Kazi kuu ya lugha ya kufundishia ni nini? Kama lugha hiyo ni Kiingereza, je, kazi yake (kuu) ni kumfundisha mtu ajue Kiingereza? Na kama lugha hiyo ni Kiswahili, je, kazi yake (kuu) ni kufundisha Kiswahili?Ili mwanafunzi wa biolojia au udaktari aelewe namna ya kumfanyia upasuaji chura kwa kutumia dawa ya (kuleta) usingizi iitwayo ‘chloroform’ ni mpaka kwanza aelezwe hivi kwa Kiingereza: “administer chloroform as anesthetic before dissecting the frog”?
Hoja kuu ni moja tu hapa – je, ni lugha ipi nzuri ya kumfundishia mtu: Je, ni lugha ambayo yeye na mwalimu wake wanaielewa vizuri na ambayo wanaitumia kwa mawasiliano ya mara kwa mara na ya kila siku au ni lugha ambayo wote wawili wanaitumia kwa nadra na mmojawapo au wote hawaielewi vizuri? Kama nikitumia Kiingereza nitapata taabu kupita kiasi kukuelezea hiki ninachoelezea hapa na hata kushindwa kukiwakilisha kikakamilifu na kama yule ninayemwelezea naye atapata taabu sana kuelewa kwa nini tung’ang’anie tu ‘kuelezana bila kuwasiliana’ vilivyo? Kwa nini tupoteze vyote viwili – kupata maarifa na kujifunza lugha zote mbili vizuri – kwa undumilakuwili wa kisera?
Sasa kama hatuwasikilizi hawa walimu wa Kiingereza – kina Mabala na Martha Qorro – na watafiti waliolitafiti kwa kina hili suala tumsikilize nani? Na kama hata mijadala ya humu humu Wanazuoni ambayo inanoga na kukolea zaidi pale tunapotumia lugha ambayo wengi wetu tunaielewa vizuri, yaani Kiswahili, na ambayo kiukweli ndiyo wananchi wengi tunaitumia zaidi kwenye madaladala, masokoni, majumbani, makanisani, mashambani na hata mashuleni. Si tujikite tu katika kufundisha Kiingereza kama lugha (ya pili/lugha ya kigeni) ili tuielewe vizuri kabisa huku tukitumia lugha yetu nzuri ya Kiswahili kufundishia Sayansi, Historia, na Jiografia ya milima yetu ya Kilimanjaro, mito yetu ya Tanganyika, makaa yetu ya Mchuchuma, mbuga zetu za Serengeti, madini yetu ya Buzwagi na mengine mengi tu?
—
Kwa kiasi kikubwa tukiwa shule za sekondari tunafundishwa/tumefundishwa kwa Kiswahili japokuwa vitabu ni vya Kiingereza. Sasa kwa nini haturasimishi tu hilo? Nasikia hata vyuoni kwa kiasi kikubwa ni hivyo hivyo i.e. maprofesa mnaongea Kiswahili na wanafunzi wenu ila wakati wa kuwatahini mnawatahini kwa Kiingereza, sasa si muwaache tu watumie hicho hicho Kiswahili kuwaelezea jinsi walivyoelewa hata kama hapa na pale watakuwa wanachomeka hayo maneno ya Kiingereza. Isitoshe maneno mengi ya kitaaluma asili yake ni Kigiriki/Kiyunani, Kilatini na Kiarabu.
Pia inabidi tukumbuke kwamba wapo ambao wanatoka vizuri tu Darasa la Saba halafu wakifika Kidato cha Kwanza mambo yanaharibika kwa sababu ya badiliko la ghafla la lugha ya kufundishia. Hili lilikuwa wazi sana ambapo wale ngangari sana – kina Ulimboka Stephen – tulikuja kuwashangaa Kidato cha 3 wanakuwa wa kwanza ilihali tulikuwa tunawaona vilaza tu Kidato cha 1 na cha 2, kumbe muda wote huo walikuwa wanahangaika na lugha kwanza, sasa hao waliweza, je, wale ambao hawakuweza japo walikuwa ni wanafunzi wazuri tena ‘waliofaulu’ Darasa la Saba?
