Utangulizi

Nia hasa ya uchambuzi huu ni kutoa ushauri kwa wakristo katika suala la kujikinga na Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19). Wengi wetu tunavyojua ugonjwa huu ni hatari na umeua watu wengi duniani kwa kipindi kifupi sana. Ni janga la dunia linalogusa kila familia kiafya, kiuchumi, kijamii na kiroho. Hivyo, ni muhimu wakristo kuwa mstari wa mbele kujikinga na kuzuia maambukizi dhidi ya ugonjwa huu kwa sababu zifuatazo:

Kwanza, katika kipindi hiki cha janga la mlipuko wa UVIKO-19, kumekuwa na nadharia nyingi potofu zinazosababisha watu kuamini kwamba ugonjwa huu sio wa kweli, kwamba hakuna janga la dunia (pandemic denialism), ugonjwa huu umetengenezwa, barakoa zimewekewa vimelea vya ugonjwa, mashine za kusaidia kupumua (ventilators) zinaua watu, chanjo hazifai na mambo mengine potofu mengi yanayoshangaza. Kwa bahati mbaya, tetesi na nadharia potofu zimeshika kasi pengine kuliko habari sahihi na za kweli kuhusu ugonjwa huu na kinga zake. Nyingine zimechukua taswira ya kiroho, na kusababisha wakristo wengi kuchanganyikiwa, wakikataa tahadhari za kinga, hasa chanjo. Nafasi ya kanisa ni kueleza ukweli. Kueleza ukweli juu ya afya na hatua za kisayansi ni sehemu ya injili ambayo kanisa limehubiri kwa muda mrefu kupitia hospitali zao.

Pili, wakristo hufanya shughuli za ibada makanisani mahali ambapo kuna mikusanyiko ya watu, wakiimba, kusali na kushirikiana kwa ukaribu. Kama pasipokuwa na tahadhari madhubuti, ibada zinaweza kuwa na hatari kubwa sana ya kusambaza ugonjwa huu, na kusababisha watu kuugua, na kupoteza maisha, labda bila hata wahusika kufahamu sehemu walipopatia maambukizi.

Tatu, tangu mwanzo wa janga hili hadi hivi karibuni, viongozi wa kikristo (Kanisa Katoliki, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Kanisa la Waadventista Wasabato na Assemblies of God) wamekuwa wakitoa nyaraka mbalimbali kuwaasa waumini wao kuchukua tahadhari wakati wa maambukizi ya virusi vya korona. Nyaraka hizo zilisaidia sana kupunguza maambukizi yaliyokuwa yanazidi kuongezeka kwa ajili ya watu kukutana bila kuchukua tahadhari. Watu huthamini sana miongozo ya kichungaji inayotoka kwa walezi wa kiroho pengine kuliko hata ile inayotoka kwa viongozi wengine wa jamii. Lakini kwenye suala la chanjo, viongozi wengi wamechelea kutoa muongozo bayana kwa waumini wao na wengine wamefikia hata kuwaelekeza waumini wao kukataa chanjo.

Makala haya yanalenga kuongea na mkristo wa kawaida kuelimisha kuhusu njia za kujikinga na ugonjwa huu, na kujadili wajibu wa kila mkristo katika kupambana na kuutokomeza kabisa ugonjwa huu ambao umesumbua dunia kwa zaidi ya miezi 18 sasa.

Kutokana na maelezo hayo hapo juu, sisi kama wakristo na wanazuoni, tunapenda kuainisha kwa maelezo sababu kumi za kwa nini ni muhimu kila mkristo kupata chanjo.

  1. Chanjo zinaokoa maisha

Kwa zaidi ya mwaka sasa, wakristo kote ulimwenguni wamekua wakifanya maombi rasmi mara nyingi Mungu atoe suluhisho la janga la UVIKO-19. Chanjo nyingi zilianza kufanyiwa utafiti na baadhi kuthibitishwa kuwa na ufanisi wa kuzuia ugonjwa huu. Upatikanaji wa chanjo bora na salama, ndani ya muda mfupi sana katika historia ya utengenezaji wa kinga ya magonjwa ya mlipuko, umeonekana na wengi kuwa kama ‘muujiza wa kisayansi’.

Hadi sasa kuna chanjo 29 zilizoidhinishwa na nchi mbalimbali. Lakini ni 7 tu zimeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani na kuwekwa kwenye mpango wa COVAX, mpango ulioanzishwa ili kusaidia nchi maskini ziweze kupata chanjo kwa gharama nafuu. Chanjo hizi 7 ni:

Chanjo hizi zimeonesha ufanisi wa hali ya juu sana katika kuzuia ugonjwa mkali na vifo.

