Ufuatao ni uhakiki mahsusi uliotolewa Zanzibar na Salma Maoulidi wakati wa uzinduzi wa kitabu cha ‘Mwanamke Mwanamapinduzi: Biubwa Amour Zahor’ kilichoandikwa na Zuhura Yunus
Heko!
Ninaamini wapo waliostahili heshima ya kuhakiki wasifu wa Bi. Biubwa Amour Zahor hii zaidi ya mimi kutokana na ukaribu walionao na mhusika mkuu wa kitabu; ama kutokana na upeo wao juu ya zama za na maudhui ya kitabu hiki. Huenda pia kutakiwa mimi kuhakiki andiko hili ikawa barka kwa vile itawezesha kupatikana kwa uchambuzi ambao haufungamani na mitizamo au ‘uwenyeji’ wa hao wandani wake.
Kuchapishwa kwa kitabu hiki ni jambo la kujivunia kwa jamii ya jinsi ya kike Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, bila kujali itikadi zao kisiasa au nasaba zao. Mhusika Mkuu anastahili heko kwa kuridhia kusimulia sehemu ngumu ya maisha yake na hususan juu ya ushiriki wake katika tukio na kipindi tata cha historia ya Zanzibar, yaani harakati nzima zilizosababisha Mapinduzi ya mwaka 1964.
Kwa muda mrefu kumefanyika jitihada kadhaa kumshawishi Bi. Biubwa Amour Zahor, pamoja na wanawake wengine, kusimulia na kuandika juu ya maisha yao ili kunawirisha mseto wa simulizi zilizotamalaki juu ya harakati za uhuru wa Zanzibar.[1] Bila ya shaka Zuhura Yunus amefanikiwa kumlainisha mmoja wa wanawake mashuhuri katika medani za harakati za kisiasa Zanzibar zama za kudai uhuru.
Ni mara chache mwana wa Zanzibar anamulikwa; ana fursa ya kupaza sauti yake; ana mamlaka kamili juu ya dokezo la kudhihirisha na kiasi cha kufichua uhondo wake; anasimulia ukweli wake; na anatandika dhamira yake. Ni nadra zaidi kupata andiko ambalo si la kisomi lenye kuibua na kuzingatia masuala ya kijinsia. Basi, faida kuu ya kitabu hiki iwe kupanua simulizi hai za historia ya Zanzibar sambamba na kushamirisha mijadala ya kitaaluma na kijamii kuhusu urathi wetu!
Upekee na Unyeti wa Kitabu cha Mwanamke Mwanamapinduzi: Biubwa Amour Zahor
Hakuna simulizi kuu au muhimu kuliko nyingine, simulizi sahihi au potofu inayohusu uzoefu wa mtu. Mtu ana haki ya kuwa na hisia zake, kuwa na maoni yake na kumbukumbu zake. Huu ni wasifu na kwa bahati ni wa mtu ambaye wasifu wake unaandikwa katika uhai wake. Takriban miaka 60 imepita toka tukio la Juni 1961 lilofungua kitabu.
Siasa za Zanzibar na hususan tukio la Mapinduzi ya mwaka 1964 ni mada inayowavutia wengi waliomo Zanzibar na walio nje ya Zanzibar. Mapinduzi ni alama kuu ya siasa za Zanzibar. Ndio kiini na kina; ndio mwanzo na mwisho wa kila kinachoandikwa juu ya Zanzibar. Kabla kitabu cha Mwanamke Mwanamapinduzi: Biubwa Amour Zahor, vitabu juu ya wanamapinduzi viliwahusu wanasiasa au wanaharakati wa jinsi ya kiume tu.[2] Maisha ya kisiasa na kijamii kwa muda mrefu yaliandaliwa na kusimuliwa kwa mtizamo mkavu na mgando wa kijinsia ambapo aliyeonekana na kutikisa ni ‘mwanamume’ aliyekidhi vigezo vyote vikuu vya ulwa; aliyekidhi sifa za kulinganishwa kwenye mizania ya mfumo kandamizi uliokuwa unagombaniwa.[3]
Kamwe wanawake hawajawahi kuandikwa au hata kutajwa kana kwamba walikuwa hawapo kipindi hicho muhimu; au kana kwamba walikuwa watazamaji tu, hawakuhusika. Ingawa kwenye moja ya picha maarufu ya kikao kati ya wadau muhimu wa Mapinduzi kutoka chama cha ASP na Umma Party anaonekana mwanamke miongoni mwa wahusika wakuu wa kiume hakuna mwandishi wa ndani au nje aliyeona haja kuhoji au kuandika juu ya uwepo wake kwenye hadhira hiyo kwa wakati huo.

Picha maarufu inayomuonesha Biubwa Amour Zahor akiwa mwanamke pekee akiwa na wanamapinduzi wanaume.
Mwanamke huyo ni Biubwa Amour Zahor. Hivyo, kwa mara ya kwanza, neno “Mwanamapinduzi” linarudi katika asili yake— “Mwana” katika jamii ya Kizanzibari ina maana nyingi. Mojawapo ni kumaanisha mtoto wa kike, yaani binti. Pia ni kiambatanisho kinachotumika kutambulisha jinsi ya mtoto katika kumbariki jina kwa mfano Mwanabaraka, Mwanahamisi au Mwanawetu n.k. Kadhalika ni jina lililotumika kuwatambulisha wanawake wenye darja au vyeo kutoka utawala wa jadi wa Zanzibar mfano Mwana Fatuma na Mwana wa Mwana ambao waliwahi kuitawala Zanzibar au sehemu za Dola la Zanzibar kabla ya ujio wa Waomani. Hivyo, matumizi ya neno hili kwenye jina la kitabu linasisitiza umiliki wa wanawake katika Mapinduzi ya 1964 baada kupokwa au kufifishwa uwepo wao kwa muda mrefu.
