WAJIBU-JAMII WA MWANAZUONI WA AFRIKA

 

Issa Shivji

 

Utangulizi

Mhadhara huu utajikita kwenye mjadala juu ya mambo ambayo yanafaa
kuzungumziwa na kubishaniwa katika jukwaa la wanazuoni. Sifa muhimu ya
mijadala  inayojumuisha wanazuoni ni
uwezo wao wa kusikiliza maoni ya wenzao kwa utulivu; kujenga hoja; kukosoa hoja
na kutokana na mgongano wa hoja kuzalisha hoja mpya, au mbadala, ambayo
itasukuma mbele ufahamu na fikra. Kuna thesis,
yaani hoja ya msingi, kuna anti-thesis,
yaani hoja gonganishi, na kuna synthesis,
ambayo inazingatia mawazo yanayojitokeza kwenye thesis na anti-thesis, na
kuibua hoja mpya, au hoja mbadala. Lengo langu ni kutumia njia hii ya ubishani
wa kisomi kujenga hoja zangu.

Kabla sijaanza kuwasilisha hoja za mhadhara wangu, ningependa nieleze, japo
kwa ufupi, kwa nini ni muhimu kuibua suala la dhima (commitment) na wajibu-jamii (social
responsibility
) wa wasomi wakati huu. Kwa mtazamo wangu, nadhani kuna
sababu kubwa zifuatazo. Katika miongo miwili au mitatu ya mwanzo wa Chuo hiki,
na hata vyuo vingine barani Afrika, suala la nafasi na wajibu wa wasomi
lilikuwa linajadiliwa sana. Kwa kiasi kikubwa tuliweza kudadisi dhima yetu,
wajibu-jamii wetu na mchango wetu kwa jamii zetu.  Kadhalika, kulikuwa na juhudi kubwa, kuweka
mazingira yanoyafaa kwa ajili ya kuendesha mijadala bila hofu. Pale ambapo
watawala wa serikali au viongozi wa Chuo walipojaribu kubana nafasi ya
mijadala, wanafunzi na walimu waliungana kupinga hatua kama hizo.

Kuanzia miaka ya 80 uhuru huo adimu na muhimu wa kitaaluma ulianza
kubanwabanwa. Hali hii ilienda sambamba na nchi zetu kusalimu amri kwa taasisi
za kifedha za kimataifa na wafadhili. Tukalazimishwa kubadili sera za kitaifa
na kufanya mageuzi yaliyokumbatia sera ambazo kwa pamoja sasa tunaziita za uliberali
mambo-leo (soko huria, ubinafsishaji, uhuru wa uwekezaji, ushindani, haki sawa
kwa wananchi na wawekezaji, kwa maana haki sawa kwa wanyonyaji na wanyonywaji,
n.k.). Kwa taasisi za elimu ya juu, mageuzi hayo yalimaanisha kuwa na sera za
kuchangia gharama za elimu (cost-sharing).

Sera hizi hazikupitishwa na kutekelezwa bila upinzani. Katika vyuo vingi
vya Afrika, pamoja na chetu, kulikuwa na upinzani. Kutokana na kuwepo kwa
dalili za kubanwa kwa uhuru wa kitaaluma, vyama vya wanataaluma vya taasisi
sita za elimu ya juu vilipitish The Dar
es Salaam Declaration on Academic Freedom and Social Responsibility
   (‘Azimio
la Dar es Salaam juu ya Uhuru wa Kitaaluma na Wajibu-Jamii’) mnamo mwaka wa
1990.  Na Katika mkutano wa CODESRIA
wasomi na wanazuoni wa Afrika walikutana Kampala na kupitisha ‘Azimio la Kampala
juu ya Uhuru wa Taaluma na Wajibu-Jamii wa Wananzuoni’ ambalo lilitambuliwa
rasmi na Umoja wa Afrika.

Hata hivyo, hali ya kudidimizwa kwa uhuru wa taaluma haikubadilika sana.
Kulikuwa na mazingira ya hofu na kujidhibiti (self-censorship). Hali ambayo imeendelea kuwepo hadi leo.

Kutokana na sababu mbalimbali, mnamo mwaka wa 2008, Chuo Kikuu chini ya
uongozi wa Profesa Mukandala kilizindua Kigoda cha Taaluma Cha Mwalimu Nyerere.
Katika miaka mitano, Kigoda kilijaribu kutengeneza mazingira na nafasi ya
kuibua na kuendeleza mijadala ya wazi na yenye lengo la kuwatoa hofu wasomi ili
waweze kuzingatia ukweli kwamba hakuna jambo lolote ambalo ni nyeti ambalo
haliwezi kujadiliwa hadharani. Nilifurahi nilipomsikia Profesa Penina akitupa
matumaini kwamba utamaduni huu, ambao bado haujakomaa, utaendelezwa. Nakutakia
kila la heri dadangu.

Kipindi hiki bado ni kigumu. Ni juu yetu wasomi, kwanza, kuilinda nafasi
hii adimu, na pili, kupanua nafasi hii ili wanafunzi na walimu waweze kujadili
na kuhoji bila hofu wakiwa ndani na nje ya vyumba vya mihadhara. Katika hali halisi ilivyo, hii labda
ni ndoto yangu, lakini huwezi kujenga mustakabali mwema bila kuwa na ndoto.

Kutokana na sababu hizi, nimeona nirejea suala hili nikitumia nafasi hii
adimu niliyopewa na wanakigoda.

