Nimepumzisha kalamu yangu kwa muda. Nina sababu lukuki kwa nini sijaandika makala muda mrefu. Hata hivyo, haya si ya kusimulia wakati huu. Kwa muda sasa huwa ninaazimia kuchangia masuala kadhaa yenye umuhimu mkubwa kwa hatima yetu kama watu na kama nchi.

Kwa vile tunaelekea kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mnamo tarehe 8 Machi nimeona haja ya kumulika machache kuhusu utata wa mada ya usawa na usawia wa kijinsia. Hivyo, niweke wazi hamu yangu kuwa makala hizi zitasomwa kwa chachu na uwazi, kwa hamu ya ‘kuuona’ upande wa pili, kwa kutafakari na kwa kujihoji badala ya kawaida yetu ya kulumbana na kubeza.

Wengi wetu hutambua mambo kwa mujibu wa “utambuzi wetu wa dunia” ama worldview. Hii huhabarishwa (na huhabarisha) na imani zetu, mirengo yetu; upeo wetu na hata unyofu au ugando wetu kimtizamo. Kwa miaka mingi nimekuwa katika harakati za kutetea utamaduni na utawala wa haki, usawa na uwajibikaji. Nimeingia na kudumu katika harakati hizi kwa vile ninaamini katika utu na utukufu wa mwanahawa na mwanadamu popote alipo, vyovyote alivyo.

Kama wanaharakati wengi waliotutangulia, nimebaini kuwa masuala ya haki, usawa, uwajibikaji, heshima na hisani si mepesi. Hugubikwa na jinsi tunavyofahamu, kuzingatia na kuamini suala la uhuru, haki, stahili na utu. Nikiwa mfuasi wa umajumui na harakati za ukombozi na mageuzi nimebaini muda mrefu kuwa wengi wa viongozi vinara wa harakati hizi ingawa waliamini kila mmoja kwa namna yake suala la ukombozi, wengi hawajaunga mkono moja kwa moja au kuendeleza harakati za usawa kwa upana wake.

Inawezekana walizungumzia suala la usawa wa fursa za kisiasa, kiuchumi, na kijamii lakini mara nyingi walikuwa hawatizami kuwa jinsi ya kike inastahili kile walichokuwa wakipigania. Uhuru, haki, stahili na utu waliokuwa wakiupigania wakiamini unawahusu jinsi ya kiume tu kwani kamwe dhana yao ilikuwa sio kuufumua mfumo kandamizi kwa mtindo wa kimageuzi bali walitaka kubadilishwa sura ya nani anafaidi mfumo kandamizi. Badala ya kutawaliwa na wanaume wazungu tu, au waarabu   au wahindi tu au wageni tu walitaka wanaume wenyeji wapate fursa hizo, sio raia wa jinsi nyingine.

Msimamo huu ndio uliosababisha harakati nyingi za viongozi kutothamini michango ya wanawake. Hivyo, historia nyingi ya harakati zinakosa kumbukumbu za michango ya hali na mali ya wanawake. Vitabu vingi haviwataji hao wanawake.

Mifumo mingi ya vyama na juhudi za harakati nazo hazijakuwa na juhudi za kweli kujumuisha wanawake katika uongozi wake. Badala yake wanawake wameendelea kutengewa vitengo au jumuiya ambazo hutumika kuendeleza ubaguzi, unyanyapaa na unyanyasaji uliopo wa kijinsia. Baadhi ya mifumo hii ikiakisi mahusiano ya kaya na si ya weledi au harakati. Ndiyo maana wanamapinduzi kama Biubwa Amour Zahor walitegemewa kupika chai wakati wale ambao walikuwa hawana uzoefu kama wake wakikalia viti vikubwa na kumpimia au kumuamulia rizki yake.

Kwa muda mrefu nikitatizwa na kinachosababisha mtu anayejiita mwanamapinduzi au mwanaharakati au muumini au mpenda maendeleo kupinga mtu mwingine kupata au kufaidi kile anacholingania nafsi yake kwa sababu tu yu jinsi ya kike! Au kwa sababu tu ni mtoto! Au kwa vile tu ni mtu mwenye ulemavu!

Kinachosikitisha zaidi ni zile sababu zinazotumika kuhalalisha dhulma hii dhidi ya wengine ikiwemo mila na desturi, mapokeo ya kiimani na hata sayansi! Nitajadili taathira ya hali hii katika makala zangu zijazo. Kwa leo nataka kuishia na chimbuko la mitizamo hasi dhidi ya jinsi ya kike.

Muda mwingine unaumiza kichwa kujaribu kufahamu mambo ambayo kwa wengine wanaweza kuona jibu lake ni rahisi. Jana nilikuwa bandarini ninaongea na msukuma mkokoteni baada ya vijana kadhaa wa bodaboda kunizonga na kunisakama na ofa za “boda boda!” Mwanzo nilinyamaza lakini walipozidi kunizonga nikawauliza, “umri huu nikitaka kitu sijui kusema?”

Kumbe jibu langu lilimgusa yule msukuma mkokoteni. Yeye aliona vijana wana kila haki ya kuniuliza. Temna hata kama ni mara khamsini.

Nilishangazwa sana na jibu lake nikataka kujua zaidi. Akaniambia kuwa mimi sijui wala sifahamu nini ninahitaji hivyo lazima vijana wanisaidie kujua nini shida yangu. Nikamuuliza mbona watu wengi walikuwa wamekaa hapo (na wengi walikuwa wanaume) hawafuatwi au kuulizwa tena kwa bughdha kama nilivyofanyiwa mimi?

Jibu la mwendesha mkokoteni huyo ndilo lililonimaliza. Akasema kuwa “Wewe ni mwanamke na mwanamke siku zote ni mtu wa kuambiwa tu!” Kwa ufafanuzi na uzoefu, waliokuwa wananighasi ni vijana ambao ninawazaa na hata kuwajukuu. Hakuna hata mmoja niliyemuaga nilipotoka kwangu au niliyemshirikisha katika mipango yangu pale bandarini.

Hata hivyo, kuna watu katika jamii wanaona wana haki ya kuingilia uhuru wangu, maamuzi yangu na maisha yangu, tena kwa mabavu, kwa sababu tu wanaamini kwa vile wao ni wanaume basi mimi sio lolote mbele yao hata kama nimewazaa na kuwalea; au nimewaajiri; au ni raia mwenye hali na hadhi kikatiba kama wao.

Mitizamo hiyo imetamalaki karne hii ya 21 tena si kwa watu wa makamo tu, lakini pia miongoni mwa vijana. Ni mitizamo inayokwamisha jitihada zozote za kufanya marekebisho au kuleta mageuzi ya kifikra, mwenendo au mifumo. Ni fikra zinazokinzana na dhana ya usawa, utu, ubinadamu, ihsani au Ubuntu.

Kwa bahati mbaya ni mitizamo inayowakabili wanawake wengi kila siku, kila saa, kila dakika wanapotaka kudai na kufaidi uraia wao, utu wao na uhuru wao. Ni mitizamo ambayo kwa muda mrefu imekumbatiwa, imechimbiwa na kuenezwa bila ya kuhojiwa. Na ni mtizamo inayoendelea kunyima Watanzania wote, wa kike na kiume, wadogo kwa wakubwa, wenye ulemavu na wasio na ulemavu upeo wa fikra, uwezo wa kujali (empathy) utu, ubinadamu na uzalendo.