HALI YA ELIMU KATIKA MIAKA 50 YA UHURU WA
TANZANIA

(1961 – 2011)

Na

JACKSON MAKWETTA

(Watu wenye akili huweka akiba yao katika
maarifa – Mithali 10:14
)

II. VUGUVUGU LA UJENZI WA SHULE NA VYUO VIKUU NA
MATATIZO YAKE

I.                       
UTANGULIZI

1.             
Nikiangalia matatizo yanayoikabili sekta ya elimu nchini, machozi
hunilengalenga hasa kutokana na kutambua ukweli kuwa ubora wa Taifa lolote lile
hutegemea na ubora wa elimu itolewayo kwa watu wake.  Maana yake ni
kwamba, Watanzania tukitaka kuharibu ubora wa Taifa, letu njia nyepesi ni kuua
au kuharibu misingi ya kupatia na kutolea elimu bora.  Kwa hiyo Watanzania
tukikiuka misingi ya kutolea na kupatia elimu bora misingi hiyo
itatukiuka.  Pia soma viambatanisho vilivyoambatanishwa kwenye makala
haya.

2.             
Kuna wakati Tanzania ikisherehekea uhuru wake, hayati Mwalimu Julius K. Nyerere
Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanzanaia aliulizwa swali lifuatalo na waandishi
wa habari kutoka nje ya nchi.  Kitu gani hasa kinawafanya Watanzania
msherehekee siku hii ya Uhuru wenu?   Hayati J.K. Nyerere aliwajibu
kuwa Watanzania walikuwa wakisherehekea siku ile kwa sababu ya kuwa hai
hadi siku ile
.  Huenda jibu lile lilikuwa sahihi.  Hata sisi
tungeulizwa swali kama lile leo bila shaka tungejibu kama alivyojibu hayati
J.K. Nyerere.

Mwezi uliopita kulikuwa na makongamano mengi nje
na ndani ya Chuo hiki, kuhusiana na suala hili na mengine mengi.  Kwa hiyo
mimi sina geni katika suala hili, ila inawezekana kutoa mawazo yale yale kwa
njia tofauti kama wasemavyo waswahili kitambaa kimoja lakini mivalio
mbalimbali.

3.             
Je hali ya elimu nchini ikoje?  Kuna wakati nchi yetu ilisifika sana kwa
kufanikisha Elimu ya Msingi kwa kutumia njia za kimapinduzi chini ya ushauri wa
mzee Nicholas Kuhanga.  Wakati huo Tanzania ilitoa Elimu ya Msingi na
Elimu ya Kisomo bure kwa watoto na watu wazima wote.  Vilevile Serikali
ilitoa elimu ya sekondari na ya vyuo vikuu kwa malipo kidogo.  Kumbuka
elimu hiyo ilithaminiwa kote duniani.  Dosari kubwa katika utoaji wa elimu
ya sekondari na ya vyuo vikuu ni kwamba, kwa muda mrefu hata baada ya Tanzania
kupata uhuru iliendelea kutolewa kwa watu wachache sana.  Leo elimu ileile
inatolewa kwa watu wengine zaidi na kwa gharama nafuu zaidi.

  

II.            
VUGUVUGU LA UJENZI WA SHULE NA VYUO VIKUU NA MATATIZO YAKE

4.             
Ni katika miaka ya hivi karibuni tu ndipo vuguvugu la ujenzi wa shule za
sekondari za serikali, za binafsi na vyuo vikuu lilianza kujitokeza na kusababisha
leo Tanzania kuwa na vyuo vikuu na vyuo vishiriki kufikia 40. Leo shule za
sekondari na vyuo vikuu vinaota kama uyoga. Pongezi ziwaendee wananchi na wote
waliohusika na ujenzi wa shule hizo. Kwa upande wa sekondari watu binafsi
wanajenga shule hizi kwa kutegemea fedha zitokanazo kwa wazazi wa watoto wakati
kwa upande wa vyuo vikuu watu binafsi wanajenga kwa kutegemea mikopo toka BODI
YA MIKOPO. Kwa hiyo bila mikopo hiyo (Loan Board). Baadhi ya vyuo vikuu
haviwezi kudumu.

