Tafakuri ya wazi juu ya
Operesheni Tokomeza
Issa Shivji
Profesa Mstaafu wa Kigoda Cha Mwalimu Nyerere
Aibu, aibu, aibu. … aibu ya kitaifa! Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili
uliosababisha mateso, ukatili, udhalilishwaji, upigaji na hatimaye vifo vya
wananchi ni aibu kubwa kwa taifa letu. Sio aibu tu bali ni janga la kitaifa
linalohitaji kufanyiwa tathmini na tafakuri na wananchi wote katika ujumla wao
na kujiuliza: tunaelekea wapi? Nini kimesababisha vyombo vya dola na mfumo wetu
wa kisiasa kukosa kabisa uwajibikaji kiasi kwamba vyombo vilivyopewa jukumu la
kuyalinda maisha, utu na heshima ya wananchi, vigeuke kuwa watesaji na wadhalilishaji
wa wananchi hao hao! Kwa nini hatujifunzi? Kwa nini hatujirekebishi?
Katika historia yetu tumewahi kuwa na janga kama hili mnamo
mwaka wa 1976 kutokana na Operesheni
Mauaji huko Shinyanga na Mwanza. Mwalimu Nyerere aliwalazimisha viongozi wa
kisiasa, akiwemo Mzee Mwinyi, kujiuzulu
na watendaji wengine, wakiwemo wakuu wa jeshi la polisi na usalama katika ngazi
ya mkoa, kuchukuliwa hatua za kisheria na kuadhibiwa ipasavyo. Tukio la operesheni Tokomeza linafanana sana
na tukio la Operesheni Mauaji, lina sura ileile ya utesaji, udhalilishaji,
ubakaji, na uporaji wa mali ya wananchi.
Matukio mengine ya aina hiyo, japokuwa hayakuwa makubwa kiasi hicho, yamewahi kutokea
huko nyuma. Katika awamu ya pili,
kulikuwa na uaaji wa wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero mnamo
mwaka 1986, na madhara na mateso waliyoyapata wananchi wakati wa Mwembechai.
Katika awamu ya tatu ilitokea kashfa ya waandamaji huko Pemba kuuliwa na
wengine kudhalilshwa kiasi kwamba tukio hili lilileta aibu kubwa sana kwa
taifa. Kwa jumla, matukio kama haya, yaani utumiaji wa mabavu na vyombo vya
mabavu – polisi, usalama, maaskari wengine kama wanamgambo, askari wa wanyama pori
n.k. – yameongezeka awamu hadi awamu kiasi kwamba katika awamu ya nne
tunashuhudia mauaji na mateso ya wanahabari na wananchi yakiongezeka mara dufu.
Hili la operesheni Tokomeza ni kilele.
Sasa tufanyeje?
Uwajibikaji
Mawaziri wanne wamelazimishwa kuachia ngazi kwa kubeba dhamana
ya kisiasa. Na wamepongezwa! Mengi mengine yanazungumziwa kwa mtazamo wa
kichama na kisiasa. Wengine wanaenda mbali kusema kwamba Waziri Mkuu pia
anatakiwa kujiuzulu. Haya yanaeleweka kwa
sababu tukio lenyewe limeamsha hisia za watu na watu wanataka kuona waziwazi
kwamba hatua za maana zinachukuliwa kuwatuliza.
Ni kweli kabisa kwamba tukio hili ni kashfa kubwa sana ya
kitaifa. Katika mfumo wa kibunge (parliamentary
system), Serikali nzima pamoja na mkuu wa serikali, yaani waziri mkuu,
wangejiuzulu na labda uchaguzi mkuu ungeitishwa. Lakini katika mfumo wetu wa
kirais (presidential system), mkuu wa
serikali sio Waziri Mkuu. Ni rais, na rais pia ni mkuu wa nchi. Kwa hivyo,
kujiuzulu kwa Waziri Mkuu hakuna uzito. Kwa upande mwingine, huwezi kutegemea
rais mwenyewe na serikali yake kujiuzulu kwa sababu, rais pia ni mkuu wa nchi.
Na huwezi ukawa nchi bila kiongozi mkuu; kutakuwa na ombwe la uongozi.
Kwa upande wangu, ili kuonyesha kwamba tukio hili
linachukuliwa kwa uzito wake, na hisia za wananchi zinajibiwa zipasavyo, mambo
mawili yafuatayo yanaweza kufanyika mara moja:
Moja, Rais kuvunja Baraza lake lote la Mawaziri, kama
alivyofanya Mzee Mwinyi miaka ya tisini. Hatua hii itakaribiana na uvunjaji wa
serikali. Hii itakuwa ni dalili ya uwajibikaji wa kisiasa.
Pili, watendaji,
wakiwemo wale katika ngazi za juu, wafikishwe mbele ya mahakama kwa mashtaka ya
kijinai. Mwanasheria Mkuu amependekeza uundaji wa Tume ya Kimahakama. Hii ni
njia moja wapo lakini mara nyingi njia hii hutumika kama mbinu za kufunika
kombe ili mwanaharamu apite. Nionavyo, labda safari hii, Rais Kikwete anaweza
kutumia njia mbadala ya kuteua Mchunguzi huru (independent investigator and
prosecutor) ambaye atakusanya ushahidi na kuandaa mashtaka ya kupeleka mbele ya
Mahakama.
Na katika uchunguzi huu, watendaji wote wanaohusika, pamoja
na wa kijeshi, usalama, na wa kiraia, wachunguzwe na kushtakiwa bila kujali
nyadhifa zao.
