Tuwaonao kwenye Ripoti
ya CAG kuhusu ESCROW

Sasa macho na masikio ya wadadisi wa
mambo yameelekezwa Ikulu. Juma hili Rais atawajulisha wananchi uamuzi wa
Serikali kuhusu mapendekezo ya Bunge kuhusiana na utoaji wa fedha katika
akaunti ya ‘Escrow ya Tegeta’. Yanatarajiwa maamuzi magumu.

Ili kutuandaa na kitakachojiri, Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Ikulu ikatoa tamko siku ya sherehe za miaka 53 ya uhuru wetu
– 09/12/2014 – lililobeba maneno haya
: “….Kufuatia kupokea nyaraka hizo,
Rais Kikwete ameelekeza kuwa Ripoti ya CAG iwekwe hadharani kwa ajili ya umma
kuweza kuisoma na kujua nini hasa kimesemwa na kupendekezwa na Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali [CAG]. Rais Kikwete ameelekeza kuwa Ripoti
hiyo itangazwe kwenye magazeti yanayosomwa na watu wengi na kwenye mitandao ya
kijamii, ili Ripoti hiyo iweze kupatikana kwa Watanzania wengi….”

Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotuchambulia ripoti ya CAG kwa
umahiri mkubwa Bungeni naye akaandika maneno mazito kuhusu sakata hilo katika
ukurasa wake kwenye mitandao ya jamii na kuhitimisha hivi:
“….Ikulu
imeagiza Taarifa ya CAG ichapwe kwenye magazeti, jambo ambalo halijapata
kutokea huko nyuma kwani sio mara ya kwanza PAC kutumia Taarifa ya CAG
kuwajibishana….”

Baada ya kusoma matamshi hayo na aliyoripotiwa akiyasema Mdhibiti na
Mkaguzi wa Hesabu za Serikali aliyeteuliwa hivi karibuni
, wadadisi tulihoji
mtandaoni: “Ripoti
ya CAG ina kitu tusichokijua kuhusu ESCROW?”
Mwandishi mmoja mwandamizi akajibu
bila kusitasita: “Ndiyo….Tatizo Watanzania huwa hatusomi ingawa ni wasemaji
sana.”

Changamoto hii imetugusa na hivyo
tumeisoma tujionee wenyewe nini kilichomo na nani waliomo humo. Ufuatao ni
udadisi wetu kuhusu hayo. Tumezingatia kuwa, kwa kawaida, huwa kuna mstari
mwembama kati ya hali halisi na tafsiri ya hali halisi hiyo unaopelekea kuwe na
tofauti za kiuchambuzi na kimaoni. Hivyo, hii ni ‘tafsiri tunduizi’ tu ya kile
tunachokiona na wale tunaowaona humo. Ni haki yetu sote kuhoji tafsiri na
watafsiri.

Inaitwa “Taarifa
ya Ukaguzi Maalum Kuhusiana na Miamala Iliyofanyika Katika Akaunti ya ‘Escrow’
ya Tegeta, Pamoja na Umiliki wa Kampuni ya IPTL.”
Kuhusu “Madhumuni na Wigo
wa Ukaguzi Huu” kipengele cha 1.4 katika “Utangulizi” kinatoa angalizo hili
muhimu: “Madhumuni ya kufanya ukaguzi huu maalumu ni kumwezesha Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali kutoa mapendekezo yake kuhusiana na utaratibu
uliotumika kutoa fedha kutoka akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyokuwa katika
Benki Kuu ya Tanzania. Ukaguzi huu maalum umefanyika kwa kuzingatia matakwa ya
viwango vya kimataifa vya ukaguzi na kuzingatia hadidu za rejea kama zilivyoridhiwa
na pande zote. Hata hivyo ukaguzi huu hautoi maoni ya ukaguzi (audit opinion)
badala yake unatoa mapendekezo yanayolenga katika kushughulikia mapungufu
yaliyobainika katika ukaguzi huu. Ingawa matokeo ya ukaguzi huu yanajumuisha
uchambuzi wa masuala ya kisheria, ukaguzi huu hautoi maoni juu ya kuwa au
kutokuwa na hatia kwa mtu, chombo au taasisi yoyote iliyohusika katika ukaguzi
huu.”

Hitimisho la kipengele hicho linatoa
mwanya huu kwa wale ambao pengine wana asichokijua CAG: “Ukaguzi huu ulijikita
katika uchambuzi wa nyaraka, taarifa na kumbukumbu kama tulivyozipokea kutoka
katika taasisi husika ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano na wahusika
mbalimbali katika suala la malipo yaliyofanyika kutoka katika akaunti ya Escrow
ya Tegeta, umiliki wa IPTL na utekelezaji wa mkataba wa ununuzi wa umeme toka
lPTL. Endapo nyaraka, taarifa ama kumbukumbu nyingine zitapatikana vinaweza
kubadili mwelekeo wa maoni na hitimisho la ukaguzi huu.”

Kipengele cha 1.1 cha “Utangulizi”
chenyewe kinatuelezea “Chimbuko la Ukaguzi” ambapo tunaona kuwa: “ Ukaguzi huu
umetokana na barua…ya tarehe 10 Juni 2014 kutoka kwa Mh. Waziri Mkuu. Kabla ya
barua hii, ukaguzi huu ulikwishaombwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
kupitia barua…ya tarehe 12 Machi 2014 na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kupitia barua … ya tarehe 20 Machi 2014. Barua ya Mh. Waziri Mkuu imefanya
rejea katika maombi yaliyotangulia kutoka kwa Katibu wa Bunge na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini. Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi iliwasiliana na Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini na Katibu wa Bunge kupitia barua…ya tarehe 17
Aprili, 2014 ili kukubaliana juu ya hadidu za rejea zitakazoongoza ukaguzi huu.
Hadidu za rejea husika ziliridhiwa na taasisi hizo mbili kupitia barua…ya
tarehe 5 Mei 2014 kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini na barua …ya
tarehe 03/05/2014 kutoka kwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya

Muungano wa Tanzania.”

Kwa maana nyingine, miongoni mwa waliooomba
ukaguzi huo ufanyike ni walengwa wa ukaguzi huo. Je, walitaka ukaguzi
uwasafishe? Au hawakujua wanaokaguliwa ni wao?

Sura ya pili ya Taarifa ya CAG
inaanza kwa kurejea historia ya jinsi ambavyo uhaba wa maji na upungufu wa umeme
ulipelekea Serikali kupitisha Sera ya Nishati ya mwaka 1992 “iliyoruhusu
uwekezaji binafsi katika sekta ya nishati.” Huo ukawa mwisho wa “TANESCO pekee”
kuwa “ndiyo iliyokuwa na jukumu la kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme.” Kwetu
wadadisi wa wawekezaji huo ndio ulikuwa mwanzo wa Fungate
la Uwekezaji na Migogoro ya Maslahi
. “Katika kutekeleza sera hiyo na
kuchukua hatua za dharura,” CAG anaendelea kututaarifu, “Serikali ilialika
wawekezaji binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa umeme.”

