Utangulizi
Kitabu cha Biubwa Amour Zahor: Mwanamke Mwanamapinduzi kimeandikwa na Zuhura Yunus, mwandishi wa habari na mtangazaji wa kimataifa katika Shirika a Utangazaji BBC. Kimechapishwa na E&D Vision Publishing Limited, Dar es Salaam mwaka 2021.
Anwani/Jina
Mwandishi Zuhura Yunus amekipa kitabu chake jina/anwani “Biubwa Amour Zahor: Mwanamke Mwanamapinduzi.” Anwani hii inachukua mfumo wa wasifu (biography) yamkini kumuelezea Biubwa na maisha yake na ushiriki katika Mapinduzi ya Zanzibar, 1964. Kiambatanishi katika anwani hii yaani Mwanamke Mwanamapinduzi kinajaribu kutoa taswira ya maudhui mapana ya mwandishi ikiwa, mosi, ni sehemu ya mwanamke katika historia ya Zanzibar na, pili, ushiriki wa kipekee wa Biubwa katika Mapinduzi ya Zanzibar. Anwani hii imelenga kututanabaisha mchango wa Biubwa, kama mwanamke katika harakati na hasa mchango wake, dhoruba mbalimbali katika maisha yake pamoja na ushiriki wake kwenye Mapinduzi.
Jalada
Jalada la mbele la kitabu hiki lina picha ya Biubwa katika mfumo wa vintage, Biubwa katika ujana wake. Katika picha hii, sura ya Biubwa inaashiria mwanamke mrembo, mkakamavu na jasiri. Weupe wake na nywele ndefu zinaweza kukueleza japo kwa kidogo asili na utambulisho wake. Picha ya namna hiyo pia iko kwenye jalada la nyuma lakini ni ya kuchora na imechorwa na mchoraji maarufu, Mohammed Raza.
Dhamira ya mwandishi
Katika maelezo yake katika kurasa za shukrani, mwandishi anaandika kwamba dhamira yake kuu ni kuwaasa Waafrika kuandika historia zao wenyewe na kuondokana na kadhia ya waandishi wa nchi za Magharibi kutuandikia historia yetu. Pili, mwandishi anakiri kwamba dhamira yake ilikuwa kutaka kuandika na kutuelezea sehemu ya mwanamke katika historia za kitaifa (national histories). Aghalabu, kufasiri sehemu ya mwanamke katika michango mbalimbali katika historia ikizingatiwa historia imehodhiwa na sauti ya wanaume (uk. viii). Naye Biubwa katika usuli anakiri hili:
Siku zote zikiandikwa siasa za nchi zetu huelezwa wanaume tu; michango ya wanawake mara nyingi husauliwa. Lakini baadhi yetu tumechangia na tumeona mengi ya historia ya nchi yetu (uk. xiii).
Mathalan, dhamira kuu ya mwandishi ni mchango wa Biubwa katika historia ya Zanzibar. Mwandishi amefanikiwa katika kuulezea mchango wa Biubwa, ambao kwa kiasi kikubwa ni mchango wa akina mama katika historia ya Zanzibar.
Mandhari
Mwandishi wa kitabu hiki anatupeleka katika mazingira ya Zanzibar ya kabla, wakati na baada ya Mapinduzi ya 1964. Tunafahamu sehemu ya Mapinduzi ya 1964 katika historia ya Zanzibar. Matukio ya Jumapili tarehe 12 Januari 1964 yalibadilisha mandhari ya siasa ya Zanzibar kabisa. Kitabu hiki kimejikita katika muktadha wa Mapinduzi ya 1964 yaani, kabla, wakati na baada ya Mapinduzi yale.