***

Mhadhara huu una sehemu nne. Katika sehemu ya kwanza nitaeleza mwanazuoni
ni nani.  Katika kueleza dhana ya
mwanazuoni sina budi nieleze pia dhana ya msomi na pia nibainishe tofauti
iliyopo kati ya msomi na mwanazuoni. Sehemu ya pili nitazungumzia uhusiano kati
ya wasomi/wanazuoni na tabaka-jamii, social
class
. Katika sehemu ya tatu nitadadisi dhana ya wajibu-jamii, kwa kutoa mifano
hai. Na mwisho nitagusia wajibu-jamii wa mwanazuoni wa Afrika na kutoa rai
yangu kwenu.

I. Mwanazuoni ni nani?

Mwanazuoni ni nani? Je, kuna tofauti kati ya mwanazuoni (intellectual) na msomi (intellect worker/intelligentsia)? Ndiyo,
ipo tofauti. Wanazuoni wote, au karibu wote, ni wasomi lakini siyo wasomi wote wanakuwa
wanazuoni. Mara moja moja inatokea kwamba mtu ambaye hajawahi kusoma katika
taasisi yeyote ya elimu huwa mpevu kifikra na kwa hiyo huwa na sifa za
mwanazuoni. Lakini hii ni nadra sana. Kwa kawaida wanazuoni wengi huwa wasomi.
Kwa hivyo, hatuna budi tuanze kwa kueleza wasomi ni nani.

Msomi huishi kwa nguvu-akili wakati mvujajasho huishi kwa nguvu-mwili. Kwa
maneno mengine, mfanyakazi huishi kwa jasho lake lakini msomi huishi kwa ubongo
wake.  Katika mfumo wa kibepari hii ni
aina mojawapo ya mgawanyo wa kazi. Na tofauti kati ya msomi na mfanyakazi ni
kubwa na ya kipekee. Inakuzwa, inatuzwa.

Msomi hujivunia utaalamu na uelewa wake. Na kusema ukweli wasomi
wanakubalika katika jamii kama wanataaluma ingawa utaalamu wao unaweza ukawa
mkubwa juu ya jambo dogo. Elimu ya kibwanyenye huigawanya taaluma katika
visehemu vidogo vidogo. Kwa hivyo, kwa mfano, msomi wa uchumi siyo mtaalamu wa
uchumi kwa ujumla, bali anaweza akawa mtaalam wa fedha tu, au wa sarafu tu, na
asiwe na ufahamu wowote wa uchumi kwa ujumla.
Msomi wa sheria anaweza akawa mtaalamu wa masoko ya hisa tu.  Anawashauri wacheza “kamari” katika soko hili
– ni wakati gani mwafaka wa kununua hisa na wakati gani wa kuziuza ili
kujiongezea faida na utajiri. Mfano mmojawapo wa mtaalamu wa masoko ya hisa na
fedha ni George Sorros. Anajulikana kama msomi aliyejitajirisha kwa
kuhamishahamisha fedha kutoka soko moja kwenda soko lingine. Baada ya
kutengeneza faida na kutajirika kwa njia hii sasa anafadhili mashirika yasiyo
ya kiserikali ya kutetea mfumo wa demokrasia ya kiliberali katika nchi nyingi,
pamoja na Afrika. Huyu ni msomi; anachuma fedha na kuishi maisha ya anasa na ya
heshima kwa kutumia akili zake “shupavu” za kucheza “kamari”.

Wako wasomi wa aina nyingi tu – wakuu wa mashirika ya biashara,
wahandisi, wanasheria, wanasiasa, wanaharakati, wahadhiri, watumishi wa ngazi
ya juu katika serikali, biashara, viwanda, na wengine wengi. Lakini wengi hawa
siyo wanazuoni.

Wanazuoni hutofautishwa na wasomi kwa sifa kama sita hivi.

Moja ni kwamba mwanazuoni
huchambua mambo kihistoria. Tukio au
jambo limetoka wapi, liko wapi na linaelekea wapi. Mwongozo wake ni kuchambua
mielekeo. Tukifananisha na mpiga picha, tunaweza kusema kwamba mwanazuoni
hupiga video, sio picha. Hii haina maana kwamba kila mwanazuoni ni
mwanahistoria. La hasha! Haiwezekani. Lakini kila mwanazuoni ana mwelekeo wa
kihistoria katika uchambuzi wake.

Pili, na hili lina uhusiano wa
karibu na hilo la kwanza, ni kwamba anaangalia mambo – hususan ya kijamii –
katika uhusiano wake na mambo
mengine. Kwa mwanazuoni, hakuna jambo lisiloingiliana na lingine. Kuweza
kuelewa muingiliano ni muhimu, badala ya kulitenganisha tukio au jambo na
muktadha wake. Kwa mfano, huwezi kuelewa chanzo au vyanzo vya umaskini katika
jamii bila kuelewa historia yake na uhusiano wake na utajiri. Umaskini na
utajiri ni kama mapacha na vina historia moja. Matajiri wachache wananeemeka na
umaskini wa wengi. Kwa hivyo, kuna muingiliano kati ya umaskini na utajiri.
Hata hivyo, baadhi ya wasomi huchambua umaskini bila kuangalia historia yake na
kuchukulia, bila kudadisi, kana kwamba umaskini umekuwepo tangu enzi za kale na
utaendelea kuwepo milele, isipokuwa labda unaweza kupunguzwa. Tuna mashirika
mengi yanayozungumzia upunguzwaji wa umaskini (poverty  alleviation) badala
ya utokomezaji wa umaskini. Na huwezi kutokomeza umaskini bila kuelewa vizuri
chanzo cha umaskini, uhusiano wake na utajiri na mfumo wenyewe unaozaa matabaka
ya waliyonacho na wasiyonacho.