Hivyo basi (inasemekana) “tarehe 27
Agosti 1994” ndipo “Wizara ya Maji Nishati na Madini iliingia katika Memoranda
ya Makubaliano (MoU) na Kampuni ya Mechmar ili kuleta suluhisho la kukabiliana
na upungufu wa umeme.” Mwaka huo huo “Kampuni ya IPTL ilianzishwa chini ya
umiliki wa Kampuni ya Mechmar kutoka Malaysia na Kampuni ya VIP Engineering and
Marketing (VIP) ya Tanzania. Kampuni ya MECHMAR ilimiliki asilimia 70 na VIP asilimia
30 ya hisa za IPTL.”

Hiki ni kile ambacho wadadisi wa
wawekezaji tunakiita ‘Utanzaniashaji wa Uwekezaji wa Nje’ tukimaanisha kitendo
cha kampuni ya nje kuingia ubia na kampuni ya ndani au yenyewe kujisajili kama
kampuni ya ndani ili kupata faida ambazo ni mahsusi kwa makampuni ya ndani.
IPTL ilizaliwa hivi ndio maana kirefu chake, kama kilivyo kwenye taarifa ya CAG,
ni “Independent Power Tanzania Limited.” Ilibatizwa ‘Utanzania’.

Taarifa ya CAG ina “Jedwali T1” la
mikataba 4 iliyoingiwa katika utekelezaji wa mradi wa uzalishaji umeme wa
Megawati (MW) 100. Cha kudadisi kwa kina ni mwachano wa tarehe ambazo mikataba
hiyo baina ya IPTL na TANESCO (wa kwanza na, kwa tafsiri yetu, wa nne) na baina
ya IPTL na Serikali (wa pili na wa tatu) iliingiwa. Mkataba wa kwanza ni wa “Kununua
Umeme” na uliingiwa tarehe “26 Mei 1995”. Wa pili ni wa “Utekelezaji wa Mradi
wa Kufua Umeme Megawati 100” ulioingiwa tarehe “8 Juni 1995”. Kisha wa tatu ni
wa “Dhamana” ulioingiwa tarehe hiyo hiyo ya “8 Juni 1995.” Halafu wa nne ni wa
“nyongeza” na uliingiwa siku iliyofuata, yaani “9 Juni 1995.”

 Hii nyongeza ndiyo kiini kikuu cha utata na
utatanishi. Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG, ni nyongeza “kwa” – ama kwenye – mkataba
wa kwanza. Na inatutaarifu kuwa “Dhima ya Mkataba” huo wa nyongeza niKuelekeza ukokotoaji wa viwango vya
tozo (tariffs) ya ‘capacity charges’” pamoja na “Kuainisha washirika wa
Makubaliano ya “‘Escrow.’”

Lakini nini maana ya ‘Escrow’? Kwa
tafsiri nyepesi kabisa ya kilei, tuchukulie kuwa Chaupele ana ugomvi na
Chausiku kuhusu kibarua alichompa. Chaupele anataka kumlipa mwenzake kiasi
anachoona ndicho kinachoendana na ubora wa kazi aliyoifanya kwa mujibu wa
makubaliano yao. Lakini Chausiku hakubaliani na kiwango hicho maana anaona ni
kidogo ukilinganisha na jasho alilovuja. Wakati wanaendelea kutafuta suluhu
wanaamua hela ambayo Chaupele atakuwa anatakiwa kumlipa Chausiku ishikwe na mtu
wa tatu asiye na maslahi yoyote au upendeleo wowote kwa mdau yeyote.
Anachaguliwa Chaurembo na kuziweka kwenye kibubu.Wote wanakubaliana kuwa mara
tu suluhu hiyo itakapopatikana ndani au nje ya mahakama, na kuthibitika/kuthibitishwa pasipo shaka kuwa hakuna mgogoro baina yao kuhusu
malipo hayo, basi Chaurembo atazitoa hizo fedha kwenye kibubu na kumpa mhusika
mmoja au kuwapa wahusika wote wawili kwa mujibu wa makubaliano ya suluhu. Hicho
kibubu maalum ndiyo akaunti ya Escrow.

Mfano huo unatusaidia kuelewa kwa
urahisi maelezo yafuatayo kutoka kwenye Taarifa a CAG tukichukulia kuwa
Chaupele ni TANESCO, Chausiku ni IPTL na Chaurembo ni Benki Kuu ya Tanzania
(BOT): “Kutokana na kutoridhika kwa TANESCO na viwango vya tozo vilivyokuwa vinatumiwa
na IPTL, TANESCO ilisitisha kumlipa IPTL malipo ya ‘capacity charges’ badala
yake tarehe 5 Julai, 2006 mkataba wa akaunti ya Escrow ulisainiwa kati ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya IPTL wakati Benki Kuu
ya Tanzania ilikuwa Wakala wa utekelezaji wa mkataba huo kwa mujibu wa
Kipengele Na.6.8 (b) cha Mkataba wa Kununua Umeme (PPA) ambapo fedha zote za ‘capacity
charges’ zilikuwa zikilipwa katika akaunti hiyo.”

Labda tujiulize kwa nini Chaupele awe
TANESCO na sio Serikali au Wizara ya Nishati na Madini? Tukiidadisi Taarifa ya
CAG tutaona kuwa kwa kiasi kikubwa kwenye suala la akaunti ya Escrow ya Tegeta,
TANESCO ndiye huyo huyo Wizara ya Nishati na Madini pia ndiye huyo huyo
Serikali hivyo wote ni Chaupele tu. Tuanze na nukuu hii iliyopo ukurasa wa 11:
“Kwa mujibu wa kipengele Na.1.1 na Na 7.1 cha Makubaliano ya Escrow Benki Kuu
ya Tanzania (BoT) ilikubali kuwa wakala wa akaunti ya Escrow ambayo
ilifunguliwa kufuatia makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania kupitia Wizara
ya Nishati na Madini na Kampuni ya IPTL yaliyofikiwa tarehe 5 Julai, 2006.”
Nukuu hii kutoka kwenye sehemu ya kwanza ya hadidu ya rejea ya tatu nayo inathibitisha
hilo: “Kuchunguza sababu za kufungua akaunti maalum (Escrow Account) na pia
chanzo cha mgogoro kuhusu tozo kati ya TANESCO na IPTL na kuthibitisha kuwa
mgogoro uliamuliwa kwa faida ya pande zote mbili yaani Serikali (TANESCO) na IPTL.”

