Mwanzoni mwa mwezi huu nililitembelea jiji la Berlin. Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika katika jiji hili ambalo nililisikia kwa mara ya kwanza nikiwa mwanafunzi wa darasa la tano. Katika somo la Maarifa ya Jamii tulifundishwa kuhusu Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884/85 ambao uliligawa bara la Afrika miongoni mwa mataifa ya Ulaya. Kadhalika Ukuta wa Berlin una kumbukumbu katika historia ya Afrika na ulimwengu wa sasa.

Hivi karibuni pia kumekuwa na vuguvugu la kubadilisha majina ya mitaa hapa Berlin kwa kuondosha majina ambayo yanahusishwa na ukatili wa utawala wa Kijerumani na badala yake kuweka majina ya wapigania uhuru na watetezi wa haki za binadamu. Mfano, mtaa wa Wissmannstrasse ulipewa jina la Lucy Lameck – mwanamajumui wa Afrika na mtetezi wa haki za wanawake ambaye alikuwa kwenye baraza la mawaziri la Tanganyika baada ya uhuru. Hivyo, historia na urithi wa jiji hili ziliifanya safari yangu kujawa na hamasa, tafakuri na udadisi.

Nitatumia tafakuri ya safari yangu kufafanua hoja ambayo naiibua katika makala haya. Hoja hiyo ni kwamba ingawaje watu wa Afrika wana haki na wanastahili maisha bora, kuna sababu za kihistoria, kiuchumi na kiikolojia zinazotahadharisha kuwa sio sawa kuiga maendeleo na mitindo ya maisha ya Kimagharibi. Leo hii dunia inakabiliwa na majanga makubwa ya kiafya (UVIKO-19), kiuchumi na kiikolojia (mabadiliko ya tabia nchi) ambayo ni matokeo ya moja kwa moja ya kuvurugika kwa mfumo wa mahusiano kati ya jamii, uchumi na mazingira. Mfumo huu ambao ndiyo msingi wa ‘maendeleo’ ya mataifa haya ya Magharibi unaendeshwa sasa na dhana ya ukuaji  wa uchumi na faida kwa gharama yoyote ile (ikiwemo afya ya binadamu na mazingira). 

Mjadala kuhusu Mnara wa Domino
Jioni ya siku nilipotoka Berlin kurejea mjini Bayreuth, Mashariki Kusini mwa Ujerumani kulikuwa na mjadala kwenye mtandao wa Club House juu ya Mnara wa Kibiashara wa Domino unaotarajiwa kujengwa Zanzibar. Mradi huu unaotarajiwa kuipaisha Zanzibar kama kitovu cha utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati utagharimu dola za Kimarekani bilioni 1.3 sawa na takribani shilingi za Kitanzania trilioni 3. Utachukua eneo la mita za mraba 370,000 na utakuwa na nyumba za kuishi 560 na hoteli mbili za kifahari. Utakuwa mnara wa pili kwa urefu barani Afrika baada ya mnara mashuhuri wa Cairo, nchini Misri.

Wazungumzaji wengi kwenye mjadala huo walikuwa ni wachumi, na wataalamu wengine kwenye sekta za utalii na uwekezaji. Waziri mwenye dhamana pia alijiunga baada ya kupata taarifa za mjadala huo. Kwa sehemu kubwa wazungumzaji walionekana kuvutiwa sana na mpango huo. Niliposikiliza hoja zao ni kama vile wataalamu hawa walikuwa wasemaji wa serikali na wawekezaji.

Hatimaye, mchangiaji mmoja (mwandishi huru wa habari) ambaye ni Mzanzibari kutoka Pemba alichagiza mjadala huo kwa kuuliza iwapo mradi huo mkubwa utakuwa na manufaa kwa Mzanzibari wa kawaida. Alitoa mfano kwamba kwao Pemba kuna kisiwa, si mbali kutoka nyumbani kwao ambacho hutumika kwa shughuli za kitalii. Lakini si yeye wala baba yake amewahi kufika pale!