Tatu, mwanazuoni huamini
kwamba ukweli haugawanyiki, the truth is
the whole.
Maana yake ni kwamba huwezi kupata ukweli wa jambo kama
hujaliangalia jambo hilo katika muktadha wake. Nikitoa ule mfano maarufu,
huwezi ukasema kwamba tembo ni kama kamba nene kwa sababu umegusa mkia wake au
kwamba tembo ni mpana kwa sababu umegusa sikio lake. Ili kujua ukweli wa umbo
la tembo ni lazima uangalie umbo lake zima.

Nitoe mfano mwingine. Ukitaka kuchambua muundo wa kiti, huwezi ukachambua
miguu yake tu. Wala huwezi kusema kwamba sehemu za kiti ni miguu na sehemu za
kukalia na kuegemea. Ukijumlisha sehemu hizo hutapata kiti, utakachopata ni
rundo la mbao! Ukitaka kuelewa muundo wa kiti kizima, huna budi uchambue jinsi,
na katika uhusiano upi, sehemu zake zote zimeunganishwa.

Nne, mwanazuoni ni wakala wa
mabadiliko ya hali iliyopo, na siyo mtumwa wake. Dhamira yake ni kuigeuza na
siyo kuigandisha hali iliyopo. Dhamira yake ni kuleta hali bora katika jamii,
hususan kwa walio wengi. Yeye daima ni mpambanaji. Anapambana dhidi ya dhuluma,
uonevu, ukandamizaji na uovu mwingine popote pale ulipo. Ndiyo dhamira yake,
ndiyo maisha yake, ndiyo uhai wake.
Anajitambulisha na wapambanaji wenzake bila kujali wanakotoka, makabila
yao, au rangi yao.

Jamaa mmoja alimwandikia Che Guevara kwamba kutokana na majina yao
kufanana labda wao ni ndugu wa damu. Che alimjibu kwamba yeye haoni kwamba wao
ni ndugu: ‘Lakini’, namnukuu, ‘kama wewe unachukia uonevu popote pale ulipo,
basi sisi ni ndugu, makamaradi’ ….  bila
kujali kama sisi ni ndugu wa damu.

Tano, mwanazuoni hujali, na
kupigania maendeleo ya wanadamu, maendeleo ya wote, siyo ya wachache.

Sita, ili kukidhi uelewa wa
jamii na mazingira yake na ya ulimwengu, mwanazuoni hujikita kwenye uchambuzi
wa kina, uchambuzi ambao unaongozwa na nadharia iliyopevuka. Ndiyo maana
wanazuoni wengi, hususan wa Afrika, wanavutiwa zaidi na nadharia ya kimapinduzi
ya usoshalisti. Kwa mwanazuoni huyo, ufahamu/elimu ni zana ya kukosoa hali
ilivyo bila kusita na kuielekeza kwenye kubadili jamii, siyo bidhaa ya kuuzwa.
Katika kusisitiza umuhimu wa nadharia ya kimapinduzi Amilcar Cabral, mkombozi
na kiongozi wa Guinea Bissau, alisema: Bila nadharia ya kimapinduzi hakuna
mapinduzi yatakayoshinda.

Ni wazi kwamba sio kila
mwanazuoni ana sifa hizo zote kama itaeleweka vizuri zaidi katika sehemu
inayofuata kuhusu wanazuoni na matabaka ya kijamii.

II. Wanazuoni wa tabaka

Wanazuoni ni sehemu ya jamii na wana uhusiano na jamii. Hawawezi kudai
kwamba wao ni wachambuzi tu wa mambo na kwamba taaluma yao haiguswi kwa namna
yoyote ile na matakwa, hofu, hisia, matumaini, fikra, itikadi na mitazamo ya
jamii. Kwa kuwa jamii yenyewe ya kibepari imegawanyika katika matabaka na
makundi basi wanazuoni pia huwa wasemaji wa tabaka fulani au kundi fulani, ama
bila kujua au bila ya kujitangaza.

Tabaka linalotawala hutawala pia mawazo, fikra na itikadi, ndiyo maana
katika mfumo wa kibepari itikadi ya kibwanyenye hutawala. Wanazuoni na wasomi
wengi hutumikia tabaka-tawala kwa njia moja au nyingine kwa kujenga na
kusambaza itikadi yao. Hata hivyo, wanazuoni wachache hutamani kujiunga na
wanyonge na kuwatetea. Hao ndiyo wanazuoni wa kimapinduzi. Hakuna mwanazuoni au
msomi asiyejikita ama kwenye tabaka-nyonyaji au tabaka-nyonywaji. Wote hujikita
kwenye tabaka fulani hata kama hawajitambui au kujitambulisha hivyo.  Na mara nyingi, unaoonekana kama mgongano wa
kimawazo au kinadharia ni mgongano wa mtazamo uliojikita kwenye tabaka au kundi
fulani. 

Mwanazuoni hufanya uchambuzi wa kijamii ili ayaelewe vizuri mazingira kwa
shabaha mahsusi ya kuboresha hali ya maisha ya waliowengi. Yeye huanika uovu
wote hadharani bila kujipendekeza. Katika hili uchambuzi wake unakuwa kamilifu
bila kujali utamfurahisha nani na utamuudhi nani, na hata kama akisakamwa na
wenye mamlaka na madaraka katika jamii, – wakiwemo watawala wa kisiasa au
watawala watarajiwa, au watawala wa kiuchumi, – hasiti kusema ukweli kama
uchambuzi wake unamuelekeza kufanya hivyo. Kwa vyovyote vile, mwanazuoni
mwanamapinduzi hawezi kukosa kuchukiwa na watawala na wenzao wa tabaka la
kisiasa, political class.  Kama mwanafalsafa wa kimapinduzi Karl Marx
alivyosema:

It is certainly not our task to build up the future in advance and to
settle all problems for all time, but it is just as certainly our task to
criticise the existing world as ruthlessly in the sense that we must not be
afraid of our own conclusions and equally unafraid of coming into conflict with
the prevailing powers.  