Ndio maana kwenye sayansi ya siasa ni
vigumu kujibu swali la ‘Serikali ni Nani’? Huu mchanyato na mtanziko
unajumuisha ukweli kuwa hata Chaurembo wetu BOT, pamoja na uhuru wake wote wa
kitaasisi dhidi ya Wizara ya Fedha, naye ni (sehemu ya) Serikali. Miingiliano
hii ya kitaasisi ndiyo imelifanya hili sakata la Escrow liwe tata na tete
zaidi.

Tukumbuke kwamba tumeshaona kuwa mkataba
huo wa kununua umeme ulisainiwa  Mei 1995
na kuwekewa nyongeza inayohusu Escrow Juni 1995. Japo Taarifa ya CAG
inajichanganya kidogo kuhusu lini hasa – kati ya mwaka 1997 na mwaka 1998 –
ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme hatimaye ulikamilika, inabainisha kuwa
uzalishaji haukuanza punde. Kwa nini? Jibu mojawapo la moja kwa moja linapatikana
kwenye nukuu hii iliyopo ukurasa wa 8 wa Taarifa hiyo: “Mwaka 1998 TANESCO
ilifungua shauri dhidi ya IPTL Na. ARB/98/8 katika Baraza la Kimataifa la usuluhishi
wa Migogoro ya Uwekezaji (International Centre for Settlement of Investment
Disputes-ICSID) ikidai kusitishwa kwa PPA kutokana na ukiukwaji wa baadhi ya
vipengele katika utekelezaji wake. Kutokana na shauri
hilo, Mkataba wa uzalishaji umeme pamoja na kwamba uliingiwa mwaka 1995 na
ujenzi wa mitambo kukamilika mwaka 1997, uzalishaji wa umeme ulianza Januari
15, 2002 (commercial operation date). Hivyo kwa kuwa mkataba ni wa miaka 20
unategemewa kuisha mwaka 2022.”

Labda jibu jingine linapatikana
kwenye nukuu hii kutoka kwenye kipengele kinachoongelea “Historia ya Mkopo wa
IPTL” kilichopo ukurasa wa 43 hadi 44: “Baada ya kuingiwa kwa Mkataba wa Kununua
Umeme (PPA) baina ya TANESCO na IPTL; Kampuni ya IPTL iliingia mkataba na Umoja
wa Mabenki ya Malaysia (Consortium of Malaysian Banks) tarehe 28 Juni 1997 kwa
ajili ya mkopo wa jumla ya kiasi cha Dola za Kimarekani 105 ,000,000 ili
kuwezesha ujenzi wa mradi wa ufuaji wa umeme uliopo Tegeta. Mabenki hayo ni
Sime Bank Berhad (kiasi cha Dola za Kimarekani 10,000,000), BBMB International
Bank Ltd (kiasi cha Dola za Kimarekani 55,000,000), na Sime International Bank
(kiasi cha Dola za Kimarekani 40,000,000).”

Kwa mantiki hii, mwaka 1994 wakati
IPTL inaanzishwa na mwaka 1995 wakati inaingia mikataba minne ama haikuwa na
uwezo wa kifedha wa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme au kama ilikuwa nao,
basi uwezo huo ulitoweka ilipofikia mwaka 1997. Lakini dhana za ubepari
zinatufundisha kuwa eti biashara, hasa kubwa kubwa, hazifanyiki bila mikopo
mikubwa. Hivyo, labda uwezo wa IPTL kuwekeza ulikuwa unapimika hivyo.

Cha kustaajabisha ni kuwa, kwa mujibu
wa Taarifa ya CAG: “Jumla ya kiasi cha USD 85,862,022 kati ya USD 105,000,000
ndicho pekee kilichopokelewa na IPTL kati ya mwezi Agosti 1997 na Desemba 1999.”
Jambo la kushangaza zaidi ni kuwa wakati wa lililokuwa zoezi la ufilisi wa IPTL
mwaka 2012 wadeni wanne “waliojitokeza na kuainisha madai yao ya jumla ya Sh. 321,041,365,000, USD 145,628,784.43 na GBP 1,439,836.50” walikuwa ni pamoja
na makampuni mawili ya ujenzi – “Watsila Tanzania Ltd” na “Watsila Netherlands
B.V.” Wakati “Maelezo ya Deni” la huyo wa kwanza ni “Mkataba wa Uendeshaji na
Ukarabati” ya huyo wa pili ni “Mkataba wa Ujenzi.”

Udadisi wa kina wa mikopo na madeni
hayo unaweza kutusaidia kuelewa kwa nini, kwa mujibu wa CAG, wanasheria walioishauri
TANESCO walitofautiana kuhusu kiwango ambacho kiliwekezwa na IPTL. Kampuni moja
ya wanasheria iliona hivi: “Mapendekezo ya Mkono & Co. Advocates katika
kipengele cha 7 na 8 katika taarifa yake kwa Bodi aliishauri TANESCO kuwataka
IPTL kufanya marekebisho ya gharama za uwekezaji (Capacity Charges) kwa
kuzingatia mtaji wa Shilingi 50,000 na kuanzisha madai dhidi ya IPTL ili
kurejesha fedha zilizolipwa zaidi kutokana na kutumika kwa mtaji wa Dola za Kimarekani
Milioni 38.16 katika ukokotoaji wa tozo za uwekezaji isivyo sahihi. Pia TANESCO
ilishauriwa kutoa tamko la kutokubaliana na tozo hiyo (Invoice Dispute Notice)
na endapo hakutakuwa na suluhisho, TANESCO na IPTL wangepaswa kufungua akaunti
maalumu ya Escrow kwa haraka kwa mujibu wa Kipengele Na. 6.8 (b) cha PPA.”

Kampuni nyingine ya wanasheria iliona
hivi: “Katika uchunguzi wao Hunton and Williams waliainisha kuwa ujenzi wa mitambo
ya IPTL kwa kutumia mtaji (Owners Equity) wa TShs 50,000 haileti mantiki katika
uhalisia wake kinyume na ilivyoainishwa na Mkono &. Co. Advocates. Vilevile
Hunton and Williams ilibainisha kuwa mtaji wa USD 38.16 Milioni uliokuwa ukitumiwa
na IPTL katika ukokotoaji wa ‘capacity charges’ haukuthibitika usahihi wake
kama ilivyokuwa imeamuliwa katika Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi ICSID
tarehe 12 Julai 2001 (ICSlD 1). Hata hivyo kwa kutolipa gharama za uwekezaji (capacity
charges), TANESCO hawakuwa na nafasi ya kushinda katika shauri hilo na hivyo kushauriwa kukaa
pamoja na IPTL kujadili na kukubaliana juu ya mtaji halisi uliowekezwa na
wanahisa (Owners equity).”