Tumepoteza watu wengi sana waliokuwa na uwezo njiani kwa sababu hii. Na wapo wengi tu waliopita ambao hicho Kiingereza wala hawakijua vizuri ila ni wahandisi, wanahisabati na madokta wazuri tu. Kwa nini? Wamewezaji kuwa hivyo japo Kiingereza ni mgogoro? Kwa sababu Kiingereza siyo lugha kuu waliyokuwa wanatumia kujifunzia. Mimi nimesoma PCM kwa muda A-Level na nakumbuka tulikuwa tunajadiliana na kufundishana Hisabati, Fizikia na Kemia kwa Kiswahili. Kilicho muhimu ni kuwasiliana na kuelewa/kueleweshana. Hivi kumwelezea Freud na zile ID, Ego na Superego mpaka kwa Kiingereza ndiyo mtu ataelewa? Kwanza hiyo ‘Ego’ yake wala siyo ile ya kwenye Kiingereza!
Tanzania hatuna Sera ya Lugha ya Taifa! Hii ni sababu kubwa kwa nini mjadala wa lugha ipi itumike kufundishia bado unaendelea. Mjadala huu ulianza mwaka 1977 na andiko la Materu na Mlama. Mwaka kesho 1917, kama tutaendelea kujadili, tutafikisha miaka arobaini! Hakuna nchi duniani iliyoleta mapinduzi ya kielimu bila ya kuwa na sera ya lugha ya taifa! Hakuna nchi duniani iliyoendelea bila ya kutumia lugha ya taifa katika mfumo wake wa elimu! Ramani ya dunia inaonesha kuwa nchi zote ambazo hazitumii lugha ya taifa katika kufundishia elimu bado ni maskini! Kiingereza bado hakijawa lugha ya taifa Tanzania, pamoja na kuwa ni lugha rasmi! Tanzania bado kuna mkanganyiko: huwezi kuwa na lugha ya taifa halafu usiitumie katika kuendeleza taifa kupitia elimu! Sera ya Elimu ya 2014 nayo ina mkanganyiko: huwezi kuwa na lugha mbili tofauti za kufundishia katika mfumo ule ule wa elimu. Nadhani kuna hofu kuwa ikiwa Kiswahili kitatumika mpaka sekondari, vijana wengi sana watafaulu na Serikali itapata mzigo wa kuwasomesha Chuo Kikuu! Jee, Kiingereza ni chujio la kupunguza wanaoweza kuingia kidato cha tano na sita na mpaka chuo kikuu?
Siku zote, napingana na matumizi ya Kiingereza katika kufundisha.
Napingana na wanaosema Kiswahili hakijitoshelezi. Ipi lugha inayojitosheleza ulimwenguni?
Fikiria, mwanafunzi anayefundishwa masomo ya Kiingereza kwa Kiswahili, akiingia chumba cha mtihani ana kazi zifuatazo:
Mosi, kusoma swali kwa Kiingereza.
Pili, kulitafsiri swali kichwani liwe katika Kiswahili.
Tatu, kufikiria jibu kwa Kiswahili.
Nne, kulitafsiri kwenda Kiingereza.
Tano, kuandika jibu.
Linaweza onekana jambo dogo. Lakini, ni kielelezo kuwa lugha mama ya mtu ndiyo ingeleta ufanisi zaidi katika kumfundisha.
Watu wanasema, Kiswahili kina maneno magumu. Yanaonekana magumu kwa sababu hatutaki kuyatumia. Hivi, lugha uliyokuwa ukiizungumza inakuwaje na, maneno magumu zaidi ya lugha unayojifunzia shuleni tena ukifundishwa na mwalimu anayekufundisha lugha hiyo kwa kutumia lugha ileile uliyokuwa ukiizungumza?
Kama taifa tunahitaji kufikia muafaka wenye tija kwa elimu yetu. Muafaka ni kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia na Kiingereza kifundishwe kama somo.