Na Isaack Mdindile

@isaac29g

Hapa Sao Paulo, Brazil. Joto katika moto wake, ni kali halikaliki. Kila kona ni korona, ndiyo habari ya mjini. Nimeamka na hisia ya hasira. 

Serikali imeamuru kufunga karibu kila kitu hapa. Haturuhusiwi kutoka nje. Ni mfungo wa lazima.

 Ratiba zimevurugwa na maisha siyo yale nilizoea. Mikono ilizoea kupeana, miili kukumbatiana, vidole kujikuna usoni, na lazima kunawa kila mara. Nafikiri kwa sauti ndefu! Je, hizo sabuni na maji ya kunawa kila wakati tunatoa wapi?

Hili janga limekuja na majanga lukuki. Ni vita ya afya, uchumi, na kila kitu, maana vitu vyote vinahusiana. Lakini maisha kwanza, maana uchumi tunaweza kuurekebisha huko siku za usoni. 

Rais wa nchi, Jair Messias Bolsonaro, anaita hii korona ni mafua tu na suala la uchumi ni muhimu zaidi. Anasisitiza tusali makanisani na kufunga kula. Ila waziri wake wa afya, Luiz Henrique Mandetta, anasema tuepuke misongamano na tufuate maelekezo ya wataalamu wa afya na shirika la afya duniani. Wenye nchi wapo njia panda, hawajui wamfuate nani.

Sasa kila mtu amekuwa msemaji wa ugonjwa uletwao na virusi vya corona ulioanza mwaka 2019 (COVID-19). Balozi wa mtaa hapa anaitisha mkutano wa hadhara ili kuwaambia wananchi kuwa wasikusanyike hadharani! Nimegundua tuna vita ya mawasiliano pia. 

Italia wanasema walikosea. Rais Donald Trump wa Marekani amechanganyikiwa, anawaza uchaguzi. Hata familia ya Malkia wa Uingereza imeathirika. Virusi havichagui wala kubagua, sisi ndiyo tunabagua. 

Historia ni mduara kama siyo mzunguko. Kama kawaida pia, katika hii vita panzi ndiyo wanaumia zaidi. Kabla ya virusi hivi, kila mtu alionekana kuwa na furaha, angalau,huko mitandaoni, sasa huzuni na woga zimepamba nyuso nyingi.Woga umetamalaki katika kila rika na dira, hadi makanisani na misikitini. 

Wengi wanaona huu ndiyo mwisho wa dunia. Binafsi, nafsi yangu haiamini huo mchepuo. Kuna kupindisha na kupishana tafsiri. Raisi hapa ndiyo wa kwanza kupuuza maelezo ya wataalamu wa afya. Rais ametengeneza chaneli mitandaoni na kuungana na baadhi ya wachungaji (hiyo ndoa yake sasa) kupinga tafiti na kusema hii korona imetengenezwa na serikali ya kikomunisti ya China. Kweli matokeo ya kujumlisha upumbavu na ushabiki uliopitiliza wa dini (fanaticism) ni gharama zaidi kuliko kutafuta chanjo ya hivi virusi na dawa ya kutibu ugonjwa huu?

Na baada ya siku kadhaa, anapiga simu Uchina ili kuomba ushirikiano katika hii vita mbivu.

Hasira inaingilia machoni, nasugua na nakohoa kwa mikono yote. Ghafla, nakumbuka kwamba hairuhusiwi. Kweli, kumbukumbu ni dawa, binadamu ameitumia sana ili kuishi duniani. Kupoteza kumbukumbu kwa watu ni hasara isiyositirika wala kusameheka. 

Siku hizi sisikilizi tena utabiri wa hali ya hewa kwa siku zijazo. Napuuza, maana iwe mvua au jua, bado nitabaki ndani. Binadamu na mbwembwe zote za fedha na teknolojia, amefyata mkia kwa molekula. Kweli, maisha ni fumbo la umbo, hayatabiriki.

