RASIMU HII YA KATIBA ITATETERESHA NA HATIMAYE KUVUNJA MUUNGANO
Utabiri wa Mtoto wa Mkulima
Mjadala wa Rasimu ya katiba ya
kwanza na ya pili umejikita zaidi katika mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba
kuwepo kwa Muungano wa Serikali Tatu. Msukumo wa kuitaka hoja hii ikubalike
umetuondolea umakini wa kutathmini hata huo muundo wa Serikali tatu unaopendekezwa.
Cha kushangaza zaidi ni pale wajumbe wa Tume wakiongozwa na Jaji Warioba
mwenyewe, wanapotutaka tuukubali mfumo wa Serikalu tatu bila tafakuri. Rai
yangu kwa Watanzania ni kuwa ‘tusifunge milango ya kujifunza kuhusu katiba
tunayoitaka eti kwa kuwa tu Tume, chama cha siasa, ‘Jukwaa la katiba’, au nguli
mwingine yeyote ametushawishi tuikubali’. Nadhani tuwapongeze Tume ya Katiba
kwa kazi nzuri kwa sababu kuna baadhi ya mambo kwenye hiyo Rasimu ni muhimu
sana. Lakini Tume haina budi ituachie uhuru wetu wa kuijadili Rasimu hii na
kuitolea maoni na maamuzi kwa nafasi zetu. Mimi ningependa kuchukua nafasi
yangu kama mtabiri tu. Natumia uhuru
wangu wa kujieleza kutokana na Kifungu cha 18 cha katiba na wajibu wangu kwa
taifa kama mwanazuoni. Mwaka 2012 mchambuzi na mtabiri wa masuala ya kisiasa Mutahi Ngunyi (Kenya) alitabiri kabla
ya uchaguzi kuwa Ushirika wa JUBILEE (Uhuru Kenyatta na William Ruto) nchini
Kenya ulishashinda uchaguzi huo tangu
tarehe 18 Disemba 2012 pale tu daftari la kuandikisha wapiga kura lilivyofungwa
rasmi. Kwa maono yake, ingawa hakupenda litokee hilo, walakini JUBILEE ilikuwa
na mtaji mkubwa zidi ya CORD (Raila Odinga) katika kile alichokiita ‘the tyranny of numbers’. Watu wengi
waliunanga utabiri huo, lakini mwisho wa siku sote tunafahamu yaliyotokea.
Nadharia ya miungano ya Profesa
Mwesiga Baregu, inatuambia kuwa kuna misukumo ya aina nne inayozifanya nchi ziungane.
Wa kwanza ni upendo/udugu na historia
ya ushirikiano ambayo nchi hizo imekuwa nazo. Ya pili ni nchi kutarajia kuwa itanufaika kiuchumi/maendeleo ndani ya muungano. Tatu, ni tishio la kushambuliwa kivita huzifanya nchi kuungana ili ziwe
salama zaidi. Nne, nchi moja yenye nguvu
kulazimisha nchi ingine/zingine kuwa katika muungano kwa kuwa ina uwezo wa
kulipa gharama za kuendesha muungano. Kwa ujumla, misukumo hiyo hutegemeana na
mazingira halisia ya nchi hizo au ukanda huo. Kwa Tanzania, ingawa, udugu na historia ya pamoja ndio tunavyovisisitiza
katika utangulizi wa Rasimu, walakini wachambuzi wengi wamewahi kuandika tangu
miaka ya 1960 kuwa ni tishio la ndani juu ya ulinzi na usalama wa nchi na lililotokana
na ‘vita baridi’ kuwa ndio mambo yaliyotusukuma kuungana mwaka 1964. Ningependa
kuafikiana na hoja hii, lakini swali la msingi katika mjadala wetu ni mambo
gani yanatusukuma kuendelea kuwepo kwenye muungano baada ya miaka 50 sasa?