Ufanisi hupimwa kwa njia kuu mbili:

Pamoja na kwamba chanjo hizo 7 zimeonesha ufanisi wa hali ya juu katika utafiti wa majaribio ya kitabibu zilizosababisha kuidhinishwa kwa matumizi,9–15 baadhi ya nchi zimefanya utafiti halisia wakati wa matumizi na chanjo hizo zimeonesha tena ufanisi halisia wa hali ya juu sana. Nchi hizi ni Uingereza (Pfizer na Oxford/Astrazeneca),16–20 Israeli (Pfizer),21,22 Marekani (Pfizer, Moderna na Johnson & Johnson),23,24 na Bahrain (Sinopharm, Pfizer, Oxford Astrazeneca na Sputnik).25

Baada ya kuja kwa aina mpya ya kirusi cha korona kiitwacho delta (11/05/2021), ufanisi wa chanjo dhidi ya maambukizi ulionekana kupungua kidogo, lakini bado chanjo zimeonekana kuwa thabiti katika kuzuia ugonjwa mkali, kulazwa na vifo vitokanavyo na delta.17,20,25–27 Kwa mfano, hivi karibuni nchini Afrika Kusini chanjo ya Johnson & Johnson imeonekana kuwa na ufanisi mkubwa katika kukabiliana na delta pamoja na aina zingine za kirusi cha korona.28

  1. Chanjo ni jibu la maombi kwa Mungu kutukinga na UVIKO-19

Chanjo za korona zilizoidhinishwa na Shirika la Afya Duniani sio za ‘majaribio’ bali zimethibitishwa kuokoa maisha ya watu wengi sehemu mbalimbali duniani. Kwa mfano, ufuatiliaji wa karibu wa takwimu za afya ya jamii nchini Uingereza, unaonesha hadi juma linaloishia tarehe 26/08/2021, muitikio wa chanjo umekadiriwa kuzuia ugonjwa mkali na kulazwa (hospitalisation) kwa watu 143,000; na kuepusha vifo vya watu kati ya 102,500 na 109,500.27 Tukiangalia matokeo haya kwa jicho la kikristo, hatuachi kustajaabia kazi kubwa ambayo Mungu ameifanya kwenye kipindi kifupi sana kupitia wahudumu wa afya na wanasayansi, ya kuokoa maisha ya watu wengi waliokuwa wakifa, kwa mamia na maelfu kila siku.

Wakristo kukosa mwelekeo bayana na chanya kuhusu chanjo, inamaanisha kwamba hatutambui kazi kubwa ambayo Mungu tayari ameshaifanya kujibu maombi ya watu wake dunia nzima, waliomlilia usiku na mchana, kuomba suluhisho la ugonjwa huu. Pia inatukumbusha enzi zile za Agano la Kale, wakati Musa alivyomsimamisha nyoka wa shaba jangwani:

Watu wakaenda kwa Musa wakamwambia, “Tumetenda dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu na wewe. Mwombe Mungu atuondolee hawa nyoka.” Kwa hiyo Musa akawaombea watu. BWANA akamwambia Musa, “Tengeneza nyoka na umweke kwenye nguzo. Na itakuwa kila anayeumwa, akimwangalia huyo nyoka atapona,” Kwa hiyo Musa akatengeneza nyoka wa shaba naye akamweka juu ya nguzo. Na kila mtu alipoumwa na nyoka na kumwangalia huyo nyoka alipona (Hesabu 21:7-9)

Ni maombi yetu kwamba wakristo wengi wasikatae chanjo na kuangamia kwa kukosa elimu ya chanjo au maarifa yatakayowasaidia kufanya uamuzi sahihi. Ni maoni yetu kwamba, viongozi wa makanisa mbalimbali wangetamka waziwazi kuwashauri waumini wapate chanjo kwa ajili ya kujikinga wao binafsi, na kuwakinga wengine dhidi ya UVIKO-19.

  1. Kila mkristo ana wajibu wa kujilinda na kulinda afya za wengine

Ingawa dawa na afua (interventions) za kiafya (pamoja na chanjo) huwa ni hiari ya mtu, chanjo ni tofauti na afua nyingine za afya kwa sababu ina faida mbili. Kwanza, kutoa kinga binafsi kwa yule aliyechanjwa. Pili, kutoa kinga ya jumla kwenye jamii (community immunity/herd immunity).

Faida hiyo ya pili ni ya muhimu zaidi kuliko ya kwanza. Hii ni kwa sababu ndio inasaidia kutokomeza janga la magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Ingawa kupata chanjo ni hiari ya mtu binafsi, matokeo ya kupata au kutopata chanjo, yanaathiri jamii nzima, ama kwa faida au kwa hasara.

Mtu anayekubali chanjo, huwa amechangia kuleta kinga ya jamii. Anayekataa chanjo, ingawa hajachangia kinga ya jamii, hufaidika kwa uamuzi wa yule aliyekubali chanjo. Lakini watu wengi wakikataa chanjo basi wanapunguza au kuzuia jamii kwa ujumla kufaidika na kinga. Kadri watu wengi zaidi wanavyochanjwa ndivyo jamii inavyopata kinga ya jumla.

Chanjo hupunguza sana uwezekano wa kupata au kusambaza maambukizi ya korona. Kwa mfano, chanjo iliyopo nchini Tanzania sasa hivi ya Johnson & Johnson, imeonesha uwezo wa kupunguza uwezekano wa maambukizi kwa asilimia 76.7.23 Ina maana bado kuna uwezekano asilimia 23.3 wa kupata na kueneza maambukizi, uwezekano ambao ni mdogo na wa muda mfupi sana kwa sababu wanaopata maambukizi baada ya kuwa na kinga kamili ya chanjo (breakthrough infections) huugua kidogo na kwa muda mfupi tu (siku kama 3-4). Asiyepata chanjo, na bila kuchukua tahadhari yoyote, huwa na uwezekano mkubwa (100%) wa kupata na kueneza maambukizi kwa watu wengine, hata kama yeye binafsi hana dalili yoyote – huweza kueneza maambukizi kwa muda wa siku 10 au zaidi.29

Kwa maana hiyo basi, mtu aliyekataa chanjo, anaweza kupata maambukizi kwa urahisi sana na kuyasambaza kwa wengine. Kwenye ibada, kama kuna mtu mmoja mwenye virusi vya korona, na mtu mwingine mwenye udhaifu (vulnerable) na wote hawajapata chanjo, wala hawajavaa barakoa, ni rahisi sana kueneza maambukizi na kusababisha mtu kuugua ugonjwa mkali, na hata kufa kwa UVIKO-19, ugonjwa ambao kwa sehemu kubwa unazuilika.