Ni ukweli kwamba sekta ya utalii ni moja ya sekta ambazo sio jumuishi na hudumisha dhana ya ukoloni. Hata kinachoitwa uchumi wa bluu ambacho ndiyo msingi wa miradi kama Domino ni “unyang’aji wa bluu” tu. Yaani ni kuwanyang’anya watu wa kawaida rasilimali zao kwa maneno yaliyobuniwa kuhalalisha uporaji.

Agosti/Septemba 2019 nilikuwa Zanzibar, eneo la Paje. Hoteli nyingi (kama sio zote) za kitalii zinaendeshwa na wageni. Ingawaje nilifikia hotelini sikupenda kula hotelini kwa sababu haikuwa rahisi kupata aina ya chakula nilichopenda. Pia gharama ya chakula cha hoteli ni kubwa sana, hivyo niliona ni afadhali kwenda kula kwenye migahawa. Hivyo, niliamua kutembea ufukweni na maeneo ya pembezoni lakini sikuona mgahawa wala wauzaji wadogo wadogo isipokuwa wanaotoa huduma za usafiri (skuta).

Niliporudi hotelini nilimuuliza mhudumu mmoja kwa nini wauzaji wadogo wadogo hawaonekani karibu? Alinijibu kuwa hawaruhusiwi, japo wakati mwingine wapo lakini wanajificha vichakani kwa sababu askari wakipita wanawakamata.  Alinieleza pia jinsi ilivyowawia vigumu kupata samaki kutokana na ushindani mkubwa kutoka kwa hoteli za kitalii. Nilimuuliza, lakini utalii si unaingiza fedha nyingi ambazo hutumika kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla? Alinijibu kwa masikitiko:

Kwani hujaona maisha yetu yalivyo? Hakuna kitu, wanakula [watawala] wenyewe! Kwanza hizo pesa zinaletwa kwenu: ndiyo hizo zinajenga madaraja na maflai-ova

Tofauti na dhana muflisi ya ‘trickle down effect’ wanayotuaminisha wachumi wetu wakimaanisha kuwa mafanikio ya kiuchumi juu yatatiririka na kuwafikia wa chini, uchumi wa kitalii unaua uchumi wa watu wa pembezoni.  Ngorongoro na maeneo mengi ya hifadhi ni mifano ambayo haki za kiuchumi na kijamii za wananchi zimekuwa zikikiukwa kwa jina la uhifadhi na utalii. Hiyo ni mifano ya unyang’anyi wa kijani.

Mnamo Mei 12, 2021, Taasisi ya Kimataifa ya Watu Asilia (Indigenous Peoples Rights International), kwa kushirikiana na taasisi nyingine 124, na watu binafsi 229 kutoka nchi 51 duniani iliwasilisha waraka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuelezea kusikitishwa kwao na tishio la kuwaondoa wafugaji asilia 73,000 kutoka katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Aprili 16, 2021, wakati akiwaapisha viongozi wateule ikulu, jijini Dar es Salaam, Rais alitoa tamko ambalo liliashiria kuwa eneo la hifadhi la Ngorongoro lipo katika hatari ya kutoweka kutokana na ongezeko la watu. Ikumbukwe kuwa haja ya kutaka kuwaondoa wafugaji asilia kutoka Ngorongoro sio hoja ngeni.

Katika kitabu chao cha Maasailand Ecology, waandishi Homewood na Rodgers (1991) wanaeleza kuwa utafiti wao ulitarajiwa kutoa ushahidi wa kuhalalisha mpango wa kuwaondoa wafugaji asilia kutoka katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Kinyume na matarajio ya mpango huo ambao ulifadhiliwa na UNESCO, matokeo ya utafiti yalionesha kuwa sio tu kwamba wafugaji asilia hawaharibu mazingira asilia, bali makatazo au mazuio wanayowekewa kwa jina la uhifadhi na utalii ndiyo yanaathiri ikolojia ya eneo hilo linalodhaniwa kuwa linalindwa kwa kuwaondoa watumiaji asilia. Watafiti hawa wanasema kuwa kukataza kulisha mifugo na utumiaji wa moto unaotumiwa na wafugaji kudhibiti ubora wa nyasi ndiyo sababu ya kuibuka kwa mimea vamizi ambayo Rais Samia amedokeza katika tamko lake.