Swali hilo bado linahitaji jibu
sahihi: IPTL iliyokopa mabenki mwaka 1997 ilikuwa na mtaji kiasi gani na
wanahisa wake – MECHMAR na VIP – waliwekeza mtaji halisi upi? Pia swali la
kujiuliza ni kwa nini Taarifa ya CAG, japo haimtaji kwa jina Andrew Chenge kuwa
ndiye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inaonesha kuwa aliyekuwa Mkurugenzi
Mkuu wa TANESCO hakupata jibu kuhusu maombi ya ushauri wa kisheria kuhusu maoni
kinzani ya wanasheria hao binafsi waliolishauri shirika hilo umma. Hili ni
muhimu maana Chenge
ametajwa katika orodha ya waliopata fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow
,
tena ‘vijisenti’ vingi sana – Shilingi bilioni 1.6 za Kitanzania.

Hebu turejee nukuu husika ukurasa wa
21 wa Taarifa ya CAG: “Kufuatia maoni ya kisheria ya Mkono & Co. Advocates
kutofautiana na maoni ya Hunton and William LLP, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji
wa TANESCO Bw. …. Huysen alimuomba ushauri Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia
barua …. ya tarehe 05 Julai 2004 ambapo ushauri wa Mkono & Co. na Hunton
and William uliambatanishwa….Kufuatia kutojibiwa kwa barua…ya tarehe 05 Julai 2004
na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. …. Huysen
alimuomba Katibu Mkuu Nishati na Madini kupitia barua …ya tarehe 23 Septemba 2004…kuwasiliana
na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupata majibu ya Barua … ya tarehe 5
Julai 2004….Pia Mkurugenzi Mtendaji alimuomba ushauri Msajili wa Hazina kupitia
barua…ya tarehe 16 Agosti 2004 kufuatia mgongano huo wa maoni ya kisheria….” Ni
nani huyo alikuwa Msajili wa Hazina wakati huo?

Huysen na
NetGroup Solutions (Pty) Ltd. yao ya Afrika Kusini walikuwa na matatizo yao ya
uendeshaji wa TANESCO
yetu na kina Rutabanzibwa wanastahili pongezi kwa (kulazimika)
kuwaondoa nchini lakini kwenye hili la kutafuta bila ajizi ushauri wa wenye
dhamana ya mali ya umma ni haki yake tumpe heko. Japo Rutabanzibwa
ameorodheshwa  katika “Kiambatanisho Na.
1” cha “Mahojiano/Majadiliano yaliyofanyika wakati wa ukaguzi huu” katika
Taarifa ya CAG, insha ya taarifa hiyo haisemi kama alitoa maelezo ya kwa nini
Huysen hakujibiwa au/na kama hatimaye alijibiwa baadaye. Labda Hansard za mahojiano/majadiliano
yake na CAG ina mwanga zaidi. Ila kilichopo kwa sasa kuhusu hilo ndani ya insha
hiyo bado ni giza nene maana baada ya hapo kilichofuata ni Escrow.

Insha ya Taarifa ya CAG inasema hivi:
“Barua…ya tarehe 06 Desemba 2005 kutoka kwa Mkono & Co. Advocates kwenda
kwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini Bw. Patrick Rutabanzibwa ilirejea
mazungumzo ya tarehe 05 Desemba 2005 ambapo iliamuliwa kuwa Kampuni ya Mkono
& CO. Advocates iandae rasimu ya makubaliano kwa ajili ya ufunguzi wa
akaunti ya Escrow.” Wale wanaoamini kuwa ‘njia ya kwenda kuzimu imenakshiwa na
nia njema’ wanaweza kusema huko ndiko uamuzi mwema wa kuanzisha akaunti maalumu
ya kutuokoa na kadhia ya kuilipa kupita kiasi IPTL unakotupeleka Watanzania. Hapa
inabidi tuweke tuo na kurejea maneno haya ya mwandishi mkongwe, Nizar
Visram,  katika makala yake ya IPTL
haina jipya, tulipaswa kuwa wakali tangu 1994
ya kwenye  gazeti la Raia
Mwema
: “Mnamo…1994 mkataba wa maelewano (MoU) ulifikiwa na kuthibitishwa na
mwanasheria mkuu wa nchi, kuwa ulikuwa mzuri na wa manufaa kwa nchi. Hatukujali
tahadhari iliyotolewa na washauri wa TANESCO (kampuni
za Acres kutoka Canada na Hunton and Williams kutoka Uingereza
) kuwa
uwekezaji huo ulikuwa ni kitanzi kwa sekta ya umeme na kwa uchumi wa nchi yetu.”

Kinachoshanganza sana ni kuwa, kwa
mujibu wa Taarifa ya CAG, mwanahisa mmojawapo wa IPTL ndiye alikuwa wa kwanza
kwanza kutujulisha kuwa kitanzi hicho kinatunyonga. Je, ni uzalendo ulimfanya
afanye hivyo? Pengine aliona fursa inayoweza kujitokeza Escrow kutokana na migogoro?
Au ni yale yale tu ya kumwona adui wa adui yako kuwa ni rafiki yako kwa kuwa
mtasaidiana kupambana na adui wenu mmoja?

Taarifa ya CAG inaelezea hivi ‘kisa
mkasa’ hicho cha kustaabisha kwenye ukurasa wa 18: “Ukaguzi umebaini kuwa
katika kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO cha tarehe 01 Aprili 2004,
TANESCO walifahamishwa na mmoja wa wanahisa wa IPTL, kampuni ya VIP kuhusu
mambo kadhaa ambayo yanaashiria kuwa TANESCO inalipa viwango vya ‘tariffs’ vya juu
isivyostahili. Baada ya kupata taarifa hiyo, Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO
ilianza kuchunguza usahihi wake kwa kuiteua kampuni ya Mkono & Co.
Advocates ili kufuatilia taarifa hiyo na kutoa ushauri. Pia Bodi iliwateua
(miongoni mwa wajumbe wa Bodi) Bw. Anorld Kilewo, Dr. Enos Bukuku na Bw. B.
Mrindoko kuunda kamati maalumu ili kufuatilia kwa ukaribu taarifa hizo.”

