MMETUPORA KILA KILICHO CHETU, TUACHIENI NYERERE WETU
Na Mwl. Sabatho Nyamsenda
Wanyonge
walia, waporaji washerehekea
Siku ya leo nchi yetu inaadhimisha miaka 14 tangu
kuondokewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Hivyo, leo ni siku ya
furaha na huzuni; ni siku ya harusi na matanga. Kwa waporaji, wanyonyaji,
wabaguzi wa rangi, wadini na wakabila, leo ni siku ya kunywa mvinyo na
kusherehekea. Ule mwiba uliowachoma siku zote na kuwakosesha raha hatimaye
uliondoka siku kama ya leo, nao wakapata nafasi ya kutamba.
Kwa wanyonge –
wakulima wadogo, wafugaji wadogo, warina asali, waokota makopo, wafagia
barabara, wabeba zege, machinga, mama ntiliye, wafanyakazi wa ngazi za chini, na wote wanaoishi katika dhiki na kukosa
huduma bora za afya, maji, elimu na malazi – leo ni siku ya huzuni. Lile jabali
lililoongoza mapambano yao hatimaye lilistaafu rasmi kazi ya kupambana siku
kama ya leo. Nyerere, msemaji wa wanyonge, akaacha kusema. Kambarage, mshairi
wa makabwela, akaacha rasmi utunzi wa mashairi. Julius, mfasiri wa vitabu,
akaweka kalamu chini huku akiwa amekamilisha kutafsiri kwa Kiswahili kitabu cha
mwanafalsafa wa Kiyunani, Plato, kiitwacho ‘‘The Republic’’. Mwalimu wa
wanyonge akakoma kufundisha. Akatulia tuli. Akalala usingizi wa kudumu.
Tufurahie maisha yake kuliko kuomboleza kifo chake
Je, ni sahihi kwa
wanyonge kulia? Ni haki kwa wanyonge kuomboleza? Kulia na kuomboleza ni haki ya
kila ampotezae mpendwa wake. Lakini kwa kuwa Nyerere alikuwa binadamu wa
kawaida na sio malaika aliyeshushwa toka angani hatukutegemea kwamba ataishi
milele. Binadamu huzaliwa, hukua, huzeeka, huugua, hufariki. Ndicho
kilichotokea kwa Mwalimu. Pengine siku ya leo yapaswa kuwa siku ya kufurahia
maisha ya Mwalimu kuliko kuhuzunikia
kifo chake. Kwa maana hiyo, siku kama ya leo twapaswa kuzitafakari kwa kina
fikra zake na jinsi tutakavyozitumia kuendeleza mapambano ya wanyonge.
Nyerere hajafa, sisi ndio Nyerere
Aina hii ya kumwenzi
kiongozi wa mapambano kwa kuendeleza yale aliyoyapigania niliiona kwa
Wavenezuela walipoondokewa na shujaa wao wa mapinduzi ya kidemokrasia, rais wa
wanyonge, Hugo Chavez, alipofariki mwezi machi mwaka huu. Nilipowaona katika
televisheni mamilioni ya wanyonge wa Venezuela wakitiririkwa na machozi,
nilidhani huo ndio mwisho wa mapinduzi ya kijamaa ya kibolivari (The Bolivarian Socialist Revolution)
waliyoyaasisi wanyonge wa nchi hiyo wakiongozwa Chavez.
Kilichonitisha zaidi
ni jinsi viongozi wa mataifa ya mabeberu, na hasa Barack Obama wa Marekani,
walivyotoa kauli za kusherehekea kifo cha gwiji hilo la mapambano. Na mabeberu
walikuwa na haki kushangilia kifo hicho kwani ni Chavez aliyehakikisha kuwa
utajiri wa mafuta ya nchi hiyo unaenda kuwafaidisha wanyonge kwa kuwapatia
hudumu bora za kijamii zisizo na malipo. Mawakala wa ubeberu nchini Venezuela wakisaidiwa
na majasusi wa Marekani walijaribu kumpindua Chavez lakini mamilioni ya
wanyonge waliandamana hadi aliporejeshwa madarakani.
Lakini kauli za wanyonge
wa Venezuela zilinipa matumaini: pamoja na kutiririkwa machozi, walipohojiwa na
waandishi wa nchi za Magharibi juu ya kifo cha kiongozi wao, walijibu: ‘‘Chavez
hajafa. Sisi ndio Chavez’’. Kwa kauli hiyo wanyonge walikula yamini kuendeleza
mapinduzi ya kijamaa na kuhakikisha kuwa utajiri wa nchi yao unaendelea kuwafaidisha
wanyonge badala ya kikundi kidogo cha mawakala wa mabeberu na mabwana wao.
