Hayawi hayawi sasa yamekuwa. Kwa mara ya tatu bila upatu wala utata, hatimaye Lula Inàcio da Silva ameibuka mshindi kwenye kinyang’anyiro cha urais nchini Brazil. Uchaguzi huo ulifanyika nchini humo tarehe 2 mwezi Oktoba 2022 na kurudiwa tarehe 30 ya mwezi huo.

Brazil ni nchi kubwa kwa uchumi na kijiografia katika bara la Amerika Kusini na Latini Amerika. Kwa sensa, ina idadi ya watu zaidi ya milioni 217 na Pato la Taifa la wastani wa Dola za Kimarekani trilioni 1.833. Mwaka huu imesherehekea kihekaheka miaka 200 ya uhuru kutoka kwa Wareno (1822-2022).

Ni nchi ambayo kwa utajiri wake wa kitamaduni, maliasili na mapinduzi yake kiuchumi imekuwa ni mfano wa kuigwa hasa kutoka nchi za dunia ya tatu, na Afrika kiupekee zaidi. Kwa sababu hiyo, matukio ya kisiasa kama uchaguzi wa Rais mwaka huu umetiliwa na kufuatiliwa kwa uzito mkubwa duniani. Sasa ni dhahiri kwamba ushindi wa Lula unafanya bara la Amerika Kusini kuongozwa zaidi na Serikali za itikadi za mrengo wa kushoto.

Ama kweli, ulikuwa ni ushindani wa kukata na shoka. Lula ameongoza kwa asilimia 50.9 na Jair Bolsonaro kwa asilimia 49.1. Mathalani, Bolsonaro anaingia katika historia ya kisiasa ya Brazil kama Rais pekee aliyeshindwa kuchaguliwa (licha ya kutumia vyombo vya dola na mali za umma kwenye kampeni za uchaguzi) kwa muhula wa pili.

Rais Mteule Lula mwenyewe amesema kuwa huu sio ushindi binafsi na chama chake tu, bali ni ushindi wa demokrasia na haki jamii dhidi ya udikteta. Ni ushindi wa wanaharakati wa mazingira hasa ya Amazonia. Ni ushindi kwa watu weusi na watu wa asili (kama vile wamaasai wetu), ambao ndio waathirika zaidi wa sera za kibeberu za Bolsonaro. Sera za ukoloni wa ndani kama wasemavyo wanasosholojia—kuchukua ardhi kwa mabavu, kuwataka watu wa asili wachukie dini zao, wajikatae na waachane na mfumo wa maisha yao.

Lakini, ni lipi funzo muhimu, kama lipo na kama tunataka, Watanzania tunaweza kujifunza kutoka Brazil hasa kwenye suala nzima la kuendesha demokrasia ya vyama vingi? Na zaidi, ni fursa zipi zinafunguka kwa bara la Afrika kutokana na huu ushindi wa Lula? Haya ni baadhi ya maswali na masuala ambayo makala haya yatajaribu kuyajibu.

Brazil chini ya Utawala wa Bolsonaro
Itakumbukwa kuwa Jair Bolsonaro, wa mrengo-mkali wa kulia, na rafiki wa karibu wa Donald Trump, alichaguliwa kuwa Raisi mwaka 2018 kwa ushindi wa asilimia 55 dhini ya Fernando Haddad, wa chama kimoja na Lula aliyepata asilimia 45. Na wadau wa siasa wanasema kwamba Bolsonaro alishinda hivyo kwa kishindo kwa sababu tu Lula alifungwa makusudi ili kumdhoofisha kisiasa. Na Lula, licha ya uwezo, nyenzo na kupewa mwaliko wa hifadhi nje ya nchi, alikataa na kukubali kifungo kwa kashfa za rushwa kipindi cha Serikali yake.

Mungu si Athumani, baadaye mnamo mwaka 2019 Mahakama Kuu ya Brazil ilikaa tena na kupitia tena hukumu na mchakato mzima wa kifungo chake. Bila ajizi ilitanabaisha mapungufu makubwa ya hukumu na hivyo kumuachia huru na kuruhusiwa kugombea tena. Kwa kiasi fulani historia ya Lula inafanana na kufaana na hayati Nelson Mandela.