5.             
Hata hivyo mwamko wa wazazi kupenda elimu umesababisha elimu kupatikana kwa
njia za ulanguzi. Shule za binafsi ni za watu wenye uwezo, kama zilivyo
hospitali binafsi. Leo shule za serikali ndizo shule za watu wa kawaida. Tatizo
jingine linatokana na wamiliki wa shule za binafsi ni kuwarubuni walimu wa shule
za serikali ili wajiunge na shule zao na ili kuwapata huongeza mishahara na
marupurupu mengine mengi. Matokeo ya kufanya hivyo ni shule za binafsi
kufaulisha watoto vizuri kuliko shule za serikali. Leo baadhi ya wazazi wako
tayari kupelekea watoto wao katika shule za binafsi hata kama wamechaguliwa
kwenda katika shule za serikali. Wazazi hawaelewi kwa namna gani shule yenye
wanafunzi zaidi ya 300 inaweza kuendelea kielimu wakati ikiwa na walimu watatu
au wanne tu. Shule tunazo lakini zinakabiliwa na uhaba wa kila kitu (walimu,
vitabu, maabara, vyumba vya madarasa, mabweni, matundu ya vyoo, nyumba za walimu,
maktaba n.k.) Maneno ya kuzingatia hapa ni UHABA na UKOSEFU wa walimu wa
masomo, huduma ya maji, umeme, zahanati, mabweni, viwanja vya michezo, vifaa
vya michezo na kadhalika. Msamiati huu pia unatawala vyuo vikuu, vya ualimu,
shule za Elimu ya Msingi, vyuo vya ufundi na kadhalika. NI UHABA NA UKOSEFU wa
mahitaji katika kila ngazi ya elimu. Shule za sekondari za kata au shule za
madiwani zote zinakabiliwa na uhaba na ukosefu wa mahitaji ya shule.

6.             
Kutokana na UHABA NA UKOSEFU huo elimu inaporomoka KATIKA NGAZI ZOTE.
Hii ndiyo hali ya elimu nchini. Watanzania wanaopenda ukweli wanajua ukweli
huu.
Kazi kubwa ya wanafunzi wa vyuo vikuu ni kutafuta ukweli wa mambo.
Vyuo visipofanya hivyo vitapoteza umuhimu wa kuwepo kwake. Tume ya elimu ya
1982 inasisitiza suala hili. Naomba wale ambao hawajasoma ripoti ya TUME YA
ELIMU
ya mwaka 1982 na mapendekezo ya tume yake waisome. Sehemu kubwa ya
mapendekezo yale ni muhimu zaidi leo kuliko mwaka 1982. Inasikitisha kuona kuwa
Watanzania wengi hatuna muda wa kusoma vitabu au maandishi! Tuna muda wa
kufanya mambo mengine! Binafsi naamini kuwa TUME ya 1982 ilifanya kazi nzuri.
Wajumbe wa tume ile wengi wao wangali hai. Kwa namna gani wanashirikishwa
katika kuboresha elimu nchini ni swali zuri la kujiuliza. Kwa tabia ya
Watanzaia si rahisi kuwashirikisha watu wengine katika mambo yetu. Kwa mfano,
Mwalimu Nicholas Kuhanga aliyefanikisha UPE katika nchi yetu kwa nini
tusimshirikishe katika uboreshaji wa elimu nchini?

7.             
Leo shule za sekondari na vyuo vikuu vinaongezeka wakati ubora wa elimu unazidi
kupungua. Kwa mfano, katika matokeo ya mwaka 2010 nusu ya vijana wa Kidato cha
nne waliofanya mtihani wa Taifa hawakufaulu. Hata katika miaka mingine, vijana
wengi wanafaulu kwa viwango vya chini yaani, divisheni 3 na 4 na idadi ya wale
wanaoshindwa mitihani ya mwisho inazidi kuongezeka. (Tazama kiambatanisho)
kuonyesha kuwa ubora wa elimu nchini unaporomoka. Labda wengine hawapendi
kusikia maneno, kushuka kwa ubora au kuporomoka kwa elimu. Naomba watushauri
tutumie maneno gani?