Tena wanyonge wa
Venezuela wameonyesha mshikamano wa kitabaka na wanyonge wa nchi nyingine kama
Cuba, Ecuador, Nicaragua na Bolivia ambazo zote zinaongozwa na serikali za
kijamaa. Mathalani, Cuba yenye madaktari wengi waliobobea huwapeleka Venezuela
ili kutoa huduma za afya kwa wanyonge mijini na vijijini, wakati Venezuela
ikiipatia Cuba mafuta kwa bei rahisi na kuisaidia kiuchumi ili iondokane na
hali ngumu inayosababishwa na vikwazo vya Marekani.
Kambarage mpinga unyanyasaji
Historia ya Kambarage
inaonyesha kuwa tangu akiwa mdogo alichukia kila aina ya uonevu, ubaguzi,
unyanyasaji na ukandamizaji. Akiwa mtoto mdogo, Kambarage alikuwa akimsindikiza
mama yake shambani ; mama akiwa analima, Kambarage alikuwa akimbembeleza
mdogo wake. Huruma ilikiwa ikimwingia Kambarage kumwona mama yake akifanya kazi
za suluba siku nzima bila kupumzika. Hivyo akabuni mbinu ya kumpumzisha mama
yake. Akawa anamfinya mdogo wake, na kitoto kile kichanga kikawa kikitoa kilio
kikali, kilio kilichomfanya mama adhani kuwa kichanga yule ana njaa. Hivyo, mama
akaacha kulima na kuja kumnyonyesha mwanawe. Kamnyonyesha mtoto, lakini pia
kapumzika. Kambarage alitabasamu na kujiona mshindi, hata kama ushindi wenyewe
ulikuwa wa muda mfupi tu.
Miaka mingi sana
baadaye kitoto hiki, ki-Kambarage, sasa akiwa kijana wa umri wa miaka 22 na
mwanafunzi wa Makerere aliandika insha ya kiswahili iliyoitwa ‘‘Uhuru wa
Wanawake’’. Ndani ya insha hiyo kijana Julius aliichambua na kuilaani mifumo ya
jamii zetu za Kiafrika iliyokuwa ikiwakandamiza na kuwanyanyasa wanawake kana
kwamba wao si binadamu kamili. Na ni mfumo wa kikoloni ulichochea moto na
kuhalalisha mfumo dume.
Insha hiyo, ambayo ambayo
ilishinda tuzo ya Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki kwa wakati huo, na sasa
imechapwa katika kitabu, inaishia na kisa cha kifaranga cha tai
kilichochanganywa na kuku, kikalishwa chakula cha kuku, hata chenyewe kudhani
ni kuku. Lakini tai huyo alipopelekwa kilimani na mtaalamu wa wanyama, na
kuambiwa: tai, wewe sio kuku, kwako ni angani, hivyo ruka uende angani. Tai
akaruka na kupotelea mawinguni. Kwa kutumia mfano huo, Nyerere akawataka
wanawake kutokubali madhila ya mfumo kandamizi unaowaaminisha kuwa wao ni kuku,
warukia chini, ilhali wao ni tai, warukia juu. Hivyo walipaswa kuruka na kupaa.
Hata hivyo mtazamo wa
Mwalimu haukuwa finyu kwa kudhani kuwa ni wanawake pekee ndio waliokandamizwa
na kunyimwa fursa. Mfumo wa kibepari, ambao kwa wakati huo ulichukua sura ya
ukoloni, uliwakandamiza wanyonge wote, wake kwa waume, katika Afrika na mabara
mengine. Hivyo, wanyonge wote walipaswa kupambana na kuushinda ukoloni. Ndio
maana Nyerere alikuwa mbele kuongoza mapambano dhidi ya ukoloni, ubaguzi wa
rangi na ukandamizaji, katika Afrika na dunia nzima kwa ujumla.
Julius
asiyenunulika
Shuleni Tabora, Julius
alipewa ukiranja. Hii ilitokea baada ya yeye kuamua kuacha shule kutokana na
kunyamazishwa na mwalimu mkuu wakati wa mdahalo. Kambarage alikuwa ametoa hoja
za kupinga uonevu na unyonyaji wa serikali ya kikoloni hali iliyomwudhi mwalimu
mkuu wa kizungu na kumwamuru akae chini. Kwa nini anyamazishwe? Mwanafunzi huyo
aliamua kufunga virago vyake na kurudi kwao lakini utawala wa shule kwa
kushirikiana na serikali ya kikoloni walimkatiza na kumrudisha shuleni kisha
wakampatia uongozi.