Wadadisi wa historia ya uwekezaji
nchini Tanzania hawajasahau sehemu hii ya pili ya Azimio
la 14 la Bunge Juu ya Mkataba Baina ya TANESCO na RICHMOND DEVEVELOPMENT
COMPANY LLC la mwaka 2008
: “Aidha, Kamishna wa Nishati, Ndugu Bashir
Mrindoko naye achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kumshauri Katibu Mkuu
wake mpya kuhusu udhaifu wa Richmond Development Company LLC ambao ulijulikana
dhahiri na Wizara mwaka 2004 kwenye Mradi wa bomba la mafuta. Ndugu Mrindoko
ndiye aliyeiandikia barua Kampuni hiyo kusitisha Mkataba wake na Serikali mwezi
mmoja tu kabla ya mchakato wa Zabuni ya umeme wa dharura haujaanza.” Lakini watu
wenye utu wanatuasa kuwa kosa moja lisiwe kisingizio cha kumhukumu mtu kwa kosa
lingine. Kwa mantiki hii ya ‘ubinaadamu’, inashauriwa tusimhukumu, anayesemekana
ukurugenzi wake ulileta tija na ufanisi TANESCO kuliko wa wengine, kwa sababu
tu aliwahi kuhusishwa pamoja na Chenge kwenye kashfa ya Rada
badala yake tumpongeze hasa ukizingatia Taarifa ya CAG imemuandika hivi: “Katika
vipindi tofauti mwaka 2008, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dr.
ldrisa Rashid alifanya mawasiliano mbalimbali na IPTL kuhusiana na madai ya
TANESCO kwa IPTL yaliyotokana na kutozwa zaidi kiwango cha tozo ya uwekezaji
(capacity charges)”. Ila  Dakta
Bukuku ametajwa na kina Chenge kwenye orodha ya waliopokea fedha za Escrow

kupitia akaunti ya James Rugemalila wa VIP iliyofunguliwa kwenye Benki ya
Mkombozi, kiwango chake nacho si haba – Shilingi milioni  161.7 za Kitanzania. Pia kwa kuwa (bado)
hatujui majina yote kabisa ya waliopokea fedha hizo kupitia benki hii ama ile
ye Stanbic, mazingira haya ya iliyokuwa kamati maalumu ya kuishauri TANESCO
kuhusu IPTL yanaibua maswali mengi kuliko majibu.

Ndio maana inabidi tujiulize sana kwa
nini VIP ‘iliitonya’ TANESCO. Swali lingine la kujiuliza tena baada ya taarifa
kinzani kujitokeza wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya PAC Bungeni na wa kile
kilichoitwa utetezi wa Serikali ni kwa nini miaka 10 baadaye CAG anaelezwa
yafuatayo kuhusu jinsi TANESCO ilivyojitokeza kama mmoja wa wale wadai 4 wa
IPTL wakati wa jaribio la kuifilisi: “Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO kupitia
barua…ya tarche 19 Agosti, 2014 iliyosainiwa na Mwenyekiti wake Jenerali Mstaafu
Robert Mboma…kwenda kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
ilielezea kutokifahamu kiapo cha tarehe 12 Aprili , 2012 kilichotolewa na Bw.
Godwin Simba Ngwilimi kwa niaba ya TANESCO kuthibitisha madai ya jumla ya
Shilingi bilioni 321. Barua hiyo ilibainisha kuwa deni la TANESCO lililotolewa
kiapo halifahamiki kwa Shirika na kwamba kiapo hicho kilikuwa ni matakwa binafsi
ya Bw. Godwin Ngwilimi na ushauri wa wataalam wa masuala ya fedha kutoka
Castalia LLC ambao walipewa kazi hiyo na Kampuni ya Wanasheria ya Mkono &
Co, na kwamba TANESCO hawakuwahi kupokea ushauri rasmi kutoka kwa Castalia LLC
kuhusiana na madai hayo kabla au baada ya notisi ya Mfilisi wa Muda. Mwenyekiti
wa Bodi ya TANESCO alibainisha kuwa Menejimenti ya Shirika haikuidhinisha suala
la Bw. Godwin S. Ngwilimi awasilishe madai yake kwa Mfilisi kwa niaba ya
TANESCO. Pia ilielezwa kuwa madai haya yaliyowasilishwa dhidi ya IPTL ni madai
ambayo yalikuwa tayari ndio msingi wa shauri la ICSID Na. ARB/10/20 (ICSID 2)
ambalo lilikuwa bado halijaamuliwa hivyo TANESCO isingeweza kuwasilisha madai
yanayohusu masuala ambayo bado hayajaamuliwa na ICSID.” Sasa aliwezaje kuapa
kisheria hivi hivi tu?

Inakuwaje VIP hiyo hiyo iliyowahi
kuiomba Mahakama iiweke IPTL iwekwe kwenye ufilisi na kukubaliwa ufilisi wa
muda mwaka 2008 ndiyo hiyo miaka 5 baadaye inafanya hiki kinachoelezwa kwenye
ukurasa wa 51 wa Taarifa ya CAG: “Katika vipindi mbalimbali kampuni ya IPTL
iliwekwa katika ufilisi wa muda na ufilisi kamili, ambapo mnamo tarehe 30
Agosti 2013 VIP Engineering & Marketing kupitia Ngalo &. Co advocates
kwa barua Na. NCA/DSM/1332/ 13 baada ya kutangazwa tarehe 26 Agosti 2013, iliwasilisha
Mahakama Kuu ya Tanzania ombi la kuondoa shauri la ufilisi wa IPTL.”? Jibu
tunalipata katika ombi la tatu kati ya matano iliyoyaomba mahakamani.

Ombi hilo linasomeka hivi kwenye
Taarifa ya CAG: “Kwamba Mfilisi wa Muda akabidhi mali zote za IPTL, ikiwa ni pamoja
na mtambo wa kuzalisha umeme kwa Pan Africa Power Solutions (T) limited [PAP]
ambaye amedhamiria kuwalipa wadai wote halali wa IPTL na kuongeza uwezo wa
mtambo hadi kufikia MW 500 na kuuza umeme kwa TANESCO kwa bei ya kati ya senti
6 hadi 8 za Dola za Kimarekani kwa uniti baada ya kuzingatia maslahi ya umma kama
ilivyonukuliwa hapa chini: “that the
provisional liquidator shall hand over oil the off airs of IPTL including the
IPTL Power Plant (the plant) to PAP, which has committed to pay off all
legitimate Creditors of IPTL and to expand the plant capacity to about 500MW
and sale power to TANESCO at a tariff of between Us cents 6 and 8/Unit in the
shortest possible time after taking over in the public interest
.”

Utata unazidi kuigubuka jitihada hii
pale tunapogundua kuwa miongoni mwa wale ambao walipata fedha zilizotolewa
kwenye akaunti Escrow ni Phillip Saliboko ambaye alipata Shilingi milioni 40. 4
za Kitanzania. (Alikuwa) nani huyu? Taarifa ya CAG kwenye ukurasa wake wa 43
inamtambulisha hivi”: “Katika utekelezaji wa majukumu yake, Kampuni ya IPTL
imekuwa ikidaiwa na wadai mbalimbali wa ndani na nje ya nchi. Tarehe 16 Machi 2012,
Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya Mh. Jaji Kaijage ilitoa uamuzi kwamba kampuni
ya IPTL iendelee na ufilisi kamili na kumteuwa aliyekuwa mfilisi wa muda wa
IPTL, Bw. Phillip Saliboko Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA kuwa mfilisi kamili
(Kielelezo 97). Kufuatia uamuzi huo, Bw. Saliboko alitoa notisi kupitia
magazeti mbalimbali kati ya tarehe 3-5 Aprili, 2012 iliyowataka wadai wote wa IPTL
kuwasilisha madai na taarifa zao kwake kabla ya tarehe 24 Aprili, 2012 ili
kufanikisha zoezi la ufilisi lililotokana na amri tajwa ya Mahakama Kuu ya
Tanzania.”