8.             
Sisemi kuwa elimu imekufa bali nasema ubora wa elimu umepungua (vijana
wengi kushindwa mtihani wa kidato cha nne). Pia tathimini iliyofanywa hivi
karibuni kuhusu hali ya elimu katika nchi za Uganda, Kenya na Tanzania
imeonyesha kuwa Tanzania inatoa elimu hafifu kuliko katika nchi za Uganda na
Kenya. Ubishi kuhusu vigezo vilivyotumika katika zoezi hili unaweza kuendelea
ila naomba tutenganishe utaalamu na siasa. Kwa mfano, kuna baadhi ya wanasiasa
wanapendekeza kuwa mitihani ifutwe katika ngazi zote fulani za elimu. Lakini
hawapendekezi njia gani zitumike katika kupima elimu itolewayo nchini. Hata
hivyo sielewi lengo lao ni nini hasa. Watanzania tukikiuka misingi ya
kutolea na kupatia elimu bora, misingi hiyo itatukiuka.

9.             
Lazima tujiulize maswali yafuatayo kuhusu Elimu itolewayo katika nchi yetu:
Tunataka nini katika elimu yetu .Tunataka elimu yetu itatue matatizo gani? Je
elimu hii inatatua au inaongeza matatizo? Je tunataka elimu ya bure na ya
lazima kwa watanzania wote na ifikie ngazi gani? (MSINGI AU Y A SEKONDARI AU
VYUO VIKUU) Je kuna uhusiano gani kati ya maendeleo katika elimu na maendeleo yetu
kiuchumi? Je, kwa namna gani BODI YA MIKOPO itaweza kukidhi mahitaji
ya vyuo bila kufanya mabadiliko ya kimsingi katika sera ya Elimu? Kwa nini
watoto wa matajiri ambao tangu elimu ya awali, msingi na sekondari wamekuwa
wakisoma katika shule za binafsi kwa gharama kubwa leo wanaomba mikopo na
serikali inawapa mikopo hiyo. Tatizo hili halijatatuliwa
.

III.          
TANZANIA IMEPIGA HATUA KUBWA KATIKA ELIMU LAKINI

10.          
Katika makala haya nazungumzia mafanikio na matatizo ya elimu katika miaka 50
ya uhuru wa Tanzania. Takwimu kuhusu idadi ya shule, vyuo, walimu, na wanafunzi
zinapatikana kwa urahisi kutoka wizara husika. Takwimu hizo zinaonyesha
kuongezeka kwa kila kigezo cha kutolea na kupatia elimu nchini. Nashauri
tuzitumie vizuri taarifa hizo. Kwa mfano, idadi ya shule za sekondari za
serikali imeongezeka sana. Hali kadhalika, idadi ya walimu wa shule hizo,
lakini vipi uwiano kati ya walimu na wanafunzi katika shule hizi?
Ukweli ni kwamba walimu ni wachache kwa uwezo wa kufundisha na kwa idadi
yao.
Kutokana na uchache na uwezo wao mdogo wanafunzi katika ngazi zote za
elimu nchini hawapati “dozi” kamili ya elimu
wanayotakiwa kupata hali inayosababisha wanafunzi kumaliza elimu wakiwa
hawajapata “dozi” kamili ya elimu wanayotarajia kuipata. Kwa hiyo
Watanzania tusishangae kwa nini nchi yetu ni ya mwisho katika utoaji wa elimu
bora katika Afrika ya Mashariki. Kamwe vijana wetu hawataweza kupata elimu
bora ya Msingi au ya Sekondari au Vyuo Vikuu kwa kukaa tu katika majengo
yaliyoandikwa
“Shule” au Chuo kikuu
. Kamwe vijana hawataweza kupata elimu ya
ngazi yoyote ile kwa njia ya OSMOSIS. Upatikanaji wa elimu bora una
kanuni na misingi yake. Tukikiuka misingi ya utoaji elimu bora misingi
itatukiuka. Kama elimu bora ni ufunguo wa maisha bora basi elimu mbaya ni
ufunguo wa maisha mabaya.