Kwa muhtasari, anachosema Marx ni kwamba kwa hakika siyo kazi ya
wachambuzi/wanafalsafa kutanguliza kujenga mustakabali na kutatua matatizo yote
kwa enzi zote, lakini ni kwa hakika pia kazi yao ni kukosoa hali ya ulimwengu
uliyopo wakati huo bila kusita na kutokuhofia matokeo ya uchambuzi wao hata
kama haya yatawaingiza kwenye misuguano na wenye madaraka.

Niongeze kusema kwamba ni wazi kabisa kwamba wanazuoni wanaotetea hali
ilivyo bila shaka hawatakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wale
wanaofaidika na hali hiyo. Kwa upande mwingine, wale wanaotaka kubadili hali
kwa mtazamo wa wavujajasho watakuwa na hali ngumu, watasakamwa, watatungiwa
uongo, watadhalilishwa na hata kujeruhiwa au kuuliwa. Kwao hii siyo hoja.
Katika misitu ya Bolivia, wakati Che Guevara alipokutana uso kwa uso na
wanajeshi mamluki wa Serikali, mmoja wao alimtambua na kulenga bastola yake
kwake. Lakini alikuwa anasitasita kuifyatua. Che akamwambia, kwa sauti ya
utulivu, ‘Unasita nini. Fyatua risasi yako, utakuwa umemuua mtu tu!’, kwa maana
kwamba huwezi kuua fikra na mtazamo wa mwanamapinduzi na kweli kabisa mpaka leo
fikra za Che zimedumu.

Katika historia yetu ya mapambano ya ukombozi tuna mifano mingi ya
wanazuoni waliojitolea mhanga kwa sababu ya msimamo wao kuwa upande wa umma.
Patrice Lumumba alitaka nchi yake iwe na uhuru kamili ili iweze kutumia utajiri
wake kwa manufaa ya, siyo Wakongomani tu, bali kwa manufaa ya watu wa Afrika
kwa sababu Lumumba alikuwa muumini wa Umajumui wa Afrika (Pan-Africanism). Aliuliwa kikatili na wakala wa CIA. Kwame Nkrumah
wa Ghana aliuchambua na kuukusoa mfumo wa ukandamizaji wa kibeberu, akitaka
kuleta umoja wa Afrika kwa sababu aliamini kabisa kwamba wananchi wa vinchi vya
Afrika wakiwa peke yao, hawataweza kumudu nguvu za kibeberu. Akapinduliwa na
waliochukua madaraka kama mwanajeshi Afrifa aliyekuwa na mawazo finyu,
wakamsakama na kumdhalilisha. Chris Hani, ambaye alikuwa na dhamira ya kujenga
Afrika Kusini Mpya kwa mtazamo wa wavujajasho, aliuliwa katika kipindi nyeti
cha mpito kutoka ukaburu kwenda ukombozi. John Garang, kiongozi wa muda mrefu
wa Sudan ya Kusini, alikuwa na msimamo wa kutokutenga na kuvunja nchi ya Sudan;
badala yake alitaka Sudan Mpya. Umma wa Sudan Kusini na Sudan Kaskazini walikuwa
nyuma yake. Inasemekana alikufa katika ajali ya helikopta. Sina hakika!

           

Muammar Gadaffi, mwanasiasa aliyekuwa na dhamira ya kuleta mabadiliko
makubwa na yenye maslahi kwa nchi na jamii yake, ingawa baadae alianza
kuyumbayumba, aliuliwa na majeshi ya mamluki yakisaidiwa na NATO. Kosa lake?
Alikuwa na mpango kabambe wa kuvuna maji yaliyopo chini ya ardhi ya jangwa la
Sahara na kueneza maji hayo katika eneo zima la Sahel. Lakini rais wa Ufaransa,
wakati ule Sarkozy, alikuwa na mpango wake mbadala. Alitaka Gadaffi akubali
kutoa idhini ili mashirika ya Kifaransa wayavune maji hayo na kuyasafirisha
kwenda Ufaransa kwa ajili ya kutengeneza maji ya chupa. Gadaffi alikataa
katakata. Akasukiwa mpango, nchi yake ikavamiwa na hatimaye akauliwa. Leo hii
nchi ya Libya imesambaratishwa na hao hao waliojiita wakombozi.  Nchi na vyombo vya habari vya Magharibi
waliwakuza sana vibaraka hao na kuwatambua kama “wakombozi”, ili kuhalalisha
maslahi yao ambayo yalikuwa sababu kuu ya kumpindua na kumuua Gadaffi.

Sasa nije kwenye sehemu ya tatu ya mada yangu – wajibu-jamii  wa wanazuoni.

III. Wajibu-jamii

Nitaeleza dhana hii ya wajibu-jamii wa mwanazuoni kwa kutoa mifano hai.

Mnamo mwaka 1988, kulikuwa na mjadala mkubwa juu ya riwaya iitwayo The Satanic Verses, yaani Aya za Kishetani. Riwaya hiyo ilitungwa
na Salman Rushdie, ambae ni mzaliwa wa India ingawa anaishi Uingereza. Ni
maarufu sana kama mtungaji wa riwaya.  Riwaya ya The
Satanic Verses
inakidhalilisha moja kwa moja Kitabu Kitakatifu cha Waislamu
yaani Quran.  Alikejeli na hata kumtukana
matusi ya nguoni Mtume Muhammad. Umma wa Waislamu ulichukizwa sana wakati
wasemaji na serikali za Magharibi walishangilia na kumuunga mkono na kumtetea
kwa msingi kwamba msanii ana haki na uhuru wa mawazo, freedom of expression, na lazima haki yake itetewe na
kulindwa. 