Ploti (Mtiririko wa kitabu)
Kitabu hiki kimegawanywa katika sura kumi na saba (17). Kitabu kinaanza na Kitahanani vita vya Juni, 1961 – uchaguzi ambao ulibaini mpasuko wa kitabaka na utaifa ndani ya Zanzibar. Mwandishi Jonathon Glassman kwenye kazi yake War of Words, War of Stones: Racial Thought and Violence in Colonial Zanzibar, anaelezea chimbuko la utaifa (nationalism) wakati wa Zama za Siasa (Period of Politics), 1957-1963. Glassman anaelezea tofauti za kirangi/ukabila (racial differences) na namna zilivyozaa mgawanyiko baina ya Waarabu na Waafrika na jinsi dhana hii ilizaa ubaguzi Zanzibar.
Naye mwandishi anaelezea muktadha huu katika utangulizi wa kitabu chake kama mwanzo wa kumtambulisha Biubwa. Mgawanyo wa Uarabu na Uafrika ulidhihirika katika vyama vya Zanzibar Nationalist Party (ZNP) au Hizbu, chama cha Waarabu, Afro-Shirazi Party (ASP), chama cha Waafrika na Washirazi, pamoja na Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP). Uchaguzi wa Juni, 1961 ulianikiza tofauti za kikabila/kitabaka ambazo zilimkumba Biubwa, mwanamke Mwarabu aliyekubali kuolewa na Mwafrika (Dk. Kingwaba Hassan).
Mwandishi anayasimulia maisha ya Biubwa katika muktadha huu wa kibaguzi. Ghasia za baada ya uchaguzi wa Juni 1961 pia ni kiashirio cha maandalizi ya Mapinduzi ya 1964. Mwandishi anaelezea Taharuki ya Mapinduzi (sura ya pili). Na utata wa dhana nzima ya kumbukizi ya Mapinduzi (Memory of the Revolution) inajitokeza katika sura hii pamoja na sura nyingine za kitabu.
Sifa za ujasiri na uhodari wa Biubwa zinaelezewa vema katika sura ya Binti wa Kizanzibari. Mwandishi anatupa utambulisho wa Biubwa kuanzia asili yake, maisha ya skuli na mwanzo wa ndoa yake tata. Katika sura hii, tunapata historia ya Zanzibar, historia ya miundombinu ya Zanzibar (kama kuanzishwa kwa garimoshi la kwanza Afrika Mashariki), pamoja na historia ya majengo kadha wa kadha. Mwandishi pia anatukumbusha historia fupi ya baadhi ya majina ya maeneo mbali mbali Zanzibar (k.m Kwa Haji Tumbo).
Simulizi ya ndoa tata ya Biubwa inaelezewa kama wasifu wa uhodari wake. Uhusiano wake wa kimapenzi na Mwingereza Herbert Fawcett unaelezea uhodari wa Biubwa hata katika zama ambazo mahusiano ya namna hivo hayakuwa dhahiri. Kama mwandishi anavyoeleza, Biubwa alilenga sana Uzanzibari na si ukabila (uk.92).
Kunusurika kubakwa
Biubwa anaelezea mkasa wake aliponusurika kubakwa, zahma iliyotokea mwaka 1958. Katika kisa hiki, Biubwa hakusita kuzungumza. Kuielezea dhulma hii hadharani, kunashadidia uhodari wake. Licha ya mhusika wa jaribio lile kuwa mtu mashuhuri, Biubwa alipaza sauti.
Biubwa wa kimataifa pia anasimuliwa katika kitabu hichi hasa ziara yake ile ya Uchina alipokwenda pamoja na wenzake kupata mafunzo ya kisiasa pamoja na stadi za ufundi. Sekeseke la Abdulrahman Babu na ukaribu wa Biubwa na Bi Ashura Babu unaelezea sifa ya uwanaharakati aliokuwa nao Biubwa.
Utata wa madai ya Biubwa kumuua baba yake unaelezewa na mwandishi pamoja na majibu ya Biubwa. Utata huu umetawala pakubwa maisha ya Biubwa. Maelezeo haya kwa baadhi ya wadau wa siasa za Zanzibar ni Biubwa kutaka kujisafisha kutokana na uhusishwaji wake kwenye mauaji wa baba yake.