Simulizi ya Mwanamke Mwanamapinduzi ni ya kipekee kwa vile inamhusu mhusika ambaye umaarufu wake si kutokana na uzao wake lakini kutokana na kile alichokipitia. Simulizi hii inafanya mageuzi katika kuhabarisha historia kwa kumulika si tu ushiriki wa jinsi ya kike katika vuguvugu za mabadiliko lakini pia kumulika namna mahusiano ya kijinsia yanavyoweza kukwaza au kustawisha udumu wao katika maisha ya umma na harakati za kimageuzi kwa ujumla.
Mke au mwenza wa Ingen au Okello wakiwa Zanzibar walikuwa nani? Hakika kuna wanawake wengi ambao hawajatambuliwa si tu kwa uwepo wao lakini pia kwa uwekezaji waliofanya kwa Zanzibar. Leo, skuli zote zilizo na historia ya walimu wakuu wanawake zimebadilishwa majina na kupewa majina ya viongozi ambao tayari washatambulika na majina ya madaraja na miundombinu mingine. Kitabu kinathibitisha mchango wa elimu katika maisha ya Biubwa Amour Zahor. Kizazi cha leo kitakuwa vipi na uelewa mpana wa wahusika na michango yaliyotolewa kama rejea zetu zinabaki kuwa finyu, si wakilishi wala jumuishi?
Simulizi nyingi zinazowahusu wahusika wakuu wa kiume zina upungufu wa rejea ya kijamii. Mara nyingi simulizi zao hujikita na huhusika na mhusika mmoja tu. Hawana kawaida ya kuchangia jukwaa la umaarufu na wengine. Kitabu cha Mwanamke Mwanamapinduzi kimefanya jitihada za kipekee kuhakikisha kuwa wanawake wengine walioshiriki harakati za uhuru na Mapinduzi wanamulikwa.
Ni fakhari kubwa kuwa Mwanamapinduzi wetu kasimuliwa na mtoto wa nyumbani kwani mara nyingi simulizi juu ya wanawake katika kanda ya Afrika Mashariki husimuliwa na wageni. Kwa muda mrefu Bi. Biubwa Amour Zahor alichelea kuwakubalia wengi ikiwemo binti yake Lubayna kuandika wasifu wake kwani alitaka uandikwe na uchapishwe kwa Kiswahili ili hadhira iliyokusudiwa ifikike kwa urahisi.[4] Kuwa kitabu kinazinduliwa kwanza Zanzibar ni faraja ya ziada.
Kudhihirisha Uhusiano Wangu na Mhusika Mkuu
Ningependa uhakiki wangu ukidhi vigezo vya kuwa uchambuzi huru hivyo sina budi kudhihirisha kuwa Mhusika Mkuu ni bibi yangu.[5] Nimeona ni muhimu kulidhihirisha hili kwani linaathiri namna ninavyokisoma na kukichambua kitabu hasa yale yaliyosemwa au ambayo hayajasemwa kwani kuna baadhi ya mambo hayajawekwa wazi ndani ya kitabu hivyo kukulazimu usome baina ya mistari.

Mhakiki, Salma Maoulidi, na Mhusika, Biubwa Amour Zahor, wamekaa katikati pamoja na wanafamilia wengine wakati wa uzinduzi wa awamu ya kwanza uliofanyika Zanzibar.
Nini kimeshawishi nini kimesemwa na jinsi kilivyosemwa na nini kimeachwa? Je, ni suala la kutia ‘mambo chumvi’ au kufunika kombe? Yote mawili yanaweza kuwa yameshawishi nini kimesemwa na namna kilivyosemwa.
Ikumbukwe pia kuwa katika jamii ambamo “heshma” (respectability) ni kila kitu na kwa vile kwa maamuzi aliyoyachukua juu ya namna ya kuishi maisha yake tayari heshima ya Biubwa Amour Zahor imewekwa mashakani inawezekana kuwa kwa kuelewa hili Mhusika Mkuu ameamua kuwa ‘mchumi’ na baadhi ya maelezo. Bi. Biubwa anaweza kusimulia tukio fulani kwa mfano kazi maalumu aliyepewa na Mzee Karume kuifuata barua aliyompa Ingen au kufungwa kwake baada ya kuuwawa mzee Karume lakini bado kukawa bado na masuala mengi kuhusu muktadha mzima uliomfikisha msimulizi pale. Na hapa ndipo unapoona uchanga wa mwandishi kwani baadhi ya mambo angeweza kuyadadisi na hatimaye kutafuta muafaka wa namna ya kuyawasilisha kwenye kitabu kwa namna ambayo utu, usalama na heshima ya kila mtu inalindwa.
Inafaa pia nidhihirishe uhusiano wangu na mada yenyewe—ya ushiriki wa wanawake katika harakati za ukombozi. Hii ni mada niliyoifuatilia kwa muda na ilinishawishi kuwatafuta na kuwahoji baadhi ya wanawake wa kawaida waliowekeza katika ukombozi wetu.[6] Nilizungumza na wanawake kutoka Zanzibar na pia kutoka Tanganyika haja yangu kuu ikiwa kuweza kunasa sauti zao kabla hawajaondoka duniani. Mmoja wa wanawake niliozungumza nao kwa kirefu ni Bi. Ashura Hilal ambaye ni mmoja wa chanzo cha taarifa katika kitabu hiki.