Umma wa Waislamu walifikiri tofauti. Chuki na hasira za Waislamu
zilisambaa kwa kasi kiasi kwamba kulikuwa na maandamano, ghasia na maafa katika
nchi nyingi. Hatimaye, Kiongozi wa Kiroho wa Iran, Ayatollah Khomeini,
alimlaani Rushdie kwa fatwa na
kulikuwa na hisia kwamba angeweza kuuwawa. Rushdie alilazimika kwenda
mafichoni  huku akilindwa na askari wa
Uingereza.

Mabishano na malumbano kati ya wasomi wa Magahribi na wasomi Waislamu
yalijikita kwenye mgongano kati ya dhana ya uhuru wa mawazo, haki mojawapo ya
haki za binadamu, na wajibu-jamii wa mwanazuoni.

Shirika moja la uchapishaji wa vitabu, Penguin, walitaka kutoa toleo la India. Wakaomba ushauri wa
wanazuoni wa Kihindi. Karibu wote (Waislamu na wasio Waislamu) walipinga
kuchapishwa kwa kitabu hiki wakitoa hoja kwamba kitauchochea umma na
kusababisha umwagaji wa damu na hata kuhatarisha umoja wa nchi yao.  Hatimaye serikali ya India ilipiga marufuku
kitabu cha The Satanic Verses.  Hatua hiyo ya serikali iliungwa mkono na
wanazuoni mashuhuri wa Kihindi wakiwemo Waislamu na wasio Waislamu. Barua
iliyoandikwa katika gazeti la The Indian Post na jopo la wasomi iliuliza:
je, kupigwa marufuku kitabu hiki ni mfano wa kujenga jamii kandamizi? Gazeti la
The Times of India likajibu:

No, dear Rushdie, we do not wish to build a repressive India. On the
contrary, we are trying our best to build a liberal India where we can all
breathe freely. But in order to build such an India, we have to preserve the
India that exists. That may not be a pretty India. But this is the only India
we possess.

Tafsiri ya haraka haraka ni:

Hapana, mpendwa Rushdie, sisi hatutaki kujenga India kandamizi. Kinyume
chake, tunajaribu kwa dhati kujenga India ya kiliberali ili kila mmoja wetu
aweze kupumua hewa kwa uhuru. Lakini ili kujenga India kama hiyo, hatuna budi
tuilinde hii India iliyopo. Inawezekana India iliyopo haipendezi, lakini ndiyo India
tuliyonayo.

Mzee wetu, mwanazuoni mashuhuri, Profesa Ali Mazrui amefanya uchambuzi
mahiri sana wa kitabu cha The Satanic
Verses
akionesha kwamba Rushdie alikusudia kabisa kuwadhalilisha Waislamu
na kubeza Mtume wao ili ashangiliwe na watu wa Magharibi.  Hata baada ya kumkosoa Rushdie kwa hoja
nzito, Profesa Mazrui anahitimisha kwa kusema kwamba Waislamu wamuombe
Ayatollah Khomeini ili aondoe fatwa ya
kifo, na kama ikibidi, basi amlaani tu.

Huyu ni Profesa Mazrui, mwanazuoni mahiri wa Afrika. Mfano huu
unadhihirisha kwamba wakati mwanazuoni ana uhuru na haki ya kujieleza, lakini
pia ana wajibu-jamii ili haki yake hiyo isilete madhara makubwa kwa jamii. Na
wajibu-jamii huo siyo wa kushurutishwa kwa sheria bali unahitaji kutumiwa kwa
busara, uelewa na hiari ya mwanazuoni mwenyewe ili asiweze kufanya jambo ambalo
litaleta madhara na maumivu kwa wengine.

Nitatoa mfano mwingine mmoja kuhusu Profesa Mazrui kuonesha kwamba mara
nyingine inambidi mwanazuoni aseme ukweli
ambao wengine hawataki kuusema au kuusikia hata kama kwa kufanya hivyo
atakuwa anahatarisha usalama wake .  

Kati ya miaka ya 1971-72, nduli Idi Amin Dada aliwafukuza Waasia kutoka
Uganda. Profesa Mazrui, wakati huo akiwa Chuo Kikuu cha Makerere, aliandika
kipeperushi kiitwacho When Spain expelled
the Jews and the Moors … A Lesson in History
. Huu ulikuwa ni mfano wa
kihistoria wa karne ya 15-17 wakati Wahispania Wakristo walio wengi
walipowafukuza Waislamu wa Afrika ya Kaskazini na Wayahudi kwa sababu
hawakuonekana kama ni wenzao ingawa wengi wao walibadili dini. Idadi yao
ilikuwa ndogo lakini wengi wao walikuwa wafanyabiashara, madaktari, wenye
mabenki, wasomi na kwa ujumla wataalamu mbalimbali. Inasemekana, baada ya
kufanya kitendo hicho cha ubaguzi, uchumi wa Spain ulididimia. Profesa Mazrui
anahitimisha kipeperushi chake kwa kusema:

Yes, let me once again repeat myself – we study history in order to
understand ourselves. But we should also study it to be wiser, more humane,
less rash, certainly less brutal, and often with an eye on the future.

Tafsiri:

Naam, hebu nirejee yale niliyowahi kusema – tunasoma historia ili
tujielewe. Lakini pia inatubidi tuisome ili tuwe na busara zaidi, ubinadamu
zaidi, ili tuupunguze ujinga, na hakika tuupunguze ukatili, na mara nyingi kwa
kuangalia mustakabali wetu.