Suala la kuhuishwa huko kutoka kwenye
umauti wa kufilisiwa linajitokeza kwa uwazi zaidi ukiyadadisi maelezo kuhusu
mdai/mdeni mwingine miongoni mwa hao wadai/wadeni 4 tuliowagusia hapo juu,
yaani Standard Chartered Bank Hong Kong (SCBHK). Katika ukurasa wa 45 Taarifa
ya CAG inasema kwamba: “Ilibainika pia kuwa IPTL ilikuwa ikifanya marejesho
hata baada ya deni kununuliwa na SCBHK. Kwa maelezo ya SCBHK katika kipindi cha
Novemba 2005 mpaka Aprili 2007, IPTL ilikuwa ikifanya malipo moja kwa moja kwa
SCBHK. Hili linathibitika katika barua ya ….ya 03 Februari, 2014 kwenda kwa
Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, iliyosainiwa na Dr.
Magesveran Subramaniam Mkurugenzi wa Uendeshaji na Bw. Joseph Makandege
Mwanasheria wa IPTL, ilieleza kwamba hadi kufikia mwaka 2007 IPTL ilikwishalipa
jumla ya kiasi cha Dola za Kimarekani 58.69 milioni, ambapo kati ya hizo Dola za
Kimarekani 20 milioni zililipwa kwa SCBHK….Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mh.
Jaji Frederick Werema pamoja na mambo mengine kupitia barua…ya tarehe 2 Oktoba,
2013 kwenda kwa Katibu Mkuu Hazina Dr. Servacius Likwelile akizungumzia deni la
SCBHK alibainisha kuwa madai ya SCBHK hayana athari yoyole kwa Serikali baada
ya uamuzi wa kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow kwenda IPTL, kwa
msingi kwamba IPTL ni Kampuni iliyobaki kuwa hai. Hivyo SCBHK wanaweza
kuendelea na madai yake kwa IPTL kama wadeni wengine.”

“Baada ya kuhakiki nyaraka za deni la
SCB Hong Kong nchini China tarehe 14 Septemba, 2014” Taarifa ya CAG inasema
kuwa “ilibainika kuwa SCB HK ilinunua deni hilo mwezi Agosti 2005” na kwamba “Hati
halisi ya hisa saba (7) za Mechmar ambazo pia zilitumiwa kama dhamana ya mkopo
ziliwasilishwa na kuhakikiwa.” Hivyo basi haishangazi kuiona Taarifa ya CAG nayo
ikitoa pendekezo hili kwenye ukurasa wa 49 linaloonesha uhai wa IPTL na si wa
PAP: “Ni vyema SCBHK ikafuatilia ulipwaji wa deni lake kutoka IPTL ambaye ndiye
mdeni wake, kwa kuwa baada ya hukumu ya tarehe 5 Septemba 2013 ya Mahakama Kuu
ya Tanzania ambapo IPTL ilirejeshwa kuwa kampuni hai.” Sasa kwa nini kampuni
iliyo(kuwa) hai iingie kivingine kwenye Escrow?

Tukirejea majina yetu ya mfano wa
kutusaidia kuilewa ‘Escrowgate’, tujiulize ni nini hasa kilimfanya Chaurembo
(BOT) wetu atoe hela za Escrow kwa mtu ambaye kwa jina siyo Chaupele (TANESCO) wetu
wala siyo Chausiku (IPTL)? Kwa nini PAP ndiye alipwe na siyo IPTL kama kweli
kulikuwa na suluhu na TANESCO? Ilikuwaje jitihada zote zile, udhibiti wote ule,
mapambano yote yale na dhamana zote hizi zilizobainishwa kimamlaka na
kimadaraka katika ukurasa wa 11 wa Taarifa ya CAG zishindwe kabisa kuzuia
utoaji huo wa fedha uliofuatiwa na ugawanaji wa pesa nyingi sana na kwa kasi
mno uliojumuisha watu wenye dhamana kubwa za mali ya umma wa Watanzania: “Kipengele
Na 4.1 cha Makubaliano ya Escrow kinaipa mamlaka Benki Kuu kuwa mtoaji pekee wa
fedha katika akaunti hiyo. Kadhalika Benki Kuu iliwajibika kutoa taarifa kila
robo mwaka kwa pande zote za makubaliano kuhusiana na hali ya akaunti katika
kipindi husika kama ilivyoanishwa katika Kipengele Na. 5. 3 na 5.4 cha
Makubaliano ya Escrow. Kipengele Na. 7. 7 cha Makubaliano ya Escrow kinaeleza
kuwa iwapo wakala wa Akaunti ya Escrow kwa nia njema asipokuwa na uhakika kuhusu
upande unaostahili kulipwa fedha kutoka kwenye Akaunti ya Escrow kutokana na
mgogoro baina ya pande hizo, atasubiri hukumu ya mwisho ya msuluhishi
itakayomuelekeza upande stahili wa kulipwa fedha hizo ama makubaliano ya kimaandishi
baina ya pande husika”?

 Pamoja na maelezo mengi yaliyotolewa na vyanzo
mbadala mabarazani, mitandaoni na mitaani, wadadisi wa wawekezaji wakubwa tunaona
kuwa jibu limejifichaficha katika maelezo haya yaliyopo kwenye ukurasa wa 15 na
16 wa Taarifa ya CAG: “Baada ya kupokea taarifa ya Stanbic tarehe 28 Novemba,
2013, Bw.Harbinder Singh Sethi alimjulisha Gavana Prof. Benno Ndulu kuwa afanye
malipo husika kupitia akaunti za PAP zilizofunguliwa tarehe 28 Novemba 2013…. Baada
ya Bw. Harbinder Sethi kuiandikia BoT kufanya malipo katika akaunti za PAP
badala ya zile za IPTL, Mkurugenzi wa Fedha wa Benki Kuu Bw. J.R Angelo kupitia
dokezo sabili katika ukurasa (folio) 12 aliomba muongozo kutoka kwa Naibu
Gavana – FSD Bw. L.H Mkila na Mwanasheria wa Benki juu ya athari za kisheria
endapo Benki Kuu ingelipa fedha husika katika akaunti zilizobadilishwa.
Mwanasheria Bw. Mustafa Ismail alitoa muongozo juu ya
agizo la Mahakama la tarehe 5 Septemba 2013 linaloelekeza kuwa ‘all affairs of
IPTL should be handed over to PAP’ pamoja na stahili za IPTL katika akaunti ya
Escrow. Pia alibainisha kuwa maelekezo ya malipo (payment instructions) husika yametolewa na IPTL hivyo ni vyema
Benki Kuu ikafuata maelekezo ya

mwisho ya IPTL.”