Chapa ya Mhusika
Watu huzaliwa wakiwa na nyota zao ambazo kwa kiasi kikubwa huathiri mapendekezo, tabia ama mirengo yao ya asili. Huu ndio upekee wa mja. Mengine mtu hujifunza kwa wengine au kupitia uzoefu wa maisha. Biubwa Amour Zahor ana chapa yake. Moja ni udhati wa nafsi na kusudio. Kwa yoyote anayetaka kufahamu maamuzi na matendo yake basi hili linajidhihiri—akishaamini au akipenda basi anatenda kwa udhati, si kwa shingo upande au kwa kuonekana.
Vilevile harakati zake si ndogo na ni vigumu kumfananiza au kumkisia ‘kama wengine’. Bi. Biubwa hafungwi na ada, mitizamo ama maono. Yeye ana maamuzi binafsi akishaamini jambo. Ni mtu jasiri kwa maana ya ujasiri na inawezekana kujiamini kwake na uthubutu wa kufanya vitu hata wanaume wengine wasingeweza linawatatiza wengi wanaotaka kumpima kwa mizania ya kawaida.[7]
Biubwa Amour Zahor si mtu wa kawaida na ndivyo nyota yake ilivyojaaliwa. Hata wanawe wanalielewa hili kwani humwita “Starring”. Peke yake hii inakupa taswira ya mtu aliye Biubwa Amour Zahor. Ni mtu ‘mwenye uhai’ (energy) ama mikiki yake; ni mtu anayekuwa katikati ya na si pembeni ya mambo yaani ni Mhusika Mkuu. Katika enzi hizi za kidijitali unaweza kumuelezea kama kitufe cha utayari daima kiko hai, kimewashwa.
Kuutanguliza wasifu huu ni muhimu kama kusudio ni kumtendea Biubwa Amour Zahor haki kwa kumuweka kwenye mizania anayostahili badala ya kumfananiza na wengine au kumhakiki kwa darubini finyu ya jinsi “anapaswa awe” au kawaida iliyozoeleka kwa watu wa ‘namna’ yake.[8]
Kwa Nini ni Muhimu Kusimulia?
Miaka michache iliyopita kulifanyika uzinduzi wa kitabu kuhusu mchango wa Ali Sultan Issa na Seif Sherriff Hamad kuendeleza haki za binadamu Zanzibar. Mke wa kwanza wa Ali Sultan Issa ambaye ni dada yake Biubwa, Bi. Asha Amour Zahor, anagusiwa kwa kuchovya kwenye kitabu hicho na wala hapewi umuhimu. Anasimuliwa kama mke chapwa![9]
Bi. Asha Amour Zahor ni mfasiri wa kitabu maarufu juu ya kupinga siasa za ubaguzi wa rangi kiitwacho Uncle Tom’s Cabin.[10] Mchango wake kama balozi wa kitamaduni upo wazi kwenye simulizi hii na hata kwenye kumbukumbu rasmi.[11] Itoshe kusema kuwa kama aliyoyafanya yaonekane hata kwa “mwanamapinduzi kinara” ambaye ndiye mwenza wake si lolote, si chochote ndio maana uthubutu wa mdogo wake unawatatiza wengi.

Bi. Asha Amour Zahor, dada wa Biubwa Amour Zahor, na wanawake wenzake wakiiwakilisha Zanzibar katika mkutano wa kimataifa.
Ndoto iliyomsukuma Biubwa Amour Zahor hata akajiingiza kwenye harakati za kuleta mageuzi Zanzibar ni kuona jamii yenye usawa. Lakini je jamii inawaona kuwa watu wote, hasa wanawake, kwa namna ama mizania sawa?
Uchambuzi wangu utajitahidi kutumia zana ya kifeministi iliyobuniwa na mwananadharia mwanamke mmarekani mweusi Kimberlé Crenshaw katika kufahamu namna mkusanyiko wa hali au utambulisho tofauti wa mtu iwe jinsi, tabaka, rangi, umri/rika, elimu, utimamu wa uzima n.k husababisha kuwepo mifumo mseto ya ukandamizaji au upendeleo. Kadhalika utakopa kutoka kwa bell hooks, mwananadharia mwingine mwanamke mweusi aliyesisitiza kuwa uzoefu wetu duniani au ufahamu wetu wa mambo tofauti duniani unaathiriwa na pale tuliposimama kitabaka.
Inawezekana kuwa uandishi wa kitabu hiki umetatizika kutokana na masafa kati ya mhusika na mwandishi. Kadhalika ugonjwa wa korona umewageuza watu wengi wafungwa ndani ya majumba yao. Hata hivyo, uandishi huu ungefaidika zaidi na watu mseto ikiwemo wenzake waliobaki, watoto wake na hata ndugu zake. Kitabu kinatufahamisha tu, kwa mfano, yeye ni mtoto wa tatu lakini haisemi katika familia ya watoto wangapi.[12]
Muktadha: Zama za Harakati Zinahabarishwa na Mambo Gani?
