Rais
Magufuli amemwelewaje Profesa Mkumbo?

Chambi Chachage

“Hapa Kasi Tu!” – Tangazo la
Vodacom la Tanzania 4G

Profesa wa Saikolojia ya
Elimu, Kitila Mkumbo, amemwagiwa sifa kemkem na Rais wetu, Dakta John Magufuli.
Tukio hili la aina yake lilitokea katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam tarehe 2 Juni 2016. Ni jambo linalostahili pongezi pale kazi ya
kiuwanazuoni inaponukuliwa na hivyo kuzingatiwa na watawala na watunga sera.

Katika hotuba hiyo
iliyojaa vijembe dhidi ya Wabunge waliotolewa Bungeni majuzi kufuatia sakata la
kung’ang’ania Bunge lijadili sakata la kurudishwa nyumbani kwa baadhi ya wanafunzi
wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Rais Magufuli
anasema
:

 “Nataka
nizungumze hapa hadharani. Unajua pamekuwa na wanasiasa wengine wana maneno. Wanataka
tupeleke watu, wakachukue Digrii, mafelia. Sijui kwa sababu wanasiasa hawa ni
mafelia? Ukiangalia kwenye ripoti iliyoandikwa na Profesa Mkumbo, mwanachama
mzuri wa ACT, alizungumza wanafunzi wasizidi 1,800 ambao wangeweza wakaenda
kwenye special training, hatukumsikiliza. Tumepeleka 7,802. Wengine ni
Divisheni 4. Wako wengini Divisheni 3. Na wachache sana Divisheni 1 na Divisheni
2 – kwenda Chuo Kikuu cha UDOM.”

Kuhusu kilichopeleka
Profesa Mkumbo kutosikilizwa, Rais anatanabahisha:

 “Nimezungumza na Profesa Kikula. Kasema
alilazimishwa. Angefanyaje? Afukuzwe Chuo? Wanafunzi pale wamekaa. Ukweli
hawana qualifications za kwenda kuchukua hata Diploma. Kwa sheria tulizojiwekea
kama nchi, ukimaliza Form 4, ukipata Divisheni 1 au 2 unaenda Form 5 au Form 6.
Au unaweza ukaenda kuchukua Certificate. Ukimaliza kuchukua Certificate utaenda
kuchukua Diploma. Certificate ni miaka miwili. Diploma ni mwaka mmoja. Tiyari
ni miaka mitatu. Ni hiyo hiyo. Lakini cha ajabu zaidi, wale wanafunzi wanasoma
pale Diploma, kwenye  vyuo vya ualimu vile
kumi havina wanafunzi. Nenda Kleruu. Nenda Butimba. Nenda wapi.  Havina wanafunzi wa kutosha. Na baadaye nao,
walipoona shida shida pale wakaanza mwongozo wa mgomo mgomo, ikanisaidia mimi
kujua kuna nini pale. Unajua kuna migomo mingine ya haki haki, kuna migomo
mingine inasaidia kuondolewa tu. Ndipo nikaja nikajua qualifications zilivyo.
Nikasema hawa watu lazima waondoke. Na nilikuwa nasubiri Chuo Kikuu cha Dodoma
nao wagome, wote wangeondoka! Ni lazima tujenge principles za kujenga heshima
ya nchi yetu. Nimeshukuru wale vijana wameondoka. Wanasiasa hao hao, ati hawa
vijana wamekosa pa kulala, wamefanya nini. Nonsense. Taifa letu tuliweke mbele
kwanza, siasa zije nyuma. Na ndiyo maana mimi namsifia hapa Profesa Mkumbo
pamoja ya kwamba ni wa ACT na mimi ni CCM, kwa sababu alitoa mwongozo mzuri.
Ifike mahali Watanzania tukubali ukweli. Tuache siasa kwenye masuala ya msingi.

Swali la kujiuliza hapa ni:
Je, Profesa Kikula hakuzingatia kitu chochote alichosema Profesa Mkumbo kwa
sababu alishinikizwa na “wakubwa” waliokuwa katika Serikali ya Awamu ya Nne ya
Rais Mstaafu Kikwete? Wadadisi wa mambo tumepata fursa ya kumhoji kwa undani Profesa
Mkumbo leo kuhusu ripoti hiyo waliyoiwasilisha mwezi Septemba 2014. Majibu
tuliyoyapata yanatufanya tubaki na maswali mengi kichwani.