Wadadisi tunashawishika kuona kuwa si
kwamba ndugu Angelo tu alitumia taaluma yake ya masuala ya kifedha kuhisi –
kama sio kubaini – kuwa kuna tatizo la kisheria katika kulipa fedha katika
akaunti zilizobadilishwa kivile, bali pia alihisi/alibaini kuna tatizo katika
kulipa fedha katika akaunti zilizofunguliwa ghafla kiasi hicho. Hapa uchambuzi
wa mwachano/mpishano wa tarehe nao ni muhimu sana. Ukurasa wa 14 wa Taarifa ya
CAG ambao inasemekana ni miongoni mwa kurasa zilizonyofolewa wakati kulipokuwa
na jaribio la kuivujisha Bungeni Dodoma unamalizia na aya hii: “Kwa mujibu wa
makubaliano ya kuhamisha fedha za Escrow yaliyoingiwa baina ya IPTL na Wizara
ya Nishati na Madini tarehe 21 Oktoba, 2013 ilikubalika kuwa malipo yafanyike
kupitia akaunti iliyoanishwa katika makubaliano hayo kama ifuatavyo:” Kisha
kabla ya kueleza jina la benki – “UBL Bank (Tanzania) Ltd” – na nambari mbili
za akaunti, ukurasa unaofuatia unamtaja “Mlipwaji” kuwa ni  “Independent Power Tanzania Limited (IPTL) C/o
Pan Africa Power Solutions (T) Limited.” Kwa nini mlipwaji ilikuwa awe na
“C/o”, yaani, ‘kupitia kwa’? Swali hili tutalijibu tutakapopitia ‘ufilisi’ na
‘uhuishaji’ wa IPTL.

Kwa sasa swali la kujiuliza ni kwa
nini, kwa mujibu wa Taarifa ya CAG, takribani mwezi mmoja baadaye, yaani, “Tarehe
25 Novemba, 2013 Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu kupitia barua Kumb Na.
NC.53/135/068/11/14 kwenda kwa Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL Bw. Harbinder Singh
Sethi aliomba Taarifa za kibenki za IPTL ili kufanya malipo ya fedha za
Escrow”? “Kupitia mahojiano,” CAG anatutaarifu, “Gavana Prof. Benno Ndulu alibainisha
kuwa Benki ilihitaji maelekezo ya mlipwaji ili kufanya malipo husika.”
Hivyo,  “Kwa mujibu barua ya tarehe 25
Novemba, 2013 Kumb Na. IPTL/BOT /001/2013 Mwenyekiti
Mtendaji wa IPTL Bw. Harbinder Singh Sethi alimuandikia Gavana wa Benki
Kuu akiomba kuilipa IPTL fedha kutoka akaunti ya Escrow kupitia
akaunti zilizoainishwa katika Makubaliano ya kuhamisha fedha baina ya Wizara na
IPTL ya tarehe 21 Oktoba, 2013 ambayo yaliwasilishwa kwake. Pia alithibitisha
kushiriki kikao cha tarehe 26 Novemba 2013 kilichoitishwa na Gavana.”

Sasa ikawaje tena siku tatu baadaye
yanatokea haya yafuatayo yaliyomfanya hata ndugu Angelo aonekane walau akiliishi
jina lake lenye maana ya ‘malaika’ kwa kuomba muongozo wa kisheria kutoka kwa
wenzake wa BOT: “Baada ya kupokea taarifa ya Stanbic tarehe 28 Novemba, 2013,
Bw. Harbinder Singh Sethi alimjulisha Gavana Prof. Benno Ndulu kuwa afanye malipo
husika kupitia akaunti za PAP…zilizofunguliwa tarehe 28 Novemba 2013”? Kwa nini
kwa ghafla hivyo hata jina la akaunti linabadilika na kuwa “Jina la akaunti Pan
Africa Power Solutions (T) Ltd”? Udhibiti ule ukalishindwa hili?

Chausiku aliyekuwa IPTL akawa PAP au IPTL
amekuwa huyo huyo PAP? Chaurembo – BOT – aliwezaje kumlipa ‘Chausiku II’ katika
mazingira hayo tata ya kibenki/kifedha hata kama Chaupele – TANESCO – hakuhoji
mabadiliko hayo ya ghafla? Iliwezekanaje?

Sasa tujikite tena kwenye suala la
‘uhai’ wa IPTL ili tuweze kujibu maswali hayo. Moja ya kurasa muhimu katika
hili ni ule ule wa 14 wa Taarifa ya CAG ambao unasemekana ulinyofolewa –
unasema yafuatayo mara tu baada ya kueleza kuwa “Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno
Ndulu kupitia barua Kumb. Na. AC. 53/195/01 tarehe 24 Oktoba, 2013 kwenda kwa
Katibu Mkuu Hazina, aliishauri Serikali kupata kinga kutoka IPTL dhidi ya madai
yanayoweza kujitokeza baada ya fedha katika akaunti ya Escrow kulipwa”: “Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini alimwandikia Bw. Habinder Sigh Sethi Mwenyekiti
na Mtendaji wa IPTL barua yenye Kumb. Na.SBD.88/147/01/4 ya tarehe 20 Septemba
2013 kumtaka kuthibitisha umiliki wake wa asilimia 70 na kutoa kinga kwa Serikali,
Benki Kuu na kwa TANESCO…. Kupitia kikao cha tarehe 8 Oktoba 2013 TANESCO na
IPTL walikaa na walikubaliana kuhusu madai ya IPTL kama ilivyonukuliwa hapa
chini….”

Madai hayo yaliyonukuliwa kwa
Kiingereza ni hayo hapo mbele yakimaanisha, kwa tafsiri yetu nyepesi ya kilei,
kuwa fedha katika akaunti ya Escrow zitolewe na kupewa IPTL haraka iwezekanavyo
ili IPTL ishughulikie masuala ya wadeni/wadai wake halali kwa mujibu wa
agizo/hukumu ya Mahakama Kuu (Mh. Utamwa J.) ya tarehe 5 Septemba 2013. Malipo
yote yaliyosalia yanayostahili kulipwa IPTL yalipwe kwa mujibu wa muda
uliopendekezwa humu hapo juu ili kuiwezesha IPTL kupanga upya majukumu yake
mengine: “Monies in the Escrow Account be
released to IPTL as soon as possible to enable IPTL sort out its legitimate
creditors as per the order of the High Court (Hon. Utamwa J.) dated 5
September, 2013. All other outstanding amounts payable to IPTL be paid in
accordance with the timelines proposed herein above to enable IPTL restructure
its other obligations
.”