Maudhui makuu ya kitabu yanatokea katika kipindi kabla, wakati na baada tu ya Mapinduzi ya 1964. Kuna tabia ya kuchora matukio ya kipindi hiki kwa namna inayohalalisha msimamo uliotamalaki kuhusu harakati za siasa na hatimaye Mapinduzi ya 1964. Ikumbukwe kuwa hiki kilikuwa ni kipindi cha mabadiliko makubwa duniani kote— vuguvugu za kisiasa zilikuwa zikindirima barani Afrika na duniani kwa ujumla.[13]
Ni kipindi cha “uzao mpya” (revival) ambacho kilileta chachu mpya (dynamics) kisayansi, kijamii na kiutamaduni.[14] Kizazi cha Biubwa Amour Zahor tofauti na mama zao au hata bibi zao kilikuwa huru zaidi katika maisha ya kijamii kwani suala la kwenda skuli, kwa mfano, kwao lilianza kuwa ni jambo la kawaida kwa wasichana wa rika na tabaka lake. Bila ya shaka elimu na fursa nyinginezo zinaleta mahusiano mapya ikiwemo maingiliano baina ya watu. Binti mfalme Amal, kwa mfano, anakumbana na mwanasiasa Maulidi Mshangama el Haji naye kutoka nje ya wigo wake au desturi ya “ndoa za kupangwa.”[15]
Kitabu kinaanza na kitahanani kilichotokea Vita vya Juni 1961 Zanzibar. Mbali na kutandika historia sura hii kwa hakika ndio inayotoa mwanga juu ya hali aliojikuta nayo Biubwa Amour Zahor kutokana na uamuzi wake wa kufuata na kuishi siasa alizoziamini katika muktadha wa kisiasa uliojaa mivutano ya kiitikadi, Kijamii, na kitabaka. Namna alivyohimili mivutano hiyo ndio msingi wa uwanamapinduzi wake. Kitabu kinamalizikia Awamu ya Saba ilipomkumbuka na kumtunikia nishani ya Uwanamapinduzi mwaka 2019 takriban miak 55 baada ya Mapinduzi!
Muandishi wa kitabu hiki anastahili shangwe kwa namna alivyoweza kuuanika muktadha binafsi wa Mhusika Mkuu na kwa kiasi kikubwa ulivyoathiri matendo yake. Wakati historia ya mageuzi inaandikwa Zanzibar, Biubwa alikuwa ni binti wa miaka 22 na mama wa watoto wadogo. Alikuwa katoka kwenye mahusiano ambayo jimai hayakuwa ya kawaida na Bw. Fawcett, Mwingereza na kuingia katika mahusiano na Dr. Kingwaba, Mwafrika. Pia alikuwa mshiriki na mdau muhimu wa safu ya mageuzi Zanzibar katika chama ambacho ni nje ya asili na tabaka lake. Kwa kuangaza haya Zuhura Yunus ameweza kwa namna halisia kuonesha namna changamoto za kijinsia zinavyowakumba na kuwazonga wanawake; badala kuwaweka huru, huwaweka hatihati.
Kitabu na Mhusika ni Watata wa Historia?
Utata haupo kwa maudhui au mhusika wa wasifu. Utata upo katika “hangover” ya jamii ya Kizanzibar juu ya Mapinduzi na masalia ya Mapinduzi. Kuna mrengo wa kusimulia Mapinduzi. Haya yameturithisha ufinyu wa upeo wa simulizi juu ya Mapinduzi. Ukichanganya na desturi ya ujuaji ni vigumu kuwa na uchambuzi huru.
Mfano mdogo kati ya mwaka 1960 alipofariki Said Khalifa utawala wa “waarabu” Zanzibar ulikuwa katika mpito kwani aliyemrithi Sultan wa muda mrefu alikuwa mgonjwa na kufariki mwaka 1963 na Sultan wa mwisho alidumu miezi kadhaa tu kwenye utawala kabla ya kupinduliwa. Kadhalika wahusika kama kina Field Marshall Okello wana kipindi kifupi sana nchini Zanzibar na katika siasa za Zanzibar ingawa wanatukuzwa kuwa vinara wa Mapinduzi bila mjadala.
Shauku na matarajio wengi wanayokuwa nayo juu ya maandiko yanayohusu Mapinduzi huenda ikawa inaakisi kile ambacho kama jamii tunahisi bado hakijatimu ndani ya maisha yetu licha ya kutokea Mapinduzi. Kama ilivyokuwa kwa Biubwa Amour Zahor tulitegemea kuwa Mapinduzi yangetupa mustakabali mwema zaidi, yataleta masikilizano na maridhiano hivyo jamii ingepata faraja na uhakika zaidi. Lakini hata katika kitabu hiki bado tunaachwa na maswali zaidi kuliko majibu. Bado kitendawili cha nani alikuwa nyuma ya Mapinduzi ya tarehe 12, 1964, sio yale yaliotizamiwa, hakijateguka.[16]
Pia utulivu, haki na upendo uliokuwa unatizamiwa haujatimia kinyume na hata anavyojifariji mwenyewe Mhusika Mkuu. Mfano wa hili ni shamba linalozungumziwa katika kitabu lililopo Dunga halishi kuvamiwa. Wavamizi humkejeli Biubwa akitetea mali yake kuwa “tumepindua ili watu kama nyie wasituyanyase!” Sijui kama haya ndio madhumuni ya Mapinduzi. Linalosikitisha zaidi ni yule anayeambiwa huenda kajitoa zaidi kwenye Mapinduzi kuliko yule anayetaka kuyafaidi kwa sababu tu rangi au chama chake vinamruhusu.