Tafiti za hivi karibuni pia zikiwemo zilizofanywa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na Taasisi ya Umoja wa Uhifadhi wa Mazingira Asilia (IUCN) zinathibitisha kuwa ufugaji asilia ni moja ya mifumo endelevu zaidi kwa uzalishaji wa chakula na uhifadhi wa bioanuwai. Pamoja na tafiti hizi kubainisha kuwa mitindo ya maisha na mifumo ya uzalishaji ya jamii za kifugaji ni endelevu na rafiki kwa bioanuwai bado watawala na ‘wahifadhi’ wanawaona wafugaji kama waharibifu na hivyo ni tatizo linalohitaji ufumbuzi. Mtazamo huu umejengeka juu ya dhana za kikoloni (usasa/umagharibi) kuhusu uhifadhi na maendeleo kwa ujumla.

Jitihada za kujaribu kutenganisha watu na mazingira yao na mashindano ya kujenga majengo marefu ya kisasa pamoja na uchumi usiozingatia mahitaji ya msingi ya walio wengi umesababisha majanga makubwa ya kiafya, kiuchumi na kiikolojia. Kama nilivyodokeza hapo mwanzo, mfumo huu ambao ndiyo msingi wa ‘maendeleo’ ya mataifa haya ya Magharibi unaendeshwa na dhana ya ukuaji  wa uchumi na upanuzi wa faida kwa gharama yoyote ile. Kwa mfano, kwa mifumo yao ya uzalishaji na matumizi, nchi hizi kwa pamoja huchangia 92% ya gesi ya ukaa. Umoja wa Ulaya na Marekani peke yao walizalisha 69% ya gesi ya ukaa duniani kwa mwaka 2015. Ongezeko la joto, kujaa kwa bahari (kupotea kwa visiwa), mafuriko na ukame ni majibu/matokeo ya uharibifu unaofanywa na binadamu.

Matamanio ya kuwa kama Ulaya
Kwa mifano niliyoitaja hapo juu ni dhahiri kuwa kiikolojia tutahitaji sayari nyingine kama mataifa yote duniani yatafuata mfumo wa uchumi na mitindo ya maisha ya watu wa nchi za Magharibi.  Tayari mataifa haya yamevuka mipaka ya kiikolojia (planetary boundaries). Na sisi tunaelekea huko huko kama hatutabadilika.

Nilipokuwa Berlin, jambo nililoliona kwa haraka, ukiachilia mbali omba omba (watu wasio na malazi), ni kwamba ni mji wa kihistoria. Kuna sanamu nyingi, ukumbusho wa vita na majumba makubwa ya ukumbusho kama Ethnological Museum na Humboldt Forum iliyoibua sintofahamu siku za hivi karibuni kuhusu wizi wa kazi za sanaa kutoka maeneo mbali mbali duniani. Ndani yake pana kazi za sanaa kutoka mataifa kama Benin na mafuvu ya vichwa vya Wamaasai wa Tanzania na Waherero wa Namibia – kutaja japo wachache. Hii maana yake ni kwamba msingi wa maendeleo ya Ujerumani na mataifa mengine ya Magharibi umejengwa juu ya mauaji ya kimbari yaliyoambatana na utawala wa kikatili wa kikoloni na biashara haramu ya utumwa.

Hayakuishia hapo. Dhana za kikoloni bado zipo hai katika mifumo ya uchumi, fedha, elimu, sayansi na teknolojia. Hizi dhana za kikoloni hazithamini utu wala haki-jamii. Lengo ni moja tu – ukuaji wa uchumi kwa ajili ya kuzidisha faida kwa wamiliki wa mitaji.