Taarifa ya CAG inaendelea kwa kusema
hivi katika ukurasa huo: “Mnamo tarehe 27 Oktoba 2013, IPTL ilitoa hati ya
kinga dhidi ya madai yoyote yanayoweza kujitokeza kwa Serikali na Benki Kuu
kuhusiana na fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow mara baada ya fedha hizo
kulipwa kwa PAP. Hati hiyo ilisainiwa na Bw. Harbinder Singh Sethi Mwenyekiti
na Mtendaji Mkuu na kushuhudiwa na Bw. Joseph Makandege Katibu na Wakili Mkuu wa Kampuni ya
PTL.” Sasa hiyo kinga inatoka kwa IPTL au ya PAP ama kwa wote?

Hatuwezi kuhitimisha udadisi huu bila
kugusia kile tukionacho na wale tuwaonao kwenye suala la kodi. Kuna mstari
mwembamba kati ya kukwepa kodi (tax evasion) na kusamehewa kodi (tax exemption)
achilia mbali kudanganya kodi (tax fraud). Ukurasa wa 24 wa Taarifa ya CAG
ambao nao unasemekana ulinyofolewa ni somo tosha kuhusu mistari hii myembamba.
Tunaunukuu wote hapa na hitimisho lake lililopo Ukurasa wa 25 ambalo kwa kiasi
kikubwa ni muhtasari-hitimishi kuhusu kile kilichojiri katika Escrow:

“Katika kikao hicho [“cha dharura
tarehe 19 Septemba 2013”], Bodi ya TANESCO ilikubaliana na ushauri wa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali ulioitaka TANESCO na IPTL kukaa na kutatua madai yanayohusu akaunti
ya escrow na kubainisha kiasi kinachostahili kulipwa kwa pande husika. Baada ya
kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO Jenerali Mstaafu
Robert P. Mboma allmwandikia Katibu Mkuu wa Nishati na Madini barua…ya tarehe
19 Septemba 2013 akibainisha kuwa TANESCO itafuata maelekezo ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali na kwamba washirika wa akaunti ya Escrow watakaa kwa pamoja
kutatua mgororo wa tozo ya gharama za uwekezaji (Capacity charges) ili kubaini kiasi
kinachopaswa kurejeshwa TANESCO na kile kinichostahili kulipwa IPTL. Hivyo Bodi
ya Wakurugenzi ya TANESCO ilitoa mchanganuo wa madai yaliyopaswa kuhakikiwa
kwanza ndipo yalipwe kwa IPTL… Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini
kufuatia barua ya IPTL ya kudai kulipwa zaidi ya kiasi kilichokuwemo katika akaunti
ya escrow, alimjulisha Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Felchesmi Mramba
kuhusu madai ya IPTL kupilia barua…ya 9 Oktoba, 2013 na kuagiza TANESCO kufanya
kikao na IPTL ili kujadili madai hayo na kuwa uamuzi utakaotokana na majadiliano
hayo utasaidia utolewaji wa fedha katika akaunti ya Escrow….TANESCO na IPTL
walikaa katika kikao cha tarehe 8 Oktoba 2013 na kukubaliana kuhusu madai ya
IPTL ya USD 79,049,724.50… Katika kikao hicho TANESCO iliomba kuondolewa kwa
kiasi cha USD 33,564,004.53 ambacho kilikuwa ni riba na adhabu itokanayo na malimbikizo
ya tozo ya gharama za uwekezaji. IPTL ilikubaliana na ombi hilo endapo TRA
ingeisamehe kodi ya kiwango sawa na hicho. Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Jenerali
Mstaafu Robert Mboma kupitia Barua…ya tarehe 9 Oktoba 2013 aliijulisha Wizara
kuwa IPTL ingeidai TANESCO kiasi cha USD 45, 485, 719.97 (endapo TRA itasamehe
kodi kiasi cha USD 33, 564,004.53) ama USD 79,049,724.50 (endapo hakutakuwa na
msamaha wa kodi) zaidi ya kiasi kilichopo katika akaunti ya Escrow ya Tegeta….
Baada ya kupokea mapendekezo ya Bodi ya TANESCO kuwa fedha katika akaunti ya
Escrow zilipwe kwa IPTL, tarehe 21 Oktoba, 2013 Katibu Mkuu Wizara ya Nishati
na Madini Bw. Eliakim Maswi pamoja na Mwanasheria wa Wizara hiyo Bi. Salome
Makange kwa niaba ya Serikali waliingia makubaliano na Mwenyekiti na Mkurugenzi
Mtendaji Bw. Harbinder Singh Seth na Mwanasheria wa IPTL Bw. Joseph Makandege
juu ya utolewaji wa fedha katika akaunti ya Escrow (Agreement for delivery of
funds to Independent Power Tanzania Limited (IPTL)”

Kuhusu Mama Profesa wetu mpendwa
aliyetuongoza kwa ujasiri mkubwa katika harakati za Baraza la Wanawake (BAWATA)
dhidi ya ukiritimba wa dola hatuna mengi ya kudadisi zaidi ya kumnukuu tena
Nizar Visram: “Hawezi
waziri kuchota dola milioni moja kisha akasema amepewa zawadi au msaada wa
kirafiki au kibanadamu tu, hasa wakati waziri huyo ana dhamana ya kugawa
viwanja kwa wawekezaji.”

Msemo kuwa ‘kustaafu si kuchoka’ una
nafasi kubwa katika nchi yetu ambayo bado haijafanikiwa kuwaandaa watu wengi wa
kutosha kuchukua nafasi za wastaafu wenye utaalamu adimu. Lakini pamoja na
kuwaenzi na kuwaheshimu wastaafu wetu, wakiwemo wale walioonyesha ujasiri
mkubwa kwa kumng’oa Nduli Idi Amin aliyeivamia nchi yetu, kwa kuhakikisha
wanapata shughuli ya kufanya uzeeni yasitufanye tufumbie macho kile ambacho
wadadisi tunakiitadhana
ya mgogoro wa kimaslahi katika mapana yake
. Hili linawahusu pia watumishi
wa umma na wanasiasa wakiwamo wale ambao wanaona wanaweza kuchanganya biashara
na siasa na kuwa waadilifu badala ya mafisadi. Ni vigumu sana kutogonganisha
maslahi, hata mtu uwe na nia njema kiasi gani, ukiwa kwenye wa bodi ya
ukurugenzi wa shirika la umma na wakati huo huo upo kwenye bodi ya ukurugenzi
wa kampuni binafsi kama mabenki na mashule huria hasa kunapokuwa na miingiliano
ya uwekezaji kama iliyopo nchini. Ni heri tuwe kumoja – umma au binafsi.

Haya ndiyo tunayoyaona na hao ndio
tunaowaona kwenye Taarifa ya CAG. Ni masuala na maswali yanayoumiza kichwa na
yanayoutesa moyo. Ndio maana wadadisi wengi wa wawekezaji wanaogopa kufa kihoro
au kifisadi. Unaoitwa ujasiri wa ufisadi una(tu)tisha.

Nani atatuokoa? Kuna mwenye ujasiri wa
uwanamapinduzi? Yupo wa kujitoa mhanga?