Gharama za Mapinduzi
Simulizi ya Biubwa Amour Zahor inatuthibitishia kuwa mbali na kuhusika na Mapinduzi, wanawake wanabaki kuwa masalia ya Mapinduzi. Gharama walizolipa au kutakiwa kulipa ili kukubalika kama wanaharakati au wapinduzi ni gharama binafsi. Zuhura Yunus amefanikiwa kuonesha hili kwa namna fulani ingawa kasisitiza zaidi mpasuko na familia yake. Ukweli ni kwamba gharama alizozilipa Biubwa Amour Zahor na bila ya shaka wanawake wengine ni kubwa na za kudumu kama nitakavyothibitisha hapa.

Mhusika Mkuu, Biubwa Amour Zahor, na Mwandishi, Zuhura Yunus, wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili uliofanyika Dar es Salaam.
Mfano mdogo ni kuwa binti yake Lubayna nusra awe mhanga wa ndoa za kulazimisha maamuzi hayo yakifanywa na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Mapinduzi akiwemo Mzee Karume. Kadhalika mbali na kuwa alikuwa mjane katika kipindi hiki kigumu wakubwa zake Biubwa hawakujali hatima ya watoto wake wadogo na kazi alizokuwa akitumwa zinathibitisha hili.
Wanaoaminika “kupindua” wameendelea kutunikiwa vyeo vikubwa na serikali ndani na nje ya nchi. Biubwa, kwa upande wake, kaachwa solemba akitegemewa hata na wale walionufaika tu na Mapinduzi awaandalie chai. Ingawa kajitoa kwa uwepo na ushiriki wake katika jopo la waivishaji wa mabadiliko bado kuna watu walioona hastahili kunufaika na Mapinduzi aliyoyavulia nguo kwa hali, mali na uzima wake.
Leo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina mahusiano kamili na Oman. Raisi wa Zanzibar, Makamo wa Rais wa Zanzibar na Mawaziri wamefanya ziara Oman. Biubwa Amour Zahor haruhusiwi ndani ya Oman na hata kama akipita njia na ndege hapati visa ya kuingia na kuonana na ndugu zake. Anaendelea kuadhibiwa kwa aliyoyafanya akiwa kijana wa miaka 22.
Mfano wa pili unahusu namna hata kundi la wenzake lilivyomtendea. Biubwa kategemewa kuacha kila anachokijua na kubaki pekee bila mhimili wa maana kwa maamuzi yake ya kushiriki harakati za kisiasa. Ingawa kipindi hicho alikuwa mdogo kiumri na pia alikuwa na watoto wadogo ni wachache walioona umuhimu wa kumsaidia kwa hali na mali.
Watu kama Abdulrahman Babu (na hata Mzee Karume) kwa upande wao walipopata misukosuko walichangiwa na kuhifadhiwa na watu ndani na nje ya nchi ili wasiterereke. Ajabu ni kuwa viongozi wote wawili walikuwa ni watu wa makamu wenye mitandao mikubwa na wenye rasilimali zao hivyo walikuwa na uwezo mkubwa zaidi kuhimili vishindo. Huu si utofauti tu wa namna shida za mwanaharakati au mwanamapinduzi zinavyotizamwa kijamii lakini pia ni ishara ya ubaguzi na ukandamizaji unaomsibu mwanaharakati au mwanamapinduzi wa kike ambaye kamwe matendo yake hayatizamwi kishujaa bali kihaini na kamwe haja si kumsitiri bali kumuadhiri.[17]
Mageuzi ya Kijinsia; Kina cha Uwanamapinduzi
Rejea nyingi nilizowahi kupitia juu ya harakati za kudai uhuru au juu ya watu mashuhuri hata zile zinazowahusu wahusika ambao wanaonekana “wameendelea” (progressive) hazitoi tumaini chanya kwa mahusiano ya kijinsia. Wanamapinduzi wengi wa jinsi ya ‘me’ hulonga nadharia ya usawa lakini usawa kwao haumaanishi usawa wa kijinsia, yaani kati ya wanawake na wanaume; au hata wa kirika. Mara nyingi siasa zao huishia katika kubadilisha nafasi, si kuleta mageuzi ya msingi ya kimahusiano. Hili liko dhahiri katika madai na hata mifumo inayoendelezwa katika nyanja mbalimbali.
Hivyo, wakati Biubwa kajikomboa kifikra na kimatendo kwa kuoana na Mwafrika na hata makabila mengine, wenzake ambao wametukuzwa kwa umahiri wao hawajathubutu kuoa nje ya “milieu” yao; inawezekana wengine pia walioa wanawake ambao walitoka tabaka za juu kuliko wao lakini nadra kuoa nje ya rangi au utamaduni wao. Najiuliza, kwa mfano, wanamapinduzi wangapi ambao walikuwa si ‘Waafrika’ walitafuta wanawake wa Kiafrika kuwaoa kama vile wanaume wa Kiafrika walitafuta wanawake wa Kiarabu au Kihindi kuwaoa?
Kadhalika wakati Biubwa anategemewa kuchanganyika na kujikubalisha na hali yake mpya kama mke wa daktari na mke wa Mwafrika mara nyingi wahusika wa kiume hutofautishwa na kutarajiwa kujipambanua kwa “utofauti” unaotokana na nyadhifa zao mpya badala ya kumezwa na mfumo. Hivyo, Dokta Kingawaba kapanda chati kijamii kwa kuoa Mwarabu lakini Biubwa kashuka chati kwa kuolewa na Mwafrika, tena msomi.