Ingawa chanjo hazipunguzi maambukizi kwa asilimia 100, afua zote za kinga zikichukuliwa kwa pamoja – yaani chanjo pamoja na barakoa, pamoja na kukaa mbalimbali, pamoja na kupunguza muda wa mkusanyiko, pamoja na kunawa mikono mara kwa mara – uwezekano wa maambukizi hupunguzwa kwa kiasi kikubwa sana.

Mambo mengine yasiyozuilika au tusiyoyajua, hudhibitiwa na Mungu mwenyewe ambaye tumeshamuomba. Lakini Mungu anatutegemea sisi tujipatie maarifa na kutenda yaliyo sahihi katika uwezo wetu aliotupatia, kwa kumtii na kumpenda yeye, ikidhihirishwa na jinsi ambavyo tunawatendea binadamu wengine – kwa kuwajali na kuwakinga. Mwanafunzi Mpendwa wa Yesu alilitambua hilo alipoandika ujumbe huu:

Mpenzi wangu, nakutakia mafanikio mema ya kila aina; nakutakia afya njema

ya mwili kama ulivyo nayo rohoni (1 Yohana 3: 1)

  1. Kupata chanjo ni kutenda haki, kusambaza upendo na kujenga amani

Neno la Mungu na injili ya Kristo inasisitiza kupenda na kutoa haki. Tunaelezwa kuwa ufalme wa Mungu ni Haki, Amani na Upendo. Mambo haya matatu yanategemeana. Haki huimarisha amani na upendo.

Kazi kuu ya ukristo ni kujenga ufalme wa Mungu na tunajenga ufalme huu kwa kutenda matendo ya haki, amani na upendo. Haki inaanza na kuwajibika (angalia sababu ya 2 hapo juu) kwa maamuzi yako binafsi ambayo yana athari kwako mwenyewe, yanamuathiri mwingine au kuathiri jamii kwa ujumla. Kwa kuwa chanjo haikulindi wewe tu bali pia jamii nzima, ni muhimu kwa kila mkristo kupata chanjo kama tendo la haki kwenye jamii.

Aidha, chanjo ni ishara ya upendo maana ni tendo la kujali wengine. Kama wakristo, tunausiwa kumpenda jirani yetu. Bwana Yesu Kristo alisema, “mpende jirani yako kama nafsi yako”. Hivyo, ingawa chanjo ni hiari, mkristo ana jukumu la kufanya maamuzi yanayozingatia upendo. Tena Bwana Yesu anatuambia hiyo ni moja ya amri kuu.

Tukitafakari hili kwa kina tunaona umuhimu wa mkristo kupata chanjo. Chanjo inajenga amani kwa kuwa ugonjwa wa UVIKO-19 ni hatarishi kwa usalama wa dunia na pia kwa watu binafsi. Kwa muda mfupi, watu wengi duniani na nchini Tanzania wamefariki kwa ugonjwa wa UVIKO-19 kuliko waliofariki kwa vita au machafuko ya kisiasa. Hivyo, tuko kwenye vita ambayo suluhisho lake ni amani. Chanjo ni njia moja fanisi zinazoweza kuleta amani katika jamii. Hivyo, mkristo akipata chanjo ametenda haki, kujenga upendo na kusambaza amani.

Kwa kuwa kuna viongozi wa kiimani wamepinga chanjo kama suala la kiroho, ni muhimu wakristo waelimishwe kuhusu umuhimu wa chanjo kwa kuangalia Injili ya Kristo na mafunzo ya kweli yanayozingatia neno la Mungu na kazi ya kanisa duniani.

  1. Kupata chanjo ni tendo la Imani

Wakristo wengine wanafikiria kwamba kukataa chanjo ya UVIKO-19 kunaonesha jinsi imani yao ilivyo thabiti kwa Mungu. Wanaofikiria hivyo wangekuwa katika nafasi ya Yesu kwenye kinara cha hekalu, wangeepuka kutumia ngazi kushuka chini na kuamua kujitupa chini ili kuthibitisha kwamba kweli wanaamini ahadi za Mungu. Lakini hiyo sio imani bali ni uzushi (presumption) – ni kile Yesu alichokiita ‘kumjaribu Mungu’:

Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako’ (Mathayo 4: 5-7)

Ni wakati gani kumtumaini Mungu kunakuwa kumjaribu Mungu? Mtu anapochukua hatua zinazomweka katika hatari ili amlazimishe Mungu amwokoe. Tuepuke uongo wa Ibilisi. Imani ya kweli hudhihirishwa kwa matendo mema. Yakobo anauliza:

Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? (Yakobo 2:14)

Kisha Yakobo anajibu:

Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu (Yakobo 2:17-18)

Hivyo basi, imani yetu ituhamasishe kuchukua hatua sahihi. Mungu anao uwezo wa kutubariki bila sisi kufanya chochote, lakini biblia inakemea uvivu. Vivyo hivyo, Mungu anaweza kutulinda bila chanjo, lakini ni wajibu wetu kuchanjwa.