Kiuhalisia, udugu na historia ya
pamoja ni misukumo dhaifu sana. Historia inatuonyesha kuwa misikumo hii
imeshindwa kuulinda Muungano wa Somalia na Somaliland, kama vile ilivyoshindwa
kuzuia Eritrea isijitenge kutoa Ethiopia. Kwa Tanzania bado msukumo huu ni
dhaifu pia. Msukumo wa tishio, ingawa
umekuwa na nguvu siku za nyuma, hauna mashiko tena. Watu watazungumzia siasa za
ndani na mashindano ya kushika Dola kwa upande wa Zanzibar, lakini tumechagua
mifumo ya kidemokrasia na nchi hizi mbili, Zanzibar na Tanganyika zinaweza
kujiendesha bila wasiwasi. Msukumo wa nguvu
unakosa uhalisia kwa Tanzania kutokana na hali yetu ya kiuchumi. Sio Tanganyika
wala Zanzibar mwenye uwezo wa kulazimisha muungano na kubeba gharama zitokanazo
na muungano huo. Lakini msukumo ya kunufaika
kimaendeleo ya kiuchumi ndio msukumo ambao unaleta maana zaidi kwa kuwa ndio
ambao unazifanya jumuiya nyingi Afrika na kwingineko ziendelee kuundwa na kudumu. Kwa tathmini
yangu Rasimu hii ya katiba
itateteresha Muungano na baadae kuuvunja kabisa kwa sababu zifuatazo:
Kwanza, inatengeneza Serikali
ambayo itakosa Uhalali kwa Raia. Uhalali ninaouzungumzia hapa sio ule tu wa
kupiga kura ya maoni na kupitisha katiba, bali wananchi kuendelea kuiona
Serikali yao inafaa muda hadi muda. Kwa mujibu wa mambo ya Muungano, Serikali hii
itatoa huduma za aina mbili tu kwa wananchi. Itatoa hati za kusafiria na
kushughulikia mambo ya uhamiaji, na pili itatoa ‘ulinzi na kuhaikisha usalama
wa raia na mali zao’. Ingawa hizi huduma ni za muhimu, lakini ni vigumu kuamini
kuwa hivi ndio vipaumbele vya Watanzania. Yawezekana utendaji wa hao walinzi wa
amani na usalama utaboreshwa, lakini ilivyo sasa wengi wao tunawaona kama
‘maadui kuliko walinzi’. Natabiri kuwa Serikali inayotengenezwa na Rasimu hii itakuwa
ni ya kujihudumia zaidi (self serving)
kuliko kuhudumia wananchi. Ibara ya 10 (c) ya kwenye Rasimu inayozungumzia
uwezeshwaji wa kiuchumi ni kama matakwa (wishes)
tu ambayo Serikali hiyo haitayatekeleza kwani siyo mambo ya Muungano. Matokeo
yake basi Serikali hii itakosa uhalali wa kuendelea kuwepo, kwani haitagusa
vipaumbele vya wananchi kama vile afya, elimu, ujenzi wa miundombinu n.k.
Nachelea kufikiri kuwa tutakuwa na Rais ambaye atanadi sera ya kutujengea
mahusiano mazuri ya kimuungano na kimataifa, amani na usalama (tu) wakati sisi watoto
wa wakulima tunataabika na umaskini! Kwa mtazamo wangu Rasimu hii inaikuza tu
iliyokuwa Wizara ya Muungano na kuiongezea mamlaka ya kidola.
Pili, Rasimu hii inaunda Serikali
ambayo, ingawa itakuwa na nguvu za kijeshi, lakini itakosa nguvu za kiuchumi. Ibara
ya 231 ya Rasimu inaonyesha vyanzo vya mapato ya Serikali. Yawezekana
ukusanywaji wa mapato utaboreshwa zaidi, kama vile faini za Trafiki barabarani,
na ushuru wa bidhaa, lakini Tume ya Katiba ilitambua wazi kuwa mapato hayo
hayatatosha kuendesha Serikali, ndipo wakapendekeza kuwepo kwa michango kutoka
kwa Serikali washirika. Ukiangalia Mashirikisho yaliyopo duniani, kama vile
Marekani, Urusi, Canada na Australia, mpango wa Tanzania ni wa kipekee. Mbaya
zaidi ni kuwa upekee huu hausaidii kujenga muungano. Rasimu hii inatungenezea
Serikali ya Muungano itakayoendeshwa kwa kutegemea maelewano mazuri kati ya
Rais wa Muungano na wale wa Serikali washirika. Huu ni msingi dhaifu wa
kuendesha Serikali. Na serikali isiyo na mapato ya uhakika ni kama ‘kasha
tupu’. Ripoti ya Tume inaonyesha walitathmini muundo wa Shirikisho la Urusi.