Nchi ya Brazil kipindi cha Lula ilifika mbali na kusifika kama mfano katika kuzalisha chanjo, katika kutokomeza njaa, na kuwekeza kwenye elimu na teknolojia. Chini ya Bolsonaro, Brazil ilirudi nyuma na kuyumba sio tu kidemokrasia bali, na mbaya zaidi, kwenye huduma za jamii, haki za kinadamu na mazingira pamoja na uhusiano wa kimataifa kuzorota kwani kwa kiasi kikubwa alijikita kwenye dhana zinazopinga masuala hayo.

Kiuhalisia, Bolsonario aliibuka kama mtu asiye sehemu ya kundi la ndani kabisa kwenye siasa, pamoja na kuwa mbunge kwa miaka 28 huko Rio de Janeiro. Aliibuka kama moto wa mabua na kuwa maarufu kupitia mitandao ya kijamii akinadi ahadi hewa kama uzalendo, mtetezi wa familia, mcha Mungu na mpingaji wa utoaji mimba, ndoa za jinsi(a) moja na dawa za kulevya. Na mbaya zaidi alitumia hizo ajenda ili kujinufaisha tu kisiasa.

Mathalan, kipindi janga la UVIKO-19 lilipokuwa limepamba moto, Bolsonaro alipinga na kuchelewesha kwa makusudi chanjo kwa wananchi. Hali ilikuwa tete mpaka pale taasisi kama Kanisa hasa la Katoliki na Mahakama Kuu zilipoingilia kati na kutetea sayansi. Isingekuwa uimara wa taasisi na ukomavu wa asasi za kiraia, basi Bolsonaro angeweza kubadilisha Katiba na kuhalalisha udikteta ambao Brazil ilipitia miaka ya 1964 hadi 1985.

Tofauti na Bolsonaro, uhusiano kati ya Brazil na Afrika chini ya Raisi Lula sio tu uliimarika bali ulipewa umuhimu unaostahili. Kwa mfano, kipindi cha Lula, balozi za Brazil hapa Afrika ziliongezeka kutoka 17 hadi 37 hapo mwaka 2010. Lakini kwenye utawala wa Bolsonaro uliipa Afrika kisogo na kisigino. Ni kweli, Bolsonaro ameshindwa huu uchaguzi, lakini hilo halitoshi. Kazi zaidi ya vuguvugu na utoaji wa elimu ya kiraia na kuimarisha sheria za utawala bora zinahitajika. Kama vile kwetu Tanzania kuna mwenendo na muendelezo wa Umagufuli bila Magufuli, pia hapa Brazil bado kuna dhana ya Ubolsonaro. Upo wa hali na mali tena ni wa hali ya juu sana.

Ndio sababu, mpaka naandika haya makala Rais Bolsonaro bado hajamtambua Lula kama mshindi na zaidi anachochea maandamano nchi nzima. Atashindwa tu! Kiufupi, Bolsonaro anahaha sio tu kwa kushindwa, bali na kwa hofu ya uwezekano wa kufunguliwa mashtaka siku za usoni.

Ubolsonaro wa hao waandamanaji umekuwa kama udini. Ni kama ugonjwa fulani wa kupumbaa kihalaiki na kiakili. Kinachotokea ni mashabiki wa Bolsonaro kuabudu/kumezeshwa na kufuata mtu/dhana/miungu fulani ‘kizezeta’ tu bila chembe wala cheche za udadisi wowote.

Ni lipi funzo Watanzania tunaweza kujifunza kutoka Brazil?
Mosi, ni utamaduni wa uwazi wa hali ya juu—siyo tu kwenye uchaguzi. Sitaki nifanye mlinganisho wa Tanzania na Brazil. Lakini hapa Brazil ni vigumu sana kuona watu wanapita barabarani wakati taa nyekundu bado inawaka hata kama hakuna gari linapita.

Nipo hapa Brazil kwa miaka nane sasa. Ukiingia kwenye mabasi ya mwendokasi ambayo hayana konda wa kudai nauli ni vigumu sana kuona watu wanatumia huo usafiri bila kulipa. Kwanza wanajisikia aibu kutumia mali za umma bila kulipa wala kutunza. Ndiyo kusema wana uwajibikaji, uadilifu, na utii wa sheria bila shuruti wa jumla wa kijamii wa hali ya juu. Tujifunze na kufundwa!

