wa corona.
Wizara imeendelea kutoa taarifa mbalimbali na kuweka msisitizo kuhusu umuhimu wa kujikinga na maambukizi. Picha hiyo hapo chini kutoka kwenye ukurasa wa pili wa Taarifa kwa Umma Kuwepo kwa Mgonja wa Corona Tanzaniani mfano mmojawapo. Kilicho muhimu sana ni kuhakikisha tunayatekeleza maelekezo hayo kwa kuzingatia dhana ya kuzuia na/au kupunguza mlipuko.
Kwa ujumla, dhana ya #PunguzaMlipuko dhidi ya kasi ya kuenea kwa maambukizi ya corona (#FlattenTheCurve) ni dhana inayolenga kuzuia au kupunguza matukio ya mlipuko na ongezeko la corona katika jamii hasa maambukizi mapya ambapo kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali wa masuala ya afya ya mwanadamu wanakiri kuwa mapambano hayo lazima yahusishe mkakati wa pamoja kwenye kuboresha huduma za kijamii kama zilivyoelezwa hapo juu. Lakini pia msisitizo unawekwa kutoa taarifa mapema pale unapohisi dalili za maambukizi ya corona zikiwemo homa na mafua makali, kuumwa kichwa, maumivu ya misuli na mwili kuchoka, kukohoa na kubanwa mbavu na kupumua kwa shida ili unapogundulika umeathirika uweze kupatiwa matibabu kabla athari haijawa kubwa.
Hakika hii ni dhana ambayo inaendana kabisa na msemo wetu wa heri kinga kuliko tiba, hivyo, tujikinge na kuwakinga wenzetu ili tuhakikishe sekta na mfumo wetu mzima wa tiba hauelemewi.





Sawasawa.
Sawasawa…kuna haja ya wataalamu wa masuala ya afya, elimu ya Istilahi na Lugha kuja na kisawe/msamiati utakaokuwa na umajumui katika kuielezea dhana ya "FlattenTheCurve".. Asante
Kongole kongole
Shukrani mkuu
Kongole mkuu nakubali sana
Akhsante sanaaa mkuu