Kuchanjwa ni udhihirisho wa imani yetu katika vitendo. Hii ndiyo aina ya imani inayotunusuru. Na ndiyo maana wale wanaochanjwa wengi wapo salama.30

  1. Chanjo za UVIKO-19 zilizoidhinishwa ni salama

Kuna tetesi nyingi za uzushi zinazokuza madhara ya chanjo za UVIKO-19 ili kuficha ukweli na kukatisha watu tamaa wasipate chanjo. Ukweli ni kwamba kwa watu wengi sana, chanjo hazina madhara makubwa isipokuwa maudhi madogo madogo, kitu ambacho ni cha kawaida kwa dawa na chanjo nyingine. Maudhi ya chanjo ni kama kuumwa kichwa, homa, uchovu wa mwili, na mahali palipochomwa sindano kuuma – na kwa kawaida, yote haya huisha ndani ya siku mbili tu. Kwa watu wengi, maudhi yanaweza yasijitokeze kabisa.

Madhara makubwa ya chanjo ni ya nadra sana, na hutokea ndani ya mwezi mmoja, na uwezekano wa kutokea ni mdogo kuliko uwezekano wa kupata ajali ya gari. Kwa mfano, mtu 1 kati ya 2,900,000 waliopata chanjo ya Johnson & Johnson anaweza kufa kwa tatizo la kuganda damu kutokana na chanjo hiyo.31 Uwiano huu ni mdogo sana ukilinganishwa na uwezekano wa kufa kwa ajali ya gari. Kwa Tanzania, takwimu za mwaka 2019 zinaonesha kuwa takribani watu 3 kwa kila watanzania 100,000 wako kwenye hatari ya kufa kwa ajali za barabani.32 Nchini Uingereza kila mwaka mtu 1 kati ya 20,000, huweza kufa kwa ajali ya gari,31 Hata hivyo,pamoja na hayo hakuna mtu anayesita kupanda gari.

Zaidi ya hapo, aliyekataa chanjo akipata UVIKO-19, ana uwezekano mkubwa (asilimia 30-70) wa damu kuganda kwa sababu ya korona.33 Kwa kifupi, uwezekano wa kuganda damu au kufa kutokana na chanjo ni mdogo sana na nadra ukilinganisha na uwezekano wa kuganda damu kutokana na maambukizi ya UVIKO-19 kwa mtu ambaye hajapata chanjo.

Wakristo wengi wakielimishwa, wataridhia kuvumilia maudhi madogo madogo ili kuchangia ile faida kubwa ya kinga ya jamii, ambayo inaweza kuokoa maisha ya wengi.

Ingawa chanjo ni hiari, kama inavyoainishwa na Serikali ya Tanzania, kwa wakristo, Yesu aliagiza wema wa wafuasi wake uwe zaidi ya ule wa Waandishi na Mafarisayo (Mathayo 5:20). Kama mkristo mmoja anayo fursa ya kutenda mema kwa jamii, kuokoa maisha ya wengi kwa gharama ndogo sana binafsi (maudhi madogo madogo ya chanjo), basi kwetu wakristo, fursa hiyo inatakiwa tuichukulie kama wajibu. Hivyo basi, msukumo (motivation) wa chanjo kwa mkristo, si sahihi kuishia tu kwenye kujifikiria faida yake binafsi au afya yake mwenyewe, bali pia kama dhamira ya kujali mchango wake kusaidia afya ya jamii kwa ujumla wake.

  1. Kukataa chanjo huchangia kudorora kwa tahadhari nyingine

Kukataa aina moja ya kinga, huchangia kuzorota kwa tahadhari nyingine. Kwa mfano, wakati viongozi wa makanisa waliposisitiza kuhusu kuchukua tahadhari, waumini wengi walisikiliza na kutii. Walipoacha kusisitiza na kupuuzia uwepo wa ugonjwa, au walipolikalia kimya suala la chanjo, waaumini nao waliacha kuchukua tahadhari nyingine. Ukipata fursa ya kutembelea makanisa mengi utaona kwamba hata utaratibu wa kuvaa barakoa wakati wa ibada umeachwa na kwingine hata na maji tiririka na sabuni kwa ajili ya kunawa mikono hakuna.

Sayansi inaonesha kukiwa na mkusanyiko wa watu ndani ya jengo, pasipo na mzunguko mzuri wa hewa, watu wakiongea au wakiimba bila kuvaa barakoa, hushirikiana hewa inayopumuliwa (shared respiratory air with expired aerosols). Kama wote hawajavaa barakoa, hatari ya maambukizi huwa ni kubwa.5,34 Kukiwa na hatari kubwa ya maambukizi inamaanisha kwamba kama mtu mmoja tu ana virusi vya korona (hata bila kuwa na dalili), maambukizi huweza kutokea kwa vile vimelea vya kirusi huyu hudumu angani kwenye hiyo hewa wanayoshiriki kwa muda mrefu. 5 Iwapo kwenye mkusanyiko huo kuna mtu mmoja tu mwenye udhaifu kiafya (vulnerable person) basi madhara ya maambukizi yatakuwa makubwa.

