SUPERWOMAN: VIPI KUHUSU USUPA ULE WA MWANAMKE?

Jasper “Kido” Sabuni

@KidoJapa

Kuelekea siku ya wanawake, baadhi ya wasanii wanawake, chini ya mwamvuli wa Wasafi, wameachia wimbo uitwao Superwoman. Kwa ujumla wimbo huo unaeleza juu ya ujasiri na uhodari wa wanawake katika dunia ya sasa. Kwa kiasi chake pia, wimbo huo ninaufananisha mahadhi na maudhui sawa na wimbo wa Davido wa Wonder Woman. Yote ya yote, wimbo huu umejawa na tija na binafsi haunikereketi masikioni na kuniudhi machoni, badala yake unanikonga na kuniburudisha moyo.

Kama kazi yeyote ya sanaa, wimbo huu umeniburudisha na pasi shaka umenielimisha na kuniongezea uelewa wa masuala kadhaa. Kubwa kuliko yote hata hivyo ni kwamba wimbo huu umenifikirisha. Fikra zangu zilizokuwa zimeduwaa baada ya kunyeshewa na mvua ziliamshwa na tenzi za wasanii. Hata hivyo ni video ya wimbo huo haswa iliyonifikirisha haswa. Nayo ilinifanya kujiuliza maswali kadhaa wa kadhaa.

Je, tafsiri ya Super Woman ni ipi? Ni ile ya wasanii waliovaa nguo za vitenge na kujistiri kwa nguo ambazo zinaweza kudhaniwa kuwa za staha katika macho ya wengi (wanaume haswa)? Je, usupa wa Gigi ni ule aliovaa kama trafiki (askari wa usalama barabarani)? Vipi kuhusu yule Gigi wa Kampa Papa? Je huyo sio supa? Nao uzuri wa Rosa Ree unaambatana na lile gauni refu alilolivaa? Vipi kuhusu yule Rosa Ree wa “nguo korofi”? Je yule sio supa?

Miongoni mwa watu waliooneshwa kama ma-super woman ni pamoja na Waziri Ummy Mwalimu na Mama Janet Magufuli, je hawa ndio ma-super women? Vipi kuhusu Nandy wa katika Kata akiwa juu ya kiuno cha Ommy Dimpoz? Je, hakufaa kutokea nae akikatika kivile? Vipi kuhusu washereheshaji video (video vixen)? Je, wao sio ma-super women? Mbona wasitokee wao na atokee Naibu Spika Tulia Ackson? Hata Mkuu wa wetu wa Wilaya pendwa… je, usupa wake ni kama kiongozi tu? Kwani hakuwa supa alivyokuwa mlimbwende/mwanamitindo? Mbona picha zake za hivyo nazo zisioneshwe?

Binafsi sina tatizo sana na taswira inayojaribu kujengwa na video husika; hata hivyo, nina ukakasi na kukwazika na unafiki unaodhihirika na kudhihirishwa kiujumla na wimbo huo. U-super wa mwanamke unaishia kujikita zaidi katika macho ya siasa hasa za chama tawala katika mwaka huu wa uchaguzi mkuu, uongozi wa juu na hata elimu ya juu pamoja na mafanikio makubwa kitaaluma, kifani na kiajira. Vipi kuhusu nafasi kama za sanaa? Binafsi kwangu Jaydee na Grace Matata ni Super Women katika namna yao na Vanessa ni Super Woman kwa namna yake. Lakini namna ya Vanessa inaweza kufumbiwa macho ilihali Vanessa anaweza akawa anaonesha ujasiri wake katika kuamua anatokelezea vipi na kwa muktadha upi, licha ya kwamba mitoko yake inaweza kutokuakisi kwa kiasi kikubwa na inayodhaniwa kuwa ni mila na desturi yetu.

Inasikitisha pale ambapo wasanii wanatumia jukwaa lao wenyewe kujichafua wao wenyewe. Katika wimbo huu, hilo linaweza lisionekane moja kwa moja, lakini tafsiri ya nyuma ya pazia ni kuwa, usiwe kama wasanii na uwe kama Dokta Asha-Rose Migiro, Mama Gertrude Mongela, Mama Samia Suluhu Hassan na  Waziri Ummy Mwalimu. Kidogo ukitaka kuwa msanii basi uwe msanii mjasiriamali kama Shishi Baby naam Shishi Baddest (ambaye kwangu mimi ndio katamba kuliko wote wimbo mzima); na kwa huyo Shilole tagi kubwa kwake ni la Ujasiriamali na sio la Usanii.

Hali hii ya kuichukulia sanaa kutokuwa Supa hata hivyo haijaanza na wimbo wa Superwoman. Katika kipindi cha Bartenderwiki kadhaa nyuma, cha hapo hapo Wasafi, Rose Ndauka aliulizwa iwapo mwanaye wa kike akimuambia anataka kuwa kama msanii mwenzake Gigi Money atalichukuliaje. Rose alihamaki kidogo na kusema dhahiri kuwa isingekuwa poa. Kwa maana nyingine, taswira ya Gigi siyo poa kwa mwanaye kwani Gigi siyo Supa vya kutosha kuwa kioo au loli modo (role model) wa mwanaye.

Kuelekea siku ya mwanamke, wakati tukiendelea kuufurahia wimbo huo, pengine ni wakati nasi kama jamii, hususani kwa wanawake katika tasnia ya sanaa, kujitafakari kuhusu Usupa wa Wanawake katika Sanaa. Ni muhimu sana kufanya hivyo kuliko kuendelea kujidunisha kwenye makucha pekee ya siasa, uongozi na taaluma.

Mwisho, ningalifurahi zaidi siku nyingine katika jitihada kama hizo endapo shughuli zote zingeweza kufanywa na wanawake, kwani naamini wapo wanawake wenye utashi na uwezo wa kuongoza video kama au hata kuliko Kenny/ Kenneth aliyeongoza video ya wimbo huo. Na hata utayarishaji wa muziki na hatua nyingine zote zingeweza kufanywa na wanawake wenyewe ingekuwa balida sana. Asanteni kwa wimbo huu.

Kwa mawasiliano zaidi: kidojasper@gmail.com/ +255 712 568 699