Kama walimu wa
kikoloni walidhani kwa kumpa ukiranja walikuwa wamemnunua Julius basi walikuwa
wakiota ndoto mchana kweupe. Ukiranja wa shule ulimpa Kambarage haki ya kupata
nusu lita ya maziwa kila siku, ilhali wasio viranja walipata robo lita. Ni
Kambarage, si mwingine, aliyeongoza mgomo wa wanafunzi kupinga ubaguzi huo na
kudai wanafunzi wote wapate mgao sawa wa maziwa. Mgao huwa wa kibaguzi ukakoma.
Tayari Nyerere alishaanza kupigania usawa.
Miongo kadhaa baadae
serikali ya kikoloni ilimpatia ujumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika
(ubunge kwa wakati huo). Walidhani wamemnunua na kumnyamazisha. Lakini alipoona
hoja zake hazipewi nafasi Nyerere alijiuzulu ubunge huo na kuyarejea maisha
yake ya dhiki aliyokuwa akiishi baada ya kuacha kazi ya ualimu. Alikataa
kuwasaliti wanyonge.
Kipo kisa katika
kitabu cha Mohamed Said kiitwacho Uamuzi wa Busara wa Tabora kinachoonyesha maisha aliyoishi Nyerere baada ya kuacha
kazi ya ualimu iliyokuwa na mshahara mnono kwa wakati huo ili kuongoza
mapambano ya uhuru. Familia yake ikakosa hata mlo wa kueleweka. Siku moja,
akiwa hana hata senti moja mfukoni, Mwalimu aliamua kutembea kwa mguu toka
nyumbani kwake Magomeni hadi Kariakoo, akitegemea huenda atabahatisha kupata
chakula. Njiani akakutana na mzee Msume Kiate, mwana TANU ambaye alikuwa
akifanya biashara ya kuuza samaki. Baada ya kusikiliza shida ya Mwalimu, mzee
Kiate akampatia shilingi mia mbili akanunue mahitaji yake. Na baada ya hapo mzee
Kiate na wana TANU wenzake walijitolea kuihudumia familia ya Mwalimu kwa
chakula na wakaendelea kufanya hivyo hata baada ya uhuru kupatikana.
Tunapomkumbuka Nyerere tunapaswa pia kuwakumbuka mashujaa wengine, kama Mshume
Kiate, ambao vitabu vingi vya historia havitaji majina yao.
Mwalimu Nyerere, kiongozi wa makabwela
Kitabaka, Mwalimu
hakuwa katika kundi la makabwela. Kwa kuzaliwa katika familia ya kichifu tayari
alikuwa na fursa ambazo watoto wengine hawakuwa nazo. Moja ya fursa hizo
ilikuwa elimu. Lakini elimu ikamfungua na kuiona dunia. Kadiri ilivyomfungua
ndivyo ilivyomtenganisha na watu wake. Toka Butiama akaenda Musoma, toka Musoma
akapita Mwanza, Shinyanga hadi Tabora. Akavuka
mipaka ya kijiji na mikoa. Akavuka mipaka ya nchi, akaenda Uganda. Akavuka
mipaka ya bara, akaenda Uingereza. Elimu yake haikumvusha mipaka ya ramani tu
bali mipaka ya kitabaka. Kadiri alivyoongeza vidato na shahada ndivyo alivyolihama
tabaka la “walalahoi”.
Lakini japokuwa kitabaka alikuwa katika “walalahai”
kabla ya uhuru, na kuhamia katika “walalaheri” baada ya uhuru, Mwalimu
mwenyewe aliamua kwa makusudi kabisa kuliasi tabaka lake. Hivyo usomi wake
haukuwa na bei (exchange value) bali
ulikuwa na thamani (use value). Katika
fikra za Mwalimu, msomi anayejitapa kuwa yeye hawezi kutumika kwa wanyonge
mpaka alipwe kiasi fulani cha fedha huyo si binadamu kamili bali ni mtumwa.
Binadamu pekee mwenye bei na anayeuzika sokoni ni mtumwa.
Ndio maana hata baada ya kutoka Uingereza, akiwa
Mtanganyika wa kwanza kupata shahada ya umahiri (master’s degree), Mwalimu hakuhangaika kutafuta fursa za kujitajirisha
na kuishi maisha ya anasa. Kwa kuwa maslahi hayo ya kitabaka alishayaaga
haikuwa vigumu kwake kuachia nyadhifa zenye malipo manono ili akawapiganie
wanyonge.
