Tumkumbuke Mwalimu, Tumuenzi Kwa Vitendo

Na Bashiru Ally

Ndugu zangu nawaasa, tumkumbuke
Mwalimu,

Sifa zake na siasa, ni hazina maalumu,

Tutumie kila fursa, kutenda kama
Mwalimu

Tumkumbuke Mwalimu, tumuenzi kwa
vitendo.

Alikuwa ni shujaa, wa kueneza upendo

Alikuwa mjamaa, msomi na mzalendo,

Hakuwa mwenye tamaa, kifikra na
vitendo,

Tumkumbuke mwalimu, tumuenzi kwa
vitendo.

Alikuwa mtetetezi, wa walonyimwa uhuru,

Alipinga waziwazi, siasa za kikaburu,

Alipinga ubaguzi, udini na ubeberu,

Tumkumbuke Mwalimu, tumuenzi kwa
vitendo.

  

Aliamini kwa dhati, katika kujitawala,

Rushwa aliidhibiti, kwa haki alitawala,

Dhamana hakusaliti, kwa kuitamani  hela,

Tumkumbuke Mwalimu, tumuenzi kwa
vitendo.

Alikuwa muandishi, wa vitabu na makala,

Alikuwa ni mcheshi, hasa kwenye
mijadala,

Alichukia uzushi, utandawizi na hila,

Tumkumbuke Mwalimu, tumuenzi kwa
vitendo.

Kumbukumbu ya Mwalimu, isifanywe kwa
msimu,

Liwe ni letu jukumu, kutenda kama
Mwalimu,

Nia hii ikitimu, atatulipa Karimu,

Tumkumbuke Mwalimu, tumuenzi kwa
vitendo.

Twakuomba Mola wetu, ibariki Tanzania,

Lilinde na Bara letu, dhidi ya
maharamia,

Warehemu ndugu zetu, wote walotangulia,

Ewe Mola ibariki, Afrika na watu wake.