Ndani hakukaliki, sijakariri huu mfumo mpya. Sina mazoea wala mazoezi. Nasikia joto, nafungua madirisha na kubadilisha nguo kila wakati. Inabidi kubadilisha hewa pia. Hali ya hewa ya baridi napendelea zaidi, kwa ajili ya mapato. Samahani, namaanisha mapafu. Afya na uchumi vimeungana, kama buibui katika mtandio wake, walishanena mababu/mabibi zetu. 

Kwa haya maisha ya karantini, nisipopata taarifa iliyotufikia hivi punde (breaking news) nasikia kama kuumwa, na kuachwa na nyakati. Kukaa chonjo, ndiyo chanjo. Kuna vyanzo vya habari kuwa namba kamili za wagonjwa na vifo vya hii korona vinafichwa. Lisemwalo lipo….

Sasa serikali ya Brazil inafanya kazi kubwa, pamoja na kila mara kufuta twiti za Rais maana zinawachanganya raia. Bunge limepitisha bajeti ya dharura kwa ajili ya wavujajasho ili kujikidhi na mahitaji muhimu. Watapokea kama shilingi laki mbili na nusu, kwa mwezi, katika kipindi cha miezi mitatu. 

Hapa najifunza kuwa nchi ikiwa na taasisi imara na huru, na kwa bahati mbaya mkapata Rais kichaa, bado haki za raia na demokrasia zinalindwa. Tunahitaji taasisi huru, kama vile tume huru ya uchaguzi!

Turudi kwenye kona ya korona…

Binafsi, hii karantini imenifanya kuamka mapema, nafanya dua, naenda bustanini, kulisha mifugo, kujisomea, kuandika shajara (diary), kufanya mazoezi na kulala mapema. Tulinde maisha yetu na tuwapendao, tunaishi mara moja, maisha ni mamoja.

Mtaani ninapoishi majirani wanapinga hii karantini, kujitenga na kutengwa. Nawasoma. Hatuna utamaduni wa kukaa bila kufanya kitu, upekee ni msamiati na ukimya ni utumwa kwa wengi wetu.

Kuna baadhi ya habari hapa zinaibua maswali na kuleta ukakasi. Eti wazee na wenye magonjwa ya moyo, kisukari na wavutaji ndio walengwa wa hii korona, hivyo tuwatenge, na wanapokufa unasikia; “amekufa mzee mmoja na korona kwani alikuwa na ugonjwa wa kisukari.” Hii hainipendezi kabisa.

 Hawa ni watu na majina yao siyo sensa wala namba fulani. Hakuna ambaye ni mfano wa kundi la hatari. Tuache lugha za kunyanyapaa. Tulinde wote popote. Unajua, watu kufa bila vipimo, bila kuagwa na kuzikwa kama wanyama au kuchomwa moto ni huzuni isiyozeeka wala kuelezeka.

Tembea uone.

Ndani mwangu, kimyakimya, pale tumbo linakaa, kuna mwangwi wa sauti, ikisema hiki ni kipindi cha pekee, tulihitaji nyakati hizi ili kutafakari kipaumbele (sio vipaumbele) katika maisha yetu kwa ujumla. Hivyo tusinawe tu mikono, na vichwa, tuoshane miguu pia. Bado ni Pasaka, tusisahau. 

Kukaa nyumbani na kusali siyo dhambi wala uhaba wa imani, bali ni ukomavu wa upendo. Upendo ndio amri kuu na ndiyo unaokoa. Kufuata maelezo ya watalaamu na kujilinda ni shauri la kidini zaidi kuliko unavyofikiria. 

Kila uchao natenga muda wa kusikiliza mapigo yangu ya moyo na  kujikumbatia. Nasikiliza lugha ya mwili, na natoka nje na kusikiliza ndege wa porini wakiimba. Yote haya ni muhimu mno kwa afya ya roho mwilini. 

Sasa nimetoka kuoga na kubadilisha nguo. Kitu cha kwanza, nimerudi bafuni tena kunawa mikono. Ama kweli hizi ni zama za kipekee.