JINSI YA KUHADAA KWA TAKWIMU: UTALII NA UKUAJI UCHUMI TANZANIA
Profesa.
Chachage Seithy L. Chachage
22 Oktoba 2005
Napenda kukiri wazi kuwa wengi wetu si wataalamu wa
uchumi, na wala hatuna utalaamu wala ujuzi walionao wa kuyaanisha masuala hayo.
Lakini kwa kuwa kila kuchapo sisi sote ni waathirika wa takwimu zitolewazo na
wachumi, na hasa wanasiasa wetu katika kipindi hiki wakati kura zikitafutwa kwa
udi na uvumba, yabidi kuyasaili baadhi ya mambo ambayo wanatuambia.
Swali
ambalo wengi tumekuwa tunajiuliza ni: hivi tunapoambiwa kuwa uchumi umekuwa
ukikua kwa kutumia vigezo vya pato la taifa, mbona ufukara umekuwa ukiongezeka
siku hadi siku miongoni mwa makabwela ambao ni asilimia 90 ya watu wa nchi hii?
Huo uchumi ambao umekuwa ukiongezeka umekuwa ukienda wapi au ukimfaidisha nani?
Je, hizi ahadi za kujenga uchumi kakamavu ambazo wanaopigania kinyang’anyiro cha
kututawala katika miaka mitano ijayo zinazingatia kiasi gani matatizo ambayo
yamekuwa yakiwapata wanyonge?
Si masuala mepesi, lakini inabidi tuyatafakari
kwa faida yetu.
Waziri
Mkuu wa Uingereza wa mwishoni mwa karne ya 19, Bwana Disraeli aliwahi kutamka
kuwa kuna aina tatu ya uongo: uongo, uongo laanifu na takwimu. Kama
tutakubaliana na mwanasiasa huyu, basi takwimu ambazo zimekuwa zikitangazwa
kuhusu baadhi ya sekta za uchumi ni kidhihirisho cha maneno haya. Mfano wa
sekta mojawapo ni ile ya utalii.
Kwa miaka kadhaa sasa Watanzania na watu wa
dunia nzima wamekuwa wakiambiwa na vyombo vya habari kuwa kutokana na kulegeza masharti ya uchumi
na kuingia katika mfumo wa soko huria (utandawazi), kumekuwa na ongezeko kubwa
la vitega uchumi katika sekta ya utalii kutokana na kuuza mashirika na
makampuni ya kitalii yaliyokuwepo, kuyakodisha na uwekezaji wa mitaji kutoka
nje ya nchi.
Hakuna
ubishi kuhusu kuongezeka kwa vitega uchumi, kama inavyojidhihirisha wazi
kutokana na ongezeko la mahoteli na shughuli zingine ambazo zinahusiana na mambo ya kitalii. Vyombo vya habari
vimekuwa vikiyaainisha yale ambayo yamekuwa yakitamkwa na wanasiasa, watawala
serikalini, watunga sera na hata baadhi ya wasomi ambao wamefanya utafiti
katika nyanja hiyo. Hawa wote wamekuwa wakionyesha jinsi sekta ya utalii
inavyochangia katika pato la taifa, ongezeko la ajira, “kupunguza umasikini” na
maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Kwa mfano ilidaiwa kwamba utalii uliingiza
kiasi cha dola milioni 725 kutokana na nchi kupata watalii 525,122 mwaka 2001,
na pato hili likaongezeka hadi dola milioni 731 kutokana na kupata watalii
576,000 mwaka 2003. Imedaiwa kwamba sekta ya utalii imekuwa ikiiingizia nchi
fedha nyingi za kigeni—asilimia 25, na kuchangia katika pato la taifa kiasi cha
asilimia 16. Kutokana na mchango huo, utalii umefikia kiasi cha kuwa injini ya
ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kwa wale ambao wamewahi kuziangalia takwimu za nchi
ya jirani—Kenya, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikivuma kwa miaka mingi na
kuongoza katika shughuli za utalii
Afrika Mashariki nzima, watagundua mara moja kwamba takwimu hizi zina
mushkeli! Kenya ilitembelewa na watalii 750,000 mwaka 2002. Hawa ni zaidi ya
wale waliotembelea Tanzania. Lakini mapato ya fedha za kigeni kutokana na idadi
hiyo yalikuwa dola milioni 285!