IV.          
TUNAPITA WAKATI MGUMU KATIKA MASUALA YA ELIMU

Watanzania tunapita wakati mgumu kiasi kwamba
hata kubaki hapa tulipo ni kazi ngumu, kurudi nyuma ni kazi rahisi, kwenda
mbele ni kazi ngumu zaidi. Breki za gari tulilopanda hazishikiki. Kuna hatari
ya gari kurudi nyuma. Gari hili ni nchi yetu ya Tanzania. Nchi ikirudi nyuma
tutapoteza hata mafanikio kidogo tuliyoyapata katika miaka 50 ya uhuru. Hali
inazidi kuwa mbaya. Vyanzo vya maii vinakauka, nchi inakosa umeme,
gharama za huduma muhimu zinazidi kupanda, vijana wanakosa aiira na nguvu kazi
yao haitumiki
. Maana yake ni kwamba mapendekezo yoyote ya kuboresha elimu
lazima pia yaonyeshe nchi itapata wapi fedha ya kufanyia kazi hiyo? Kwa
kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa ushuru na kupunguza rushwa, Tanzania
ingeweza kupata fedha za kutosha za kuboreshea elimu yake. Fedha ya misururu ya
magari makubwa yaendayo Zambia, Malawi na Congo kila siku inatumikaje? Watu
wamepata wapi fedha ya kununua utitiri wa malori, magari madogo na mapikipiki
yanayosababisha barabara zisipitike katika miji yetu? Pamoja na umaskini wetu
lazima Watanzania tujue kuwa maendeleo yetu yataletwa na sisi wenyewe kwa
bidii, maarifa, nidhamu, na kwa kuiitegemea.
Serikali ina uwezo mkubwa wa
kutunga sheria na kuweka taratibu za kusimamia uchumi lakini haina uwezo wa
kusimamia taratibu zake. Ni nchi zenye serikali imara kama Marekani ndizo
zinaweza kusimamia uchumi wake. Kwa mfano serikali bila kupanga imekabidhi
uchumi wa Tanzania kwa watu wachache ambao inashindwa kuwatoza kodi. Kwa nini
tusichukue hatua zifuatazo:-

·     
Tulipe kodi na ada za shule kwani kujitawala ni kujitegemea

·     
Tufufue au kutilia mkazo siasa na Elimu ya Kujitegemea.

·     
Tuchangie gharama za maendeleo kwa kufanya kazi ndogondogo za mikono

·     
Kwa nini kazi ya kufyeka nyasi katika shule isifanywe na wanafunzi?

·     
Tusimamie vizuri shughuli zote za maendeleo ili kuzuia ufujaji wa fedha.

·     
Serikali isimamie elimu itolewayo nchini ili kuondoa Ulanguzi, Utapeli na Uchakachuaji.

·     
TCU iongezewe madaraka zaidi kuhusiana na vyuo vikuu.

·     
Tuongoze ufanisi katika kazi zetu na kupenda kufanya kazi.

·     
Tubane matumizi na kutumia vizuri kila senti tunayopewa

·     
Tuache rushwa, ufujaji mali na uvivu

·     
Tupunguze sherehe, tafrija, mikutano, semina na kongamano

·     
Tutumie vizuri wakati

·     
Tupunguze michango ya starehe (Inner party, Send-off, Bag Party, Kitchen Party
na Wedding party)

·     
Tupunguze migomo badala yake tujue kwa undani sababu ili kama ni uzembe hatua
kali ziwe zinachukuliwa kwa wahusika mapema.

·     
Kama idadi ya wanafunzi wa kwenda vyuo vikuu huwa haijulikani hadi mwezi mmoja
kabla ya vyuo kufunguliwa tunategemea nini. Tujisahihishe.  Nani alaumiwe?
Kama migomo huzaa matunda kwa nini ifutwe.

·     
Tuanzishe michango ya maendeleo ya elimu badala ya michango ya Harusi.

·     
Tubadili mwelekeo wetu au mtazamo wetu kuhusu umuhimu   wa mambo
(mindset). Kwa mfano kuongeza ubora wa elimu bila kuwashirikisha wananchi
katika gharama hizo.

11.          
Kama kuna wakati mzuri wa kubadili mambo au kufanya mapinduzi katika elimu basi
wakati huo ni sasa.  Mwamko wa watu wa kuelewa maana na umuhimu wa kutoa
elimu kwa watoto wao umeongezeka.  Matatizo ni mengi, na hakuna nchi isyo
na matatizo.