Mosi, kwa hakika timu ya
Profesa Mkumbo iligundua kwamba mwaka 2014 UDOM ilikuwa na rasilimali – yaani
walimu, maabara, madarasa na fedha – zinazotosha kudahili wanafunzi 1080 tu.
Lakini pia ilisisitiza kwamba kama UDOM inataka kudahili seti nyingi zaidi ya
idadi hiyo, basi itabidi ziendane na uwiano wa vipindi vya ufundishaji
vitakavyokuwa vinafanyika kwa siku. Kwa maana hiyo, kama ikitaka kudahili seti
mbili – yaani maradufu – ili wawe wanafunzi 2160 basi ingebidi kuwe na vipindi
viwili kwa siku. Kanuni hii ya ukokotoaji iliwafanya wahitimishe kwamba itabidi
UDOM iongeze rasilimali maradufu, au hata mara tatu, kwa kadri ya idadi ya
wanafunzi itakaotaka kuwadahili. Kwa mantiki hiyo, tunaweza kusema ingehitajika
kuongeza rasilimali takribani mara saba ili kuwadahili wanafunzi wapatao elfu
7.

Pili, timu ya Profesa
Mkumbo iligundua kwamba kulikuwa na maabara manne ya sayansi ambayo ujenzi wake
ulikuwa bado haujakamilika. Hivyo, wakapendekeza kwamba ujenzi uharakishwe. Kwa
maana nyingine, tunaweza kusema kuongezeka kwa rasilimali hizi kungeweza
kuiwezesha UDOM kuongeza idadi ya wanafunzi.

Tatu, akina Profesa
Mkumbo waligundua kwamba walimu waliokuwepo wakati huo – yaani 171 – wanatosha
kufundisha tu wanafunzi wapya 1,080 kwa uwiano wa 1: 6. Hivyo  walipendekeza waongezwe kwa kuwa walikuwa wanafundisha
wanafunzi wengine pia. Lakini kwa mantiki hiyo hiyo, tunaweza kusema bado
ingebidi UDOM iongeze rasimali watu ili kukidhi hitaji la kuongeza zaidi udahili
wa wanafunzi hao.
 

Je, hakuna chochote
kilichozingatiwa miezi mitatu baadaye?
Chama cha Wafanyakazi
wa Elimu ya Juu (THTU) Tawi la UDOM kinadai
hiki ndicho hasa kilichotokea
:

 “Kuanzia Novemba 2014, Chuo Kikuu cha Dodoma
kilianza kupokea wanafunzi wa kusomea stashahada maalum ya diploma ya Elimu,
Sayansi, Hisabati na Tehama (DE-SMICT). Lengo kubwa la programu hii maalum ni
kutimiza azma ya serikali kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo la walimu wa
sayansi katika shule za sekondari nchini. Serikali iliamua kuwaleta wanafunzi
hawa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) badala ya ku[wa]peleka kwenye vyuo vya ualimu
ikiamini kwamba UDOM kuna miundombinu ya kutosha hasa majengo na [rasilimali watu]
ya kutosha kuweza kuhifadhi wanafunzi hao. Menejimenti na jumuiya nzima ya UDOM
iliona ni heshima kupewa jukumu hili na kulipokea kwa mikono miwili. Kukubaliwa
na kupokelewa jukumu hili UDOM ililazimika kujipanga upya kimkakati, kimfumo
pamoja na kufanya mabadiliko kadha wa kadha katika utendaji wake wa kila siku
ili kuweza kuhimili jukumu hili kubwa la kitaifa. Mojawapo ya hatua
zilizochukuliwa ilikuwa kuunda Kikosi Kazi (Steering Committee-SC) cha kushauri
namna ya kukabili jukumu hili.”

THTU
kinaendelea kusisitiza kwamba kabla “ya kuanza kufundisha, SC ilipendekeza
mikakati, mifumo na mabadiliko yaliyokuwa ya msingi ili kukabili swala hili.
Changamoto kubwa, ilibainika ni, ufundishaji wa hawa vijana. Masuala
mengine yahusuyo malazi na malezi kwa ujumla wake yaliandaliwa ingawa hayakuwa
na changamoto kubwa kama suala la UFUNDISHAJI. Suala la ufundishaji
lilihitaji jicho la pekee kwani vijana hawa waliopokelewa ndiyo kwanza
wamemaliza kidato cha nne, hivyo bado ni wadogo kwa kiasi fulani na pia
hawakupaswa kufundishwa kama wenzao wanaosomea masomo ya shahada na
kuendelea
.”

Kuhusu udahili wa awali,
THTU inasema: “
Vijana takriban 2000 walipokelewa,
wakafundishwa na (semester) [muhula] wa kwanza ukamalizika vizuri bila migogoro
mikubwa.” Kama idadi hii ni sahihi, basi tofauti yake na kilichoshauriwa na
akina Profesa Mkumbo ni wanafunzi 920. Lakini kama rasilimali ziliongezeka
katika kipindi hicho cha miezi mitatu, je, tunaweza kuhitimisha hawakumsikiliza
Profesa?

 

Na,
je, huu mfumo wao wa kuwagawa haushahibiani na lile pendekezo la Profesa
Mkumbo: “Masomo yote ya UALIMU yawe na wanafunzi 120 katika mkondo mmoja”;
“Masomo yote ya SAYANSI ASILIA yawe na wanafunzi 80 kwa mkondo mmoja”; “Masomo
yote ya TEHAMA yawe na wanafunzi 60 kwa mkondo mmoja”?

