Taifa Stars Nayo Inahitaji Kocha Kijana?

Kwa mara nyingine tena timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeshindwa kufuzu kusonga
mbele katika mashindano ya kimataifa ya kandanda. Imetolewa na timu ya Taifa ya
Msumbiji, Black Mambas. Visingizio vinaendelea
kutolewa kuhusu kipigo hicho.

Licha ya kuishirikisha ‘kamati ya ufundi’, timu yetu
imebwagwa. Pamoja na kuwepo kwa posho za kutosha kuulipa msafara wa viongozi wa
michezo walioongozana na timu yetu, ‘tumepigwa bao’. Japo tuna kocha mwenye
uzoefu wa siku nyingi, tumeambulia kichapo.

Pengine sasa ni wakati mwafaka wa kuwa na kocha kijana
wa kuwanoa vijana wenzake. Labda wataelewana zaidi. Si vijana ndio wana mawazo na
maono mapya? Kama asilimia kubwa ya wachezaji ni vijana kwa nini kocha awe mzee
ilhali vijana wapo wamejaa tele?

Hata huko kwenye ligi za kimataifa makocha vijana si
ndio wanazidi kuja juu – kina Pep Guardiola? Na hata miondoko yao inafananafanana,
yaani, imekaa kiujanaujana kuanzia kwenye mavazi, maneno na mbinu?  Si nasi tuanze basi ‘ujanaishaji’ wa kocha wa
Stars?

Au tunasubiri tupate kwanza Rais Kijana Ikulu mwaka
2015 ndio atuletee Kocha Kijana? Kama matokeo ya timu yetu ya taifa ya mpira ni
kielelezo cha utendaji wetu kama taifa, si tuanze na Kocha Kijana tuone
utendaji wake utakavyousonda kidole wa Rais Kijana?

Makala mbalimbali kuhusu ujio
wa makocha wapya wa mpira walio vijana
, yanadai wao wako tayari kuthubutu.
Ni vigumu kwao kufanya maamuzi ya kihafidhina hata inapobidi kufanya hivyo ili walau
kupunguza uwezekano wa kushindwa. Wanataka ‘makubwa’.

Diego Simeone, kocha wa Atletico Madrid, ni mmoja wao.
Katika mechi ya fainali ya kombe la vilabu mabingwa wa Ulaya alitaka sana
kutwaa kombe. Aliyekuwa mfungaji wake mahiri, Diego Costa, hakuwa fiti. Ila alimpanga
tu. Wakapoteza nafasi ya pekee.

Yupo pia Andre Villas-Boas (AVB) katika
kundi hilo la makocha
. Pamoja na umahiri wake vijana wenzake waliokuwa
wanaichezea timu aliyokuwa anaifundisha waliacha kumsikiliza ‘dogo’ mwenzao.
Hivyo, ujana wake sio uliompa uhalali kuwa kocha wao.

Obama ni rais mwenye mvuto wa pekee kwa baadhi ya ‘marais
vijana’ kama Maurinho alivyo kwa baadhi ya hao ‘makocha vijana’. Lakini kuvaa
na kuongea kama Obama na Maurinho hakumfanyi mtu kuwa rais au kocha mzuri. Wao
wana uzoefu wao wenyewe .

Uthubutu wa ujana una umuhimu wake. Ila unahitaji
uzoefu. Uzee ulipoanza kumuingia kiongozi wa zamani wa Ethiopia – aliyewaongoza
vijana wenzake waliovaa
kaptula na kufuga afro
kuingia madarakani kimapinduzi katika barabara za
Addis – aliliona hilo.

Baada ya uzoefu huo, hayati
Zenawi alisema hivi
: “Tofauti kubwa kati yangu – Meles wa sasa – na Meles
wa miaka 35 iliyopita ni kuwa nikiwa kijana nilikuwa na ujasiri na uthubutu wa
kuzifikia mbingu kwa kishindo. Meles wa sasa hana tena ujasiri na uthubutu
huo…Kwa nini? Kwa nini hofu ya Mungu imeingizwa kwa Meles? Nadhani kwa kiasi fulani
ni kwa sababu ya uzoefu wa kushindwa na kufanikiwa, uzoefu wa maisha wenyewe
ambao unamfanya mtu awe na hekima na wakati huo huo kupungukiwa na ujasiri na
uthubutu. Kama tutaweza kuunganisha hekima itokanayo na umri/uzee pamoja na
ujasiri na uthubutu wa ujana basi tunaweza kuondokana na uwendawazimu wa
kurudia kile kile [ambacho tumekuwa tunakirudiarudia Afrika na kutegemea
matokeo tofauti]”

Taifa Stars itaendelea tu kuwa kichwa cha mwendawazimu
alichokiongelea Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, kama tutaendelea tu kurudia
kile kile (ushirikina, ubadhirifu na uzembe ) na kutegemea matokeo tofauti
(kucheza Kombe la Dunia, Kombe la Afrika na Kombe la Mabara). Haitajalisha kama
tuna Kocha Kijana au Kocha Mzee.