12.          
Elimu kwanza.  Inaelekwa treni la elimu liko nje ya reli

Watanzania tunawezaje kulirudisha treni katika
njia yake.  Tazama katika baadhi ya shule za Elimu ya Msingi bado baadhi
ya wanafunzi wanamaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma na kuandika na ½
ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne wanafeli mtihani wa mwisho.  Kama
watoto wanamaliza elimu ya msingi bila elimu ya msingi wataendeleaje
mbele?  Ni Elimu gani hii ambayo haimwezeshi mwanafunzi kuwaelezea watu
kile anachokijua au kubuni na kuibua mambo, kufikiri kisayansi, au kupeleleza
na kuchambua mambo, kuumba vitu, kutafuta njia sahihi za kutumia katika kutatua
matatizo yake.  Tukubali kuwa elimu yetu ni butu.  Tofauti na wenzao
walioachwa nyuma baada ya kumaliza elimu ya Msingi hawa hawawezi kulima, wala
kupalilia mimea isipokuwa kupiga simu, kupiga stori, kukaa vijiweni, kuzurura
mitaani na kucheza disco. Lakini ajabu ni kwamba vijana hawa wanataka makuu,
wanataka wakipanda mahindi asubuhi wavune jioni.  Mara wakianza kazi wanataka
kuwa na simu pana, gari la kuendea kazini na nyumba nzuri ya kuishi.  Pale
wanapokosa vitu hivi hupauka akili na   huwafanya wafanye
yasiyotegemewa.  Vijana hawa ni wengi na wanaongezeka kila mwaka. Serikali
isipowatumia vijana hawa watu waovu watawatumia.

V.            
HAJA YA KUTUMIA UZOEFU ULIOKO NCHINI

13.          
Duniani hakuna kidumucho isipokuwa mabadiliko.

Watanzania wana haki ya kupata kilicho bora
katika nchi yao ikiwa ni pamoja na kuwatumia watumishi bora waliostaafu na
vijana wenye akili kwa faida ya nchi yao.  Tabia ya kuwatenga au
kutowatumia watu hawa ni tabia mbaya inayodidimiza nchi yetu.  Kuwatenga
watu kwa sababu za kisiasa au kwa sababu ya kuwaogopa au kwa sababu ya roho
mbaya ni ufisadi wa aina yake.  Wenzetu huko Ulaya ambako tunaiga mambo
mengi wanafanya hivyo. Si vema kwa baadhi ya Watanzania kuonekana hawatakiwi au
wanaishi kwa hisani ya watu fulani. Wale wenye uwezo au madaraka wanaweza
kumuua raia yoyote au kumtesa au kumtenga kwa sababu zozote zile ila hawawezi
kunyang’anya utaifa na uraia wake, hawawezi kumfukuza katika nchi yake.

14.          
Tume ya elimu chini ya uenyekiti wangu ilichambua hali ya elimu iliyokuwa
ikitolewa wakati ule hapa nchini.  Pia ilitembelea nchi nyingi
zilizoendelea na zisizoendelea ili kujifunza taratibu zao za utoaji
elimu. Tume ilijifunza mengi na kutoa mapendekezo kwa serikali.  Ni
muda mrefu umepita (1982). Kama serikali inatekeleza au haitekelezi mapendekezo
ya Tume mimi sina la kufanya.  Ajabu tangu nitoe ripoti ile sijawahi
kuitwa au kuulizwa lolote na wizara husika kuhusu elimu isipokuwa ninyi
leo.  Kwa maoni yangu hii ni kasoro kubwa katika nchi yetu.  Nchi
haifaidiki na utajiri wa uzoefu wa watu walio nje ya mkondo wa serikali kwa
sababu ya sababu zisizoeleweka (wataalamu majaji, wanajeshi, walimu, mawaziri
hawatumiki).  Watu hawa ni hazina ya nchi na si tishio kwa yeyote. 
Nchi hii ni yetu sote.  Tusiwaenzi watu waliostaafu baada ya kufa kwa
kuhudhuria mazishi yao.  Tusisubiri watu wafe ndio tuseme mazuri yao.

VI.          
BAADHI YA VIKWAZO VILIVYO MBELE YETU

Huenda mapendekezo ya Tume ya MAKWETTA
yamepitwa na wakati.  Hofu yangu ni kwamba tangu Tume ile itoe mapendekezo
yake kwa serikali sijawahi kuitwa kutoa ushauri au ufafanuzi wowote kuhusu
mapendekezo ya Tume.  Napendekeza iundwe Tume nyingine kwa madhumuni
yaleyale ili kukidhi mazingira ya Karne ya 21.  Tusichezee elimu madhara
ya uharibifu yatakuja jitokeza miaka michache ijayo.