Kwa
mujibu wa THTU, tatizo lilianza hivi: “Kutokana na ufanisi uliopatikana katika
mwaka wa masomo 2014/15, Serikali na UDOM waliamua kuleta tena wanafunzi
wengine kwa muhula wa 2015/16. Idadi ya hawa wanafunzi ni takriban 6000.
Kulingana na idadi hii kuwa kubwa mno, upatikanaji wa waalimu wa sayansi
wanaoweza kuenea/kutosha mikondo yote iliyogawanywa ulishindikana.”

Lakini,
je, Profesa Mkumbo alisema haiwezekani kudahili wanafunzi 6000? Au alisema
ukitaka kudahili wanafunzi wengi inabidi uongeze rasilimali kadri
unavyowaongeza, yaani, kwa uwiano stahiki? THTU inadai kwamba jitihada
zifuatazo za kuiongezea UDOM uwezo zilifanyika ila zikagonga mwamba:

“Ili
kuhakikisha kuwa wanafunzi hawarudi nyumbani wala kwenda barabararani, uongozi
wa CNMS [Koleji ya Sayansi Kavu na
Hisabati] 
ulijitahidi
kuushirikisha uongozi wa chuo na kuomba msaada kila palipoonekana kuhitajika
msaada huo. Baadhi ya maswala muhimu yaliyotakiwa kushuhulikiwa ni kuwaongezea
uwezo wa kupata waalimu wa ziada, kupata sehemu za kufundishia na kupata vifaa
vya maabara. Hata tunapoandika hivi sasa, DVC-PFA, pamoja na kupokea nyaraka
mbali mbali zinazomwomba aagize vifaa na madawa ya maabara (laboratory
equipments and reagents) hajanunua hata kitu kimoja. Wanafunzi wamefundishwa
bila kupewa mazoezi ya vitendo yanayokidhi mahitaji kwa sababu za kiburi cha
DVC-PFA. Katika jitihada za kutafuta waalimu wa ziada, DVC-ACR amekataa
katakata kutoa mwongozo wa kimaandishi ama ushauri wowote utakaowasaidia
viongozi wa CNMS kuboresha hali ya ufundishaji.”

 Jumuiya ya
Wanataaluuma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) nayo
inadai
:

“Mgogoro
huu umepotoshwa kutokana na ukweli kwamba [walimu] wanalazimika kufundisha
historia ya [sayansi] badala ya sayansi kwa vitendo.Ukosefu wa nafasi na vifaa
vya maabara ni tatizo kubwa ambalo limelalamikiwa kwa muda mrefu lakini hoja
inayoonekana zaidi ni malipo ya waalimu. Mfano katika Chuo cha Sayansi Asilia
na Mahesabu kinachohusika na masomo ya Fizikia, Kemia, Baolojia na Hesabu
maabara zake hazina vifaa vya kutosha kukidhi mahitaji ya ufundishaji pamoja na
koleji husika kutuma maombi karibu kila mwaka.”

Katika
mazingira haya, ni vigumu kwa wadadisi wa mambo kuamini kwamba wanafunzi
waliorudishwa nyumbani wamerudishwa kwa sababu akina Profesa Kikula
hawakumsikiliza Profesa Mkumbo kuhusu kudahili wanafunzi 1080. Tunachoona ni
kwamba Serikali haikusikiliza ushauri wake kuhusu kuongeza rasilimali za
kutosha.

Matokeo
yake wanaodaiwa kuwa “wanafunzi hewa” wanatumbuliwa hata kabla Waziri wa Elimu
hajajiridhisha kikamilifu. Kama umakini mkubwa wa kujiridhisha umefanyika, kwa
nini Rais Magufuli amesema maneno haya jana: “Ninafahamu Profesa Ndalichako
anapitia ili orodha ya vijana wa UDOM waliofaulu, Divisheni 1 na Divisheni 2,
tutahakikisha tunawetengenezea mazingira ya kwenda kusoma. Waliofeli wakatafute
mbinu nyingine za kujiunga na vyuo vyenye saizi yao”? 

Hata
kama kuna waliomo na wasiokuwemo, waliofeli na waliofaulu, ni pedagojia gani
hiyo inayofundisha kusimanga wanafunzi hadharani kuwa ni “vilaza”? Hivi
Saikolojia ya Elimu aliyoibobea Profesa Mkumbo inasema nini kuhusu hili? Ni
udhaifu kwa Serikali kukiri kosa na kuomba msamaha? Ni nini hasa kimepelekea
uharaka huu wa kuwarudisha nyumbani vijana kana kwamba walijidahili wenyewe?

Je,
hizi ni zama za hapa kazi tu au hapa kasi tu?