Tarehe 31 Oktoba 2022 ilifanyika sherehe kubwa makao makuu ya nchi ya Tanzania mjini Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri iliyolenga kuzinduliwa kwa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi. Zoezi hilo la kukusanya takwimu hizo lilifanyika kwa takribani wiki moja kuanzia Siku ya Sensa, Jumanne tarehe 23 Agosti mwaka huu. Hivyo, ni miezi takribani miwili na ushehe tangu sensa hiyo ifanyike.
Bila shaka wataalamu wa takwimu bado wanapitia taarifa nyingi zilizokusanywa wakati wa sensa kukidhi mahitaji mbalimbali ya wanatakwimu na wadau wengine wa taarifa kuhusu idadi ya wakazi wa Tanzania, mchanganuo wao kiumri, aina ya makazi yao, aina ya vyanzo vyao vya mapato, aina ya elimu na ujuzi walionao, aina ya magonjwa wanayougua na yanayowaletea vifo, na kadhalika. Ingawa siku hizi taaluma ya teknohama imerahisisha njia za kuchakata takwimu za sensa ukilinganisha na teknolojia iliyokuwepo katika kuchakata sensa za nchi hii zilizokuwepo hapo awali tangia mwaka 1910, ilipofanyika sensa ya kwanza, hadi hizo sensa zilizofuata hususani baada ya kupata uhuru, kama vile sensa za miaka ya 1967, 1978, 1988, 2002 na ile ya 2012, bado itakuwa ni mapema mno kusema uchakataji wa takwimu zote zilizokusanywa utakuwa umekamilika. Hivyo, itakuwa ni sahihi kusema uzinduzi huu ulilenga kuupatia umma picha kubwa tu ya matokeo ya sensa ya 2022.
Kuwepo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwenye Uwanja wa Jamhuri katika uzinduzi wa matokeo haya ya sensa peke yake siko kulikoibua mjadala kama huu ambao makala haya yanauchangia. Tafakuri tunduizi inaonesha kuwa kama wasaidizi wa Rais wangekuwa makini walau wangemuepusha na kikombe cha kuwa ndiye aliyesoma takwimu za matokeo ya sensa. Badala yake ingekuwa ni heri kama walau takwimu zingesomwa na Mtakwimu Mkuu wa Shirika la Kiserikali linaloshughulika na masuala ya Takwimu liitwalo National Bureau of Statistics (NBS). Kama zilivyo taasisi nyingi za Serikali, NBS nayo ina makao yake makuu yapo Dodoma.
Kwa maoni yangu, ilitakiwa wataalamu wa takwimu wabashiri mapema kuwa kungezuka mijadala kuhusu usahihi wa takwimu zilizotokana na sensa mara baada ya kuzisoma. Kwa kubashiri hivi, wataalamu hawa, ilibidi wakumbuke kuwa hizi ni takwimu za awali. Ni taarifa za mwanzo zinazotokana na nadharia na uhakiki anuwai kuhusu jinsi mchakato wa sensa ulivyofanyika, pamoja na matukio kadhaa yaliyojitokeza wakati wa – na hata kabla na baada ya – sensa.
Nadhani wasaidizi wa Rais walikuwa sahihi kuhusu siku ya uzinduzi wa maandalizi ya kutekeleza mpango wa sensa tarehe 22 Mei 2021. Walishauri uzinduzi ufanyike na ulifanyika katika viwanja vilivyopo katika Barabara ya Jakaya Kikwete karibu na Kituo Kikuu cha Mikutano cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiitwacho Jakaya Kikwete Convention Center. Uzinduzi huo ulifanyika mbele kabisa ya jengo liitwalo Takwimu House ambalo ndilo makao makuu ya NBS.
Walikuwa sahihi katika ushauri uliohakikisha kuwa sherehe hiyo ya uzinduzi wa matayarisho isingekuja kulalamikiwa kwa kuwa kubwa kupindukia na yenye kuhusisha watu wengi hivyo kutumia rasilimali nyingi mno kama ilivyokuwa hafla ya uzinduzi wa matokeo ya kwanza ya sensa. Pia, ingawa Rais alikuwepo kwenye uzinduzi huo, yeye alikuwa pale kama utambulisho tu wa nchi kutoa ishara kuwa shughuli ya sensa ni muhimu kitaifa. Kwa siku ile kusingetarajiwa kuwepo takwimu zenye kuweza kubishaniwa na wadau. Pia wanataaluma wa tasnia ya takwimu kama Mtakwimu Mkuu na wanatakwimu wenzake ndiyo walioonekana kubeba dhamana ya kutamka mambo yoyoye yanayohusu utaalamu wa sensa.
Mijadala iliyoibuka baada ya kuzinduliwa kwa matokeo ya awali ya sensa umetawaliwa na pande mbili kuu. Wale wanaosifu kazi iliyofanyika na uchambuzi usio na ukosoaji wa takwimu zilizotamkwa na Rais, kwa upande mmoja. Kwa upande wa pili, ukosoaji wa kile kinachotamkwa kama matumizi mabaya ya rasilimali za nchi kwa kufanya sherehe kubwa kwenye uwanja wa michezo pamoja na ukosoaji wa usahihi wa takwimu zenyewe alizotamka Rais wakati wa uzinduzi. Kuhusu usahihi wa takwimu kuna wakosoaji kama Fatma Karume waliofanya utani kuwa labda Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imejifunza kuchakachua takwimu toka kwa Tume ya Uchaguzi (NEC) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwanza, kwa upande wa wakosoaji, kuna wanaohoji, na mimi nakubaliana nao, umuhimu wa kwenda kwenye uwanja mkubwa wa michezo kufanya uzinduzi wa matokeo ambayo kwa kweli ni ya awali,wakati ambao nchi inapitia kipindi kigumu cha mgawo wa maji katika miji mikuu kama Dar es Salaam, pamoja na matatizo mengine mengi kuhusiana na nishati ya umeme na mafuta yanayotumika kwenye magari na mitambo. Wakosoaji wanasema, je, washauri wa Rais hawakujua kuwa sherehe kama ile ya wakati wa uzinduzi wa matayarisho ya utekelezaji wa sensa mwezi ingetosha? Hela ambayo ingeokolewa si ingeweza kutumika kwenye kuongeza nguvu ya rasilimali za kushugulikia suala la kukosekana kwa maji mijini na tishio la ukame nchi nzima linaloweza kuzaa kipindi cha njaa hasa kwa wale wananchi wasio na kipato cha kutosha kununua chakula?