Nakala 1000 za kipeperushi hicho zilisambazwa katika jiji la Kampala na
watu kwa utashi wao wenyewe walianza kutoa nakala zaidi.  Ingawa Mazrui kwa ubunifu mkubwa hakusema
waziwazi kuhusu kufukuzwa kwa Waasia, ujumbe wake ulikuwa wazi. Hakuna mtu
ambaye angeshindwa kufananisha yaliyokuwa yanatokea nchini Uganda na yale
yaliyonukuliwa na Mazrui kutoka katika historia ya kale. Ilibidi Mazrui afunge
virago na kuondoka akihofia kushughulikiwa na Iddi Amin Dada. Lilikuwa ni jambo
la ujasiri kwa upande wa Mazrui lakini alikuwa anatekeleza wajibu-jamii wake
wakati baadhi ya wasomi wenzake walikuwa wameamua kukaa kimya na wengine
walikuwa wakishangilia siasa za uzawa za Iddi Amin. Lakini Iddi Amin baada ya
kuwafukuza Waasia aliwageukia Waganda ili kuendesha utawala wake wa kikatili
kwa zaidi ya miaka minane.

Sasa nimalizie na sehemu yangu ya mwisho, wajibu-jamii wa mwanazuoni wa
Afrika.

 

IV. Wajibu-Jamii wa Mwanazuoni
wa Afrika

Kwa muhtasari ningependa kusisitiza mambo matatu juu ya dhima (commitment) yetu kama wanazuoni na
wajibu-jamii wetu.

Moja, tunahitaji uelewa na
ufahamu wa kutosha wa historia ya bara letu kwa mtazamo wetu. Ninasisitiza mtazamo
wetu
, siyo historia tuliyolishwa na kumezeshwa na wasomi na wanazuoni wa
kibeberu wa Magharibi. Katika hili nidokeze, kwa maoni yangu, mahali pa
kuanzia.

Kipindi cha nusu karne ya uhuru wetu tunaweza kukigawa katika awamu
mbili.  Kipindi cha miaka 25 ya mwanzo
nakiita kipindi cha utaifa (yaani nationalism)
na kipindi cha miaka 25 iliyofuata
tunaweza kukibatiza jina la uliberali-mambo leo (yaani neo-liberalism). Itikadi iliyotuongoza
katika awamu ya kwanza ilikuwa ya utaifa. Kuna sifa mahsusi ya itikadi ya
Utaifa katika Afrika. Utaifa wa nchi (territorial
nationalism
) ulizaliwa na itikadi ya Umajumui wa Afrika (yaani Pan-Africanism). Kizazi cha kwanza
ambacho kilipigania uhuru kilijikita kwenye umajumui wa Afrika. Kwa hivyo,
umajumui wa Afrika ulitangulia utaifa wa nchi na siyo kinyume chake. Historia
hii inatutofautisha kabisa na Umoja wa Ulaya, ambao huwa mara kwa mara
tunaurejea kama mfano wa kuigwa. Tofauti ya pili ya kimsingi kati ya Umoja wa
Ulaya na Umoja wa Afrika tunaotamani ni kwamba nchi za Ulaya zina historia ya
ubeberu na ukoloni, historia ya kututawala, wakati sisi hatuna historia
inayofanana. Ukweli ni kwamba sisi tulitawaliwa.

Kwa hivyo, siyo jambo la kushangaza kwamba kizazi cha waasisi wetu tangu
mwanzo kilianza kujadili suala la kuunganisha nchi zao.  Waliposhindwa ndipo walipoanza kujenga utaifa
wa nchi zao. Wakala mkuu wa kujenga utaifa akawa dola tuliyorithi kutoka kwa
wakoloni. Huu moja kwa moja ni mgongano kwa sababu dola yenye sifa za kikoloni
itakuwaje chombo cha kujenga utaifa?

Kulikuwa na mielekeo miwili katika itikadi ya utaifa. Mwelekeo wa utaifa
wa mrengo wa kushoto (yaani radical
nationalism
) na mwelekeo wa utaifa wa mrengo wa kulia (yaani narrow nationalism).  Utaifa wa mrengo wa kushoto hujikita kwenye
ukombozi na mabadiliko makubwa. Kielelezo cha utaifa wa mrengo wa kushoto ni
Mwalimu Nyerere; kielelezo cha utaifa wa mrengo wa kulia ni wengine wengi ambao
utaifa wao ulizizamisha nchi na jamii zao kwenye tope la uzawa, ukabila, udini
na ubaguzi wa rangi.

Kwa maoni yangu, utaifa wa kinchi ulishindwa (yaani the national project failed). Uliberali mambo-leo umedhihirisha
wazi kwamba utaifa uliojikita kwenye kinchi ulikuwa dhaifu kiasi kwamba
uliposhambuliwa na itikadi ya uliberali mambo-leo, ambao wanauita utandawazi,
ulisalimu amri. Utaifa wa kinchi haukuweza kuhimili mashambulizi ya hali, mali
na itikadi ya nchi za kibeberu. Ukweli huo ndiyo umewafanya wanazuoni wa
Afrika, ingawa siyo wengi, kufikiria upya dhana na itikadi ya umajumui wa
Afrika. Mwalimu katika hotuba yake ya mwaka 1997, wakati wa kuadhimisha miaka
40 ya uhuru wa Ghana, alikiri kwamba kizazi chake kilishindwa kujenga umoja wa
Afrika.  Aliwasihi Waafrika wa kizazi
kipya, – viongozi, wanazuoni na vijana, – kuelekeza nguvu zao kwenye kujenga
umoja wa Afrika, badala ya kuzama kwenye utaifa finyu wa vinchi na makabila
yao. Bila umoja, Mwalimu alisisitiza, Afrika haina mustakabali mwema. Aliwaonya
Waafrika wasijitumbukize kwenye ukabila au uzawa au utaifa wa vinchi. Wasione
fahari kushangilia vinchi vilivyogawanywa kwa mipaka ya wakoloni. Hii ilikuwa
ni alama ya utawala wa kikoloni, siyo utambulisho wao, aliwakumbusha.