Hivyo basi, ingefaa wakristo tuwe na mwelekeo chanya kuhusu kinga zote zilizothibitishwa (zikiwemo chanjo dhidi ya UVIKO-19). Kufanya hivi kutasaidia sehemu za ibada zisiwe sehemu za kusambaza magonjwa na kusababisha vifo.

  1. Kufa kwa sababu ya kutojikinga kwa makusudi siyo mapenzi ya Mungu

Mojawapo kati ya ujumbe mkuu kutoka kwa wachungaji na wakristo wengi wakati wa misiba, ikiwa ni pamoja na inayosababishwa na korona, ni kwamba mapenzi ya Mungu yametimia. Kwa upande mmoja inafariji kujua kwamba aliyefariki alikuwa amekaa vizuri na Mungu. Pia tunakubali kabisa kwamba mapenzi ya Mungu hukamilika kwa njia mbalimbali.

Lakini usemi wa ‘mapenzi ya Mungu’ unaweza kusababisha watu kuacha kuwajibika kwa kuchukua tahadhari, au kwa kutathmini mambo yaliyosababisha mtu kupata maambukizi. Kwa upande mwingine ukizungumzia kuhusu matendo ya binadamu yaliyosababisha mtu fulani kuugua na kuzidiwa hata kufa, mara nyingi hukatizwa na sauti zinazosema, acha tu maana yote hayo ni mapenzi ya Mungu. Hivyo basi, kunakuwa na utamaduni unaojijenga wa kutotathmini matendo yetu na kutumia ‘mapenzi ya Mungu’ kama kisingizio cha kuficha kutowajibika kwetu.

Tunaamini inaweza kuwa mapenzi ya Mungu kwa mtu kufa, lakini kwamba ni kifo gani kinamkuta mtu, hasa kwa sababu zitokanazo na afya, hilo liko mikononi mwetu. Ni wajibu wetu kutenda haki na yaliyo mema kwa nguvu zetu zote, akili zetu zote na moyo wetu wote, na ikiwa mtu amefariki dunia, tunaweza kuwa na amani mioyoni mwetu, tukijua kwamba tumefanya wajibu wetu, na yaliyotokea ni mapenzi tu ya Mungu kwani hatujachangia kwenye kuleta ugonjwa au kifo. Ni vyema nafsi zetu zisituhukumu kwa hilo ili tuwe na ujasiri mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa:

Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake, ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote. Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lolote tuombalo, tunalipokea kwake, kwa kuwa tunazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake (1 Yohana: 3 18-22)

Kama tumechangia katika kueneza maambukizi na mkristo akaugua na kufa, itaondoa ujasiri wa kusema kwamba yalikuwa ni mapenzi ya Mungu. Yesu alikuja ili tuwe na uzima, kisha tuwe nao tele. Anasema:

Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele (Yohana 10:10)

Tunachojaribu kusema ni kwamba kuna haja ya kuweka msisitizo mkubwa katika ibada zetu makanisani wa kuwataka washirika/washiriki waache uzembe na kutokujali, badala yake wazingatie hatua zote za tahadhari kwa ajili ya kujinga binafsi na kuwakinga wengine.

  1. Maombi yanatakiwa kuambatana na kutii

Maombi ndio njia kuu tuliyopewa wakristo kuwasilisha hoja zetu mbele za Mungu. Sambamba na maombi ni muhimu kusikiliza sauti ya Mungu inasema nini katika janga hili na kutii maagizo yake. Mara nyingi huwa tunaomba tukitegemea majibu fulani kama ilivyo mitazamo na matarajio yetu. Lakini Mungu hujibu zaidi ya matarajio, na kama wakristo hatutakuwa makini, tunaweza kushindwa kutambua majibu ya maombi.

Kwa mfano, tunaweza kumuomba Mungu pesa za kununua chakula, lakini Mungu anaweza kujibu kwa kutuletea chakula chenyewe, au tunaweza kumuomba Mungu chakula, lakini yeye akatupatia fursa ya kazi ya kufanya ili tupate kipato cha ziada kukutana na hitaji.

Inawezekana tumemuomba Mungu ufumbuzi wa tatizo la UVIKO-19, na inawezekana tumepewa majibu kwa kupatikana chanjo, lakini kwa sababu sisi tunategemea muujiza wa aina nyingine, labda tunashindwa kufahamu jibu la Mungu linapokuja, hasa kama tunahitajika na sisi kufanya wajibu fulani.

Kuna baadhi ya wakristo wakishauriwa kupata chanjo wanasema kwamba wao wameshamuomba Mungu kuwalinda na ugonjwa huu. Hii inaonesha baadhi ya wakristo wamejikita kwenye theolojia ya ‘AU’. Yaani, maombi AU tahadhari, badala ya kufuata theolojia ya ‘PAMOJA NA’: Yaani maombi PAMOJA NA tahadhari.

