Moshi na Machozi

Polisi na Raia

Jasho na Damu

SEHEMU YA HOTUBA YA RAIS 31 DISEMBA 2010

Najua wapo baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa ambavyo vimepanga mikakati ya kuendeleza malumbano ya uchaguzi na kutaka Watanzania waishi kama vile nchi ipo kwenye kampeni za uchaguzi.Wamepanga wakati wote kutafuta jambo au hata kuzua jambo ili kuwachochea wananchi waichukie Serikali. Wamepanga kuchochea migomo vyuoni na maandamano ya wananchi mara kwa mara. Kwao wao huo ndiyo mkakati wa kujijenga kisiasa ili kujiandalia ushindi kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.

Nawatanabaisha ndugu zangu myajue hayo ili msipoteze muda wenu muhimu wa kujiendeleza na kugeuzwa kuwa mbuzi wa kafara kwa ajili ya kuendeleza maslahi ya kisiasa ya watu fulani. Kwa jinsi watu hao walivyokuwa wabinafsi na wasivyokuwa na huruma na wenzao, wako tayari kuchochea ghasia bila kujali madhara yatakayowakuta watu watakaoshiriki. Wao hasa wanachotaka ni ghasia kutokea na vyombo vya dola kuingilia ati waiambie jumuiya ya kimataifa jinsi Serikali yetu ilivyo katili. Nawasihi ndugu zangu msiwasikilize wala kuwafuata wanasiasa hawa.

Nawaomba, wakiwafuata wakumbusheni kuwa wao wanazo fursa nyingi za kusema wayatakayo Bungeni na kwingineko, waache kuwatumia kama chambo au wahanga wa maslahi yao.