Wakati wa ghasia za Juni 1961, Dokta Kingwaba alitegemewa kwa ajili ya kazi yake kuacha familia yake ambayo ilikuwa katika hatari kubwa kwenda kuwahudumikia wengine. Hii imeonekana ni kawaida na hata inaonekana ni jambo la kishujaa. Hata hivyo, kazi alizozifanya aliyekuwa mwenza wake, Biubwa Amour Zahor, kama ilivyokuwa kwa dada yake, Asha Amour Zahor, hazionekani ni za kishujaa.[18]
Wengi watajaribu kusoma nyuma ya pazia na hata kutoa tafsiri nyingi juu ya nini hasa akifanya. Wanasahau kuwa kila kazi ina hadidu rejea yake; ina mtekelezaji wake na ina majukumu ya kutimizwa. Suali lisiwe nani katimiza bali katimiza kwa kiwango kipi cha ufanisi?
Mahusiano ya mhusika mkuu na wahusika wa jinsi ya kiume waliokuwa karibu naye walimzidi umri— si Mzee Karume, si Abdulrahman Babu, si Bw. Fawcett au Dokta Kingwaba. Kutokana na tofauti yao kiumri hawa watu amekutana nao vipi? Hili peke yake linataka uchanganuzi wake. Kitabu kinaonesha kuwa Biubwa alikuwa na kipawa fulani na waliokuwa wenza wake awe mzungu au Mwafrika. Pia, kuwa alikuwa na ukaribu na Mzee Karume jambo ambalo halijawafurahisha waliozoea kupiga ramli za mahusiano.
Biubwa ni mwanamke aliyesoma kwa enzi yake na ni mtu anayejihabarisha kwa desturi yake ni mbukuaji. Kwa uelewa alionao juu ya mambo na kujitambua kwake kunamuweka katika mgongano na wale wanaoamini kuwa wao ni maalumu na walichonacho ni maalumu. Kwa mtizamo wa tamaa yeye ni kama ngawira na kama kitu cha tunu ambacho mwanzo kinafurahisha lakini uhalisia wake— anajiamini, muwazi, jasiri na mwenye uthubutu—unageuka kuwa shuburi. Viongozi wengi wanaharakati wanahubiri usawa ila haina maana wanaamini usawa au kuukumbatia na utamaduni wetu wa uongozi na kisiasa unadhihirisha hili
Mbali na kuanika mfumo dume uliotapakaa katika kila nyanja ya maisha, kitabu pia kinaibua madhila sugu ya ukatili wa kijinsia, ubaguzi wa kijinsia na masuala tata ya ndoa za kulazimisha; ubakaji; kutengwa kwa wanawake “waasi” ili kuwaadhibu na kuwaweka katika mstari. Hii inaondoa dhana kuwa harakati za kudai haki, utu na uhuru zinakosa doa la ubaguzi ama hazijagubikwa na upendeleo.
Mchango wa Mwanamke Mwanamapinduzi Kuweka Bayana Uhalisia wa Mapinduzi
Kwa namna ya pekee simulizi inamulika ushiriki au michango ya wanawake katika Zanzibar tuliyoirithi na vikwazo walivyokumbana navyo.[19] Simulizi hii inaweka bayana matabaka na migawanyiko ambayo inachepuza mseto wa jamii ya Kizanzibari—suala la mjini-shamba; Mwarabu- Mwafrika[20]; Mji Mkongwe-Ng’ambo; Pemba-Unguja; mzawa-mhamiaji; mpinduzi-mwanaharakati; mwanamke mtulivu na muasi!
Kadhalika simulizi hii inatudhihirishia kuwa jamii tofauti zilishiriki katika harakati za kuleta mabadiliko Zanzibar na kuwa hata katika jamii moja kulikuwa na utofauti wa itikadi au hali za watu au mwamko n.k. Si kila kitu ni cheusi au cheupe. Hivyo mbali na kinachoaminika kulikuwa na mseto wa watu katika kila chama na harakati za kipindi hicho. Unapotizama picha za wanamapinduzi unaona Wazanzibari wa kila rangi ingawa wengi ni wanaume.
Funzo jingine ni kuwa si kila mtu au kila jamii ilitafsiri maslahi kwa namna sawa kabla au hata baada ya Mapinduzi. Wako walioneemeka na waliojineemesha na wako waliotoa mchango wao, wakatumika na wakaendelea na maisha yao au wakatoswa. Biubwa Amour Zahor ni miongoni mwa watu wachache waliokuwa karibu na mamlaka tokea kipindi cha Mapinduzi lakini hajajinufaisha kwa namna yoyote kutokana na ukaribu huo. Badala yake ametoa msaada kwa watu wengi ambao wamekuwa wakizungushwa na watendaji au viongozi kwa kufikisha madhila yao panapostahili. Kwa kufanya hivi haonekanii kuwa mzalendo bali shawishi!
Suala jingine linalosisitizwa sana kwenye kitabu ni tofauti ya rangi kama ndio moja ya migawanyiko iliyosababisha mpasuko ndani ya familia ya Amour Zahor pamoja na hata katika jamii. Bila ya shaka “upendeleo” uwe wa rangi au kijinsia ni moja ya namna utawala unagawa watu ili kuwadhibiti vizuri. Sasa ndoa na Dokta Kingwaba kwa mfano ilipingwa kwa sababu yeye alikuwa ni Mwafrika au hili lihalalishe hatua iliyochukuliwa na wapinduzi kuingia nyumba za watu na kuwaoa watoto wa kike kwa nguvu?