Iweje kwamba Kenya iliyopata watalii
wengi zaidi ipate theluthi moja ya fedha za kigeni ya zile ambazo Tanzania ambayo
ilikuwa na watalii wachache? Miujiza gani hii ya kiuchumi na ni baraka gani
ambazo Tanzania inazo mabazo Kenya haina?
Kila aliyemdadisi inabidi ajiulize
maswali zaidi kuhusu mchango wa sekta hii: inabidi aziangalie upya takwimu za
sekta hii na kulinganisha na mchango wa sekta zingine za uchumi hapa nchini.
Kwa kufanya hivyo, itagundulika wazi kwamba hizi takwimu ni sehemu ya siasa za
kimataifa za ulipaji na upunguziwaji wa kulipa madeni. Inabidi nchi zetu
ziuonyeshe ulimwengu kwamba uchumi unakua kutokana na kufuata sera za magharibi
na kukaribisha wawekezaji, ili zisamehewe madeni. Kuonyesha kuwa kuna matatizo
ni kufru katika muktadha wa sera za kiuchumi za dunia ya leo.
Kama ni kweli kwamba sekta ya utalii
iliiingizia nchi dola milioni 731 mwaka 2003, ambazo ni asilimia 25 ya mapato
ya fedha za kigeni, inamaanisha kwamba mapato ya fedha za kigeni mwaka huo
yalikuwa dola milioni 2,924 (au bilioni 2.9 kwa kifupi). Lakini takwimu za hali
ya uchumi wa taifa za mwaka huo zinaonyesha tofauti: mapato ya fedha za kigeni
mwaka huo yalikuwa dola milioni 1,142 (au dola bilioni 1.1 kwa kifupi)!
Hizo
takwimu za serikali za hali ya uchumi kwa mwaka huo zinaonyesha kuwa mauzo ya
mazao ya kilimo (kahawa, pamba, katani, chai, tumbaku, karafuu na korosho)
yalichangia dola milioni 222.7 au asilimia 19.5.
Kadhalika, mauzo ya bidhaa zingine (madini, bidhaa za viwandani, samaki na
mazao ya baharini (marine products), maua na mboga na utalii) yalichangia dola
milioni 919.7 au asilimia 80.5 ya mauzo yote ya nje.
Katika hizi dola milioni 919.7, sekta ya madini peke yake ilichangia
dola milioni 548.3 au asilimia 48 ya mauzo yote ya nje. Dhahabu peke yake
ilichangia dola milioni 499 au asilimia 43.7 ya mapato yote. Bidhaa za
viwandani zilichangia dola milioni 99.9 au asilimia 8.8 na mauzo ya samaki na
mazao megine ya baharini yalichangia dola milioni 136.2 au asilimia 12. Uuzaji
wa maua na mboga ulichangia dola milioni 13.7 au asilimia 1.2 za mauzo yote ya
nje. Katika hizi ripoti za hali ya uchumi wa taifa, hakuna takwimu za utalii na
mchango wake katika upatikanaji wa fedha za kigeni haujaanishwa hata kidogo!
Ikumbukwe kuwa sekta ya utalii iko chini ya Wizara ya Mali Asili na Utalii na
takwimu za mauzo ya samaki zimeanishwa wazi, lakini si za utalii. Na takwimu za
hali ya uchumi wa taifa ndizo zitumikazo katika upangaji wa mipango ya kitaifa
ikiwa ni pamoja na kupanga bajeti ambayo ni sehemu ya maamuzi ya kupanga kama
sekta ipi ipewe kipaumbele au ipi ni muhimu.
Hadi kufikia hapo, yabidi tujiulize kama kweli utalii unachangia
hicho kiasi kinachodaiwa na wanasiasa wetu. Cha kwanza kinachojitokeza wazi ni
kwamba hizo takwimu za watalii na mchango halisi wa sekta hii katika uchumi ni
za kubunia, na zinaficha mambo mengi sana, ikiwa ni pamoja na unyonywaji na
ufukarishwaji wa nchi na watu wake. Fedha nyingi zinatumika kuutangaza utalii
na vivutio vyake; na inadaiwa kuwa idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka.