Cha kushangaza, hawakutilia maanani shirikisho hilo ambalo kwa makusudi kabisa
limeweka biashara za kimataifa, rasilimali za shirikisho na kodi za shirikisho
kuwa mambo ya Muungano wao. Inashangaza pale Rasimu (Ibara ya 228) inapoipa Serikali hii mamlaka
ya kukopa wakati haitakuwa na vyanzo vya mapato ya uhakika ya kulipa deni hili!
Tatu, natabiri hatari ya kuwepo
kwa misuguano kati ya Serikali ya Muungano na Serikali Washirika ambayo itazua
maswali kuhusu uhalali wa muungano. Katika suala la kuchangia uendeshwaji wa
Serikali ya Muungano, Rasimu haituambii itakuwa katika uwiano gani! Ripoti
zinaonyesha katika kipindi cha nyuma Zanzibar walikuwa wanapata mgao na sio
kuchangia uendeshwaji wa Serikali ya Mungano. Katika uwiano wowote wa kuchangia
utakaopangwa, ni rahisi kwa Tanganyika na Zanzibar kuona kuwa Serikali ya
Muungano ni ya ‘kinyonyaji’ kwa kuwa itanyang’anyana mapato na Serikali
washirika ili ikajihudumie wakati wao wana jukumu kubwa la kuwahudumia wananchi
na ambao ni walipa kodi. Nachelea kufikiri nini kitatokea kama watakaoongoza
Serikali hizi, watatoka katika vyama tofauti vya siasa!
Nne, napenda kusisitiza kuwa wanaosema kuendesha Serikali ya Muungano kutaongeza gharama wasibezwe hata kidogo. Uendeshaji
wa Ofisi ya Rais na Makamu wake, Bunge, Mahakama, Wizara 15, Balozi zote za
Tanzania na Taasisi zingine za kimuungano sio jambo dogo. Gharama hii kwa sasa,
imejificha ndani ya muundo wa Serikali mbili. Nafahamu kuwa kuna mambo ambayo
katiba ya Muungano ya sasa inayatambua kama Mambo ya Muungano lakini
hayaendeshwi kimuungano. Muundo wa serikali mbili uliifanya Tanganyika kubeba
mzigo huu bila kujua uzito wake. Profesa Samuel Mushi alishawahi kuandika kuwa
muundo wa serikali tatu utawafanya Tanganyika na Zanzibar kutambua na kuzitetea
rasilimali zao dhidi ya Serikali mshirika (economic
nationalism). Mimi nasisitiza kuwa muundo huu utawafanya wananchi waanze kuuliza
maswali hata kuhusu kugharamia Muungano. Kwa kuwa hawatapata majibu
ya kuridhisha, watakosa imani na muungano.
Rasimu hii inatuandaa kisaikolojia
kuuvunja muungano. Ibara ya 269 ya Rasimu inatuambia kuwa (c) kutakuwa na
mgawanyo wa rasilimali (e) mgawanyo wa watumishi na (f) mgawanyo wa madeni.
Hupaswi kuwa ‘nguli’ kujua kuwa huu ni mwanzo wa kutengana rasmi. Wanatuambia ‘tunapaswa
kujiandaa kusaikolojia kukubaliana na muundo wa muungano wa serikali tatu’. Tatizo
sio serikali tatu, tatizo Serikali hiyo itasimamia mambo gani, na ipo kwa ajili
ya nani? Katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Taifa, Mwalimu
Nyerere anasema, walipounda Muungano wa Serikali mbili, waliangalia uhalisia wa
nchi hizi mbili kigiografia (ukubwa wa nchi), idadi ya watu, na uchumi wao.
Hawakutaka kurudufisha tu miundo ya kanda zingine bila kuangalia uhalisia wa
mazingira yao. Mambo haya bado yana umuhimu leo kama ilivyokuwa 1964. Napenda Watanzania
watambue kuwa, pamoja na kuwa kulikuwa na kero za Muungano, lakini ni muundo wa
serikali mbili ulioufanya Muungano wetu udumu hadi leo hii.