Hata baada ya kukaa Ikulu kwa zaidi ya miaka 20,
alifanikiwa kujenga kajumba kadogo na ka kawaida kabisa kijijini Butiama, na
nyumba yake ya Msasani aliijenga kwa mkopo ambao hata hivyo alishindwa kuumalizia, na kuiomba serikali
imalizie mkopo na kuchukua nyumba hiyo. Serikali ya Mwinyi ikafanya hivyo
lakini ikampatia Mwalimu nyumba hiyo. Mwaka 1966 Mwalimu alikata mshahara wake
kwa asilimia 20. Wakati huo alikuwa akipokea shilingi 5,000/=, hivyo akabakia
na shilingi 4,000/= na hakuwahi kujiongezea mshahara mpaka anaondoka
madarakani. Hivyo, wapo watumishi wengi kabisa wa serikali, wakiwemo maprofesa,
waliopokea mshahara mkubwa kumzidi.
Azimio
liliwajali wanyonge
Lakini kutopenda mali inaweza kuwa hulka ya mtu
yeyote kabisa. Mkristo au mwislamu mzuri, anayeamini katika pepo ya baadae,
hawezi kujikita katika anasa za kidunia. Ila Nyerere alifanya hivyo si kwa
sababu ya ukristo wake, ila kwa sababu ya itikadi iliyomwongoza, itikadi ya
kijamaa. Ndiyo maana, baada ya kuwaona viongozi wenzake wanatumia nyadhifa zao
kujitajirisha, aliasisi Azimio la Arusha, ambalo pamoja na mambo mengine
liliwazuia viongozi kumiliki nyumba za kupangisha, kupokea mishahara miwili au
zaidi na kumiliki hisa au kuwa wakurugenzi katika kampuni za kibepari.
Kupitia Azimio la Arusha, njia kuu za
uzalishaji-mali na rasilimali za taifa, kama viwanda, mabenki, misitu, madini, ardhi,
njia na vyombo vya usafiri wa anga, reli na maji, viliwekwa mikononi mwa umma.
Umma wa wanyonge ulichagua serikali kwa njia ya kidemokrasia, serikali ambayo
ilipewa jukumu la kusimamia rasilimali hizo kwa niaba ya wanyonge. Faida
inayozalishwa ilitakiwa kwenda kuwahudumia wanyonge, na sio kikundi cha
watawala. Azimio lilisisitiza juu ya kuwajali wakulima vijijini, na kuonya juu
ya misaada kutoka ughaibuni.
Azimio
likahujumiwa na kupinduliwa
Kama inavyofahamika, wanyonge, wake kwa waume,
vijana kwa wazee, waliandamana nchi nzima kuunga mkono Azimio la Arusha.
Lilikuwa ramani yao kuelekea nchi ya usawa na matumaini. Lakini hata hivyo,
utekelezaji wa Azimio uliwekwa mikononi mwa watu walewale walioanza
kujitajirisha. Japo katika miaka ya 1970 sera za kijamaa zilifanya vema na serikali
ikaanza kuonyesha mafanikio katika kutoa hudumu bora kwa jamii bila malipo, hali
ilibadilika katika kipindi cha miaka ya 1980.
Nchi za kibeberu, Marekani na Uingereza, zilishikwa
na waumini wa sera za uliberali mambo-leo na hivyo kuzilazimisha nchi maskini
kufuata sera hizo kwa kubinafsisha kila kilichotaifishwa, kufuta ruzuku katika
kilimo na vyakula, na kuacha mara moja kutoa huduma zisizo na malipo. Ndani ya
nchi, tena Mwalimu akiwa bado madarakani, sera hizi zilipata mashabiki wengi.
Wachache walijionyesha waziwazi. Wengi walijificha na kuendelea kuhujumu chini
chini.
Nchi ikiwa imetoka vitani, bidhaa za msingi zikawa
hazipatikani. Zilikuwa zimehodhiwa na kikundi cha watu wachache, baadhi wakiwa
katika dola na baadhi nje ya dola. Hivyo, baada ya vita vya Uganda, Mwalimu
alikuwa na vita viwili vya kupigana: vita dhidi ya wahujumu uchumi/ujamaa ndani
ya nchi, na vita dhidi ya mabeberu nje ya nchi. Makundi hayo yalikuwa
yakishirikiana kwa ukaribu sana, na hata yakafanikiwa kuupindua Ujamaa baada ya
Mwalimu kung’atuka.