Mungu hufanya kazi kupitia sisi (Warumi 8:28) hivyo kama tukiacha kushirikiana na Mungu, tutakuwa tunakwepa wajibu wetu kama wakristo. Kwa sababu tayari tumepewa ufumbuzi mkubwa wa kisayansi kuhusu kupunguza maambukizi ya UVIKO-19, itakuwa ni vyema wakristo tukumbushane kuhusu maombi PAMOJA NA kuishi kwa hekima tukitumia maarifa tuliyopewa na Mungu katika kuudhibiti ugonjwa huu. Mtume Paulo anasema:

Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana nyakati hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana (Waefeso 5:15-17)

Kinachoendelea sasa miongoni mwa wakristo ni kufanya maombi huku wakikataa chanjo au hata tahadhari nyingine. Tunapochagua silaha moja na kuacha nyingine (theolojia ya ‘AU’) inakuwa ni kujidhoofisha wenyewe. Kinga thabiti ya kuzuia maambukizi ya korona inatokana na kutumia silaha zote kwa pamoja, yaani maombi (uhitaji wa kinga na uponyaji vilivyo juu ya uwezo wetu) PAMOJA NA kuchukua tahadhari na kukubali chanjo (kinga zilizo ndani ya wezo wetu).

  1. Chanjo sio Mpinga Kristo

Katika tetesi, dhana potofu na na nadharia-njama (conspiracy theory) zilizojitokeza katika kipindi hiki cha korona, ni hofu iliyojengwa na vikundi fulani vya wahubiri, wakitishia wakristo kwamba chanjo inawapa watu alama ya 666 ya ‘mnyama’ wa pili aliyendikwa katika kitabu cha Ufunuo sura ya 13. Mnyama huyu wa pili au ‘Mpinga-Kristo’, anaelezwa kuwasababisha wanadamu kumsujudia mnyama wa kwanza, kuwakosesha wanadamu na kufanya ishara. Mnyama huyo anaelezewa zaidi:

Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake. Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita (Ufunuo 13:12-14)

Andiko hili liliandikwa na Yohana katika karne ya kwanza. Waliandikiwa wakristo wa zamani wasikubaliane na tawala zinazopingana na Mungu. Na kwetu sisi wakristo wa leo ujumbe wake wa kinabii kwetu unahusu tu mamlaka zilizopo na zijazo duniani zinazopingana na Mungu. Mamlaka inayosaidia raia wake kupata afya, au kujikinga na maradhi, haipingani na Mungu, kwa sababu uponyaji na afya hutoka kwa Mungu.

Tetesi kwamba chanjo ya kuzuia ugonjwa wa korona ndio alama ya mpinga Kristo, ni dhana potofu isiyoendana na tafsiri sahihi ya Neno la Mungu.

Hitimisho

Uchambuzi huu ulilenga kutoa sababu kumi za msingi za kwa nini wakristo wanawajibika kupata chanjo ya UVIKO-19. Tumefanya hivi ili kutoa elimu mahususi kwa wakristo tukijaribu kufafanua dhana au mitizamo ambayo imetumika chini ya vivuli vya kiimani kukinzana na kupingana na jitihada za kupambana na maambukizi na madhara ya UVIKO-19.

Kwanza tumeonesha kua mlipuko wa UVIKO-19 umeandamana na uzushi na habari au taarifa nyingi zisizo za kweli juu ya chanzo, malengo ya kusambaa, kinga, na tiba ya ugonjwa huu. Pia kumekuwepo na jitihada kubwa zilizojikita katika nadharia-njama zinazowatia watu hofu kuhusu hatari za njia za kujikinga na ugonjwa huu hasa matumizi ya chanjo. Kwa bahati mbaya sana, wakristo wengi wakiongozwa na baadhi ya makanisa au watumishi mashuhuri, wamejielekeza zaidi kutafuta na kukumbatia taarifa zisizo sahihi na za kutunga kuliko kutaka kuujua ukweli wa kisayansi na maelekezo ya neno la Mungu.

Kwa kufanya hivyo, kumekua na kusahau kile neno la Mungu linasema juu ya wajibu wa mkristo kiimani na kimatendo, na jinsi mawili haya yanavyodhihirisha uhalisia na usahihi wa imani yetu katika jamii tunayoishi. Uongo, uzushi na taarifa potofu vimetumika kama silaha ya kuwashawishi wakristo kudharau au kuepuka kinga kwa usalama wao wenyewe na ule wa wanaowazunguka, hivyo kutozingatia amri ya “mpende jirani yako kama nafasi yako”.

Kwa kutumia neno la Mungu Pamoja na ushahidi wa kisayansi, tumeona sababu nyingi za kwa nini ni wajibu wa mkristo kukubali chanjo ya UVIKO-19. Tumeona kwamba chanjo za UVIKO-19 zinaokoa maisha na ni jibu la maombi yetu kwa Mungu. Kukubali chanjo ni kutenda haki, ni kusambaza upendo, ni kujenga amani na ni tendo la imani. Chanjo za UVIKO19 zilizoidhinishwa ni salama na sio Mpinga Kristo. Kila mkristo ana wajibu wa kujilinda na kulinda afya za wengine na kukataa chanjo huchangia kudorora kwa tahadhari nyingine za kujinga na UVIKO-19. ‘

Pia tumeonesha kuwa maombi kwa Mungu yanatakiwa kutojikita kwenye yale tu tunayotaraji bali pia kuambatana na kutii kila ambacho Mungu ataamua kutenda. Kama vile haitoshi tumeona kwa nini sio sahihi kwa wakristo kuruhusu vifo vinavyozuilika na kuamini vimetokea kwa mapenzi ya Mungu. Kukataa chanjo ya UVIKO-19 na hivyo kuruhusu vifo miongoni mwetu na kwenye jamii kwa vile tumekataa kinga ni kujidanganya kuwa vinatokea kwa mapenzi ya Mungu.