Mwalimu alitoa ushawishi wa kiitikadi na kisiasa kwa kutumia kipaji
chake. Sisi wanazuoni tunatakiwa kwenda mbali zaidi. Tueleze awamu hii ya
mashambulizi mapya ya kibeberu dhidi ya nchi za Afrika kwa mtazamo wa
kihistoria. Kwa muhtasari, nataka nijenge hoja ya kuwafikirisha.

Sifa kuu inayoutambulisha mfumo wa kibepari ni ulimbikizaji wa mtaji bila
kupumua (endless accumulation).
Katika kipindi hiki cha ubepari wa kimataifa, ambao unajidhihirisha kwetu kwa
jina la uliberali mambo-leo, ulimbikizaji wa mtaji ni ulimbikazji wa kiporaji (primitive accumulation). Ndiyo mwelekeo
wa ulimbikizaji unaotawala – uporaji wa rasilimali na maliasili; udidimizaji wa
hali ya maisha ya wavujajasho; upanukaji wa sekta isiyo rasmi – (eti sekta
isiyo rasmi!) – ambayo unaongeza maradufu unyonyaji wa wavujajasho; ukuaji wa
sekta ya fedha – mabenki, mashirika ya bima, soko la hisa, n.k. –  ambayo ni mirija ya kunyonya mtaji wetu;
ukopeshaji wa fedha na mabenki ya kibiashara na kutufanya tulipe madeni pamoja
na riba na gharama zingine ambazo zinatufanya tuwe watumwa milele; na njia nyengine.

Hizi ni njia za kisasa za kulimbikiza mtaji kwa kupora jasho la
wavujajasho na rasilimali na maliasili za nchi zao. Lakini kimsingi,
ulimbikizaji huu hauna tofauti na ulimbikazaji wa kiporaji wa enzi ya biashara
ya utumwa. Uhusiano wetu na Ulaya ulianza zaidi ya karne tano zilizopita,
zikiwemo karne mbili za biashara ya utumwa. Ni bara la Afrika tu lililokumbwa
na janga hili. Mwanasiasa-uchumi mmoja (Bagchi, 2005) anajenga hoja kwamba
biashara ya utumwa ilikuwa na mchango wa kipekee katika ulimbikizaji wa mitaji
na maendeleo ya nchi za Ulaya. Isitoshe, anadai kwamba biashara hii ndiyo
iliyowezesha nchi za Ulaya kushindana katika soko la bidhaa na nchi za Kiasia
na hatimaye kuwatawala. Nieleze kidogo. Hoja yake ni kwamba, mazao – miwa,
viazi, mahindi, na malighafi nyingine kama pamba n.k. – yaliyolimwa na watumwa
wa Kiafrika huko Marekani na katika visiwa vya Carribean kwa gharama ndogo sana
yaliziwezesha nchi za Ulaya kumudu lishe bora kwa wafanyakazi wao ambayo
iliwasaidia kuongeza ufanisi wao kiuchumi, kwa upande mmoja, na kuyatuliza
mapambano ya tabaka la wafanyakazi kisiasa, kwa upande mwingine. 

Kwetu sisi, biashara ya utumwa ina nafasi ya kipekee kwa sababu siyo tu
jambo la kihistoria bali inatusaidia kuelewa na kuchambua hali halisi ya leo,
au utumwa mambo-leo.  Kama nilivyoainisha, njia ya kulimbikiza
mtaji kwa kupora ilitawala wakati wa utumwa; na njia hii imerudi kwa sura mpya
katika kipindi hiki cha uliberali mambo-leo.

Mwanazuoni wa Afrika anayejali hana budi aielewe historia hii. Suala la
historia siyo suala la kulaumiana, bali ni nyenzo ya kutuongezea uelewa na
kuongoza uchambuzi wetu wa hali halisi.

Jambo la pili ni kuhusu
nadharia ya kufanyia uchambuzi. Nadharia (theory) ni ufahamu wa hali ya juu – higher form of knowledge. Katika fani
hii ya kujenga nadharia sisi wenyewe kutokana na hali yetu halisi, wanazuoni wa
Afrika, tumekuwa nyuma sana. Na hii siyo kwa sababu hatuna uwezo, bali ni kwa
sababu tumekuwa wepesi kukubali unyonge wetu. Hatuna kiburi cha uanazuoni. Kama
ilivyo mifumo ya uchumi wetu, sisi huzalisha malighafi, husafirisha nje na
kununua kutoka nje bidhaa zilizotengenezwa. Vilevile wasomi wetu hukusanya data
ghafi (raw data) na kuwapelekea
wasomi wa Magharibi. Wao huchambua na kujenga nadharia ambayo sisi humeza bila
kuhoji.