Nikiwasikia wanasiasa wetu wakisema kwamba wanataka Tanzania iwe kama Ulaya, Zanzibar iwe kama Dubai au Japan, napata wasiwasi mkubwa. Hii ni kwa sababu historia ya Ulaya sio tu kwamba ni ya mauaji na uporaji, bali Ulaya ya sasa imefikisha dunia kwenye majanga makubwa ya kiuchumi na kiikolojia. Kutokana na ukubwa wa majanga haya, sio rahisi kuyaondoa!

Pamoja na wapiga debe wa mradi wa kibiashara wa Domino  kudai kwamba mradi huo utakuwa na manufaa kwa ustawi wa watu na mazingira, tafiti zinaonesha kuwa ujenzi wa visiwa bandia kama vya Dubai huvuruga mikondo ya asili, makazi ya viumbehai wa baharini, na nyasi za baharini ambazo ni muhimu kwa viumbe waishio baharini na wale wanaowategemea kwa chakula. Pia, tafiti hizi zinaonesha kuwa ujenzi wa visiwa (bandia) ndiyo sababu kuu ya kupotea kwa miamba ya matumbawe (coral reefs) kwa kasi zaidi katika historia ya binadamu.

Upotevu wa miamba ya matumbawe huacha fukwe nyingi katika hatari ya kukumbwa na mafuriko kirahisi. Vile vile huiondolea bahari uwezo wa kunyonya hewa ya ukaa. Gharama za ubandia ni kubwa kwa afya ya binadamu na mazingira.

Mwanazuoni Frantz Fanon aliitahadharisha kwa ukali Afrika isiige Ulaya na badala yake ibuni ulimwengu mpya na binadamu mpya ambaye hamasa yake haitokani na mifumo na mitindo ya maisha ya jamii za Ulaya. Fanon yuko sahihi leo kuliko alivyonena miaka 60 iliyopita. Kwa sasa mfumo wa uchumi na mitindo ya maisha ya jamii za Magharibi inapata shinikizo kubwa kutoka kwa jamii za nchi hizo. Kuna makubaliano  miongoni mwa wanazuoni wa mataifa haya kuwa uchumi wao unahitaji mabadiliko makubwa ili uweze kukidhi matakwa ya Maendeleo Endelevu (rejea kitabu hichi).

Wanazuoni wa Kiafrika vilevile wamekuwa wakihoji ukuaji wa uchumi ambao hauzingatii maswali ya kimaadili kuhusu ajira endelevu, ukosefu wa usawa na majanga ya kiikolojia bali hutukuza uzidishaji wa faida kwa wachache wenye mitaji (wawekezaji) badala ya wengi ambao wanaonekana kero mjini (wamachinga na mama lishe) au wale wanaodaiwa kuwa eti ni wavamizi-waharibifu (wafugaji).  Chapisho la Franklin Obeng-Odoom Africa:_On_the_Rise_but_to_Where? (Afrika inakua lakini kwenda wapi?) na Moses Khisa Whose Africa is Rising? (Afrika ya nani ndiyo inakua?) miongoni mwa mengine mengi huchagiza mjadala huu. Ukuaji ambao unawezeshwa na madeni (debt-financed growth) na hauwanufaishi walio wengi umeanza kupata pingamizi kutoka kwa wananchi ambao ndiyo wabeba gharama.

