
Ama kweli “kila zama na kitabu chake”. Maneno hayo yalipatiwa umaarufu na Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, almaarufu Mzee Rukhsa. Wapo tunaoamini kuwa ni ‘kijembe’ kilichoashiria kuwa awamu ya ‘kubana’ imepita na imeingia ya ‘kuachia’.
Hakika katika kipindi cha uongozi wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Kambarage Nyerere, almaarufu Mwalimu, kulikuwa na hali fulani ya kubana uhuru. Japo chama tawala cha enzi zake ndicho kiliongoza harakati za kutupatia uhuru kutoka kwa wakoloni, kiliuwekea mipaka mingi. Tulikuwa huru lakini uhuru huo ulidhibitiwa ama kuhodhiwa kupitia kuwa na chama kimoja tu, magazeti ya aina moja tu, na vyama vya wafanyakazi na wakulima vya aina moja tu.
Lakini ni ukweli usiopingika kuwa misingi mikuu ya uhuru iliwekwa katika awamu hiyo hiyo hasa wakati wa kipindi cha mpito kuelekea awamu iliyofuatia. Mwanzoni wa utawala wa Mwalimu ndipo tulipopata kaulimbiu ya uhuru na kazi. Kisha mwishoni mwa utawala wake ndipo tulipoanza kusimika kile magwiji wa sheria wanachokiita muswada wa haki (bill of rights) katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) ya Mwaka 1977.

Ndiyo maana ni muhimu kusisitiza leo kuwa haya masuala mawili – haki ya kuwa huru na kufanya kazi – ni pacha kifalsafa, kisiasa na kiutendaji. Ni sehemu mbili za shilingi. Ni kweli hata watumwa hufanya au hufanyishwa kazi. Lakini kuna tofauti kubwa pale unapofanya kazi kwa utashi wako mwenyewe bila shuruti. Unakuwa huru kufanya kile chenye tija kwako na kwa wanaokuhusu.
Msingi huu wa uhuru tuliousimika mwaka 1984 na kuuimarisha mwaka 2005 kwenye mabadiliko ya 14 ya Katiba ya JMT unapaswa kulindwa kama mboni za macho yetu. Uzoefu wa ‘kubana’ na ‘kuachia’ au ‘kuuma’ na ‘kupuliza’ tulioupitia kupitia mabadiliko ya awamu za uongozi wa Marais wetu wote ni fundisho tosha kuwa uhuru ni adimu na adhimu.
Kwenye suala la kazi hebu tujikumbushe Ibara ya 22 ya Katiba ya JMT inavyosema: “(1) Kila mtu anayo haki ya kufanya kazi; (2) Kila raia anastahili fursa na haki sawa, kwa masharti ya usawa, ya kushika nafasi yoyote ya kazi na shughuli yoyote iliyo chini ya Mamlaka ya Nchi.”
Ibara ya 23 ya Katiba ya JMT nayo inaliongezea uzito suala hili la kazi hasa katika muktadha wa kipato: (1) Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa za kazi wanayoifanya; (2) Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki.”
Stahiki ya kulipwa au kuongezewa mshahara stahiki kumbe ni suala la kikatiba. Ni haki ya kikatiba kama vile ambavyo kulidai ama kuliongelea ilivyo haki. Lakini katika zama hizi tunazohubiriwa kuwa ni za sekta binafsi kuwa injini ya maendeleo basi haki ya kufanya kazi inafungamana ‘kupita maelezo’ na uhuru wa maoni na kujieleza pamoja na haki ya kutafuta habari/taarifa na kufanya mawasiliano.

Yule Rahab muuza maua mahiri mitandaoni hawezi kufanya kazi hiyo ya kujiajiri bila haki, uhuru na fursa ya kuwasiliana kupitia mitandao ya kijamii kama Instagram, Twitter, Facebook , LinkedIn, na Clubhouse. Ndiyo, na yule Mudi Mabiriani pia. Bila mitandao hiyo Haki Ngowi atapataje ujira stahiki? Hali kadhalika wale akina Kwanza TV wanaotegemea ‘uchuuzi wa habari’ kupitia kile kinachoitwa ‘vitivii vya mikononi’. Wanamuziki wetu akina Roma Mkatoliki nao wanategemea YouTube na kadhalika.
Waliofanya haya Mabadiliko ya Kumi na Nne ya Katiba ya JMT mnamo mwaka 2005 hakika waliona mbali: “Ibara ya 18 ya Katiba inafutwa na kuandikwa upya kama ifuatavyo: Kila mtu: (a) anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; (b) anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi; (c) anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake; na (d) anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.”
Bila haki hiyo ni vigumu kuwa huru kufanya kazi zenye tija katika zama hizi za mapinduzi ya nne ya viwanda yaliyojikita katika teknolojia. Inakuwa ni vigumu mno kubuni na kuvumbua yatakayotuletea maendeleo zaidi maana ubunifu na uvumbuzi kwa kiasi kikubwa unategemea kuchakatwa kwa taarifa, maoni na habari kati ya wabunifu na wavumbuzi. Na katika karne hii ya 21 mitandao ndiyo karakana kuu na huru ya kuchakata hayo kwa kasi ya ajabu – ndiyo ulingo ‘huria’ ambao wakufunzi magwji na wanagenzi mahiri hukutana kubadilishana mawazo kuhusu maarifa na mbinu mbalimbali mubashara.

Zama hizi ni za udadisi na uvumbuzi huria. Tusipitwe na wakati. Mitandao ni fursa ya ajira na ujira.
Uhuru na kazi. Uhuru uendelee. Kazi iendelee.
Ni kweli, uhuru uendelee.
Bila uhuru, hakuna maendeleo.
Ni furaha yangu kuwa sasa tupo hapa kwa upya wetu.
Uhuru na kazi👏👏👏
Hakika!
Uhuru unachangia kiwango kikubwa katika maendeleo kwa kuwa uhuru unaongeza ubunifu
Asante sana Dr Chambi, makala yameshiba na yanatoa ‘shule’ zaidi.
Ni kweli! Kivumbi ni hapo kwenye kufikia uhuru halisi