Kwa ujumla, rai yangu kwenu ni kwamba kuna haja ya kufanya utafiti wa
msingi na wa maana katika hali yetu halisi (basic
research
). Kutokana na tafiti hizo tutaweza kujenga nadharia
zitakazotuelekeza na kutuongoza juu ya namna ya kuleta mabadiliko ya maana.
Katika Chuo hiki tulianza vizuri lakini tukakumbwa na hizi sera tulizoletewa na
ubeberu; sera kama za ushindani, biashara na utafiti wa kisera wa kutoa majibu
fastafasta. Kwa mfano, ziko wapi tafiti zinazotuonesha jinsi jamii zetu
zilivyobadilika chini ya uchumi na utawala wa uliberali mambo-leo? Ziko wapi
tafiti zinazobainisha muundo wa matabaka katika jamii yetu, mijini na vijijini?
Ziko wapi tafiti zinazobainisha sifa za dola na siasa tulizonazo? Ziko wapi
tafiti zinazobainisha wakala wa kusukuma gurudumu la maendeleo yetu? Ziko wapi
tafiti zinazobainisha muundo na mtindo wa mshikamano baina ya tabaka/matabaka
ya ndani na ubeberu, na kuainisha sifa na athari za ubeberu mambo-leo? Tafiti
kama hizo ndizo zinaweza kutusaidia kubadili hali halisi na kuchagua tufanye
nini, kwa ajili gani na kwa manufaa ya nani. Tafiti kama hizo ndizo zinazoweza
kutusaidia kujenga nadharia zetu sisi wenyewe ambazo zitatusaidia kuamua nini
tukubali na nini tukatae kutoka nje; zitatuwezesha kutofautisha mahindi na
makana.

Tafiti za msingi kwa ajili ya kujenga nadharia zetu, zinahitaji mazingira
mwafaka. Tunahitaji mazingira yanayofaa katika taasisi zetu za elimu ya juu ya
kujadili, kudadisi, kuhoji na kutokubali chochote ambacho hakina ushahidi na
hoja.  Tusijenge mazingira kandamizi ya
hofu kiasi kwamba vijana wakose kupumua. Na miongoni mwetu tusiwanyamazishe
wale ambao tunatofautiana nao. Njia mojawapo ya kuua hoja na mawazo mbadala ni
kujenga mazingira ya kuogopesha, yaani
intimidation
. Kila anayehoji siyo mchochezi. Kila anayekuwa na mawazo
mbadala siyo mamluki. Yeyote anayekataa kujipendekeza siyo mpinzani.  Tutafakari.

Jambo la tatu ni kujihoji sisi
wenyewe, wasomi na wanazuoni. Tunawajibika kwa nani na kwa nini. Je,
tunatekeleza wajibu wetu ipasavyo? Nimesema kwamba katika mfumo huo wa
kibwanyenye kuna matabaka yanayozaa itikadi na mitazamo yake. Sisi wasomi na
wanazuoni hatuwezi kujidanganya kwamba hatuna upande. Upande tunao. Tujitambue.
Tujiulize, sisi ni wanazuoni wa nani, tabaka gani, tuko upande gani?

Sisi, nyie na mimi, ni tabaka la vibwanyenye, petty-bourgeoisie.  Tuna
chaguo; ama kukumbatia mtazamo, itikadi, maslahi na fikra za mabwanyenye na
masahiba wao, mabeberu, au kuwa na mtazamo wa wavujajasho na kutetea maslahi
yao. Nimetumia neno chaguo maksudi.
Mfanyakazi hana chaguo, mama nitilie hana chaguo, machinga hana chaguo. Kwao
haya ni maisha yao. Mfanyakazi ni mfanyakazi; mama nitilie ni mama nitilie;
machinga ni machinga. Lakini sisi, kwa lugha nyepesi niseme, walalahai, tuna
chaguo. Tunaweza kuchagua kuwa upande wa walalaheri au upande wa walalahoi.

Chaguo ni letu. Tutafakari. Tuamue. Tutende. Tusijipendekeze kote kote;
tutaanguka, na pamoja nasi tutayaangusha matumaini ya waliowengi kwetu.

Ahsanteni.

     Marejeo:

Bagchi, Amiya Kumar, 2005, Perilous Passage: Mankind and the Global
Ascendancy of Capital
. New York: Rowman & Littlefield.

Baran, P. A., 1969, ‘The Commitment of
the Intellectual’, in The Longer View.
New York & London: Monthly Review Press.

Chachage, C. S. L., 2008, ‘The
University as a Site of Knowledge: The Role of Basic Research’, in Chachage
Seithy L. Chachage, Academic Freedom and
the Social Responsibilities of Academics in Tanzania
. Dakar: CODESRIA.

Cabral, Amilcar, 1969, ‘The Weapon of
Theory’, in Amilcar Cabral, Revolution in
Guinea: An African People’s Struggle,
London: Stage 1.

Harvey, D., 2005, A Brief History of Neo-liberalism, Oxford: OUP.

Luxembourg, R., 1913, The Accumulation of Capital, London:
Routledge.

Marx, Karl, 1867, Capital, vol. I, Part VIII, ‘The so-called Primitive Accumulation’.
Moscow: Progress Publishers.

Mazrui, Ali, 1973, ‘When Spain
expelled the Jews and the Moors’, Africa
Today
, Vol. 20, No. 1, United States Policy toward Africa (Winter, 1973),
pp.73-75. Published by: Indiana University Press Stable URL: http://www.jstor.org/stable/4185282.
Accessed:  06/04/2014 10:25

Mazrui, Ali, 1989,  ‘The Satanic Verses or a Satanic Novel?’
Moral Dilemmas of the Rushdie Affair’, based on a lecture originally given at
Cornell University, Ithaca, New York on 1 March 1989.

Mwalimu Nyerere Chair in Pan-African
Studies, 2010, Chachage’s Intellectual
Versatility,
Dar es Salaam: University of Dar es Salaam.

Nyerere, J. K., 1997, ‘Without unity,
there is no future for Africa’, speech at the 40th Indedpendence
Anniversary of Ghana, in New African,
February 2006.

Shivji, Issa G., 2009, Accumulation in an African Periphery: A
Theoretical Framework
. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota.

Toussaint, E., 1999, Your money or your Life! The tyranny of
global finance
. London: Pluto Press.

Williams, Eric, 1964, Capitalism and Slavery. London: Andre Deutch.