Lakini
kihalisia watalii ambao wamekuwa wakija nchini kwa ajili ya vivutio hivyo si
wengi kwa kiasi kinachodaiwa, kwani, kwa mfano, Tourism Master Plan inaonyesha
kuwa kati ya watalii 502,000 wanaodaiwa
kuingia nchini mwaka 2000, wale waliokuja kwa ajili ya mapumziko au kutembelea
vivutio hawafiki hata nusu. Asilimia 25 ya hao wanaodaiwa kuwa ni watalii
walikuwa wafanyabiashara, asilimia 12 ni watu waliokuja kutembelea ndugu zao au
marafiki, asilimia 12 walikuja kuhudhuria mikutano na makongamano na waliobakia
ni watu walikuja kwa shughuli zao wenyewe.
Waafrika, ikiwa ni pamoja na Watanzania walioko nje walikuwa
asilimia 40.5 ya wageni waliotembelea nchi, Wazungu walikuwa asilimia 30 na
Wamarekani walikuwa asilimia 9. Idadi halisi ya watalii waliotoka Ulaya ilikuwa
118,000 na wale waliotoka Marekani ya Kaskazini ilikuwa 31,000. Mamlaka ya
hifadhi za wanyama Tanzania (TANAPA) inaonyesha kuwa idadi ya watalii
waliotembelea mbuga za wanyama mwaka 2001 haikuzidi 120,000 nayo ilipata kiasi
cha dola 19,791,765. Kadhalika inakadiriwa kuwa mamlaka ya hifadhi ya mlima
Kilimanjaro (KINAPA) ilipata dola milioni 7, na ile ya Ngorongoro ilipata dola
milioni 6.79. Mapato kutokana na uwindaji wa wanyama pori wa kitalii yalikuwa
dola 9,021,960.
Hii inamaanisha kwamba Tanzania, kihalisia ilipata dola milioni
42.6 tu kutokana na utalii!
Hili linawezekana kuwa kweli kabisa, kwani hotuba zote za bajeti za Waziri
wa Maliasili na Utalii, katika nyongeza zake zinaonyesha kwamba chanzo cha
takwimu zake ni Idara ya Takwimu ya Taifa na si Wizara yenyewe! Lakini takwimu
za mauzo ya samaki na mali asili zingine chanzo chake ni wizara yenyewe. Iweje
Wizara husika isiwe chanzo cha takwimu, badala yake zitoke kwenye idara ya
takwimu?
Ni kwa sababu Wizara haina njia ya kupata takwimu za sekta hii: huu
ndiyo ukweli. Na kitu ambacho Idara ya Takwimu inafanya ili kupata makadirio
haya ya mchango wa sekta ya utalii ni kuchukua hesabu ya wageni wote wajao
nchini, pamoja na ile ya wale ambao si watalii, ikajumlisha na hela
zilizobadilishwa katika mabenki na maduka ya kubadilisha fedha ambazo watu
wanaletewa na ndugu au marafiki zao au zile za “wataalamu” wa kutoka nje waliopo
nchini na ndipo inapokadiriwa kuwa nchi imepata dola milioni 750 na kwamba
utalii una mchango mkubwa katika uchumi wa taifa!
Kwa mfano, wageni walioingia nchini mwaka 2003 walikuwa 576,000, na
mahesabu ya kukadiria ya Idara ya Takwimu yanadai kwamba mmapato ya wastani ya
mahoteli kwa siku ambazo mtalii mmjoja alikaa nchini yalikuwa ni dola 1,169 (au
dola 173 kwa siku). Kwa hiyo, kwa makadidirio hayo, mahoteli yalipata dola
milioni 673. Hivyo basi, hizo zilizoongezeka zaidi ya hapo (dola milioni 58)
yawezekana kuwa zilikuwa zile za kununulia vinyago, za kunywea kwenye mabaa,
kula kwenye migahawa, n.k.
Hiyo ndiyo njia pekee ya kufanya makadirio ya
mchango wa utalii, kwani, tofauti na bidhaa zingine ambazo huuzwa nje ya nchi,
utalii ni bidhaa ambayo haipelekwi nje. Kwa hiyo basi, kuna uwezekano mkubwa
kabisa kuwa mapato halisi ambayo nchi inayapata na kiasi halisi cha mapato ya
biashara ya utalii ni tofauti kabisa.
Lakini makadirio haya hayasemi ukweli wa mambo, kwani watalii
hulipia gharama zote za safari zao, ikiwa ni pamoja na zile za vinywaji, huko
huko nchini kwao wanakotoka. Hivyo basi, pesa kidogo wanazokuja nazo nchini ni
zile za kununulia vinyago tu.