Ni vyema tukajikumbusha kuwa chanzo cha maarifa ni kumcha Mungu kama alivyoandika Mfalme mwenye hekima Suleiman katika Mithali 1:7 na Mungu aliwahi kusema watu wake “wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” (Hosea 4:6). Tumche Mungu na kutumia maarifa aliyotupatia kufanya maamuzi sahihi kuhusu chanjo.

Rejea

  1. World Health Organisation. WHO Coronavirus (COVID-19) Dashboard | WHO Coronavirus (COVID-19) dashboard with vaccination data. 2021. https://covid19.trackvaccines.org/agency/who/ (accessed Sept 6, 2021).
  2. Bradshaw D, Dorrington RE, Laubscher R, et al. Tracking mortality in near to real time provides essential information about the impact of the COVID-19 pandemic in South Africa in 2020. South African Medical Journal 2021; 111: 732–40. http://www.samj.org.za/index.php/samj/article/view/13304
  3. Peiris JSM, Yuen KY, Osterhaus ADME, et al. The Severe Acute Respiratory Syndrome. 2009; 349: 2431–41. https://www.nejm.org/doi/full/10.1056/NEJMra032498
  4. WHO. Middle East respiratory syndrome coronavirus (MERS-CoV). 2021. https://www.who.int/health-topics/middle-east-respiratory-syndrome-coronavirus-mers#tab=tab_1 (accessed Sept 6, 2021).
  5. Greenhalgh T, Jimenez JL, Prather KA, Tufekci Z, Fisman D, Schooley R. Ten scientific reasons in support of airborne transmission of SARS-CoV-2. The Lancet. 2021; 397: 1603–5. https://www.thelancet.com/article/S0140-6736(21)00869-2/fulltext
  6. Mürbe D, Kriegel M, Lange J, et al. Aerosol emission in professional singing of classical music. Scientific Reports 2021 11:1 2021; 11: 1–11. https://www.sciencegate.app/document/10.1038/s41598-021-93281-x
  7. Gregson FKA, Watson NA, Orton CM, et al. Comparing aerosol concentrations and particle size distributions generated by singing, speaking and breathing. 2021; 55: 681–91. https://www.tandfonline.com/doi/full/10.1080/02786826.2021.1883544
  8. Alsved M, Matamis A, Bohlin R, et al. Exhaled respiratory particles during singing and talking. Aerosol Science and Technology 2020; 54: 1245–8. https://www.tandfonline.com/doi/full/10.1080/02786826.2020.1812502
  9. Polack FP, Thomas SJ, Kitchin N, et al. Safety and Efficacy of the BNT162b2 mRNA Covid-19 Vaccine. New England Journal of Medicine 2020; 383: 2603–15. https://www.nejm.org/doi/full/10.1056/nejmoa2034577
  10. Baden LR, Sahly HM el, Essink B, et al. Efficacy and Safety of the mRNA-1273 SARS-CoV-2 Vaccine. 2020; 384: 403–16. https://www.nejm.org/doi/full/10.1056/nejmoa2035389
  11. Voysey M, Clemens S, Madhi S, et al. Safety and efficacy of the ChAdOx1 nCoV-19 vaccine (AZD1222) against SARS-CoV-2: an interim analysis of four randomised controlled trials in Brazil, South Africa, and the UK. Lancet 2021; 397: 99–111. https://www.thelancet.com/journals/lancet/article/PIIS0140-6736(20)32661-1/fulltext
  12. Sadoff J, Gray G, Vandebosch A, et al. Safety and Efficacy of Single-Dose Ad26.COV2.S Vaccine against Covid-19. New England Journal of Medicine 2021; 384: 2187–201. https://www.nejm.org/doi/full/10.1056/NEJMoa2101544
  13. Kaabi N al, Zhang Y, Xia S, et al. Effect of 2 Inactivated SARS-CoV-2 Vaccines on Symptomatic COVID-19 Infection in Adults: A Randomized Clinical Trial. JAMA 2021; 326: 35–45. https://jamanetwork.com/journals/jama/fullarticle/2780562
  14. Bueno SM, Abarca K, González PA, et al. Interim report: Safety and immunogenicity of an inactivated vaccine against SARS-CoV-2 in healthy chilean adults in a phase 3 clinical trial. medRxiv 2021; https://www.medrxiv.org/content/10.1101/2021.03.31.21254494v1
  15. Logunov DY, Dolzhikova I v, Shcheblyakov D v, et al. Safety and efficacy of an rAd26 and rAd5 vector-based heterologous prime-boost COVID-19 vaccine: an interim analysis of a randomised controlled phase 3 trial in Russia. The Lancet 2021; 397: 671–81. https://www.thelancet.com/journals/lancet/article/PIIS0140-6736(21)00234-8/fulltext
  16. Vasileiou E, Simpson CR, Shi T, et al. Interim findings from first-dose mass COVID-19 vaccination roll-out and COVID-19 hospital admissions in Scotland: a national prospective cohort study. The Lancet 2021; 397: 1646–57. https://www.thelancet.com/journals/lancet/article/PIIS0140-6736(21)00677-2/fulltext
  17. Bernal JL, Andrews N, Gower C, et al. Effectiveness of Covid-19 Vaccines against the B.1.617.2 (Delta) Variant. 2021; 385: 585–94. https://www.nejm.org/doi/full/10.1056/nejmoa2108891