Kama tunataka muundo wa Serikali
tatu, eti ili kudumisha utambulisho wa Tanganyika kwa kuwa tunawatukuza sana
wakoloni waliotuita Tanganyika, na kwa maslahi ya kisiasa (tuongeze nafasi za
kiuongozi ili kila mtu apate kula, au baadhi yetu tunaodhani kutarahisisha
namna ya kushika mamlaka ya nchi), si budi basi Serikali ya Muungano
tukaiongezea meno ya kiuchumi na kuipa jukumu la kutuletea maendeleo. Tunaitaka
Serikali ya Muungano: Mosi, ikusanye
kodi zote (baadhi ya kodi zinaweza kuachwa kwa Serikali washirika ili waendeshe
mambo yao yasiyo ya muungano). Pawepo na ushirikiano na serikali washirika juu
ya kukusanya kodi hizo. Pili, Serikali ya Muungano ikope kwa niaba ya
shirikisho kwa kuzingatia uwiano sahihi na mahitaji ya nchi washirika. Tatu,
Serikali ya Muungano idhibiti biashara za nje. Nasisitiza, ili Serikali hii ya
Muungano ipate uhalali wa kuendelea kuwepo, ni vyema pia ikawa na wizara za
kimuungano zitakazotoa hudumu moja kwa moja kwa raia. Napendekeza hapa wizara
ya Uchumi na Mipango itakayokuwa na ushirikiano wa moja kwa moja na taasisi za
kimaendeleo za nchi washirika. Wizara hii inaweza kutekeleza Ibara ya 10 (c)
kwa umakini mkubwa. Napendekeza pia ziwepo wizara zitakazoshughulikia suala la
Elimu na Afya, kwani wizara hizi ndio uti wa mgongo katika taifa linalokusudia kupunguza
umaskini na kuleta ustawi wa jamii.
Ningependa kutanabaisha kuwa,
Serikali ya Muungano na katiba yake haitalindwa kwa mtutu wa bunduki wala Ibara
ya (8), (9), (69) na (119) zinazolenga kuweka vikwazo ili muungano usivunjwe,
bali kukubalika kwake na wananchi. Hata nchi zilizojitenga zilikuwa na katiba
na mtutu wa bunduki ambavyo havikusaidia. Tunahitaji kuitazama Rasimu hii kwa
jicho la uhalisia na sio ushabiki wa aina yeyote, au tu kwa fikra kuwa mawazo
ya Nyerere yamepitwa na wakati na sisi tunataka mabadiliko. Kuonja ni kuzuri
sana lakini angalia usije ukaonja sumu. Pale ambapo Mwenyekiti au Wajumbe wa
Tume wanainadi Rasimu hii, ningependa watueleze na matatizo ya mambo
wanayoyapendekeza, ambayo yapo wazi katika ripoti zao.
Hitimisho: Katika moja ya makala
zake katika gazeti la Citizen, Dkt. Kitila Mkumbo alitabiri kuwa Muundo wa
Serikali tatu utasambaratishwa katika Bunge la Katiba kwa kuwa CCM, ambao
hawaungi mkono serikali tatu, wanauwakilishi mkubwa katika Bunge hilo. Kwa
maoni yangu, kama utabiri wa Mkumbo utatimia, CCM watakuwa wamejali maslahi ya
Taifa kwa kiwango kikubwa sana kama wataamua kuukataa muundo huu. Kujali
maslahi ya taifa, na kukataa vitu visivyotufaa sio suala la sera ya chama, bali
ni utashi. Ingawa naamini wapo watu ndani ya CCM tangu zamani wanaotaka
serikali tatu. Mwisho, tuna zaidi ya miaka 20 sasa tangu Demokrasia ya vyama
vingi ianzishwe a miaka 50 ya muungano. Naamini wananchi wana upeo mkubwa sasa
kuweza kuamua mambo yao wenyewe. Hatuna sababu ya kutumia njia ndefu kuuvunja
muungano. Ni vyema wananchi wakaamua kidemokrasia kuendelea na muungano au la!
—
Richard Mbunda
Mhadhiri Msaidizi, Idara ya
Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. rmbunda@gmail.com