Nikiwa kama mchambuzi kazi yangu kila wakati ni kuhoji sio kuhukumu. Kila ukihoji unaweza ukapata majibu au maswali mapya ya kutanua upeo wa uelewa. Bwana Fawcett alikuwa si Mwafrika lakini pia alikataliwa kumuoa Biubwa. Jambo ninaloliona kwa hawa wanaume wote wawili ni kuwa walikuwa tayari ndani ya ndoa zao na walikuwa na familia zao. Je, hili lilichangia wazee wa Biubwa kutopendelea ndoa hizo?
Kadhalika kwani hata watu wa rangi au asili mmoja hawakataliwi ndoa iwe jambo la kuzungumza likihusu watu wa asili na jamii tofauti tu? Wazee wa Dokta Kingwaba hawajataka amuoe dadake Mussa Maisara kwa sababu alikuwa mjane na pia ‘mtoto wa mjini.’[21] Walitaka mtoto wao msomi aoe mtoto aliyetulia wa shamba.
Kwa maoni yangu haisaidii kuendeleza itikadi na fikra zenye kuhalalisha jambo kwa sababu kisiasa ina tija ya soda. Inafaa pia baadhi ya fikra na itikadi hizi zihojiwe ili zipate kutafsiriwa kwa namna ambayo itamfanya kila mwanajamii kujihoji na kutaka kubadilika.
Hitimisho
Mara nyingi uhalali wa watu unanasibishwa na kitu fulani. Kwa mfano, siasa zao na, kwa wanawake, na mwenza wake au ukoo wake. Wanawake wengi wanaotajwa katika historia, ikiwemo katika kitabu hiki wanatajwa wakinasibishwa au na baba zao au wenza wao. Hata hivyo, ukisoma kitabu hiki na simulizi za wahusika wake ni wazi kuwa wanawake hawa wamekuwa katika harakati si kwa sababu ya wenza wao. Wengi kama Ashura Hilal wamekutana na wenzi wao wakati tayari washajiunga katika vuguvugu za siasa.
Ni kuwanyima muamko wao wa haki; na hiyari yao kama watu huru kisiasa na kiitikadi kuwanasibisha hivyo. Wakati ninakua nikisikia bibi yangu akiitwa ‘shawishi’ akionekana na watu waliokuwa madarakani ikiwemo marais.[22] Inawezekana kuwa wengi hawajui kuwa wengi wa hao walioko madarakani ni wenzake kupitia safari yake ya kisiasa pamoja na utumishi serikalini.
Mageuzi hayaletwi na watu walioridhika na hali iliyopo. Huu ni ukweli wa asili. Mabadiliko hayaji kwa kutegemea tu miujiza itatokea na hali mpya itakuja bila ya kuwepo mikiki ya nafsi au kukera wengine.
Wengi wetu tumegubikwa na hofu ya nini kitakuwa? Nini ninapoteza? Watu wataelewaje? Hofu inayotufunga na kufifisha si tu ndoto zetu lakini hata utu wetu.
Bado kuna mambo mengi ya kumulika kuhusu maisha ya Biubwa Amour Zahor. Kwa mfano, kapitia mengi alipowekwa ndani baada ya kifo cha Karume. Haya hayagusii? Kadhalika kuna sehemu nyingi ndani ya kitabu anataja watu au matukio bila ya kutaja utambulisho wa wahusika tofauti na vitabu vya wanamapinduzi wanaume ambao huanikana kiunaga ubaga.
Je anajilinda? Kuna anaowalinda? Au hata yeye anajua kuwa kuna mipaka?
Bila ya shaka kitabu hiki kimefungua kurasa ya kumtafiti na kumjadili mshiriki mtata (complex) wa harakati za mageuzi Zanzibar. Tunachoweza kuvuna kutoka kazi iliyofanywa na Zuhura Yunus ni kubaini kuwa katika wakati uliokuwa si wa kawaida, Biubwa Amour Zahor kapambana na hofu ya asili.
Ahukumiwe kwa dhati ya imani yake na dhamira ya kulingania maisha yenye utu—yenye usawa, haki na ustawi kwa wote. Kamwe nafasi yake katika historia ya Zanzibar isidunishwe kupitia mitizamo iliyotamalaki hofu; au ufinyu wa kuthamini chemchemi mseto za fikra na miendeko ya kimageuzi.
[1] Miongoni mwa wanawake wa Kizanzibari walioandikwa sana na hata kuundiwa makavazi ni Sayida Salme mtoto wa aliyekuwa Sultani wa kwanza kutoka Oman wa Zanzibar na Sitti binti Saad, mwimbaji mashuhuri wa taarab aliyehifadhi sauti yake kwenye santuri huko India.
[2] Angalia kwa mfano Okello, John (1967) Revolution in Zanzibar. [Nairobi] East African Pub. House (OCoLC)600723074; Hashil Seif Hashil (2019) Mimi, Umma Party na Mapinduzi ya Zanzibar na R. K. Mwanjisi, Karume Abeid Amani, 1905-1972. East African Pub. House [1967].
[3] Hili ni muhimu kulitambua kwani wanaume ambao hawajatimiza vigezo vya ‘umaarufu’ wa mfumo tawala kwa mfano wanamapinduzi waliokuwa si wasomi au hawatoki kwenye nasaba zinazotajika pia hawajaandikwa.
[4] Kwa muda mrefu Dr. Fawcett akiishi na kufanya kazi Marekani.