Mambo ibuka katika kitabu
Kumbukizi ya Mapinduzi (Memory of the Revolution)
Wasomi wa anthrolopojia wa kijamii (social anthropologists) wametafiti dhana ya kumbukizi (memory) na uhusiano wake katika kuelezea historia. Uelezaji wa Mapinduzi umekua dhana tata katika kuelewa dhima na sababu ya Mapinduzi. Kitabu hiki kinachangia katika kuendeleza uelewa wa kumbukizi ya Mapinduzi hasa mchango wa kumbukizi binafsi (individual memory) tofauti na kumbukizi ya jumla (collective memory).
Harith Ghassany mwandishi wa Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia ameandika juu ya kumbukizi mbadala ya Mapinduzi (reinterpreting the revolution). Ghassany anatoa simulizi tofauti (competing narrative) ya Mapinduzi ili kuelezea kuhodhi wa simulizi kuu (hegemonic narratives) kuhusu Mapinduzi. Maelezo ya Biubwa yanachangia katika kuelewa yaliyojiri katika Mapinduzi kupitia kumbukizi binafsi (individual remembering). Katika sura ya kumi na moja juu ya simulizi ya Biubwa na baba yake, mwandishi anaishadadia dhana hii ya kumbukizi ya Mapinduzi:
Jambo moja ambalo linakubaliwa na pande zote kwa wanaozungumzia historia ya Zanzibar ni kwamba Mapinduzi hayakufanywa na Umma Party wala ASP lakini vyama vivyo vilishiriki kwa namna moja au nyingine baada tu ya Mapinduzi. (uk. 132)
Utata wa ‘kupotea’ na vifo vya watu kadhaa maarufu kama akina Abdulaziz Twala, Muhammed Salim Baruani, Abdallah Kassim Hanga, Saleh Sadallah, Mdungi Ussi na wengine kunaelezea dhana ya kumbukizi ya mapinduzi (memory of the revolution).
Kumbukizi ya Mauaji ya Karume
Kumbukizi ya tukio la kuawawa kwa Rais Abeid Amani Karume tarehe 7 April 1972 pia linaelezea ukinzani wa historia ya Zanzibar. Mwandishi anatuleta kumbukizi ya tukio hilo kwa mtazamo wa Biubwa. Kukamatwa kwa Biubwa na kutiwa gerezani kunaonesha jinsi tukio la mauji wa Karume lilivyochangia kuendelezwa kwa utawala wa kiimla Zanzibar.
Uhodari wa Mwanamke
Sehemu ya mwanamke katika historia ya Kitanzania na Kizanzibari inaonekana vema katika maisha ya Biubwa. Kutunukiwa kwa nishani ya uwanamapinduzi na Rais Ali Mohamed Shein mwaka 2019 kunasimika mchango wa Biubwa katika historia ya Zanzibari.
Hitimisho
Mwandishi Zuhura Yunus, kama alivyoelezea Rais Mstaafu Jakaya Kikwete katika maelezo ya kitabu, amempa Biubwa nafasi yake stahiki katika historia ya Zanzibar. Kwa kutumia lugha ya taifa ya Kiswahili, kitabu hiki kinachangia katika kuifahamu historia tata (contested history) ya Zanzibar na zaidi kumuenzi mwanamke hodari katika historia hii. Minghairi ya haya, kitabu hiki kinaibua hisia za uchungu na utata wa historia ya Zanzibar.
Hata hivyo, kitabu hiki kinachangia katika kuelewa historia hii tata.
Kitabu kwa Dar es salaam kinapatikana wapi? na kinauzwa tsh ngapi, maudhui yake ni mazuri katika utambuzi chanya wa kifikra kwa kufahamu nafasi ya mwanamke katika jamii.
TPH bookshop, Samora Avenue na maduka mengine yaliyotajwa kwenye tweets
hizi tatu hapo chini:
https://twitter.com/venusnyota/status/1458905957547847682?s=21
https://twitter.com/venusnyota/status/1458651060160110592?s=21
https://twitter.com/venusnyota/status/1460104434906812416?s=21