  18. Wei J, Stoesser N, Matthews PC, et al. Antibody responses to SARS-CoV-2 vaccines in 45,965 adults from the general population of the United Kingdom. Nature Microbiology 2021 6:9 2021; 6: 1140–9. https://www.nature.com/articles/s41564-021-00947-3
  19.  Hall VJ, Foulkes S, Saei A, et al. COVID-19 vaccine coverage in health-care workers in England and effectiveness of BNT162b2 mRNA vaccine against infection (SIREN): a prospective, multicentre, cohort study. The Lancet 2021; 397: 1725–35. https://www.thelancet.com/journals/lancet/article/PIIS0140-6736(21)00790-X/fulltext
  20. Stowe J, Andrews N, Gower C, et al. Effectiveness of COVID-19 vaccines against hospital admission with the Delta (B.1.617.2) variant. Public Health England 2021; 37https://media.tghn.org/articles/Effectiveness_of_COVID-19_vaccines_against_hospital_admission_with_the_Delta_B._G6gnnqJ.pdf
  21. Dagan N, Barda N, Kepten E, et al. BNT162b2 mRNA Covid-19 Vaccine in a Nationwide Mass Vaccination Setting. New England Journal of Medicine 2021; 384: 1412–23. https://www.nejm.org/doi/full/10.1056/nejmoa2101765
  22. Haas EJ, Angulo FJ, McLaughlin JM, et al. Impact and effectiveness of mRNA BNT162b2 vaccine against SARS-CoV-2 infections and COVID-19 cases, hospitalisations, and deaths following a nationwide vaccination campaign in Israel: an observational study using national surveillance data. The Lancet 2021; 397: 1819–29. https://www.thelancet.com/journals/lancet/article/PIIS0140-6736(21)00947-8/fulltext
  23. Corchado-Garcia J, Puyraimond-Zemmour D, Hughes T, et al. Real-world effectiveness of Ad26.COV2.S adenoviral vector vaccine for COVID-19. medRxiv 2021; https://www.medrxiv.org/content/10.1101/2021.04.27.21256193v1
  24. Thompson MG, Burgess JL, Naleway AL, et al. Interim Estimates of Vaccine Effectiveness of BNT162b2 and mRNA-1273 COVID-19 Vaccines in Preventing SARS-CoV-2 Infection Among Health Care Personnel, First Responders, and Other Essential and Frontline Workers — Eight U.S. Locations, December 2020–March . MMWR Morbidity and Mortality Weekly Report 2021; 70: 495–500. https://www.cdc.gov/mmwr/volumes/70/wr/mm7013e3.htm
  25. Mukherjee S. Morbidity and mortality from COVID-19 post-vaccination breakthrough infections in association with vaccines and the emergence of variants in Bahrain. 2021; Research Square.. https://www.researchsquare.com/article/rs-828021/v1
  26. Gray G, Bekker L-G. Update on the Janssen®(JNJ) Ad26.COV2.S vaccine. 2021. https://sacoronavirus.co.za/2021/08/06/update-on-the-janssenjnj-ad26-cov2-s-vaccine-professors-glenda-gray-linda-gail-bekker/
  27. Public Health England. COVID-19 vaccine surveillance report published – Week 36 GOV.UK. London, 2021. https://www.gov.uk/government/news/covid-19-vaccine-surveillance-report-published
  28. Gray G, Bekker L-G. Update on the Janssen®(JNJ) Ad26.COV2.S vaccine. https://sacoronavirus.co.za/wp-content/uploads/2021/08/Sisonke-Provisional-Results-6-August-2021GG2.pdf
  29. Johansson MA, Quandelacy TM, Kada S, et al. SARS-CoV-2 Transmission From People Without COVID-19 Symptoms. JAMA Network Open 2021; 4: e2035057–e2035057. https://jamanetwork.com/journals/jamanetworkopen/fullarticle/2774707
  30. Juthani P v, Gupta A, Borges KA, et al. Hospitalisation among vaccine breakthrough COVID-19 infections. The Lancet Infectious Diseases 07 Sept 2021; https://www.thelancet.com/journals/laninf/article/PIIS1473-3099(21)00558-2/fulltext (accessed Sept 6, 2021).
  31. Bandolier. Risk of death and transportation. http://www.bandolier.org.uk/booth/Risk/trasnsportpop.html (accessed Sept 6, 2021).
  32. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Takwimu za msingi. 2020 https://www.nbs.go.tz/nbs/takwimu/references/2020_Tanzania_in_Figure_Kiswahili1.pdf  (accessed Sept 12, 2021).
  33. Karlheinz Peter, Hannah Stevens, James McFadyen. People with coronavirus are at risk of blood clots and strokes. Here’s what we know so far. The Conversation 2020. https://theconversation.com/people-with-coronavirus-are-at-risk-of-blood-clots-and-strokes-heres-what-we-know-so-far-137304
  34. The Lancet Respiratory Medicine. COVID-19 transmission—up in the air. The Lancet Respiratory Medicine. 2020; 8: 1159. https://www.thelancet.com/journals/lanres/article/PIIS2213-2600(20)30514-2/fulltext

Hakimiliki

Udadisi imetumia picha hizi huria kutoka https://pixabay.com