Tatu, jambo hili lizungumzwe na kujadiliwa na taifa zima kwa
upana na undani wake bila kuficha au kulionea haya. Hakuna shule muhimu ya
kujifunza kuliko shule ya Umma. Shule ya Umma inafundisha na pia inasaidia
kujenga maadili na uwajibikaji. Katika mijadala idara zitatajwa, watu waovu
watasemwa kwa majina, maovu yanayofichwa uvunguni yatafichuliwa hadharani.
Mwishowe, ningependa kuligusia jambo moja muhimu ambalo
linaonekana halijaguswa hata kidogo.
Dola na matumizi ya
mabavu
Dola ni taasisi ya mabavu, popote pale duniani. Jeshi,
polisi, maaskari wengine kama wa wanyama pori, wa hifadhi na kadhalika ni
vyombo vya mabavu. Vyombo hivyo vya mabavu katika dola vinapata uhalali wa
kisiasa kutumia mabavu kwa sababu vinadhibitiwa na kusimamiwa na vyombo na
viongozi wa kisiasa ambao hupata uhalali wao kutokana na kuwa wawakilishi wa
wananchi. Kwa mfano, jeshi la ulinzi hutumia mabavu kuilinda nchi dhidi ya
maadui wa nje. Uwezo wa kutangaza vita na kuingiza jeshi vitani ni wa rais kama
Amiri Jeshi mkuu; na rais ni kiongozi wa kisiasa aliyechaguliwa, sio mwanajeshi.
Katika mfumo wowote ule ambao ni wa kiraia, kwa maana kuwa sio wa kijeshi (military) au wa kipolisi
(police state), vyombo vya kisiasa ndio hudhibiti na kusimamia vyombo vya
mabavu. Jukumu la jeshi la ulinzi ni kuilinda nchi. Jukumu la jeshi la polisi
ni kulinda amani, wananchi na mali zao. Majukumu haya mawili ni tofauti na
yanatenganishwa kikatiba. Hayaingiliani.
Ndio maana, jeshi la ulinzi halitumiki kudhibiti ghasia
nchini. Hii ni kazi ya polisi. Katika mazingira ya kipekee ambayo kuna hatari
ya serikali kupinduliwa kwa nguvu au kama kuna uasi ndio Jeshi la Ulinzi
huingizwa mitaani. Na jambo hili hufanyika baada ya Rais kutangaza hali ya
hatari kwa mujibu wa masharti ya katiba.
Kwa hivyo, ni kinyume na Katiba na mazoea mabaya kuliingiza jeshi la ulinzi katika mambo ya
kiraia, kama vile uhalifu au ujangili. Kufanya hivyo ni kujenga mazoea mabaya
na ya hatari sana.
Kinyume na msingi huu wa kikatiba, Operesheni Tokomeza
ilichukuliwa kama operesheni ya kijeshi. Katika washiriki 2,371, wanajeshi
walikuwa 885 au asilimia 37, yaani zaidi ya theluthi moja. Polisi walikuwa 480
au asilimia 20 tu. Wengine walikuwa kutoka majeshi mbalimbali kama la wanyapori
n.k.
Pili, operesheni hii ilisimamiwa na Jeshi la Ulinzi. Na
nikinukuu maneno ya Taarifa ya Kamati ya Bunge, “Taarifa za mwenendo wa
operesheni zilikuwa zinapelekwa moja kwa moja kwa Mkuu wa Majeshi na kwamba,
hazikumfikia Waziri wa Maliasili na Utalii.” Isitoshe, viongozi wa kisiasa kama
wakuu wa wilaya na mikoa na viongozi wa kuchaguliwa kama madiwani,
hawakushirikishwa wala hawakupewa taarifa zozote kuhusu operesheni hii. Mbaya
zaidi, baadhi yao waliteswa na kudhalilishwa na maaskari waliohusika na
operesheni kiasi kwamba Mkuu wa Wilaya ya Ulanga alijificha katika hoteli.
Kwa kifupi basi, operesheni hii haikudhibitiwa wala
kusimamiwa wala kuendeshwa kama operesheni ya kiraia (civilian operation),
badala yake iliendeshwa kama operesheni ya kijeshi (military operation). Hili
ni jambo la hatari sana na ni mazoea mabaya, hayakubaliki katika mfumo wa
utawala wa kiraia (civilian government).
Kuchanganya jeshi la ulinzi na mambo ya kiraia ni dhambi
kubwa katika mfumo wa kisiasa tunaoufuata nchini mwetu. Jambo hili halikubaliki
kabisa!.
Kwa hivyo, inashangaza kwamba hata Kamati ya Bunge haikuona
hili na badala yake ikapendekeza kwamba Serikali iandaae “operesheni nyingine
ambayo itapangwa na kutekelezwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Idara ya
Usalama wa Taifa. ” Na hoja hii inaonekana kuungwa mkono bila kutiliwa shaka na
wabunge wetu! Maana yake nini, wabunge hawajui na hawatambui kwa kuruhusu hili
wanajenga mazoea hatari? Kama ndivyo basi ipo haja ya wanasiasa wetu pamoja na
wabunge kujielimisha zaidi jinsi serikali za kiraia zilizochaguliwa na wananchi
zinavyoendeshwa.
Angalizo! Tujihadhari, tusizoee kabisa kutumia Jeshi la Ulinzi katika mambo ya ndani kwa
sababu kwa kufanya hivyo tutakuwa tunajenga mazoea hatarishi sana kwa mfumo wa
kidemokrasia.