Kadhalika, makampuni mengi ni ya kigeni na hivyo
ni hela kidogo sana ambazo zinabakia nchini kwa ajili ya kulipia gharama za
uendeshaji, kuwalipa wafanyakazi wa Kitanzania mishahara ya kitumwa kutoka na
ajira za msimu, n.k. Kadhalika, sehemu kubwa ya vinywaji na baadhi ya mahitaji
ya mahoteli na makampuni haya yanaagizwa kutoka nchi za nje.
Utalii ni sekta ambayo
imehodhiwa na makampuni ya Magharibi, na makampuni madogo yaliyopo nchini
ambayo yanadaiwa kuwa ni ya “wazalendo”, kazi yake kubwa ni udalali.
Sehemu kubwa ya mapato yatokanayo na sekta
hii yanabakia nchi za nje na nchi haifadiki kiasi kinachodaiwa kutokana na
biashara hiyo. Ikumbukwe kwamba, katika dunia hii, utalii ni biashara
inayoshikilia nambari mbili duniani baada ya ile ya mafuta na makampuni makubwa
kama vile TUI (Ulaya, zamani likiitwa Thomson), JTB na Kinki Nippon Tourist
Agency (Japan), American Express, Transat
A.T. Inc, Thomas Cook, Abercrombie,
Fitch, First Choice na My Travel, ndiyo yanayotalawala na kuhodhi biashara
yote.
Ni kwa sababu hiyo, Mashirika ya
Biashara ya Dunia kama vile WTO yamekuwa yakijishughulisha sana na uwekaji wa masharti
ya kunufaisha makampuni ya nchi za magharibi katika sekta ya utalii. Imefikia
hatua ambapo hata mabenki na taasisi za fedha za dunia, ikiwa ni pamoja na
Benki ya Dunia, Goldman Sachs au hata Meril Lynch na mengine kama makampuni ya
kidunia—Gulf and Western au Castle and Cook, yanachukua maeneo makubwa ya
ardhi duniani na kuyageuza kuwa vivutio vya utalii.
Katika nchi kadhaa, vivutio na hata hizo mbuga za wanyama zimebinafsishwa. Katika nchi zetu, wafugaji, wavuvi na wakulima wanaondolewa katika maeneo yao kwa nguvu ili yatumike na wawekezezaji. Wale walio katika maeneo yanayozunguka vivutio au ya uwindaji wanaishia kufanyiwa viini macho vya kujengewa madarasa au zahanati au kupewa madawati ya shule.
Na huku ndiko kunaitwa kupunguza umaskini, baaada ya kufukarishwa kutokana na kunyang’anywa maeneo yao au kuzuiwa kufanya shughuli zao.
Unyonyaji mkubwa uliomo katika sekta
ya utalii ndio unaopelekea kutoa takwimu ambazo hazitoi hali halisi. Na ni
takwimu hizo hizo ambazo zinapelekea nchi zetu kuwekeza fedha nyingi za kodi
katika ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya kuijenga sekta hiyo, kiasi cha
kutusahaulisha kuwa muhimu kwa nchi kama za kwetu na msingi wa maendeleo ya
kweli ni uwekezaji katika sekta ya kilimo, viwanda, madini, elimu, afya na
huduma zingingine za kijamii na kiuchumi kwa ujumla.
Kibaya kuliko vyote ni
ukweli kwamba ukuaji wa sekta hii unaambatana na udhalilishaji wa wananchi, kwa
kutumia raslimali zinazozalishwa na sekta zingine ambazo ni muhimu kwa maisha
ya wananchi.
Kadhalika, kwa visingizio vya
kuendeleza utalii wa kitamaduni na kimazingira (cultural tourism na
eco-tourism), kwa madai kuwa ni njia mojawapo ya kupunguza umaskini, inabidi
Wasonjo, Wamasai, Wazaramo waonyeshwe mbele ya watalii katika hali yao ya
udhalili, kwani watalii wanataka kuona Waafrika katika
mazingira yao ya “asili”. Hata umasikini unakuwa ni kivutio kwa wawekezaji.
Haya ndiyo yanayodhihirishwa na matangazo yanayoitangaza sekta ya utalii
ambayo yamegubikwa na ubaguzi wa rangi, udhalilishaji wa kijinsia na hata
kuutukuza ukoloni kwa kutumia majina kama ya akina Livingstone, Speke, Rebman,
Selous, n.k. katika matangazo ya vivutio vya nchi.
Inabidi tutafakari na kujiuliza mengi!