Watanzania tunaweza kujifunza uwazi hasa kwenye siasa. Katika sayansi ya siasa, kutengeneza imani na uaminifu kati ya wananchi na viongozi ni tunu muhimu sana. Sisi sote tu mashahidi kuwa hizi tunu zimeshuka sana miongoni mwetu.

Ndiyo maana kwenye chaguzi zetu nyingi, ni vurugu, woga na mabavu sana bila aibu wala tabu. Tume na taasisi zetu za uchaguzi hazipo huru. Taasisi na tume za uchaguzi hapa Brazil zimeendesha zoezi kwa umakini na utulivu mkubwa hata pale Bolsonaro na chama chake waliponena na kueneza Taarifa potofu kwamba vifaa vya kuhesabia kura kielektroniki vina mapungufu.

Funzo la pili ni muamko na vuguvugu la wananchi katika kupigania haki na wajibu wao. Wabrazil wana mwamko na uelewa mpaa sana kuhusu haki zao kama raia. Ndiyo maana hata maandamano ya sasa yanaruhusiwa na polisi wana wajibu wa kuwalinda waandamanaji.

Kwa mfano, hapa São Paulo mikutano ya hadhara inachochewa ifanyike na kuruhusiwa kisheria na kikatiba. Mikutano haitegemei wala kuegemea kauli/hisani au amri ya Rais au kikosikazi fulani. Ni muhimu Watanzania kuelewa hili kwamba hizi haki huwezi kupewa bure, bali ni kujielimisha na kuzipigania.

Nchi ni ya wananchi. Kamwe tusiachie hatma ya nchi kwa chama fulani pekee. Na furaha ya vyama vyetu hivi tawala ni kuona wananchi tunaipa kisogo siasa. Kwa hiyo, tunahitaji kwa tija na hija, huo uwajibikaji na utambuzi wa pamoja, sio tu katika madai ya Katiba mpya na sheria nzuri bali zaidi katika kuhudumiwa vizuri na Serikali tuliyoiajiri kwa kura na kodi/tozo zetu.

Umoja wa vyama vya siasa na asasi mbalimbali katika kutetea demokrasia ni funzo-gumzo lingine. Katika hotuba yake ya kwanza baada ya ushindi, Lula alianza kwa kuushukuru ushirikiano na mshikamano wa vyama vya siasa vilivyomuunga mkono. Ieleweke na tujifunze kwamba hivi vyama na asasi havikufunga ndoa ili tu kushinda uchaguzi, bali viliungana kwa lengo pana zaidi la kutetea demokrasia na utawala bora.

Vyama tawala vingi hasa Afrika vina tabia ya kuzorotesha umoja wa vyama vya upinzani. Vyama vya upinzani vinanunulika na vinaishia kugombana vyenyewe badala ya kukabiliana na adui wa kweli. Adui huyo ni matatizo halisi ya wananchi yanayohitaji sera mbadala.

Hapa Brazil vyama vya upinzani kama PT, MDB, PSDB, na PSOL viliungana siyo tu kwenye uchaguzi bali pia huko Bungeni siku za usoni katika kulinda haki za binadamu na demokrasia. Lazima vyama viaminiane, vigawane mbinu mseto, na vifanye siasa za ushindani. Ni muhimu kuonesha ukomavu wa kisiasa.

Hitimisho
Lula ameshinda uchaguzi, sawa na Haleluya! Ila kuongoza nchi kama Brazil ni suala jingine. Anahitaji timu nzuri ya kidiplomasia, viongozi weledi na wenye maono, pamoja na mshikamano wa kitaifa.

Katika muktadha huu, Lula na vyama shirikishi wana wajibu mkubwa zaidi kudhihirisha kwa matendo nia njema ya kuleta maendeleo kwa Wabrazil wote. Historia inatufundisha kwamba mapambano ya kupigania haki kule kwenye ukandamizaji hayaepukiki. Pia inatukumbusha kuwa watawala wanaotawala kwa mkono wa chuma hawawezi kudumu milele.

Viva o povo brasileiro!