[5] Mbali na kuwa na mahusiano ya mtu na mjukuu wake, Bi. Biubwa ni mmoja wa watu aliyenitambulisha kwa maandiko mseto juu ya Historia ya Zanzibar.
[6] Nimetengeneza kanda “Wanawake na Ukombozi, si lele Mama!” ambayo nimeshaionesha katika hadhira mbalimbali za kisomi na harakati kama Tamasha la Jinsia. Bado sijapata wasaa ya kuweka taarifa hizo muhimu katika maandishi.
[7] Kwa maoni yangu kitabu kizima kimesheheni mifano ya ujasiri wake ingawa kutokana na mitizamo mgando iliyotawala kuhusu heshima au dhidi ya wanawake imesababisha yeye kubezwa au kulaaniwa badala ya kutukuzwa au kutambuliwa kuwa ni kigezo cha mtu mwenye utashi na msimamo usioyumba.
[8] Hili tatizo ni kubwa zaidi kwa wanawake. Hata mwandishi kwa kiasi fulani anaonesha mrengo wake (bias). Kwa mfano, kwa vile ni binti wa Kiarabu mwenye asili ya Kiomani basi alitegemewa atakuwa taa na kusubiri jamii impangie maisha.
[9] Ingawa huyu ndiye mke wake wa kwanza anamzungumzia zaidi mwanamke wa Kiingereza anayeingia naye mahusiano. Rejea G. Thomas Burgess, Race, Revolution, and the Struggle for Human Rights in Zanzibar: The Memoirs of Ali Sultan Issa and Seif Sharif Hamad, Athens, OH: Ohio University Press, 2009.
[10] Siku za karibuni imezoeleka kuwa mume akihama chama basi mke amfuate. Uandishi wa Bi. Asha Amour Zahor unadhihirisha upeo na msimamo wake pamoja na siasa zake kuhusu mambo ya msingi ya utu iwe mwana ZNP au mke wa muasisi wa Umma Party.
[11] Picha hii kwa mfano inamuonesha Bi. Asha Amour Zahor akiwa katika Mkutano anaiwakilisha Zanzibar na wenzake. Inafaa kumtaja Ally Saleh kuwa ni miongoni mwa wachache kumtaja Bi. Asha Amour Zahor kuwa ni katika wanawake mashuhuri kipindi cha kudai uhuru ingawa anakosa kumtaja Bi. Biubwa Amour Zahor, angalia genderbalancinginitiativesinzanzibar.pdf (tzonline.org).
[12] Binafsi najua ana ndugu wa kike 7, wawili kati yao ni marehemu. Ana ndugu wa kiume pia.
[13] Jamii ya watawala wakati huu ilikuwa dhaifu kwani toka baada vita vikuu vya pili vya dunia wengi walikuwa kwenye madeni makubwa, mali zao ikiwemo mashamba zikiwekwa rehani kwa wakopa pesa.
[14] Ikumbukwe kwa mfano kuwa mtu wa kwanza Yuri Gagarin alizunguka sayari ya dunia Aprili 1961.
[15] Huyu ni mtoto aliyelelewa na Said Khalifa na Bi. Nunu na hata kuzuru naye Uingereza mwaka 1953, Angalia https://www.royalark.net/Tanzania/zanz6.htm; https://theafricanroyalfamilies.com/2022/02/14/african-royals-at-the-british-coronation-1953/; https://twitter.com/ismailjussa/status/1176978466190897153?lang=en.
[16] Kulikuwa na jitihada kutoka kambi mbalimbali za siasa za Zanzibar kugeuza hali ya mambo. Upokeaji wa tukio la Januari 12, 1964 linaashiria kuwa halijatarajiwa hivyo kuzua maswali juu ya nani alikuwa nyuma yake. Kilichokuwa na uhakika ni baada ya kutokea wazoefu wa kisiasa waliyadandia na inayosimuliwa sasa ni historia.
[17] Leo tabia kama hizi zinawapata pia wanasiasa wanawake ambao maisha yao binafsi hutumika kusitisha ndoto zao kisiasa.
[18] Kwa mfano, Biubwa Amour Zahor kaokoa maisha ya Mussa Maisara ambaye ni shemeji wa Dokta Kingawaba kwa kuendesha gari lililomfikisha hopsitali.
[19] Kwa Tanganyika maandiko hasa ya kifeminist juu ya Bibi Titi Mohamed yameweza kutupa undani tata na wa kina wa ushiriki wa wanawake uliopishana na ‘ushiriki unaotajwa wa kisiasa’.
[20] Hata siasa kati ya Mwarabu wa omani yaani Mmanga na Mwarabu wa Hadharamaut yaani Mshihiri.
[21] Kwa mujibu wa rafiki wa utotoni wa Dokta Kingwaba, Bw. Ali Himid, akimpenda Bi. Ashura Maisara toka alipokuwa anasoma. Wakati huo binti Maisara kaolewa sehemu za Gulioni walipokuwa wanakaa na wao.
[22] Kuna watu wengine walihusisha ‘uwepo’ wa Biubwa Amour Zahor na wanaharakati maarufu wakati wa Mapinduzi si kwa ushiriki wake kama mwanamke huru bali kama kitu cha kustarehesha kama ilivyo hii leo kuwa mwanamke hastahili alama nzuri au cheo kizuri mpaka awe “mchuchu” wa mwalimu au bosi.
Inastahili kusomwa uchambuzi huru kiasi wenye usongo wa mabadiliko mengi katika jamii zetu za Kiafrika.