15.          
Hapa chini natoa mapendekezo lakini mapendekezo haya yatafanikiwa tu kama
baadhi ya mambo yaliyoko yatabaki kama yalivyo.  Mabadiliko katika baadhi
ya mambo yaliyoko leo yataathiri nguzo muhimu za kutolea na kupatia
elimu.  Kwa hiyo mapendekezo yoyote kuhusu mabadiliko katika mfumo wa
elimu  nchi nzima yazingatie mambo yafuatayo:-

   
Kuongezeka
kwa idadi ya watu ambako kutasababisha kukua kwa umaskini.

   
Kuweko
kwa watu wenye uzoefu na kutotumia uzoefu wao.

   
Kupungua
au kukosekana kwa maji yanayohitajika na binadamu, wanyama na mimea (ukame)
kutokana na sababu mbalimbali.

   
Kuongezeka
kwa milipuko ya magonjwa ya hatari na vifo.

   
Kuharibika
na kuchafuka kwa mazingira (mito na vijito vyote kukauka).

   
Kushuka
kwa uchumi kutokana na kupungua kwa mafuta, gesi, maji, madini na kadhalika.

   
Uhaba
au kukosekana kwa chakula (njaa).

   
Kukua
kwa umasikini na kukosekana kwa amani.

   
Kukosekana
kwa ajira na kutotumika kwa nguvukazi.

   
Kustawi
kwa rushwa na utawala mbovu.

   
Ubaguzi
wa kipato (maskini na matajiri) na wa rangi. (watu weusi kuzuiwa kwenda Ulaya).

   
Kurudi
kwa ukoloni na utumwa mamboleo

   
Wenyenavyo
watashika mali na utawala wan nchi

   
Kustawi
kwa ukoloni mamboleo.  Nchi itageuka nchi ya ombaomba.  Kesho ni leo
na leo ni kesho.  Kwa hivo kila jambo tufanyalo au tusilofanya leo
linajenga au kubomoa misingi ya maendeleo yetu ya kesho.  The future is
now.

VII.        
HATUA ZA KUCHUKUA ILI KUZUIA KASI YA KUPOROMOKA KWA ELIMU NCHINI

16.          
Kobe hufanya maendeleo pale tu anapothubutu kutoa shingo yake  nje ya
gamba lake.  Kwa hiyo pamoja na yote yanayosemwa kuhusu elimu, ni vigumu
sana kutabiri kuhusu mambo yatakavyokuwa kesho.  Labda  tutumie ujuzi
na uzoefu wetu katika  kuelezea baadhi ya viini vya matatizo katika shule
na vyuo vyetu:-

   
Wizara
ya Elimu iunde haraka Tume ya Elimu ili kutizama matatizo ya elimu na mwelekeo
wake kwa lengo la kuzuia Tanzania kuachwa nyuma kielimu au kuzuia kuporomoka
kwa elimu.

   
Serikali
isimamie na kuratibu elimu katika ngazi zote ili kuzuia biashara na ulanguzi
katika elimu chini.

   
Kutokana
na uwezo mdogo wa walimu hasa walimu wa shule za sekondari, yaanzishwe mafunzo
ya kuboresha elimu yao wawapo kazini.

   
Serikali
itizame upya sera ya kugharamia elimu nchini ili kuhakikisha kuwa fedha ya umma
inatumika vizuri na inatolewa mapema kwa wahusika.

   
Hatua
za kuboresha elimu zianzie katika vyuo vya ualimu, vyuo vikuu na shule za
msingi na mafunzo kazini.

   
Sekta
ya ukaguzi iimarishwe kwa kuongeza wakaguzi na vyombo vya usafiri.

   
Migomo
shuleni na vyuoni inaathiri sana maendeleo ya elimu nchini licha ya kuharibu
mali ya umma. [Sera ya Mikopo bado hafifu]

   
Wanafunzi
washirikishwe katika kubana matumizi shuleni na vyuoni kwa kufanya kazi
ndogondogo zisizopoteza muda wao mwingi.

   
Wanafunzi
wajihusishe na ubora na usalama wa mazingira ya shule na vyoo badala ya kubaki
na 3Ks tu yaani KUSOMA, KULA NA KULALA.

   
Wanafunzi
washiriki katika masuala ya usafi, usalama na maendeleo ya shule au vyuo vyao.

   
Baadhi
ya wazazi watatakiwa kulipa ada yote katika vyuo vikuu ili kupunguza kuelemewa
kwa serikali katika suala hili.