Mchangiaji kwenye mjadala wa Domino kutoka Pemba, mhudumu wa hotelini Paje na Lerionka wa Ngorongoro wanayo picha tofauti kabisa ya kinachoitwa maendeleo na uwekezaji – wao wanaona uporaji na ukiukwaji wa haki za kibinadamu. Kwao mipango mikubwa kama ya Mnara wa Domino (Babeli?) au Royal Tour ni tishio! Ni tishio kwa sababu wakati Lerionka na familia yake wanatishiwa kuondolewa Ngorongoro kwa kisingizio cha ongezeko la watu, mkakati wa Royal Tour ni kuvutia utalii kwa lengo la kufikisha watalii milioni tano kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

Wafugaji kuwepo Ngorongoro ni tatizo kimazingira lakini magari 400 ya watalii kuingia hifadhini kwa siku sio tatizo! Vilevile, mbali na migogoro ya ardhi iliyopo, Royal Tour inalenga kutangazia dunia kuwa Tanzania ina ardhi ya kutosha,  hivyo wawekezaji waje kuwekeza. Dhana za kimaendeleo za kikoloni huwadunisha na kuwapuuza wazalishaji wadogo (wakulima, wafugaji, wavuvi, wakusanya-matunda) pamoja na mila, mitazamo na maarifa yao juu ya maisha, mazingira na uzalishaji. Kwa karne nyingi, lugha za kisayansi na usasa zimetumika kudunisha makundi fulani ya watu ili kuhalalisha unyonyaji wa nguvu zao na kuwapora nyenzo zao za uzalishaji mali kama njia ya kuustawisha mfumo unaojali faida kwa wachache.

Uchumi Unaojali
Historia ya mauaji na uporaji pamoja na majanga ya kiafya, kiuchumi na kiikolojia yaliyosababishwa na mfumo unaotukuza ukuaji wa uchumi na uzidishaji wa faida kwa wachache ni uthibitisho kuwa Ulaya na mataifa mengine ya Magharibi sio mfano wa kuigwa kwa Maendeleo Endelevu. Swali la msingi la kujiuliza ni namna gani tunaweza kuboresha maisha ya binadamu wote pasipo kuharibu ikolojia? Jibu lake ni mfumo mpya wa uchumi unaojali kila mtu na ikolojia.

Maradhi ya UVIKO-19 yametukumbusha kuwa hakuna usalama kwa yeyote ikiwa mmoja wetu sio salama. Ndiyo maana baadhi ya nchi kama Ireland zilitaifisha huduma za afya  (japo kwa muda) kwa sababu hakuna cha binafsi wakati wa hatari – usalama wa wote ni lazima. Mantiki hii ikitumika katika mipango na maamuzi yetu ya kiuchumi tutaweza kujenga jamii mpya au ya tofauti kama alivyotuasa Frantz Fanon. Kwenye chapisho lake “The Purpose is Man” Mwalimu J.K. Nyerere (1968:92-93) anaeleza kuwa:

Azimio la Arusha [pia] ni  mazingatio ya ubora fulani wa maisha. Umejengwa juu ya dhana ya usawa wa binadamu, kwa imani kwamba ni makosa kwa mtu mmoja kumtawala au kumnyonya mwingine, na kwa kufahamu kwamba kila mtu anatarajia kuishi katika jamii kama mtu huru anayeweza kuishi maisha bora katika hali ya amani na majirani zake. Kwa maneno mengine, kusudi la Azimio ni mwanadamu. Kwa hiyo, asili ya Azimio la Arusha, ni kukataa dhana ya ukuu wa kitaifa (national grandeur) ambayo haiendani na ustawi wa raia wake, na kukataa pia utajiri wa mali ambao lengo lake ni utajiri wa mali tu (material wealth for its own sake)! Ni kujitolea kwa imani kwamba kuna mambo muhimu zaidi maishani kuliko kujilimbikizia utajiri, na kwamba ikiwa kutafuta mali kunagongana na vitu kama utu wa binadamu na usawa wa kijamii, basi hivyo vya mwisho vitapewa kipaumbele…uzalishaji wa mali ni jambo zuri na kitu ambacho tutalazimika kuongeza. Lakini utaacha kuwa [jambo] zuri pale utajiri unapoacha kumtumikia mwanadamu na kuanza kutumikiwa na mwanadamu.