Sera za
kiporaji
Uzoefu wa zaidi ya miaka 25 ya utekelezaji wa sera
za uliberali mambo-leo umetuonyesha kuwa mfumo huu ni katili zaidi pengine
kuliko hata biashara ya utumwa na ukoloni. Rasilimali za wanyonge zinaporwa, na
wanyonge wanapojaribu kupinga hutumiwa majeshi na serikali zao au za mabeberu. Tumeyaona
hayo nchini mwetu. Pia tumeyaona barani kwetu na duniani kote mifano ikiwa ni uvamizi
wa Libya na Iraq uliopelekea kuchinjwa kwa viongozi wa nchi hizo, na mamilioni
ya wanyonge kuuawa.
Akihutubia mjini Mbeya katika sherehe za Mei Mosi mwaka 1995, Mwalimu aliziita sera za ubinafsishaji na uwekezaji kuwa ni za
kinyang’anyi. Akasema kuwa zitazalisha mabilionea, lakini watakuwa wachache.
Lakini pia zitazalisha maskini, na hao watakuwa wengi sana. Hayo ndiyo
yatokeayo nchini mwetu na duniani kote.
Jengeni
sanamu zake, sisi tutazienzi fikra zake
Mwaka mmoja kabla ya kufariki Mwalimu alikuwa
ametabiri kuwa ipo siku Tanzania itarejea katika misingi ya Azimio la Arusha.
Katika Kongamano la kuadhimisha miaka 44 ya Azimio la Arusha, Profesa Issa
Shivji naye pia alisisitiza juu ya uwepo wa dalili zinazoonyesha kuwa Watanzania
walio wengi wameanza kupigania kurudi katika misingi ya Azimio la Arusha lakini
akaonya kuwa dalili hizo zinaweza kuzimwa na kakundi ka watu wachache
kanakofaidika na mfumo uliopo.
Nafikiri kuwa miongoni mwa mbinu za kuzima dalili
hizo ni kuhodhi jina la Mwalimu huku wakijidai wanamuenzi. Eti wanamuenzi kwa kuongeza
idadi ya sanamu zake, na taasisi na viwanja vyenye jina lake ilhali Mwalimu
mwenyewe alishakataa hayo tangu akiwa hai. Wakijidai kugusia fikra zake basi
wanamhubiri kama mpenda amani na umoja. Lakini ni Mwalimu mwenyewe aliyesema
kuwa mahali pasipo na haki (justice)
wala usawa (equity) hapawezi kuwa na
amani. Pia hauwezi kuwa na umoja kati ya wanyonyaji/waporaji wachache na
mafukara wengi.
Ili nisionekane nabandika maneno katika mdomo wa
Mwalimu, nitanukuu sehemu ya hotuba yake aliyoitoa mwezi mei mwaka 1989 wakati
akifungua semina ya wazalishaji wakubwa iliyoandaliwa na Chama cha Mapinduzi:
“Si kwamba Azimio la Arusha limeondoa
umaskini hata kidogo, wala halikutoa ahadi hiyo. Azimio la Arusha limetoa ahadi
ya matumaini. Ya haki, ahadi ya matumaini kwa wengi, ndio watu wengi wa
Tanzania wanaendelea na kuwa na matumaini hayo. Madhali yapo matumaini hayo,
mtaendelea kuwa na amani… Kama wengi hawana matumaini, tunajenga ‘volcano’.
Siku moja italipuka na lazima ilipuke. Isipokuwa watu hao wajinga. Wengi wa
nchi hiyo wajinga, wanakubali kutawaliwa hivi hivi. Kuonewa hivi hivi na wingi
wanao, wajinga hao. Kwa hiyo, Watanzania hawa watakuwa wajinga, wapumbavu, kama
wataendelea kukubali kuonewa na watu wachache katika nchi yao. Kwa nini?’’
Waporaji wa rasilimali za nchi, wavunaji wa jasho
la wanyonge, vibaraka wa mabeberu (wasemao ‘tunapendwa huko nje’) hawana haki
ya kutumia jina la Mwalimu. Wametupora kila kilicho chetu (tangu viwanda,
ardhi, madini hadi nyumba), wamewanyang’anya wanyonge haki ya kupata huduma
bora za afya, elimu, malazi na chakula. Hawa hawana haki ya kutaja jina la
Mwalimu. Njia ambayo wanyonge wanaweza kumuenzi Mwalimu ni kwa kuzichambua kwa
kina fira zake, na hasa Azimio la Arusha, na kuzitumia kama silaha ya
mapambano!
Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana
kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com