   
Udhaifu
wa serikali usielezwe kwenye vyombo au taasisi zisizohusika (BODI YA MIKOPO)
na utoaji wa huduma fulani muhimu.

   
Taarifa
kuhusu uwezo wa wazazi wa watoto kiuchumi zijulikane mapema.

   
Ziundwe
BODI ZA ELIMU katika ngazi za wilaya  ili kusaidia Wizara ya Elimu 
kusimamia kwa kuwahusisha  wadau wote wa Elimu Wilayani.

   
Serikali
itizame upya sera kuhusu lugha ya kufundishia shuleni na vyuoni.  Lugha ya
“Kiswakinge” inayotumika leo shuleni inaathiri elimu.  Leo Kiingereza ni
Kiswahili cha dunia!

   
Serikali
iwe na utaratibu wa kuendelea kuwatumia walimu waliostaafu (Sera au Mwongozo)

   
Liingizwe
somo la Maadili katika ngazi zote za kutolea elimu nchini.

   
Itolewe
tafsiri sahihi kuhusu maana ya shule na kuhusu maana ya shule na mahitaji ya
shule, chuo.  Shule au chuo ni majengo, walimu bora na wa kutosha, vifaa
bora vya kutosha n.k.

   
Sera
ya elimu iwe wazi katika ngazi zote.  Je ni kutoa elimu ya bure kwa watoto
wote kuanzia Elimu ya Awali, Msingi (UPE) elimu ya Sekondari (USE) na ya a vyuo
vikuu (UUE) na kadhalika.

VIII.      
HITIMISHO

17.          
Hakuna kidumucho isipokuwa mabadiliko. Kama elimu bora ni ufunguo wa maisha
bora basi elimu mbaya ni ufunguo wa maisha mabaya.  Elimu itolewayo katika
Tanzania ni ufunguo wa maisha bora au ni ufunguo wa matatizo?  Je, vijana
wetu wanasoma kwa malengo?  Je, Elimu itolewayo nchini inakidhi malengo
yao?  Kama haikidhi kwa nini umma wa nchi hii uendelee kugharamia elimu
isiyo na manufaa?  Kama shule na vyuo vyetu havifundishi kufikiri,
kudadisi, haviumbi kazi bali vinaibua tamaa ya kupenda starehe na kazi nyepesi.
Tatizo kubwa la nchi hii ni serikali kutofuatilia, wala si tatizo la kukosekana
kwa sera.  Hili ni taifa la wasemaji maneno na siyo taifa la
watekelezaji.  Mapendekezo ya tume ya MAKWETTA ya mwaka 1982 licha
ya kukubalika na serikali yamewekwa kabatini.  Hayatekelezwi kwa sababu
wahusika hawataki kupata “taabu”.  Baada ya kuichambua tena ripoti ya TUME
mimi naona bado yana manufaa hadi leo.

18.          
Sasa naelewa kwa nini V.I Lenin alisema matumizi ya nguvu ni lazima kwa mama
aliyefikia siku za kujifungua. Kwa maneno yake Lenin alisema ‘force is a
midwifery of any society pregnant of a new one’. Kwa maoni yangu Tanzania ni
kama mama mjamzito ambaye siku zake za kujifungua zimefika lakini
hajifungui. 

Bila kumpasua mama, wote wawili mama na mtoto
watakufa.  Kwa hiyo:

·              
Mama akipasuliwa wote wawili wanaweza kuokolewa (au mmoja wao).  Tanzania
inahitaji kupasuliwa ama la sivyo itaendelea kudidimia kiuchumi milele.

·              
Nchi ya Tanzania inahitaji kiongozi shupavu mwenye msukumo, mwenye akili na
siyo mkusanyaji au mlafi, mwaminifu, mchapakazi mpenda haki na anayeona mbali.

·              
Rushwa na utawala usiothubutu. Tanzania ni kama mjamzito: Inahitaji
kupasuliwa  ili kuwaendeleza watanzania kiuchumi.

19.          
Nimekosa focus kwa sababu kichwa cha habari ni kikubwa na hakiko wazi kwa hiyo
kama makala haya hayakukidhi lengo letu naomba tusameheane.  

Tafuteni
kwanza maendeleo katika elimu na mengine yote yatafuata.

Twende pamoja

Tushirikiane;

Tuboreshe elimu,

Tujenge nchi yetu,
Tanzania