Azimio la Arusha lilikuwa azimio la uasi. Kuuasi mfumo wa kidhalimu ambao unatweza utu wa binadamu na kuyaharibu mazingira kwa ajili ya ukusanyaji wa mali usio na ukomo. Mwalimu alikufa akiamini ipo siku moja Tanzania itarejea kwenye misingi ya Azimio la Arusha.

Leo hii jamii za Ulaya zinapambana kubadili mifumo yao ya uzalishaji na matumizi ili kuepusha dunia na uharibifu ambao umeanza kujidhihirisha kupitia majanga mbalimbali kama mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo ni tishio kubwa kwa ustawi wa maisha kwa sasa. Mwezi Julai, 2011, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio la Wabhutani lililotoa wito kwa serikali za mataifa mbalimbali kutoa kipaumbele kwa furaha na ustawi wa wananchi wao katika kupima maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Tangu mwaka 2013 Ripoti ya Hali ya Furaha Duniani (World Happiness Report) imeonesha kuwa wananchi wenye furaha zaidi hawapo kwenye nchi zenye uchumi mkubwa kama Marekani na Uchina bali katika nchi zenye sera zinazojali ustawi wa watu.

Nchi za Nordiki (Finland, Denmark, Norway, Sweden, and Iceland) zimekuwa zikishika nafasi ya juu zaidi. Sababu za furaha na wananchi wa mataifa haya kuridhika na maisha ziko wazi. Ni pamoja na huduma za kuaminika za ustawi wa jamii, ubora wa taasisi, kiwango kidogo cha ubadhirifu serikalini na katika taasisi za umma, na uhuru wa wananchi kujiamulia mambo yao bila bugudha.

Pingamizi dhidi ya uchumi wa madeni na sera za uliberali-mamboleo ziliifanya nchi ya Bhuttan kuchukulia kwa makini dhana ya Furaha ya Kitaifa (Gross National Happiness). Nchi hiyo imeamua kuipa kipaumbele dhana ya Furaha ya Kitaifa kwa kutunga na kutekeleza sera mahsusi ambazo hupendelea ustawi, utoshelevu na uendelevu kwa ujumla badala ya ukuaji wa Pato la Taifa (GDP). Tofauti na nadharia za kimaendeleo ambazo hutanguliza ukuaji wa uchumi na faida, nadharia hii huheshimu uadilifu wa kiikolojia na kiutamaduni.

Uzoefu unaonyesha kwamba kuongezeka kwa Pato la Taifa hakumaanishi maisha bora kwa wananchi wa taifa husika. Wala sio kweli kwamba ukuaji wa uchumi moja kwa moja huleta ustawi wa kijamii. Mfalme Jigme Singye Wangchuck wa Bhutan ambaye ndiye aliyebuni dhana ya Furaha ya Kitaifa aliona kuwa:

Kuelekeza juhudi zote za binadamu katika ulimbikizaji wa mali ni utupu  ikiwa hakutakuwa na nafasi tena ya uhuru na furaha [kwa wananchi]

Uchumi unaojali ustawi wa watu badala ya faida, na kuongezeka kwa Furaha ya Kitaifa badala ya Pato la Taifa tu ungetazama ni nyumba ngapi za ubora wa wastani zingeweza kujengwa kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar badala ya nyumba ghali 560 za Domino ambazo kwa hakika ni Wazanzibari wachache tu wataweza kupanga! Uchumi unaojali huzingatia mahitaji ya msingi ya watu wa eneo husika: chakula chao, mavazi na malazi yao. Mwisho uchumi unaojali huheshimu mazingira kwa kutambua na kuthamini mchango, maarifa na busara za watumiaji wa rasilimali za eneo husika.

Bila shaka uchumi unaotoa kipaumbele kwa ustawi wa watu na uendelevu utakuwa na sera na mipango tofauti na uchumi unaotoa kipaumbele kwa ukuaji tu wa Pato la Taifa (GDP) kwa matarajio kwamba ukuaji huo utatitirika tu na kusababisha ustawi wa watu!

Hakimiliki

Udadisi imetumia picha huria kutoka https://pixabay.com