Je, wasaidizi wa Rais hawajui kuwa bei za vyakula hata sasa hivi zimepanda sana kila mahali nchini? Yaani hawajui gharama za maisha nchi nzima kwa ujumla, hususani kwa wananchi wa kipato cha chini, zimepanda sana? Hivi hawaelewi wako wananchi watajiuliza kwa nini wanatozwa tozo kila mahali, hata kama makali yake yamepunguzwa kidogo, huku serikali ikionekana kushabikia matumizi makubwa ya rasilimali fedha kwenye mambo ya sherehe kama ya uzinduzi wa matokeo ya awali ya sensa?
Pili, kwa upande wa takwimu za sensa, hivi washauri wa Rais hawakuwaza kabisa uwezekano wa kuwepo kwa watakaohoji takwimu zilizotokana na undeshaji wa sensa uliogubikwa na kasoro za hapa na pale zilizotangazwa moja kwa moja wakati wa kipindi cha sensa? Je, baada ya wataaalamu wa takwimu kuyaona hayo matokeo ya sensa na kukubali kuwa kuna sehemu matokeo haya yalikuwa yanakinzana na matarajio ya wanataaluma ya utabiri wa uongezekaji wa idadi ya watu nchini kwetu, tena wanataaluma ya takwimu wa taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa, hawakujiuliza mara mbili mbili kuhusu namna ya kuzitoa kwa umma takwimu hizo za awali? Je, watakwimu wetu hawa hawakuona umuhimu wa kumwepusha Rais na kikombe cha kutamka takwimu za matokeo ya awali ya sensa na wao wakabeba huo msalaba ili kukitokea kukosolewa kwa takwimu ukosolewaji huo uwe wa wao kama wanataaluma na si wa Rais ambaye yeye si mwanataaluma ya takwimu za sensa ya watu na makazi?
Hivi ni kweli kuwa wanataaluma wetu hawa hawakuwa wana taarifa za ubashiri wa wanataaluma wa idadi ya wakazi wa Tanzania tayari kuwa zaidi ya milioni 61 hata mwaka wa 2020 na 2021? Walikuwa hawana taarifa ya ubashiri wa kitaalamu wa, kwa mfano, wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam kuwa takribani milioni 7.4 kufikia mwaka 2022 toka utabiri wa milioni 7.0 mwaka 2021 na milioni 6.7 mwaka 2020? Kama walijua haya yote, ambayo yeyote anayetumia mtandao kama wa Google anaweza akajitafutia mwenyewe, je, kwa nini hawakuona ni vizuri ndio wao watamke takwimu za matokeo ya awali ya sensa ili wakosaaji wa usahihi wa takwimu za matokeo haya ya sensa wawakosoe wataalamu wa takwimu bila kumhusisha Rais?
Nilijiuliza maswali haya huku nikukumbuka jinsi marehemu Mwalimu Nyerere alivyoandika hata na kitabu ambacho kiliwakosoa Mheshimiwa John Malecela, wakati huo akiwa Waziri Mkuu, na marehemu Mheshimiwa Horace Kolimba aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa kati ya 1990 na 1995, kwa kuwatuhumu kutomshauri vizuri aliyekuwa Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa wa wakati huo, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, hususani kuhusu masuala ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Ingawa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inasema Rais halazimiki kuuchukua ushauri wa mtu yeyote, ikiwa ni pamoja na washauri wake rasmi kama mawaziri na watendaji wengine anaowateua, bado hilo peke yake haliwaondolei lawama washauri wa Rais wanaposhindwa kumshauri vizuri ili kulinda hadhi na haiba ya Urais kama taasisi iliyo alama ya utaifa wa Watanzania.
Hili ni muhimu ikikumbukwa kuwa Rais si mtaalamu wa kila kitu. Rais anawategemea washauri wake kwenye mambo mengi. Washauri wana jukumu adhimu hasa kama hawafanyi kinachoitwa siku hizi “uchawa” na kumsifia kwa kila kitu na hata kutaka kuwaaminisha wananchi kuwa Rais anajua kila kitu na ni mtaalaamu wa kila kitu.
Ndiyo maana wengine tumekuwa tunafanya uchechemuzi kuhusu umuhimu wa Tanzania kuandika Katiba Mpya inayotupilia mbali dhana ya Urais wa Kifalme na badala yake kukumbatia Urais wa Mfariji Mkuu wa nchi anayeelekezwa na Katiba kuzingatiwa ushauri unaoletewa na washauri wake waliokula kiapo kutoa ushauri huo na hivyo wao kuwajibika moja kwa moja na kutolewa kwa ushauri unaoleta madhara au maumivu ya aina yeyote kwa wananchi.